ZULIA LA FAKI 0655 340572
NILIKIONA CHA MTO URITHI WA
BABU 8
ILIPOISHIA
Yule dereva wa Muhoza
alipoondoka pale hoteli sikumuona tena. Nikalala pale hoteli hadi siku
iliyofuata ambapo nililazimika kujilipia mwenyewe chumba.
Nikafanya mipango ya usafiri
wa kwenda Afrika Kusini. Nikagundua kuwa ulikuwepo usafiri wa treni wa kutoka Zimbabwe
hadi hadi Afrika Kusini.
Nikasafiri kwa treni hadi
Cape Town. Nilipofika kwenye kituo cha treni cha Cape town, nikampigia simu
Domesan Dube kumjulisha kuwa nilikuwa nimewasili kwa treni kutokea Zimbabwe.
Dube akaniambia kuwa anamtuma
dereva wake anifuate. Baada ya kupita kama saa moja hivi, dereva huyo akawasili
na gari. Alinipakia akanipeleka nyumbani kwa Dube.
Wakati anasimamisha gari
mbele ya jumba lake la kifahari nilimuona yule msichana muuaji akitoka katika
jumba hilo. Alipungia mkono teksi iliyokuwa inapita barabarani. Teksi
iliposimama akajipakia na kuondoka.
Yule dereva hakushituka
kumuona msichana huyo lakini mimi nilishituka sana.
SASA ENDELEA
Mimi nilishituka kwa sababu
nilikuwa namfahamu na nilikuwa nafahamu visa alivyovitenda kule Botswana na
Zimbabwe.
Lakini pia nilishituka vile
nilivyomkuta Afrika Kusini wakati jana yake tu aliuaa mtu Zimbabwe.
Kitu kingine kilichonifanya
nishituke ni kuona msichana huyo alikuwa akinifuatia kwa wale wadaiwa wangu
ambapo kile nchi niliyokuwa ninakwenda nilikuwa namkuta akiwa na mtu niliyekuwa
namfuata.
Baada ya gari kusimama,
dereva alishuka na mimi nikafungua
mlango haraka na kushuka. Tayari uso
wangu ulikuwa umeshatahariki baada ya kumuona yule msichana.
Dereva alitangulia
kuingia ndani ya jumba hilo akaniambia.
“Karibu ndani”
Nikaingia ndani. Tulitokea
kwenye sebule pana iliyokuwa imepambwa vizuri.
Mimi na yule dereva
tulishituka tulipomuona mtu aliyekuwa amelala chini akiwa ametoa macho karibu
na mlango.
“Oh Bwana Dube!” Dereva
alitoa sauti ya kimako kisha akachutama na kumtazama yule mtu.
“Bwana Dube…Bwana Dube…!”
akamuita huku akijaribu kumtikisa.
Mtu huyo alikuwa kimya huku
macho yake yakitazama dari bila kupepesa. Sikuwa daktari na sikuwa na uzoevu wa
kutazama miili ya watu waliokufa lakini nilipotazama yale macho, niligundua
mara moja kuwa mtu huyo alikuwa ameshakufa.
“Huyo ndiye Bwana Dumesan
Dube?” nikamuuliza yule dereva.
“Ndiye yeye. Sijui amepatwa
na nini!”
“Kuna msichana alitoka humu
ndani wakati tunafika, ni nani?”
Dreva akatikisa kichwa.
“Sikumfahamu. Ngoja nimuite
daktari wake, labda ni presha”
Dereva huyo aliyekuwa
ametaharuki aliinuka akatoa simu yake na kutafuta namba ya daktari wa Dube
kasha akampigia.
“Bwana Dube ameaguka chini,
sijui amepatwa na nini?” alisema baada ya simu kupokelewa.
Niliisikia sauti ya upande wa
pili ikiuliza.
“Ameanguka wapi?”
“Nyumbani kwake. Nilikuwa
nimetoka kidogo niliporudi nilimkuta yuko chini lakini hasemi na inaonekana
hana fahamu”
“Subiri, ninakuja”
Dereva akakata simu na kunitazama.
“Daktari wake anakuja.
Tumsubiri”
“Kwani Bwana Dube ana tatizo
la presha?” nikamuuliza.
“Presha ni tatizo linaloweza
kutokea ghafla tu, si lazima uwe nalo siku za nyuma”
Huyo daktari alliyeitwa
aliharakisha kufika. Baada ya dakika thelathini tu aliusukuma mlango na kuingia
ndani.
Alipomuona Dube akiwa chini
hakuuliza chochote, alichutama na kuanza kumpima. Alianza kumpima presha kwa
kutumia kipimo cha kufunga kwenye mkono.
Alipomaliza aliinuka na
kutuambia.
“Nasikitika kuwambia kuwa Bwana
Dube ameshakufa. Apelekwe hospitali kwa uthibitisho zaidi”
“Ameshakufa!” Dereva wa Dube
alimaka uso wake ukionesha kutoamini.
“Apelekwe hospitali” Daktari
akasisitiza.
“Lakini ni jambo la
kushangaza sana kwa sababu niliachana naye muda mchache tu uliopita”
“Umeniambia kwamba
alianguka?” Daktari akamuuliza.
“Itakuwa alianguka kwani
tulipokuja tulimkuta hapo chini”
“Ana dalili kama ya kukabwa
kwenye shingo yake”
Dereva alizidi kupata
taharuki.
“Amekabwa? Amekabwa na nani?
Humu ndani hakuna mtu. Au aliingia mtu na kumkaba?’
“labda ni yule msichana
tuliyemuona akitoka?” nikamwambia.
“Msichana anaweza kumkaba?”
“Anaweza”
“Mimi naondoka. Nimewambia
mumpeleke hospitali. Huko atafanyiwa uchunguzi na sababu ya kifo chake
itajulikana” Daktari akatuambia na kutoka.
Nikajiambia kwamba kwa vile
suala hilo linahusu mauaji, ingebidi lifike polisi na likifika huko, mimi na
dereva wa Dube tutakuwa ndio watuhumiwa wa kwanza.
Kwa sababu ya kuogopa
ushahidi, sikueleza chochote kuhusu yule msichana, nikamuacha yule dereva
akishughulikia suala hilo. Mimi nikatafuta hoteli nikapanga chumba.
Kwa kweli suala la yule
msichana muuaji lilisumbua akili yangu. Nilishindwa kujua msichana huyo
alitokea wapi na kwanini alikuwa akiwaua wale watu. Pia nilikuwa nikijiuliza
alikuwa akiwaua kwa namna gani?
Kile kitendo cha kumuona akitoka katika jumba la Dube kilitosha
kunithibitishia kuwa ndiye aliyemuua Dube.
Nilikuwa nina pesa chache
ilizobaki ambazo zilitosha kukata tikiti ya kurudi Dar. Asubuhi kulipokucha
nikaenda kukata tikiti na kuondoka. Safari yangu haikuwa na mafanikio yoyote. Zaidi
ilikuwa ni kupata hasara tu na kupotea muda.
ITAENDELEA kesho, nini kitatokea kabla ya kuondoka Afrika Kusini, ungana nami kesho.
No comments:
Post a Comment