Tuesday, May 31, 2016

HADITHI , MWANAMKE SEHEMU YA 7

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 7

ILIPOISHIA

Nikanyanyuka na kuingia chumbani kwangu. Baada ya nusu saa nikatoka nikiwa nimeshavaa.

“Twende” nikamwambia Alphonce.

Tukatoka. Alphonce alinipakia kwenye pikipiki yake tukaelekea Mikanjuni. Nilimuelekeza mahali ilikokuwa ile nyumba ya yule msichana, tukaenda hadi mahali hapo lakini jambo la ajabu lililotokea ni kuwa ile nyumba hatukuiona. Badala yake tuliona eneo lote lilikuwa makaburi matupu ya watu wa zamani.

Nikapatwa na mshangao. Wakati naangalia angalia nikaiona pikipiki yangu ikiwa kando ya mti. Mti huo ndio ule uliokuwa uani mwa nyumba ya Zena. Kando yake palikuwa na kisima ambacho yule msichana na mwenzake walikuwa wakioga.

Wakati ule kile kisima hakukuwepo tena, badala yake tuliona dimbwinl maji ya mvua.

“Pikipiki yangu ile pale!” nikamwambia Alphonce ambaye naye alikuwa ameshangaa.

“Sasa mbona iko kwenye makaburi na hapana nyumba?” akaniuliza.

“Na mimi ndio nashangaa. Ile pikipiki niliiweka uani mwa hiyo nyumba niliyokwambia. Ule mti unaouona ulikuwa uani na lile dimbwi la maji kilikuwa ni kisima”

“Hebu twende pale karibu”

SASA ENDELEA

Tukaenda hadi pale ilipokuwa pikipiki yangu. Karibu yake palikuwa na kaburi la zamani. Lilikuwa limejengewa kiukuta kilichoandikwa jina la Zena binti Ashraf.

Tarehe aliyokufa pia iliandikwa pamoja na tarehe aliyozikwa. Alikufa tarehe kumi mwezi wa kwanza mwaka 1920.

“Yule msichana aliniambia anaitwa Zena na hili kaburi lina jina la Zena, sasa hata sielewi” nikasema.

Nikamsikia Alphonce akitoa mguno. Hakusema chochote. Nikaiangalia pikipiki yangu.

“Ichukue tuondoke, huku Tanga kuna mambo ya ajabu sana”

Nikatia ufunguo na kuikokota hadi kwenye barabara ya vumbi. Nilipoiwasha ikawaka.

“Twenzetu” Alphonce akaniambia huku akipanda pikipiki yake.

Nikapanda pikipiki yangu, tukaondoka.Tukiwa njiani tunarudi tulikuwa tunazungumza.

“Jana ulikunywa pombe?” Alphonce akaniuliza.

“Mimi situmii ulevi wa aina yoyote”

“Sasa ilikuwaje, wewe umeniambia uliingia katika nyumba lakini pale ni makaburini?”

“Yaani pamebadilika. Ilikuwa ni nyumba. Yale makaburi hayakuwepo, ndio nayaona sasa”

“Ni miujiza mikubwa lakini shukuru Mungu umenusurika na pikipiki yako umeipata”

“Aisee nashukuru sana. Na yule mwanamke nikimuona nitamkimbia mbali sana. Sitataka anikaribie, anaweza kutoa roho yangu”

“Mimi sasa naamini kweli majini wapo na wanajigeuza binaadamu”

Tulipofika Mabawa mimi nilielekea nyumbani kwangu, Alphonce akaenda kwenye shughuli zake.

Siku ile nilishinda nikiwa na mawazo ya yule msichana. Kwa kweli alikuwa amenitia hofu sana. Sikutaka nikutane naye tena. Ili kujiondoa wasi wasi niliwaeleza mkasa ule watu mbali mbali niliokuwa nawafahamu akiwemo kaka yangu. Wote walinipa matumaini wakaniambia hakutakuwa na madhara yoyote yatakayonitokea.

Baada ya wiki mbili nilikuwa narudi nyumbani kwangu kutoka kazini. Nilikuwa naendesha pikipiki yangu taratibu. Tukio lile la wiki mbili zilizopita nilikuwa nimeshaanza kulisahau.

Wakati nikiwa katika barabara ya Pangani nikikaribia kwenye mzunguko wa barabara nne uliokuwa eneo la mabanda ya papa nikamuona msichana amesimama kando ya barabara akinipungia mkono. Nilipomtupia macho mara moja nikatambua alikuwa ni Zena! Moyo ulinishituka sana.

