ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MTO URITHI WA
BABU 15
ILIPOISHIA
Nikajiambia kama hatakuwa shetani atakuwa ni mzuka. Lakini sikuelewa
ni kwanini mzuka huo uliwaua wale watu na kwanini uliniambia kuwa unajua siri za mali za babu
yangu.
Kwa vile suala la msichana huyo
lilikuwa limenipa dukuduku, nilipofika
nyumbani nikapata wazo moja. Wazo hilo lilikuwa ni kufanya utafiti ili kumjua huyo Ummy niliyemabiwa kuwa
alikufa, alikuwa msichana wa aina gani.
Alikuwa akifanya kazi gani na pia nijue kama alikuwa na uhusiano na
marehemu babu yangu.
Sikutaka tena kumpigia simu
Ummy kwa sababu huenda angeipokea na kunieleza maneno ya kunitisha.
Ili kuanza upelelezi wangu
niliona niende katika mtaa ule ule aliokuwa anaishi Ummy nitafute mtu aliyekuwa
anamfahamu nifanye naye urafiki na kisha nianze kumhoji kuhusu maisha
ya Ummy mpaka kufa kwake.
Ule mtaa nilikuwa mgeni nao, nilijua
isingekuwa kitu rahisi kumpata rafiki wa kunipa habari za Ummy lakini nilijiambia ni lazima nijitahidi kwa kadiri
ya uwezo wangu nimpate mtu ambaye ataweza kunifumbulia kitendawili cha Ummy Nasir.
SASA ENDELEA
Siku ile yule msichana
hakunipigia simu na mimi sikumpigia. Mimi sikumpigia kwa hofu niliyoipata baada
ya kuelezwa kuwa msichana huyo alishakufa. Na kama alishakufa na nimekuja
kukutana naye, basi atakuwa ni mzuka.
Asubuhi ya siku ya pili
yake nikaenda katika ule mtaa niliyokwenda
jana yake kumuulizia Ummy. Safari hii sikwenda na gari langu. Nilipanda daladala.
Sikutaka kufika tena pale
nyumbani kwa mzee Nasir. Nilizuga zuga katika nyumba zilizokaribiana na
nyumba yake nikitafuta mtu ambaye
ningeweza kufanya naye urafiki na
kumuuuliza kuhusu marehemu Ummy.
Katika kutupatupa macho nikaona sehemu iliyokuwa na meza ya kahawa na kashata. Kulikuwa na mabenchi matatu ya kukalia. Muuza kahawa aliyekuwa amevaa kofia kubwa
lililosukwa kwa minyaa kama la mvuvi wa
samaki, alikuwa amekaa upande wa pili wa meza yake akiwa na ndoo mbili, jiko na
birika la kahawa lililokuwa likifuka
moshi jikoni.
Muda ule kulikuwa na mtu
mmoja tu aliyekuwa amekaa akinywa kahawa. Nikaona niende nikakae mahali hapo ili nifikirie la
kufanya.
Mara tu nilipoketi akaja mtu
mwingine. Tukawa watu watatu.
Muuza kahawa akatutilia
kahawa bila hata kutuuliza. Ukishakaa kwenye benchi lake maana yake ni kuwa
unataka kahawa.
Nilichomsikia akiuliza ni.
“Nikutilie tangawizi?”
Alikuwa akimtazama yule mwenzangu
aliyekuja baada ya mimi.
“Ndiyo tia” Mtu huyo akamjibu.
“Na wewe?” akaniiuliza mimi.
Wakati ananitazama, sura yake ikanijia akilini
mwangu. Zilinichukua kama nukta tatu
hivi kumkumbuka Selemeni Mzaramu.
Wakati namkumbuka, yeye alishanikumbuka zamani.
“Ah! Kasim Fumbwe… kumbe ni wewe?” akaniuliza kwa mshangao.
“Mzaramu! Bado upo Dar hii!” nikamuuliza.
“Twende wapi ndugu yangu.
Tunabangaiza humu humu. Makamba alituambia tutabanana hapa hapa”
Tukacheka.
“Nikuwekee tangawizi?’ akaniiuliza tena.
“Ndiyo niwekee”
Selemani Mzaramu alikuwa
rafiki yangu wa miaka mingi. Nilisoma naye shule ya msingi hadi darasa la saba.
Wakati mimi naendelea na masomo ya sekondari, mwenzangu
hakuchaguliwa. Na baada ya hapo sikuwahi kukutana naye tena hadi siku ile nilipomuona amevaa kofia la minyaa akiuza kahawa.
Mzaramu alinisogezea kikombe
cha kahawa akaniuliza.
“Uko wapi Kasim?”
“Mimi niko hapa hapa Dar. Nilikuwa Morogoro , maisha yakanishinda,
nikarudi hapa Dar”
“Unafanya kazi wapi,
nije unipe kibarua?”
“Bado nipo nipo tu, sifanyi kazi popote. Nilikuwa na
duka Morogoro, duka likafa, nikarudi Dar baada ya babu yangu kufariki. Na ndiyo
nimeamua niendelee kuwa hapa”
“Mimi baada ya masomo
nilihangaika na malori mpaka yamenitia kilema. Sasa nipo
hapa?”
“Alah! Umepata ulemavu?”
“Mguu wangu ulivunjika mara tatu. Mfupa ulisagika vibaya.
Nimeokolewa na vyuma…”
Mzaramu alinionesha mguu wake wa kushoto baada
ya kuisega suruali yake. Mguu huo ulikuwa hautazamiki kwa mishono!
“Nje unaouna ni mguu
lakini ndani ni vyuma vitupu, yaani ulikuwa ukatwe lakini
kaka yangu alijitahidi sana kunipeleka
hospitali za pesa ambako niliwekewa vyuma. Nikasema sasa malori basi”
“Loh! Pole sana rafiki yangu.
Ulikuwa dereva?”
“Nilikuwa taniboi. Basi nilikaa
hospitali karibu mwaka mzima”
Nikatikisa kichwa changu
kumsikitikia.
“Pole sana rafiki yangu
lakini kama unapata riziki yako na maisha yanakwenda, shukuru Mungu”
“Nashukuru. Nimeoa na nina watoto wawili lakini mke wangu alinikimbia
aliposikia nitakatwa mguu. Kaniachia watoto lakini nimewalea mwenyewe na
hivi sasa wanasoma”
“Kumbe ulipata
mkasa mkubwa rafiki yangu….”
“Kula kashata” Mzaramu
akaniambia.
Nikaokota kashata moja na kuing’ata.
“Unazitengeza mwenywe?” nikamuuliza.
“Nazitengeza mwenyewe
usiku. Asubuhi nakuja nazo”
“Kwani unaishi wapi??’
“Naishi hapa hapa
Mwananyamala”
“Mtaa huu?”
“Ndiyo naishi mtaa huu huu lakini ni kule mwisho”
“Umeishi mtaa huu kwa miaka mingapi?’
“Nina miaka kumi na mitano sasa”
Nikajiambia kimoyomoyo kuwa atakuwa
anamjua Ummy ambaye alikufa miaka mitano
tu iliyopita.
“Katika mtaa huu alikuwa
akiishi msichana mmoja aliyekuwa akiitwa
Ummy Nasri…”
“Nyumba yao ile paleee lakini huyo msichana
alikwisha kufa zamani ila namfahamu sana”
ITAENDELEA kesho Usikose
No comments:
Post a Comment