Saturday, May 28, 2016

HADITHI MWANAMKE SEHEMU YA 5

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 5 na Faki A Faki 0655 340572

ILIPOISHIA

Ndani ya kile kisima kulikuwa na watu wawili waliokuwa wakioga na ndio waliokuwa wakizungumza. Mmoja akatoka na kusimama kando ya kisima hicho. Mara moja nikatambua kuwa ni yule mwenyeji wangu lakini safari hii alikuwa na umbile la kutisha sana.

Kwanza nywele zake zilikuwa nyingi na ndefu zilizoteremka na kumfikia kiunoni. Zilikuwa nywele nyeupe kama mvi za bi kikongwe. Yeye mwenyewe ngozi yake ilibadilika na kuwa nyeupe kama ya mzungu. Machoyake yalikuwa ya kijivu na mboni zake zilikuwa nyembamba na zilizosimama kama mboni za paka.

Bado alikuwa ameota manyoya marefu mwili mzima. Nikagundua kwenye miguu yake hakuwa na vitanga vya miguu kama walivyo binaadamu wote bali alikuwa na kwato nyeusi kama za farasi au punda. Hakuwa amevaa chochote. Alikuwa uchi wa mnyama!

Mwenzake naye akatoka kwenye kisima. Yeye alikuwa mwanaume lakini alikuwa na umbile kama la yule msichana. Miguu yake pia ilikuwa na kwato.

Walikuwa wakizungumza kwa lugha ambayo sikuielewa. Kwa kweli nilishituka sana. Nikapata hofu na uoga mpaka mwili wangu ukawa unatetemeka.

Nikahisii kwamba yule msichana aliyenikarisha mle ndani hakuwa binaadamu bali alikuwa jini na pale alikuwa akizungumza na jini mwenzake.

Nikatengeza mawazo kwamba huenda msichana yule aliniingiza katika nyumba ile kwa hila ili wanidhuru kwani ile damu iliyokuwa kwenye kile kisima ilikuwa ni ya binaadamu kama mimi. Na bila shaka waliingizwa mle ndani na kuuawa kikatili.

Hapo ndipo nilipochanganyikiwa nikajua kwamba dakika zangu za kuishi zilikuwa zimekaribia kwisha.

SASA ENDELEA

“Nitatokaje humu ndani?” nikajiuliza.

Nililirudisha lile pazia. Nikaenda kwenye mlango na kutoka ukumbini. Ukumbi ulikuwa kiza. Sikuweza kuona kitu. Sikuelekea upande wa uani tulikoingilia, nikalekea mlango wa mbele. Nilitaka nitoka kwa kutumia mlango huo bila Zena na mwenzake kujua. Pikipiki yangu nilikuwa nimeshaisamehe.

Kwa muda ule pikipiki haikuwa na umuhimu kwangu, kilichokuwa muhimu illikuwa ni kujisalimisha roho yangu. Nilijiambia kama nitafanikiwa kutoka mle ndani na kukimbia nitakuwa nimeweza kujisalimisha kuuawa.

Nikawa natembea haraka haraka ili niwahi kutoka kabla sijagunduliwa. Kwa sababu ukumbi ulikuwa kiza nikakumba kitu kama meza iliyokuwa imewekwa ukumbini. Niliikumba kwa nguvu hadi ikatoa mlio wa kuburuzika.

Hapo hapo nikasikia sauti ya Zena ikiuliza.

“Amour unanitafuta?”

Sikujibu kitu, nikaikwepa ile meza na kundelea kwenda mbele sasa kwa haraka zaidi.

“Amour unaondoka?” Sauti ya Zena ikasikika tena.

Sikujibu. Nikaendelea kwenda. Sasa nilikuwa nahema kwa hofu. Mdomo nilikuwa nimeuacha wazi huku mikono yangu ikiwa mbele ili niweze kuugusa mlango nitakapoufikia.

“Amour usiondoke, nisubiri”

Sauti ya Zena ilizidi kunichanganya. Ndani ya moyo wangu nikawa naomba Mungu anisalimishe.

“Yarabi nisitiri…Yarabi nisitiri…”

Mara moja nikaufikia mlango. Nikawa naupapasa haraka haraka mpaka nikaushika ufunguo uliokuwa umeachwa kwenye kitasa, nikaufungua kisha nikauvuta mlango. Mlango haukufunguka.

Nikagundua kuwa kulikuwa na vifungulio vingine vilivyokuwa chini ya na juu ya mlango. Nikapeleka mkono wangu juu na kupapasa. Nikapata kifungulio kimojawapo nikakivuta chini.

“Amour umeona nini?” Sauti ya Zena sasa ikasikika kutokea mlango wa uani.

Bila shaka alikuwa akinichungulia kupitia mlango huo. Sikutaka hata kugeuka nyuma kumtazama. Nikainama chini ili nifungue kifungulio kingine kilichokuwa chini.

“Amour usiondoke!” Zena aliendelea kuniambia.

Aliposikia nafungua kile kifungulio cha mlango cha chini akaniambia.

“Hebu nisubiri”

Sasa nikazisikia hatua zake akinifuata kwa mwendo wa haraka. Kwa vile miguu yake ilikuwa na kwato, kwato hizo zilisikika kama za farasi wa kwenye sinema, “Kwa…kwa…kwa…”

Mwili ukanisisimka. Nikajiambia sasa nakufa.

