Sunday, April 30, 2017

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 16

ZULIA LA FAKI
 
NILIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 18
 
ILIPOISHIA
 
“Maana yake mtu amekufa halafu anakuja  kuonekana tena”
 
“Sasa yule si mtu yule yule”
 
“Ni nani sasa?”
 
“Kwanza mtu akifa hawezi kuonekana tena”
 
“Mbona mimi nimemuona Ummy?”
 
“Uliyemuona si Ummy”
 
“Ni yeye. Licha ya  kunielekeza kwao alinipa  namba ya simu yake na nilimuonesha ndugu yake pale nyumbani kwao akasema ni namba  ya Ummy kweli”
 
“Kwani ulifika kwao kumuulizia?’
 
“Ndiyo, nilifika jana”
 
“Wakakuambia nini?”
 
“Wakaniambia hivyo hivyo kwamba Ummy alikufa”
 
“Si ndiyo nilivyokueleza mimi?”
 
SASA ENDELEA
 
Nilihisi kwamba maelezo ya Mzaramu badala ya  kunisaidia yalizidi kunichanganya. Mzaramu hakutaka  kukubaliana na miimi kwamba niliyemuona alikuwa ni Ummy wakati nilikuwa na imani kuwa niliyekutana naye alikuwa  ni Ummy Nasri.
 
Kitu muhimu kilichonifanya niamini kuwa niliyemuona  ni Ummy Nasri  aliyedaiwa kufa ni ile picha ya Ummy niliyooneshwa na baba yake huku mdogo wake akikiri kwamba namba ya simu niliyopigiwa na Ummy ilikuwa namba  ya Ummy kweli. Mdogo wake  huyo alikuwa ameikariri.
 
Sasa kulikuwa na vitu viwili vilivyonitia mawazo. Kwanza ni yale maelezo ya Mzaramu kwamba Ummy kabla ya kufa alikuwa na uhusiano na mzee mmoja  ambaye Mzaramu alinithibitishia kuwa ndiye yule niliyemuonesha katika  picha iliyokuwa kwenye simu yangu.
 
Picha  hiyo  ilikuwa ni ya babu yangu marehemu mzee Limbunga. Hivyo maelezo ya Mzaramu yalionesha kwamba babu yangu alikuwa na uhusiano na Ummy.
 
Kitu cha pili kilichoniitia  mawazo ni maelezo ya Ummy kwamba anazijua siri za  malli ya babu yangu.  Inawezekana kweli anaijua siri ya mali ya babu yangu kwa vile alikuwa na uhusiano naye. Ila kinachotatanisha hapo ni kuwa Ummy mwenyewe anadaiwa kuwa alishakufa.
 
Yakanijia mawazo yale yale kwamba niliouona ulikuwa mzuka wa Ummy, yaani iliwezekana kuwa Ummy alishakufa kweli lakini nilichokutana nacho kilikuwa kivuli chake. Nilishasikia hadithi nyingi za watu waliokufa kuonekana tena ikidaiwa kuwa ni mizuka  ya watu hao.
 
Lakini mara nyingi mizuka hiyo  inapotokea inakuwa na sababu.
 
Sasa nikajiambia labda nijaribu kutafuuta sababu ya kutokea kwa mzuka wa Ummy ambaye aliwaua watu wote waliokuwa wakidaiwa na  babu yangu na kusababisha nisilipwe pesa ambazo ningelipwa na watu hao.
 
Nikajiuliza kama Ummy alikuwa mzuka ni kwanini aliwaua  watu hao  halafu aniambie kuwa anaijua siri ya mali ya babu yangu na kutaka nikutane naye?
 
Kwa kweli kila  nilivyowaza  niliona sivyo na kila nilivyojiuliza sikupata jibu. Hapo ndipo nilipozidi kuchanganyikiwa.
 
“Mbona umeduwaa rafiki yangu?”  Mzaramu akaniuliza akiwa hajui yaliyokuwa  yanapita akilini mwangu.
 
Nikazinduka kutoka katika mawazo yangu na kumwambia.
 
“Nilikuwa nafikiria  hadithi uliyonieleza”
 
“Kahawa imekutosha?” akaniuliza.
 
“Imetosha. Ni kiasi gani?”
 
“Sijakuuzia, nimekupa kiurafiki kwa  vile siku nyingi hatujaonana”
 
“Asante, nakushukuru sana. Naona nikuage, tutaonana siku nyingine”
 
Nilipoondoka kwa Mzaramu nilikusudia nipite pale nyumbani kwa kina Ummy na kama nitakutana na yule mzee nisalimiane naye.
 
Wakati nipo barabarani nikitembea kwa miguu kuelekea upande ule ilikokuwa nyumba ya mzee Nasri, nikakutana na mdogo wake Ummy akitokea dukani.
 
Msichana huyo aliponiona akasimama.
 
“Kaka wewe ndiye uliyekuja nyumbani jana ukatuambia kuwa ulimuona dada?”  akaniuliza.
 
“Ndiye mimi”
 
“Jana ulitutia wasiwasi sana. Ilibidi mama aende kwa mganga kumueleza kuhusu kuonekana kwa Ummy ambaye alishakufa. Mganga akamwambia kwamba huyo aliyeonekana alikuwa Ummy kweli, amechukuliwa msukule”
 
“Amechukuliwa msukule na nani?” nikamuuliza.
 
“Huyo mganga alimwambia amechukuliwa msukule  na mwanamke mmoja ambaye aliwahi kugombana  naye”
 
“Waligombania nini?”
 
“Huyo mwanamke alikuwa akidai kuwa marehemu alikuwa anatembea na mume wake”
 
Nikayakumbuka yale maelezo ya Mzaramu. Nikafikiri kidogo  kisha nikamuuliza.
 
“Kama alichukuliwa msukule mbona yuko vizuri tu, anaongea kwenye simu na nilikutana naye Botswana, Zimbabwe na Afrika Kusini. Mtu aliyechukuliwa msukule anapanda ndege?”
 
“Hayo ni maelezo ya huyo mganga lakini baba alipoelezwa amesema hataki mambo ya kishirikina, anachojua yeye ni kuwa mwanawe amekufa, huyo aliyeonekana siye mwanawe”
 
“Mimi pia hayo madai ya kuchukuliwa msukule sikubaliani nayo. Waganga wengine wanakisia tu”
 
“lakini wewe una hakika kuwa ulimuona dada?”
 
“Nilimuona  na ni yeye aliyenielekeza nije kwenu. Mimi nilikuwa sijui kwamba amekufa”
 
“Na tangu jana hajakupigia simu?”
 
“Hajanipigia bado”
 
“Na wewe hujampigia?”
 
“Sijampigia”
 
“Ungempigia umuulize vizuri”
 
“Kusema kweli nimetishika  baada ya kusikia kuwa alishakufa”
 
“Hebu jaribu kumpigia sasa hivi?”
 
Nikatoa simu na kuitafuta namba ya Ummy, nilipoipata nikampigia.
 
Simu ikaita. Nikajua itapokelewa ili nimpe mdogo wake azungumze naye lakini simu haikupokelewa. Ilipokata nikapiga tena.
 
“Hapokei simu?” nikamwambia yule msichana.
 
“Labda alikudanganya tu?”
 
ITAENDELEA kesho hapahapa Usikose Uhondo huu nini kitatokea, je simu itapokelewa na mdogo wake atazungumza nini na dada yake ambaye anauhakika ameshafariki?
 

No comments:

Post a Comment