Hapo hapo nikaongeza mwendo. Nilitakiwa nisimame kwenye mzunguko huo wa barabara nne uliokuwa mbele yangu. Lakini sikusimama. Gari lililokuwa linakuja kutoka upande wangu wa kushoto ambalo nilitakiwa nilipishe lilinikwepa na kwenda kugonga nguzo ya umeme na kisha kuingia kwenye mfereji wa maji ya mvua.

“Nguzo hiyo iling’oka, waya za umeme zikatikisika na kutoa cheche za moto. Mimi nikaendelea kwenda mbio na kushika barabara ya Pangani kabla ya kuingia katika eneo nililokuwa ninaishi.

Nilipofika nyumbani niliingiza pikipiki yangu ndani nikakaa sebuleni na kuanza kuwaza. Nilijua kuwa nilikuwa nimesababisha ajali kutokana na kuvunja sheria za barabarani baada ya kumuona yule msichana.

Kwa vile nilikuwa na hakika kwamba namba za usajili za pikipiki yangu zilionekana, nilijiambia sitaitimia tena pikipiki yangu hadi lile tukio litakaposahalika.

Zikapita tena wiki mbili. Nilikuwa siitumii tena ile pikipiki yangu kwa kuogopa kukamatwa na polisi. Siku hiyo nilikuwa niko kazini nikawaona polisi wawili wa usalama barabarani wakiingia. Mfanyakazi wa kwanza waliyekutana naye niikuwa mimi.

Wakanisalimia na kuniambia walikuwa wanamtaka Amour.

Amour nilikuwa ni mimi.

Nikasita kuwajibu. Badala yake nikawauliza.

“Amour nani?”

“Hatujui anaitwa Amour nani, kwani hapa kuna Amour wangapi?”

“Kuna Amour mmoja tu”

“Yuko wapi?”

“Ni mimi”

“Sasa mbona hutuambii, unatuuliza maswali. Pikipiki  yako iko wapi?”

“Mmejuaje kama nina pikipiki”

“Tumeelekezwa. Tafadhali tuambie”

“Iko nyumbani”

“Ina namba hizi?”

Polisi huyo alinionesha kikaratasi kilichokuwa kimeandikwa namba za usajili za pikipiki yangu.



“Ndiyo” nikamkubalia polisi huyo baada ya kukiangalia kile kikaratasi.

“Tunakuhitaji wewe na hiyo pikipiki yako”

“Mimi nina nini na pikipiki yangu ina nini?” nikawauliza.

“Uliwahi kufanya makosa ya barabarani wiki mbili zilizopita”

“Sijawahi kufanya kosa lolote labda mmeifananisha pikipiki yangu”

“Tutajua huko kituo cha polisi. Kwa sasa tutaondoka na wewe twende nyumbani kwako tuichukue hiyo pikipiki, twende nayo kituo cha polisi”

Sikuwa na la kupinga. Nikakakamatwa. Polisi hao ambao walikuja na gari lao walinipakia kwenye gari hilo, nikaenda nao nyumbani kwangu.

Niliwatolea pikipiki yangu, walipoiona tu wakasema ndiyo waliyokuwa wanaitafuta kwa karibi wiki mbili.

Nikafikishwa kituo cha polisi. Huko ndiko nilikoelezwa kuwa tarehe fulani siku fulani nilisababisha ajali eneo la Mabanda ya Papa baada ya kuendesha pikipiki kwa uzembe na kuvunja sheria za barabarani.

Nikaelezwa kuwa kutokana na uzembe wangu wa kutosimama mahali ambapo nilipaswa kusimama ili nipishe gari lililokuwa linatoka kuliani kwangu, nilisababisha gari hilo aina ya Toyota Landa Cruiser linikwepe na kugonga nguzo ya umeme na kutumbukia kwenye mfereji.

Ingawa nilijitahidi kukana kosa hilo nilifikishwa mahakamani baada ya kulala ndani kwa siku moja. Katika mahakama ya Chumbageni nikashitakiwa kwa makosa matatu.

Kosa la kwanza lilikuwa kuendesha kwa uzembe, kosa la pili kusababisha ajali na kosa la tatu kuharibu mali na kulitia hasara shirika la Umeme iliyokadiriwa kufikia shilingi milioni kumi na mbili.

Niliyakana mashitaka yote na kumuomba hakimu anipe dhamana. Ndugu zangu walikuwa wamejitokeza kutaka kuniwekea dhamana.

HAYA JAMANI MNAYAONA MAMBO HAYO! NI MAKUBWA. SIJUI KAMA JAMAA ATAPEWA DHAMANA.

MH! HEBU TUNGOJE HAPO KESHO TUONE NINI KITATOKEA. NI KATIKA BLOG YAKO HII HII YA TANGA KUMEKUCHA. KUMEKUCHA KWELI!


No comments:

Post a Comment