ZULIA LA FAKI,0655 340572
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 9
ILIPOISHIA
Ndege ilipaa hewani kwa
takribani saa sita kabla ya kutua katika kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam.
Ndege ilipotua, abiria
walianza kushuka. Nilikuwa miongoni mwa abiria wa mwisho mwisho. Nilikuwa
nimechoka na nilionesha wazi kukata tamaa.
Wakati namalizia kushuka
ngazi ya ndege, macho yangu yalimuona mtu aliyenishitua akiwa mbele yangu.
Alikuwa ni yule msichana
muuaji! Alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa wamepanda ile ndege wakitokea
Afrika Kusini. Alikuwa amefuatana na mwanamme mmoja aliyekuwa amevaa suti
nyeusi wakizungumza.
Kusema kweli sikutambua kama yule
msichana alikuwemo ndani ya ndege ile.
Nilimgundua wakati ule wa kushuka. Yule mtu aliyekuwa amefuatana naye sikuweza kumtambua.
Tulipotoka nje ya jengo la
kiwanja cha ndege, msichana huyo pamoja na yule mtu aliyekuwa amefuatana naye walikodi
teksi na kuondoka. Na mimi nikakodi teksi na kumwambia dereva awafuate.
SASA ENDELEA
“Una maana niifuate hii teksi
ya mbele yangu?” Dereva wa teksi akaniuliza.
“Ndiyo ifuate hiyo hiyo”
“Inaelekea wapi?”
“Popote itakapoelekea”
“Ina maana wewe hujui
inaeleka wapi?”
“Kwani tatizo lako ni nini,
hapo tutakapofika utanitoza kiasi utakachotaka”
“Sawa. Nilitaka tupatane tu”
“Hatuwezi kupatana kwa sababu
sijui wanakwenda wapi”
“ Nimekuelewa”
Dereva wa teksi akaanza
kuiandama teksi iliyokuwa mbele yetu. Wakati mwingine gari lilitinga katikati
yetu lakini dereva alijitahidi kuhakikisha teksi hiyo haitupotei.
Wakati tunaendelea kuiandama teksi
hiyo, mawazo yangu yalikuwa kwa yule msichana. Bado nilikuwa nikijiuliza
msichana yule ni nani na kwanini nakutana naye katika kila nchi ninayokwenda.
Pia nilijiuliza yule mtu aliyenaye ni nani na anatoka wapi.
Nilihisi kwamba kwa vile msichana
huyo alikuwa katika jiji ambalo nilikuwa nikilijua vyema, ningeweza kufanya
uchunguzi na kumgundua.
Hata hivyo jambo moja
nilikuwa na uhakika nalo moyoni mwangu kwamba msichana huyo alikuwa wa hatari
na muuaji aliyeonekana kuwa na uzoevu wa kuua.
Mara moja niligundua kuwa
teksi iliyowapakia ilikuwa ikielekea Mbezi. Tuliendelea kuifuata hadi
iliposimama mbele ya jumba moja la kifahari. Dreva wa teksi niliyopanda alitaka
kusimama nikamwambia apitilize moja kwa moja.
“Sitaki wagundue kuwa
ninawafuata” nikamwambia dereva huyo na kuongeza.
“Utasimama kule mbele”
“Nimekuelewa”
Wakati teksi ikiendelea
kwenda, mimi nilikuwa nikitazama nyuma kwenye kioo. Nilimuona yule msichana
akishuka kwenye ile teksi pamoja na yule mwanaume aliyekuwa naye. Teksi
iliondoka na wao wakafungua geti na kuingia ndani.
Kwa vile nilikuwa
nimeshaikariri ile nyumba, nilimwambia dereva wa teksi ageuze anipeleke
nyumbani kwangu.
“Umeshawaona?” akaniulia
wakati akiigeuza teksi.
“Nimewaona. Nilitaka kujua
wanaishi wapi?”
“Kwani ni kina nani wale?”
“Nilisafiri nao kutoka Afrika
Kusini. Nilitaka kujua wanaishi wapi hapa dar”
Dereva alitaka kuendelea
kuniuliza lakini alibadili mawazo
akanyamaza kimya.
Baada ya nusu saa tu
alinifikisha katika mtaa ninaoishi. Aliisimamisha teksi mbele ya nyumba yangu
nikamuuliza gharama yake ni kiasi gani.
Alinitajia kiasi alichotaka
nikatoa pochi yangu na kumpa kiasi hicho bila kusita.
“Asante sana” nilimwambia
huku nikifungua mlango wa teksi na kushuka.
Huku nikiwa na begi langu
nilikwenda kufungua mlango wa nyumba yangu nikaingia ndani. Niliondoka kwenda
nje ya nchi kwa matumaini ya utajiri lakini nimerudi kama masikini. Safari
yangu haikuwa na mafanikio yoyote, nilijiambia kwa huzuni.
Mbali ya kutokuwa na mafanikio, ilikuwa safari ya balaa na
iliyonitia hofu kutokana na wale watu niliowafuata kuuawa mmoja baada ya
mwingine, tena wameuawa na msichana huyo huyo ambaye aliwafuata Botswana,
Zimbabwe na Afrika Kusini.
Msichana yule sasa amekuwa ni
kitendawili ambacho nilihitaji kukitegeua kadiri itakavyowezekana. Kwa vile
nilikuwa nimeikariri sura yake pamoja na nyumba aliyoingia, niliamini kwamba
ningewea kumfuatilia na kumjua vizuri.
Siku ile ikapita. Asubuhi ya
siku iliyofuata wakati nimeketi sebuleni nikitazama televisheni, niliona kitu
kilichonishitua.
Kilikuwa ni kipinidi cha
taarifa ya habari. Habari ya kwanza kutangazwa na kuoneshwa ilikuwa ya mauaji
ya mkazi mmoja wa Mbezi aliyetajwa kwa jina la Abdul Baraka.
Hilo jina lilinishitua kwa
sababu lilikuwa katika orodha ya wale wadaiwa wa marehemu babu yangu. Jina hilo
lilikuwa la kwanza na mtu huyo ndiye niliyeanza kumpigia simu lakini simu yake
haikupatikana nikaamua nimuache kiporo.
Yeye hasa ndiye aliyekuwa
tegemeo langu baada ya wale watu niliowafuata nje ya nchi kuuawa na kusababisha
nisipate kitu.
Taarifa hiyo ya televisheni
ilieleza kwamba mwili wa Abdul Baraka ulikutwa mchana wa jana yake nyumbani
kwake ukiwa umelazwa sebuleni.
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment