Thursday, May 26, 2016

HADITHI MWANAMKE SEHEMU YA 3

HADITHI

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 3

ILIPOISHIA

Nikaangaza macho yangu kumtazama. Nikamkumbuka. Alikuwa ni yule msichana niliyekutana naye sinema siku ile.

“Oh nzuri! Hujambo?” nilijibu salamu yake.

“Sijambo. Leo tumekutana tena”

“Imekuwa kama bahati. Nilikuwa natoka kununua kitabu”

“Mimi pia nimekuja kununua kitabu. Nilikuwa nahitaji kitabu cha “Mashimo Saba ya Malme Suleiman”

“Vimeisha. Kilikuwa kimebaki kimoja tu nilichonunua mimi” nikamwambia.

“Kumbe wewe pia ulikuja kununua kitabu hicho hicho?”

“Nilikuja kununua kitabu hicho”

Nikakitoa kile kitabu na kumuonesha.

Akakishika na kukitazama.

“Una umuhimu nacho sana kwa leo na kesho?” akaniuliza.

“Ni kwa ajili ya kujisomea tu”

“Basi naomba uniazime kwa siku mbili tu halafu nitakurudishia”

Sikuwa na sababu yoyote ya kukataa. Nilihisi yule msichana alikuwa akikihitaji zaidi.

“Nitakuazima, sasa sijui nitakipata vipi?”

SASA ENDELEA

“Keshokutwa nitakuwa majestic Cinema, utakuja?” akaniuliza.

“Ninaweza kuja kwa ajili yako tu”

“Basi njoo usiku saa mbili na nusu hivi utanikuta nakusubiri pale nje”

“Kutakuwa na picha gani?”

“Picha nzuri ya James Bond”

“Inaitwaje?”

“Dk No”

“Inarudia. Nakumbuka  Dk No ndio picha ya kwanza ya James Bond, ilitoka kwa mara ya kwanza mwaka 1961”

“Sijui. Mimi sikuwahi kuiona lakini ni ya Seen Conary mwenyewe?”

“Mimi pia sikuwahi kuiona ila niliisikia tu. Mbabe wake ni Seen Conary mwenyewe”

“Nimekuuliza hivyo kwa sababu kuna mtu mwingine anakuja kwenye picha za James Bond anaitwa Roger Moor”

“Ile ni ya Seen Conary si Roger Moor”

“Huyo ndiye ninayemtaka mimi”

“Basi mimi nitafika hapo Majestic Cinema keshokutwa”

“Asante kaka, ngoja niingie humu dukani nione kama nitapata vitabu vingine vya hadithi”


‘Sawa”

Msichana akaingia mle dukani na mimi nikapanda pikipiki yangu na kuondoka.

SASA ENDELEA

Yule msichana alikuwa ameniambia nikutane naye kesho kutwa saa mbili usiku nje ya Majestic Cinema. Ilipofika siku hiyo niliondoka nyumbani kwangu saa mbili usiku kuelekea Majestic Cinema kufuatia kitabu changu. Nilipofika ilikuwa saa mbili na nusu kama tulivyoahidiana na msichana huyo ambaye sikuwahi hata kumuuliza jina lake.

Nikamkuta amesimama mbele ya mlango wa jumba hilo akiwa na mavazi yake yale yale, baibui jeusi la kiiran na hijabu.

“Niko hapa nakusubiri” akaniambia.

“Nimeshakuona”

“Vipi hali yako?”

“Mimi sijambo, sijui wewe”

“Mimi mzima tu, karibu”

“Asante”

Msichana alikuwa ameshika tikiti mbili mkononi. Akanipa tikiti moja.

“Nimekukatia tikiti uingie”

“Mbona mimi sikupanga kuangalia sinema” nikamwambia huku nikipokea ile tikiti.

“Hukupanga? Si nilikwambia juzi…”

“Wewe ndio ulisema utakuja sinema, mimi nilikuwa nije kuchukua kile kitabu tu”

“Kwa vile nimeshakukatia, ingia tu tuangalie pamoja”

Wakati akiniambia hivyo watu walikuwa wanatoka ndani ya jumba hilo. Onesho la jioni lilikuwa limekwisha.

