Sunday, April 2, 2017

SIMULIZI, NIMEKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 3

SIMULIZI
 
NIMEKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 3
 
Alinisalimia kwa Kingreza kwa kutumia jina la marehemu babu yangu. Na yeye nikamjulisha kuwa Mzee Fumbwe alikuwa amefariki dunia na kwamba mimi nilikuwa mjukuu wake.
 
“Ulikuwa unataka nini?” akaniuliza.
 
“Kumbukumbu za babu zinaonesha kwamba anakudai dola milioni moja na laki tano. Mikataba yenu  ninayo hapa. Mimi ndiye mrithi wake”
 
Simu ya upande wa pili ikawa kimya. Nilipoona amenyamaza nilimwambia.
 
Ninazo hati za mahakama zinazothibitisha kuwa mimi ndiye mrithi wa marehemu. Nina cheti cha kifo chake na nina mkataba wa makubaliano yenu”
 
“Utakuja kunionesha?” Benjamin akaniuliza.
 
“Nitakuja kukuonesha ili uthibitishe kuwa Mzee Fumbwe amefariki na kwamba mimi ndiye ninayepaswa kulipwa madeni yake”
 
SASA ENDELEA
 
“Utakuja lini?”
 
“Nitakujulisha siku ambayo nitakuja”
 
“Sawa”
 
Nikakata simu kisha nikampigia Dumessan Dube wa Afrika Kusini.
 
Yeye nilizungumza naye kama nilivyozungumza na wenzake lakini yeye hakushangaa nilipomwambia Mzee Fumbwe amefariki. Aliniambia ameshapata habari.
 
“Umepata habari hiyo kutoka wapi?” nikamuuliza.
 
“Nimeipata kutoka kwa marafiki mbalimbali ambao anafanya nao biasharara”
 
“Ni vyema kama umeshapata habari. Kwa hiyo mimi ndiye mrithi wake. Nimekuta una deni la dola milioni tatu ambazo babu anakudai”
 
“Umelikuta wapi deni hilo?”
 
“Kwenye kumbukumbu zake na mkataba wenu wa makubaliano pia ninao hapa”
 
“Sawa” Dube aliniambia baada ya kimya kifupi kisha akaniuliza.
 
“Sasa ulitakaje?”
 
“Nimeona tarehe ya malipo ya hizo pesa imeshapita. Nilitaka nije Afrika  Kusini unipatie pesa hizo. Nitakuja na hati zote”
 
Baada ya kimya kingine kifupi, Dube aliniambia.
 
“Sawa. Unatarajia kuja lini?”
 
“Nitakujulisha”
 
“Sawa”
 
Kusema kweli baada  ya kuzungumza na wafanyabiashra hao waliokuwa nje ya nchi nilifarijika sana. Yule mfanyabiashara aliyekuwa Dar es Salaa ambaye simu yake ilikuwa haipatikani nilimuacha kiporo.
 
Niliona sasa urithi wa babu ulikuwa unakuja mikononi mwangu taratibu. Nikajiambia kama pesa hizo nitazipata zote ningekuwa miongoni mwa matajiri wakubwa katika jiji hili.
 
Nilimshangaa marehemu babu yangu kwa kuacha kiasi kikubwa cha pesa  nje ya nchi bila kunishirikisha mimi mjukuu wake. Kwa kweli alikuwa msiri sana na pia alikuwa tajiri japokuwa mali alizokuwa akimiliki hapo Dar bado zilikuwa ni kitendawili.
 
Sikwenda kumueleza wakili kuhusu madeni hayo. Niliacha yabaki kuwa siri yangu. Sasa nikaanza kujiandaa kwa safari ya nchi hizo tatu huku ndoto za utajiri zikiwa zimetawala akili yangu.
 
Baada ya wiki mbili nikawa nimeshapata pesa za kuniwezesha kuzuru katika nchi hizo. Mipango yangu ya safari ilipokamilika nikaanza safari yangu. Kwanza nilipanga kwenda Harare Zimbabwe. Kabla ya kuondoka  nilimpigia simu Isaac Chusama kumjulisha kuwa ninakwenda Zimbabwe.
 
“Sawa. Ukifika utanipigia simu kunijulisha kuwa umefika” akaniambia.
 
“Sawa”
 
Nilifika Harare kama saa nane mchana. Nikiwa katika kiwanja cha ndege cha Harare nilimpigia simu Chusama kumjulisha kuwa nilikuwa uwanja wa ndege wa Harare. Nilitumia simu ya malipo iliyokuwa pale kiwanja cha ndege.
 
“Kama umeshafika kodi teksi. Mwambie dereva akupeleke Chapachapa Hotel. Nimekukodia chumba namba 35”
 
“Natumaini madereva wa teksi watakuwa wanaifahamu ilipo hoteli hiyo”
 
“Wanaifahamu. Ni hoteli maarufu”
 
“Sawa. Ngoja nikodi teksi”
 
Baada ya kumaliza kuzungumza na mwenyeji wangu huyo nilitoka nje ya uwanja wa ndege na kukodi teksi. Sasa nilikuwa natumia kingereza kitupu.
 
Nilimwammbia dereva wa teksi anipeleke Chapachapa Hotel. Baada ya mwendo wa saa moja kasorobo akanifikisha katika hoteli hiyo iliyokuwa katikati ya jiji la Harare.
.
Baada ya kumlipa dereva pesa aliyotaka niliingia hotelini humo. Unapoingia unakutana na ukumbi mwanana uliokuwa na viti na meza.
 
Kwenye meza moja iliyokuwa karibu na mlango aliketi msichana mmoja mrembo aliyekuwa akinywa soda huku akisoma gazeti. Upande wa kushoto wa ukumbi huo ndio palikuwa mapokezi.
 
Nikaenda hapo mapokezi na kujitambulisha kuwa nilikuwa mgeni wa Isaac Chusama na kwamba aliniambia kuwa amenikodia chumba namba 35.
 
“Oh ndiye wewe! Hebu lete paspoti yako tuione” Mhudumu wa mapokezi ambaye alikuwa msichana akaniambia.
 
Nikampa paspoti yangu iliyokuwa mkononi kama kitambulisho changu huku tukizungumza Kiingereza.
 
Baada ya kuifungua paspoti yangu na kuiona picha yangu alinirudishia.
 
Nikapelekwa chumba namba 35 kilichokuwa ghorofa ya kwanza. Nilikuta kiyoyozi, tv na simu ya mezani iliyowekwa kwenye kimeza kilichokuwa kando ya kitanda. Pia kulikuwa na  kochi moja refu na kabati la  kuwekea nguo pamoja na meza ya kuvalia iliyokuwa na kioo kikubwa.
 
Nilipoona ile simu niliweka begi langu juu ya kochi nikaketi kitandani na kuinua mkono wa simu.
 
Simu zilikuwa zinapitia kwa opereta aliyekuwa hapo hoteli ambaye alipopokea simu yangu nilimpa namba ya Isaac Chussama.
 
Sekunde chache tu baadaye nikaisikia sauti ya Chusama.
 
“Helow!”
 
“Mimi ni yule mgeni wako kutoka Tanzania, nimeshafika katika hoteli ya Chapachapa”
 
“Umepewa chumba?”
 
 
ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu nini kitatokea baada ya kuwasili Harare na kutinga katika hoteli

No comments:

Post a Comment