SIMULIZI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 5
ILIPOISHIA
Ilipofika saa saba mchana
wakati natazama taarifa ya habari kwenye televisheni, lile tukio la mauaji
lililotokea pale hoteli lilitangazwa.
Kitu ambacho kilinishitua ni
kuwa mtangazaji alimtaja marehemu kuwa ni Isaac Chusama mtu ambaye alikuwa
hafahamiki alikuwa akifanya kazi gani. Alitaja mtaa aliokuwa akiishi na kueleza
kuwa hakuwa na mke wala watoto.
Taarifa ilieleza kuwa Chusama
alifika hapo hoteli majira ya mchana na kuzungumza na msichana mmoja aliyekuwa
ameketi kwenye ukumbi wa hoteli hiyo kabla ya kukodi chumba na kuingia chumbani
na msichana huyo.
Taarifa ya televisheni
iliendelea kueleza kuwa asubuhi ya siku ile mhudumu wa usafi wa hoteli hiyo
aliigundua maiti ya Chusama iliyokuwa imelazwa chini na kutoa taarifa kwa
uongozi wa hoteli.
SASA ENDELEA
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,
uchunguzi wa madaktari umeonesha kuwa marehemu alikabwa koo hadi mauti
yakamkuta.
Msemaji wa polisi akaeleza
kuwa polisi wanamshuku msichana aliyekuwa naye kuhusika na mauaji hayo na
wameanzisha msako wa kumtafuta.
Baada ya taarifa hiyo
kutolewa kwenye televisheni, nilibaini kuwa mtu aliyefika hapo hoteli na
hatimaye kuuawa alikuwa ni mwenyeji wangu Isaac Chusama!
Hapo niligundua sababu ni kwanini
simu nilizokuwa nikipiga zilikuwa hazipokelewi. Zilikuwa haipokelewi kwa sababu
Chusama mwenyewe alikuwa ameshauawa. Bila shaka alikuwa ameuawa siku iliyopita.
Sasa nikabaki na maswali
kuhusiana na tukio hilo.
Nilijiuliza yule msichana alikuwa nani?
Je alikuwa akijuana na Chusama?
Na ni kwanini amemuua?
Pia nilijiuliza baada ya
Chusama kuuawa, kulikuwa na uwezekano kweli wa kulipwa pesa zangu? Na ni nani
atanilipa?
Baada ya kufikiri kwa kina
niliona uwezekano wa kulipwa pesa zangu haukuwepo. Kwani licha ya kuwa ni pesa
nyingi nilizokuwa nikimdai Chusama pia nilikuwa si mwenyeji wa hapo na pengine
nisiaminike na huyo ambaye atapaswa kulipa deni hilo.
Lakini baya zaidi,
nilijiambia kama nitajitia kuwatafuta ndugu na jamaa wa Chusama ili wanilipe
deni hilo
wanaweza kuniripoti polisi na nikakamatwa na kuhusishwa na mauaji ya Chusama. Hapo
nikaingiwa na hofu.
Matumaini ya kupata pesa nilizozifuata
huko Zimbabwe
yakaanza kuota mbawa. Kule kukata tamaa na kuona safari niliyoifanya ilikuwa ya
bure, nilijikuta nikimlaumu Chusama kwa uzembe. Licha ya kutojua kama yule msichana alikuwa na uhusiano naye au la, nilimlaumu
Chusama kwa kuonesha kuwa na tamaa ya ngono iliyopitiliza.
Niliamini kuwa Chusama alipokuwa
anakuja pale hoteli alikuwa akinifuata mimi lakini ghafla akili yake ilikwenda
kwa yule msichana akasahahu kwamba nilikuwa na ahadi naye na hata nilipompigia
simu hakupokea. Matokeo yake yalikuwa ni kuuawa.
Lakini ni kwanini auawe?
Nikajiuliza na kuendelea kujiuliza, yule
msichana alikuwa nani? Ana kisa naye gani na baada ya kumuua Chusama,
alipotelea wapi?
Sikuweza kupata jibu hata la
kukisia. Nilikuwa nimeketi pale ukumbini nikainuka na kurudi chumbani.
Wakati ninapanda ngazi
nilijiambia ni vizuri niondoke haraka hapo Zimbabwe kwani licha ya kuwa
nisingepata faida yoyote kwa kuendelea kukaa hapo bali pia nilitaka kuepuka
uchunguzi wa polisi.
Nilihisi kwamba katika
uchunguzi wao polisi wanaweza kugundua kwamba Chusama alikuwa amenipangia
chumba pale hoteli na ninaweza kukamatwa na kuulizwa nilikuwa na mpango naye
gani.
Baada ya kuingia chumbani
nilichukua begi langu nikatoka kimya kimya. Nilikodi teksi na kurudi kiwanja
cha ndege. Kwa bahati njema nilikuta kulikuwa na ndege inayokwenda Botswana
ambayo bado ilikuwa na nafasi.
Nikakata tikiti ya ndege ya
kwenda Botswana.
Ndege iliondoka maasaa matatu baada ya mimi kufika kiwanja cha ndege.
Nilipofika Gaborone, nilimpigia simu Benjamin Muhoza na kumjulisha kuwa
nilikuwa katika kiwanja cha ndege cha Gaborone.
“Subiri ninatuma gari
ikufuate” Sauti ya Muhoza ikasikika kwenye simu.
“Dereva wako atanitambuaje”
nikamuuliza.
“Umevaa mavazi gani?”
“Kwanza
mimi ni mrefu wa wastani na mweupe. Nimevaa tisheti ya rangi ya samli, suruali
aina ya jinzi ya rangi ya samawati. Nimevaa miwani ya jua”
“Atakutambua. Nitakupa namba
ya usajili ya gari atakalokuja nalo”
“Sawa”
Muhoza alinitajia namba ya
usajili ya gari hilo,
aina yake na rangi yake. Nikamwambia nitalitambua litakapofika.
Saa moja baadaye nikiwa hapo
nje ya jengo la uwanja wa ndege nikaliona gari hilo likiwasili. Sikutaka kumpa dereva wa
gari hilo taabu
ya kunitafuta. Nikamfuata.
Baada ya kujitambulisha kwake
kuwa mimi ndiye mgeni wa Chusama aliniambia nijipakie kwenye gari.
Nilijipakia katika siti ya
mbele iliyokuwa kando ya dereva. Gari hilo
lilinipeleka katika hoteli moja ambapo mwenyeji wangu tayari alikuwa
amenichukulia chumba.
“Sasa acha nimfuate
mheshimiwa” Dereva akaniambia baada ya kunifikisha hapo hoteli. Akaongeza.
“Aliniambia nikishakufikisha
hapa hoteli nimfuate”
“Sawa” nikamjibu. Wakati huo
nilikuwa nimekaa katika bustani iliyokuwa mbele ya hoteli ambayo iliwekewa viti
na meza.
“Unaweza kuagiza kinywaji
unachotaka au chakula”
“Labda kinywaji tu, sitapenda
kula kitu chochote kwa sasa” nikamwambia.
Dereva huyo alipoondoka
muhudumu alinifuata na kuniuliza kama nilikuwa
ninahitaji huduma yoyote.
“Nipatie soda tu”
nikamwambia.
“Soda gani?”
“Fanta”
Mhudumu akaondoka. Baada ya
muda mfupi alirudi na kuniletea soda niliyomuagiza.
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu jamaa amewasili Gaborone, je nako nini kitatokea je, atafanikiwa nako huko. ungana nami kesho.
No comments:
Post a Comment