ZULIA LA FAKI, 0655 340572
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 14
ILIPOISHIA
“Sasa mwanangu, huyu msichana uliyekuja kutueleza
kwamba ulikutana naye na kuzungumza naye alishakufa na mdogo wake amethibitisha kwamba namba ya simu
uliyopigiwa ni ya marehemu kweli, je mpaka sasa una wazo gani?” Yule mama
akaniuliza lakini swali lake lilikuwa ni gumu kulijibu.
“Sijui nikujibu nini mama
yangu. Hiyo taarifa kwamba huyu msichna alikufa
miaka mitano iliyopita imenichanganya akili yangu” nikamjibu.
“Kwani alipokupigia simu
alikueleza alikuwa na uhusiano gani na babu yako?” Yule mzee naye akaniuliza.
“Hakuniambia kama alikuwa
na uuhusiano wowote na babu yangu
isipokuwa aliniambia alitaka anipe taarifa za mali ya babu yangu”
“Na mimi nina wazo langu” Yule msichana naye akasema na kuongeza.
“Hebu mpigie simu hapa hapa
tumsikie”
“Hilo ni wazo zuri” nikasema
na kuitazama simu yangu ambayo nilikuwa nayo mkononi.
Nikampigia Ummy Sharif Nasri.
SASA ENDELEA
Simu ilikuwa inaita lakini
ilikuwa haipokelewi.
“Simu inaita lakini
haipokelewi” nikawambia.
Niliiondoa simu sikioni
mwangu na kuielekeza kwa yule msichana.
“Sikiliza simu inaita”
nikamwambia.
Msichana aliishika ile simu
akaiweka kwenye sikio lake na kusikiliza.
“Ndiyo simu inaita kweli”
akasema.
Aliendelea kuiweka sikioni
kwake hadi simu ikakata yenyewe. Akaiondoa sikioni na kunipa.
“Simu inaita lakini hapokei” akasema tena.
“Una maana kwamba Ummy yuko hai?” Mama yake
akamuuuliza.
Msichana akabetua mabega.
“Tunachojua sisi ni kuwa
amekufa, sasa hii habari kuwa dada yuko hai hatuijui. Kama angekuwa hai si
angekuja nyumbani”
“Ni miujiza hii!” Mzee
akasema huku uso wake ukiwa umefadhaika.
“Hebu piga tena” Yule mama akaniambia.
Nikapiga tena ile
namba.
Safari hii simu haikupatikana.
“Inaita” Mama akaniuliza.
“Simu haipatikani tena” nikawambia.
“Mara moja hii!” Mama
akashangaa.
“Inawezekana ameizima”
nikawambia.
“Huyo Ummy ndiyo ameizima?”
“Ndiyo yeye. Mnaponiambia kuwa amekufa niinashangaa
kwa sababu nimemuona na nimezungumza
naye”
“Huyu huyu ambaye
umemuona kwenye picha?”
“Ndiye huyo huyo”
“Sasa ili uamini kuwa amekufa
twende nikakuoneshe kaburi lake.
Makaburi hayako mbali” Mzee akaniambia.
Mzee huyo alinichukua hadi
katika eneo la makaburi ambalo halikuwa mbali
sana. Akanionesha kaburi la Ummy Nasri. Lilikuwa na kibao kilichoandikwa jina
lake, tarehe aliyokufa na aliyozikwa.
“Kaburi lake ni hili hapa”
Sikuwa hata na la kusema.
Nilibaki kushangaa tu.
Mzee aliendelea kuniambia.
“Marehemu amelala ndani”
“Sasa mzee huyu atakuwa
nani?” nikamuuliza.
“Sisi hatumjui. Sisi
tunachojua ni kuwa binti yetu alishakufa na aliyekufa hafufuki”
“Lakini mzee fikiria kwamba
alinielekeza yeye mwenyewe kuwa nije pale nyumbani nimuulizie”
“Mtu yeyote hawezi
kukubaliana na maelezo yako” Mzee akaniambia
huku akiondoka.
“Nimekuja kukuonesha hili
kaburi ili uthibitishe kuwa Ummy alikwishakufa” akaongeza.
“Na mimi nathibitisha kuwa
nilimuona”
“Basi itakuwa ni miujiza
mikubwa”
Tukarudi pale nyumbani.
“Ni vizuri kama utakutana
naye tena uje naye hapa mguu kwa mguu” Mzee akaniambia wakati akiketi kwenye
kiti chake cha uvivu.
Wakati narudi na gari langu
nilianza kuzikumbuka zile safari za
kimiujiza za yule msichana amabaye kwanza nilimkuta Botswana. Halafu nikaenda
kumuona Zimbabwe. Nilipokwenda Afrika
Kusini nikakutana naye tena. Bado wakati narudi Tanzania nikashuka naye kwenye ndege moja ingawa wakati wa kupanda
ndege sikumuona.
Na huko kote alikuwa akiwaua
watu niliokuwa nimewafuata. Mtu wa mwisho alikuwa mkazi wa hapa hapa Dar ambaye
alishuka naye kwenye ndege.
Watu wote aliowaua walikuwa wakidaiwa na marehemu
babu yangu na mauaji yalifanyika wakati ule nafanya ziara yakufuatilia madeni.
Mwisho wa siku msichana huyo
alinipigia simu na kuniambia kuwa ana mazungumzo na mimi kuhusu mali za babu
yangu.
Aliniona Botswana. Aliniona
Zimbabwe. Aliniona Afrika Kusini lakini
hakuniambia kuwa ana mazungumzo na mimi.
Katika nyumba aliyonielekeza
niende nimeambiwa kwamba msichana huyo wanamfahamu lakini alikwisha kufa miaka mitano iliyopita.
Sasa napata picha kwamba msichana huyu hakuwa wa kawaida.
Zile safari alizozifanya kule Botswana,
Zimbabwe na Afrika Kusini pia hazikuwa
za kawaida. Niliona kama alikuwa
akiibuka tu katika zile nchi nilizomkuta. Hakuwa akisafiri. Hakukuwa na hadi
leo hakuna usafiri wa haraka kiasi kile.
Pia yale mauaji aliyokuwa
akiyafanya hayakuwa ya kawaida. Kwa mwanamke kuwaua wanaume kirahisi rahisi namna ile haikuwa kawaida.
Baada ya kuwaza hayo
nikajiuliza, yule msichana alikuwa shetani au mzuka wa Ummy niliyeelezwa kuwa
alikwishakufa?
ITAENDELEA kesho hapahapa Usikose
No comments:
Post a Comment