Nikauvuta mlango. Licha ya kufungua vifungulio vya juu na chini. Mlango haukufunguka.

Kwato za Zena zilikuwa zimeshanikaribia. Akili yangu iliunda picha nikikabwa na mwanamke huyo wa kijini na kunifyonza damu yangu kupitia kenye tundu za pua yangu…

Mkono wa Zena wenye kucha ndefu ukanishika kwenye bega. Nikaukutua…

“We Amour nini…?” akaniambia kwa hamaki baada ya kuukutua mkono wake.

Niliuvuta tena ule mlango kwa nguvu. Safari hii ukafunguka. Zena alikuwa ameshanishika shati kwa nyuma. Nikapiga hatua kutoka nje. Zena akaliachia shati.

“We Amour…utaona!” akaniambia.

Nilikuwa nimeshavuka kizingiti cha mlango.

“Hutakwenda popote” Sauti ya Zena iliyokuwa na hasira ikasikika nyuma yangu.

Wakati napiga hatua kutoka nje niliona nimetokea nje ya ile nyumba lakini Zena aliponiambia “Hutakwenda popote” nikaona nimetokea kwenye eneo jingine ambalo sikulielewa. Lile jumba la Zena sikuliona tena. Nikajiona kama nimo ndani ya pango la kutisha lenye njia nyembamba ya kupita.

Vile nilivyokuwa nakimbia niliendelea kukimbia ndani ya hilo pango nikiifuata ile njia nyembamba. Kwenye kuta za mawe za lile pango kulikuwa kumewekwa mishumaa iliyokuwa inawaka.

Kadiri nilivyokimbia nilikutana na njia zingine zilizonichanganya. Sikuweza kujua nishike njia ipi. Kadhalika kulikuwa na mashimo yaliyokuwa yakifuka moshi. Wakati nakimbia niligundua nilikuwa nikizunguka tu ndani ya pango hilo  kwani nilikuwa nikitokea mahali pale pale nilipoanzia kukimbia.

Nikajaribu kushika njia nyingine ambayo nilihisi ingeweza kunitoa ndani ya pango hilo, nikajikuta nimetokea kwenye mlango kama mlango wa nyumba. Nikaufungua ule mlango na kuchungulia ndani. Nikaona kumesakafiwa na kulikuwa na kuta kama za nyumba. Kuta hizo zilikuwa zimepakwa rangi ya samawati.

Nikaingia ndani na kukutana na hewa safi yenye harufu ya mawaridi. Sasa nilikuwa kwenye ukumbi mpana ambao haukuwa na kitu chochote. Nilitembea kwenye ukumbi huo uliokuwa kimya huku nikiwa nimejaa hofu.

Sikujua nilikuwa nimetokea katika nyumba gani na inayoshi nani. Mazingira yaliyonifikisha hapo yalinifanya nipate hofu. Nilikuta mlango uliokuwa wazi, nikaingia katika huo mlango. Nilimkuta mzee mmoja aliyevaa shuka nyeupe akiwa ameketi kwenye mswala.

Alikuwa amejifunga kilemba kirefu kama muarabu. Mwenyewe pia alionekana kama muarabu. Alikuwa na ndevu ndefu na sharafa.

Wakati naingia katika hicho chumba alichokuwemo, mzee huyo  alikuwa ameinama akisoma kitabu. Kitabu chenyewe kilikuwa ni kile nilichomuazima Zena.

Nikasimama mbele yake na kumtazama. Mzee alikuwa akiendelea kufungua karasa.

Nikamuamkia.

“Shikamoo mzee”

Mzee akainua kichwa na kunitazama. Macho yake yalikuwa madogo ya kijivu.

“Marahaba” akaniitikia. Sauti yake ilikuwa na lafidhi ya kiarabu.

“Mzee samahani, naomba msaada wako” nikamwambia.

“Msaada gani?”

“Mimi sijui nilivyofika hapa, ninaomba unioneshe njia ya kutoka nje”

“Unasema hujui ulivyofika hapa?”

“Sijui, nimejiona tu nikitokea katika nyumba hii”

“Kwani unatoka wapi?”

“Ninatoka katika nyumba ya msichana mmoja ambaye nilimuazima kitabu changu, wakati ule natoka  nikaona nimetokea kwenye pango. Baadaye tena naona nimetokea kwenye nyumba hii”

“Wakati unatoka ulimuaga mwenyeji wako?”

“Sikumuaga”

“Kwanini hukumuaga?”

Hapo nikanyamaza kimya, sikuwa na jibu. Nilishindwa kumueleza niliyoyaona kwa sababu yule mzee naye sikujua alikuwa ni nani.

Pakapita kimya cha sekunde kadhaa. Yule mzee alikuwa akinitazama akisubiri jibu langu na mimi nilikuwa nikimtazama uso wangu ukiwa umenywea ukionesha sikuwa na jibu.

“Ulifanya kosa kutomuaga mwenyeji wako na ndio sababu unahangaika. Siku nyingine usirudie kosa kama hilo” Yule mzee akaniambia.

Akanyamaza kimya kisha akanimabia.

JAMAA HAJIELEWI YUKO WAPI. JE HUYO MZEE NI NANI NA ATAMWAMBIA NINI JAMAA HUYO? WEWE UNAFIKIRI KITU GANI KITAMTOKEA JAMAA HUYO?

HUWEZI KUJUA MPAKA UTEMBELEE TENA BLOG HII HAPO KESHO.

No comments:

Post a Comment