Tulisimama kwa pembeni kuwapisha watu hao, walipomalizika na sisi tukaingia. Tulitafuta siti zetu, tulipozipata tukaketi. Saa tatu kamili trela ikaanza. Baada ya trela kwisha msichana alitoka. Baadaye alirudi akiwa na chupa mbili za soda na pakiti mbili za njugu.

“Chukua’

Akanipa chupa moja ya soda na pakiti moja ya njugu.

“Asante”

Onesho la sinema likaanza. Tukaitazama filamu ya Dk No mwanzo hadi mwisho. Mara kwa mara msichana huyo alikuwa akimshangilia James Bond kutokana na ujanja wake wa kipelelezi. Filamu ilipomalizika tukatoka.

“Si utanipeleka nyumbani?” msichana akaniuliza tulipokuwa nje ya jumba hilo.

“Kitabu kiko wapi?” nikamuuliza.

“Nilikisahau nyumbani, nitakwenda kukupa huko huko”

Nikaguna kimoyomoyo kwa vile ahadi yetu haikuwa hivyo. Nikaitoa pikipiki yangu na kuiwasha.

“Panda twende” nikamwambia.

Msichana ambaye alionesha alikuwa mzoevu wa kupanda pikipiki alikaa nyuma yangu akauzungusha mkono wake kwenye tumbo langu. Nikatia gea na kuiondoa pikipiki.

“Unaitwa nani?” Msichana huyo akaniuliza.

“Naitwa Amour na wewe unaitwa nani?”

“Naitwa Zena, unaishi wapi?”

“Ninaishi Mabawa”

“Unafanya kazi wapi?”

“Nafanya kazi shirika la STC”

“Nimefurahi sana kukufahamu Amour”

“Na mimi pia nimefurahi kukufahamu”

Tukaendelea kuzungumza hili na lile mpaka tukafika Mikanjuni. Safari hii alinifikisha hadi katika nyumba aliyokuwa anaishi. Lilikuwa jumba zuri la kifahari. Ingawa eneo hilo lilikuwa giza, jumba hilo lilikuwa linawaka taa ya umeme.

“Mimi naishi hapa” Msichana akaniambia huku akishuka kwenye pikipiki.

Nilikuwa nikilitupia macho lile jumba, nikataka kumuuliza alikuwa amepangisha chumba au alikuwa akiishi kwao. lakini nilishindwa kumuuliza ili asione ninayachunguza maisha yake.

“Nimepaona” nikamjibu.

“Karibu ndani” akaniambia.

“Asante”

“Karibu” Msichana akanisisitizia.

“Hapa panatosha” nikamwambia nikiwa nimekaa kwenye pikipiki yangu.

“Unataka uishie nje, si vizuri. Tuingie ndani. Ninaishi peke yangu tu usiogope”

“Unaishi peke yako humu ndani?” nikamuuliza.

“Nimejenga mwenyewe kutokana na biashara zangu na ninaishi mwenyewe. Msichana aliniambia huku akifungua geti.

“Karibu”

Kwa jinsi alivyokuwa akinibembeleza ilibidi nishuke kwenye pikipiki. Niliposhuka tu msihana aliishika pikipiki yangu akaikokokota na kuiingiza ndani, nikawa namfuata nyuma.

Tulipoingia ndani msichana aliiegesha pikipiki kando ya mti mkubwa uliokuwa umeota katika ua wa jumba hilo. Aliiacha pikipiki akaenda kufunga geti.

“Karibu” akaniambia huku akitangulia kwenda kwenye mlango wa kuingilia kwenye jumba hilo. Nikamfuata.

JAMAA AMESHAINGIA NDANI YA NYUMBA YA MWANAMKE HUYO AMBAYE HAMJUI. Je Nini kitatokea?

No comments:

Post a Comment