ZULIA LA FAKI, 0655 340572
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 7
ILIPOISHIA
Walipoona uso wangu ulikuwa
umeota alama ya kuuliza waliniambia.
“Tulitaka kukuchangamsha tu mgeni wetu. Tunaona umekuwa
kimya chumbani, huna mwenzako”
Hapo ndipo nilipoelewa kuwa
wale walikuwa changu doa waliokuwa wakijiuza kwenye mahoteli.
Mawazo yangu yalikuwa tofauti
na wao kwa upande mmoja na yalikuwa yanalingana na wao kwa upande mwingine.
Yalikuwa tofauti na wao kwa
upande mmoja kwa sababu kilichonipeleka Botswana hakikuwa kufuata machangudoa
na yalilingana na wao kwa upande mwingine kwa sababu wao walikuwa wakitafuta
pesa kwa njia zao na mimi vile vile nilikuwa natafuta pesa.
Nilipowaza hivyo nilijikuta
nikitabasamu.
“Karibuni” nikawambia huku
nikijiambia mwenyewe kuwa si vibaya kuzungumza nao mawili matatu kupitisha
wakati.
Wasichana hao wakaingia mle
chumbani.
SASA ENDELEA
Wote wawili walikimbilia
kukaa kitandani wakaniwekea nafasi nikae katikati yao. Nikakaa.
“Kwanini unataka kulala peke
yako wakati sisi tupo?” Msichana mmoja aliyeonekana kuwa na macho ya juu aliniuliza.
“Nimekuja peke yangu,
nitalala peke yangu. Mlitaka nilale na nani?” nikamjibu.
“Uchague mmojawapo kati yetu
sisi” Msichana wa pili akaniambia.
Kusema kweli hawakuwa malaya
wa kuweza kunishawishi. Mkorogo ulikuwa umewaharibu. Lakini nilitaka kuzungumza
nao tu nichangamshe akili yangu.
“Je kama nitawachagua nyote
itakuwaje?’ nikawauliza huku nikiwatazama kwa zamu.
“Utatuweza?” Mmojawapo
akaniuliza.
“Nisiwaweze kwani nyie ni
vyuma?”
“Sawa. Utatupa dola ngapi?”
“Tatizo litakuwa hapo kwenye
dola”
\
“Utatupa dola ngapi?”
“Sina hata dola moja”
“Si kweli. Huoneshi kuwa huna
pesa, usingekaa katika hoteli hii”
“Kwani unatokea wapi?” Msichana
mwingine akaniuliza.
“Natokea Zimbabwe”
“Wewe ni Mzimbabwe?”
“Hapana. Mimi ni Mbongo”
Wasichana hao wakaonesha
kushituka.
“Mbongo ni mtu wa nchi gani?”
“Mtanzania”
“Kumbe unatoka Tananzia?”
“Unakufahamu?”
“Sijafika lakini
tumefundishwa shuleni kwamba Tanzani ilikuwa moja ya nchi zilizokuwa mstari wa
mbele kupigania uhuru wa Afrika ikiwemo nchi yetu chini ya uongozi wa Mwalimu
Nyerere”
“Sasa kama mnajua hivyo
kwanini mnanitoza dola?”
“Ulitaka bure?”
“Ikiwezekana”
Wasichana hao walicheka kisha
wakainuka na kusimama. Bila shaka waligundua kuwa nilikuwa nikiwapotezea wakati
wao bure.
“Mbona mnakwenda zenu?”
nikawauliza.
“Sisi tuko kazini bwana.
Hamna bure hapa. Wewe hutaki kutoa pesa yako. Kwaheri” Msichana mmoja
akanniambia.
Walitoka na kuniacha. Na mimi
niliinuka nikafunga mlango wangu kisha nikarudi kitandani.
Siku ile ikapita nikiwa hapo
hoteli.
Asubuhi ya siku iliyofuata
nikiwa kwenye mkahawa wa hoteli hiyo nikipata kifungua kinywa, nilimuona dereva
wa mwenyeji wangu Muhoza akinifuata. Uso wake ulikuwa umetaharuki.
Akanisalimia kisha
akaniambia.
“Bwana Muhoza ameuawa!”
Mshituko ulinifanya niinuke
kwenye kiti na kusimama.
“Bwana muhoza ameeuawa?”
nikamuuliza kwa mshangao.
“Jana alipoondoka hapa
alikwenda katika hoteli nyingine ambako alilala na yule msichana aliyekuwa
naye. Aliniambia nimfuate asubuhi. Asubuhi nilipomfuata nikakuta taarifa hiyo.
Maiti yake ilikutwa chumbani hii asubuhi”
Nikajiambia, ni yale yale
yaliyotokea Botswana.
“Kwani yule msichana aliyekuwa
naye ni nani?” nikamuuliza yule dereva.
Dereva huyo akabetua mabega
yake.
“Simfahamu na sijui
walikutana wapi”
“Yule ndiye aliyehusika na
mauaji hayo!”
“Inaaminika hivyo kwa sababu
amekimbia”
“Hebu kaa nikueleze kitu”
nikamwambia Yule mtu huku na mimi nikikaa.
“Unajua mimi natokea Botswana.
Yule msichana nilimkuta katika hoteli niliyofikia pale Botswana. Baadaye
nilimuona akiwa na mwenyeji wangu na wakachukua chumba pale pale hoteli. Asubuhi
yake mwenyeji wangu akakutwa ameuawa katika chumba cha hoteli na yule msichana
hakuonekana. Sasa nilipofika hapa Zimbabwe nilishangaa kumuona tena akiwa na
Muhoza” nikamueleza yule mtu.
“Kwanini hukutuambia tangu
jana?”
“Nilishindwa kuwambia,
nilijua labda wanajuana”
“Sasa yule msichana atakuwa
ni nani na anatokea wapi?”
Nikaguna na kushusha pumzi
ndefu.
“Hicho ni kitendawili na
sidhani kama atapatikana”
“Anaweza kupatikana”
“Nilikuwa namdai Muhoza pesa
nyingi na tulikubaliana kwamba angenilipa hii asubuhi. Sasa sijui nitafanyaje?”
“Huyu jamaa kama ulikuwa na
mipango naye ya pesa ni bora usamehe. Kwanza mimi siwajui ndugu zake na
isitoshe alishatengana na mke wake miaka mingi iliyopita”
Nikatikisa kichwa change
kusikitika.
“Mkosi gani huu jamani…!”
nilijisemea kimoyomoyo.
ITAENDELEA kesho hapa hapa Usikose Uhondo huu nini kitatokea baada ya Mahoza nae kuuwawa na wasichana wale kuondoka, je watarudi na jamaa nini atafanya au kumkuta akiwa hotelini
No comments:
Post a Comment