Sunday, May 29, 2016

WAJASIRIAMALI TANGA WAFUNDWA



Tangakumekuchablog
Tanga, WAJASIRIAMALI Wanawake Tanga wametakiwa kutafuta masoko kwa njia ya mitandao na kulitumia soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuweza kukuza biasharazao na kuwa wafanyabiashara wakubwa wa Kimataifa.
Akizungumza katika kongamano la ufunguzi wa Tanga Woman Gala, Tawi la Tanga leo, Mratibu wa Gala, Lucy Mwinuka, alisema wajasiriamali wengi biashara zao zinashindwa kupata masoko baada ya kutegemea soko la mmoja mmoja.
Alisema mfumo wa biashara mtandaoni inaweza kumuinua mjasiriamali na kuwa mfanyabiashara m,kubwa wa Kimataifa hivyo kuwataka kubadilika katika karne hii ya Utandawazi.
“Ni ukweli ulio wazi kwa muitikio huu wa leo Tanga iko na mwamko wa wajasiriamali ambao wanataka kujikomboa na kuonyesha kuwa wanaweza, ila niwambie kuwa tufanye biashara  kidigitali” alisema Mwinuka na kuongeza
“Tunaweza kuwa wajasiriamali wa kimataifa kama tutaitumia mitandao kutafuta masoko na kuzitangaza ndani na nje ya nchi hivyo niwatake kuanzia sasa tubadilike” alisema
Aliwataka Wajasiriamali hao pia kulitumia soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujitangaza kama ambavyo wenzao wa Jumuiya hiyo wanavyotafuta masoko na kuwambia kuwa waache woga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Kiraia ya Tree of  Hop, Fourtunata Manyeresa, amewataka wanawake kujishughulisha na kazi za mikono na kuacha majumbani na kuwategemea wanaume pekee.
Alisema wanawake wako na fursa nyingi za kujikomboa na kuwa wajasiriamali wakutegemewa hivyo ni wajibu wao wa kujiunga na vikundi na kuweza kupata mikopo.
Alisema kazi za mikono zinaweza kumkomboa mwanamke kutoka katika dimbwi la umasikini na kusema kuwa wengi hawako na utayari na badala yake wamekuwa wategemezi ambao hawawezi kuwakidhi shida zao kikamilifu.
“Mimi pia ni mjasiriamali na mwenza wangu akiwa hayupo naendesha maisha nyumbani na watoto wanaenda shule bila shida yoyote, nanyi nawaomba tujifunge vibwebwe kwa pamoja na kupeana mbinu za kujikomboa” alisema Manyeresa
Alisema ili wanawake wajikomboe kutoka katika umasikini ni lazima kuwa tayari kujishughulisha na kazi ambazo wataweza kujipatia kipato cha halali na kutafuta masoko .
                                                Mwisho

No comments:

Post a Comment