ZULIA LA FAKI, 0655 340572
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 10
ILIPOKIONA
Uchunuzi wa madaktari wa
hospitali ya Muhimbili ulionesha kuwa marehemu aliuawa kwa kukabwa koo na
kukosehwa pumzi kwa zaidi ya dakika tano jambo lililosababisha moyo wake
kusimama na hivyo kusababisha kifo chake.
Sasa mshituko mkubwa
niliupata wakati picha ya Abdul Baraka ilipooneshwa. Alikuwa ni yule mtu
niliyemuona amefuatana na yule msichana
muuaji jana yake.
Hapo hapo nikajua kwamba
aliuawa na yule msichana ambaye alitoweka baada ya kufanya mauaji hayo.
Nikajiuliza ni kwanini hawa
watu wanaodaiwa na marehemu babu yangu wanauawa na anayewaua ni mtu mmoja tena
msichana, amezunguka nchi zote kuwafuata?
Jambo jingine la ajabu
nililoliona ni kuwa mauaji hayo yanafanyika wakati ule ninafuatilia madeni
hayo. Kulikoni!
Nilitamani kwenda polisi
kueleza nilichokuwa ninakifahamu kuhusu yule msichana lakini niliogopa kwa
sababu sikuwa nikijua yule msichana alikuwa nani. Angeweza kuwa gaidi au ni mtu
aliyetumwa kufanya mauaji.
Nikajiambia kama nitajitia
kimbele mbele cha kumripoti polisi ningeweza kuuawa. Nikaamua kuwa kimya.
Wiki moja ikapita. Siku hiyo
nilikuwa nimekaa nyumbani kwangu nikiwaza, simu yangu ikaita.
SASA ENDELEA
Namba iliyokuwa ikinipigia ilikuwa ngeni
kwangu. Nikaipokea ile simu.
“Hello!”
“Hello, nazungumza na Kassim
Fumbwe?’ Sauti ya mwanamke ikaniuliza.
“Ndiyo. Kassim Fumbwe. Nani
mwenzangu”
“Naitwa Ummy. Nilikuwa na mazungumzo
na wewe. Nilihitaji tukutane”
Moyo wangu ulishituka kidogo.
“Tukutane wapi?”
Mimi niko Suzy Hotel hapa
Masaki. Niko chumaba namba 35. Ukifika utanikuta”
Nikasita kidogo kabla ya
kumuuliza.
“Unanifahamu vipi?”
“Ninakufahamu. Kama unataka
kujua zaidi nitakufahamisha utakapofika”
“Hayo mazungumzo yanahusu
nini?”
“Yanahusu mali za marehemu
babu yako”
Aliponiambia hivyo sikutaka
kuendelea kumhoji, nikamwambia.
“Nisubiri ninakuja sasa hivi”
Simu ya upande wa pili
ikakatwa. Nilikuwa nimeketi sebuleni nikainuka na kutoka. Gari langu ambao
nililirithi kwa babu nilikuwa nimeliegesha nje. Nikajiapakia na kuliwasha.
Gari lilipowaka nilitia gea
na kuelekea Masaki huku nikijiuliza huyo mwanamke aliyenipigia simu alikuwa
nani na alitaka kunieleza nini kuhusu mali za marehemu babu yangu.
Kilichonifanya nikurupuke na
kumfuata haraka haraka ni ule utata wa mali za marehemu babu. Babu alikuwa
tajiri lakini baada ya kufa alionekana hakuwa na mali yoyote.
Nilitarajia kuwa mwanamke
huyo alikuwa akijua siri ya mali za marehemu babu na angenifichulia.
Nilipofika Suzy Hotel
iliyokuwa Masaki niliegesha gari katika eneo la kuegeshea kisha nikatoa simu na
kumpgia yule mwanamke.
“Nimeshafika?” nikamwambia.
“Uko wapi?” Sauti ya mwanamke
ikauliza kwenye simu.
“Niko hapa mbele
ya hoteli”
“Njoo chumba namba 35 kipo
ghorofa ya kwanza”
“Sawa”
Nikashuka kwenye gari na kuingia hotelini humo.
Nilipanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza, nikakitafuta chumba namba 35.
Nilipokiona nikakifuata na kubisha mlango.
Baada ya sekunde chache tu mlango ulifunguliwa na msichana.
“Karibu ndani” akaniambia
huku akitabasamu.
Nilipomtazama vizuri, sura
yake ikanijia akilini mmwangu.
Alikuwa ni yule msichana
muuaji niliyekutana naye Botswana,
Zimbabwe na kisha Afrika Kusini.
Nilipogundua kuwa alikuwa ni
yeye nilishituka nikarudi nyuma hatua
moja kisha nikageuka na kutoka
mbio.
“Mbona unakimbia?” Niliisikia sauti yake ikiniuliza kwa nyuma.
Sikujibu wala sikusimama. Nilishuka ngazi mbili mbili
nikafika chini. Pale chini niliona nikikimbia nitawatia watu wasiwasi
nikatembea taratibu na kutoka nje ya
hoteli. Nikajipakia kwenye gari langu na kuliondoa kwa kasi.
Bila shaka yule mwanamke
alitaka kunimaliza na mimi, nilijiambia kimoyomoyo huku nikizidi kukanyaga
mafuta.
Nilishindwa kujua aliipataje
namba yangu na alijuaje kuwa ninaitwa Kassim Fumbwe kwani aliponipigia simu
aliniuliza kama mimi ni Kassim Fumbwe.
Aliponipigia simu sikutarajia
kama alikuwa ni yeye. Si kwa sababu ya
kunitambua kuwa mimi ni Kassim Fumbwe bali vile alivyoniambia kuwa ana
mazungumzo na mimi kuhusu mali ya babu yangu.
Nikahisi kwamba likuwa akijua
mengi kuhusu mimi hasa vile ambavyo alihusika katika safari yangu nzima kutoka
Botswana, Zimbabwe, Afrika Kusini hadi kurudi tena Tanzania.
Sasa nikapata wazo moja
kwamba ni kweli alikuwa akiifahamu siri ya mali ya marehemu babu yangu kwa
sababu yeye ndiye aliyeifanya safari yangu isiwe na mafanikio. Yeye ndiye
aliyewaua watu wote waliokuwa wakidaiwa na babu yangu. Sababu za kuwaua alikuwa
akizijua mwenyewe.
Nikaendelea kujiambia, kwangu
mimi msichana huyo atabaki kuwa adui. Ingawa sikuweza kujua ni kwanini aliwaua
wale watu lakini nilijenga hofu kwamba alitaka kuniua na mimi.
Hii ndio sababu nilimkimbia
pale hoteli.
Nilipofika nyumbani nilikaa
sebuleni na kuendelea kujiwazia kuhusu yule mwanamke. Ghafla simu yangu ikaita.
Nilipotazama namba nikaona ni ile ya yule msichana. Nikaipokea.
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekuchablog, Usikose
No comments:
Post a Comment