SIMULIZI na Faki A Faki, 0655 340572
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 4
ILIPOISHIA
“Ninaongea na wewe nikiwa
chumbani”
“Sawa. Kama
utahitaji chakula au kinywaji chochote agiza tu, nimeweka oda kwa ajili yako”
“Sawa”
“Nitakuja kuonana na wewe
baada ya dakika chache”
“Nakusubiri”
Baada ya hapo kukawa kimya.
Nikaurudisha mkono wa simu kisha nikatoka humo chumbani. Nilifunga mlango kwa
funguo nikashuka chini.
Unaposhuka chini unatokea
pale mapokezi, nikaenda kukaa kwenye meza moja katika ule ukumbi. Yule msichana
niliyemuona ameketi nilipoingia alikuwa bado ameketi akisoma gazeti.
Nilikuwa nimevutiwa na umbile
lake la kupendeza na sura yake jamali.
Lakini laiti kama ningetambua tukio ambalo lingetokea hapo hoteli
ningeahirisha mapema safari yangu!
SASA ENDELEA
Baada ya kuketi mhudumu
alikuja kuniuliza kama nilikuwa nahitaji kitu,
akanipa menyu.
Kwenye menyu niliona ugali
kwa samaki. Nikatamani kula ugali wa Kizimbabwe. Nikamuagiza mhudumu huyo aniletee
ugali kwa samaki.
Wakati nasubiri nilitewe
ugali nilioagiza, nilimuona mtu mmoja aliyekuwa amevaa suti nyeusi akiingia
hapo hoteli. Alipomuona yule msichana aliyekuwa amekaa karibu na mlango alisita
kisha akavuta kiti na kuketi naye. Nikaona wanazunguma ingawa sikuweza kusikia
walikuwa wanazungumza nini.
Mhudumu alimfuata yule mtu,
nikaona anaagiza kitu. Baadaye kidogo waliletewa chupa mbili za bia na kuanza
kunywa. Mimi nilikuwa nimeshaletewa chakula nilichoagiza.
Nilikuwa nikila ugali huku
jicho langu likiwa kwa wale watu. Kama
sijakosea walikunywa bia mbili mbili. Mimi nilikuwa nimeshamaliza ugali wangu wakati
yule mtu alipoinuka na kwenda mapokezi. Alizungumza na mhudumu wa mapokeziki kabla
ya kupewa funguo.
Baada ya kupewa funguo
alirudi kwa yule msichana akazunguma naye akiwa amesimama. Baada ya muda kidogo
msichana aliinuka wakaenda kupanda ngazi.
Nilihisi kama vile yule mtu
alikuwa amechukua chumba na alikuwa akielekea chumbani na yule msichana. Huenda
walikuwa wakijuana na kwamba yule msichana alikuwa akimsubiri yule jamaa pale.
Niliendelea kuketi pale pale
nikiangalia televisheni iliyokuwa imepachikwa katika ukuta. Nilipoona muda
unazidi kwenda niliondoka nikarudi chumbani kwangu na kumpigia simu mwenyeji
wangu.
Nilitaka kumuuliza mbona
hatokei kwani muda mrefu ulikuwa umepita tangu aliponiahidi kuwa anakuja. Simu
ikaita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Simu ilipokata nikapiga tena
lakini pia haikupokelewa. Nikaamua kusubiri kabla ya kupiga tena.
Kwa vile sikuwa na kingine
cha kufanya, niliona nijilaze pale kitandani. Bila kujitambua usingizi
ukanipitia hapo hapo.
Nilipozinduka ilikuwa usiku.
Niliwasha taa kisha nikatazama saa. Ilikuwa saa mbili na robo usiku. Nikapiga
tena simu lakini bado simu ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.
Nikawa nimechukia. Nilihisi
huyo mtu aliyefanya niende Zimbabwe
hakuwa na ahadi za kweli. Nikaenda kuoga. Niliporudi nilipiga simu tena.
Nilipiga mara tatu bila kupokelewa. Simu ilikuwa inaita tu.
Nikashuka chini na kula
chakula kisha nikarudi tena juu. Nikapiga tena simu lakini haikupokelewa. Ilikuwa
kama vile simu ilikuwa peke yake au mwenye simu aliamua kunisusia.
Kusema kweli
nilichanganyikiwa. Nilikuwa sijui la kufanya. Nikalala. Asubuhi nilipoamka kitu
cha kwanza kilikuwa kupiga simu. Simu ya Chusama bado ilikuwa ikiendelea kuita
tu. Sasa nikaanza kupatwa na wasiwasi.
Nikashuka chini na kupata
kifungua kinywa. Wakati naendelea kunywa chai. Nilisikia nung’unung’u hapo
hoteli kuwa kuna mtu aliyeuawa akiwa ndani ya chumba cha hoteli.
Tukio hilo liligunduliwa na mhudumu wa usafi ambaye
aliingia katika chumba hicho na kukuta maiti ya mwanaume iliyokuwa imelazwa
chini.
Baadaye polisi walifika hapo
hoteli. Waliongozwa na baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo kuelekea katika
chumba hicho kilichokuwa ghorofa ya kwanza. Na mimi kwa kutaka kupata ukweli
niliinuka nilipokuwa nimeketi nikaelekea huko huko.
Kilikuwa chumba kilichopakana
na chumba nilicholala mimi. Mlango ulikuwa umeachwa wazi na polisi pamoja na
baadhi ya wafanyakazi walikuwa wameingia ndani.
Sikuweza kumuona vizuri mtu huyo mpaka mwili wake ulipokuwa
unatolewa ukiwa kwenye machela. Nilipomuona tu nikamtambua. Alikuwa ni yule mtu
ambaye alifika jana yake pale hoteli na kuzungumza na yule msichana na kisha
wakaondoka pamoja kuelekea chumbani.
Hata hivyo yule msichana
aliyekuwa naye hakuwepo. Ilisemekana kwamba alitoroka kabla ya tukio hilo kugundulika.
Mpaka mwili wa mtu huyo
unatolewa, polisi hawakuwa wamegundua mtu huyo alikuwa ameuawa kwa kitu gani.
Kwenye pua yake na kwenye pembe moja ya midomo yake kulikuwa na michirizi ya
damu iliyoganda.
Kulikuwa na baadhi ya
wafanyakazi ambao walichukuliwa na polisi kwenda kutoa maelezo.
Nikajiuliza kama yule
mwanamke alikuwa muuaji kweli. Hakuonekana kuwa katili. Niseme ukweli kama ndiye aliyemuua yule mtu, tukio lile lingenikuta
mimi kwani jana yake ilibaki kidogo niende nikakae naye.
Nikashukuru kwamba Mungu
alikuwa ameninusuru.
Ingawa tukio hilo lilichnaganya akili
yangu lakini kitendo cha mwenyeji wangu kutopokea simu kilinichanganya zaidi.
Niliingia chumbani na kutafakari nifanye nini. Kwa kweli sikupata jibu.
ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu nini kitatokea ni hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment