Friday, April 7, 2017

SIMULIZI, NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 6

SIMULIZI
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 6
 
ILIPOISHIA
 
Wakati namaliza kunywa ile soda nikaona lile gari likisimama kando ya hoteli akashuka dereva wa gari hilo na mtu mwingine aliyekuwa amevaa suti nyeusi. Pia alishuka msichana.
 
Watu hao watatu wakaingia katika eneo la hoteli. Kitu ambacho kilinishitua na kunipa mshangao ni kuwa yule msichana  alikuwa ndiye yule muuaji wa Isaac Chusama aliyekuwa akitafutwa na polisi kule Zimbabwe.
 
Kwa kweli nilipomuona kwa mara nyingine nilishituka sana. Yule msichana aliketi katika meza iliyokuwa mbali na meza yangu. Dereva wa lile gari pamoja na yule mtu mwingine wakaja katika meza niliyokuwa nimeketi.
 
“Mgeni mwenyewe ni huyu hapa” Yule  dereva akamwambia yule mtu ambaye alinipa mkono kunisalimia.
 
Baada ya kusalimiana naye alikaa kwenye kiti akanitambulisha kuwa yeye ndiye Benjamin Muhoza niliyekuwa ninawasiliana naye.
 
Na mimi nikamtambulisha jina langu na kumueleza kuwa nilikuwa mjukuu wa marehemu babu yangu mzee Fumbwe Limbunga.
 
SASA ENDELEA
 
“Nimefurahi kukufahamu. Uliniambia kuwa ungekuja na hati zote za marehemu Limbunga zilizohusu biashara yetu na pia hati ya mahakama inayokuthibitisha kuwa wewe ndiye mrithi wa marehemu” Mtu huyo aliniambia kwa sauti tulivu.
 
“Nimekuja na hati zote”
 
“Nitolee”
 
Nikafungua mkoba wangu ambao nilikuwa nimeuweka juu ya meza, nikatoa hati mbalimbali. Kwanza nilimuonesha cheti cha kifo cha mzee Fumbwe Limbunga akakitazama kwa makini.
 
Kisha nilimtolea hati ya mahakama iliyonithibitisha mimi kuwa mrithi wa Fumbwe limbunga. Hati hiyo niliiwekea picha yangu kama mrithi na picha ya marehemu kama mrithiwa.
 
Muhoza aliitazama hati hiyo kwa unagalifu.
 
Nilimuachia sekunde thelathini ili amalize kuisoma hati hiyo iliyokuwa imeandikwa kwa kingreza kisha nikamtolea mkataba  ambao aliwekeana saini yeye na babu.
 
Alipouona ule mkataba alinitazama akatingisha kichwa chake kuonesha kunikubalia.
 
“Nafikiri nimeweza kukuthibitishia” nikamwambia wakati akiupekua ule mkataba.
 
“Hakuna tatizo. Nimeona hapa kuwa mzee Fumbwe amefariki na wewe ndiye mrihi wake ambaye unapaswa kulipwa madeni ya marehemu”
 
Aliponiambia hivyo alinyamaza kimya kwa sekunde kadhaa kabla ya sauti yake kusikika tena.
 
“Hivi unaiendeleza ile biashara ya marehemu babu yako?”
 
Nikatikisa kichwa.
 
“Hapana. Ile biashara ilikuwa ni yake mwenyewe. Mimi sikuhusika nayo”
 
“Huwezi kuyapata yale madini ya Tanzanite?”
 
“Sijui marehemu alikuwa akiyapata wapi”
 
“Na hakuna mtu yeyote unayenfahamu anayefanya biashara ile huko Tanzania?”
 
“Labda nikuulizie halafu nikufahamishe kwenye simu”
 
Nilipomwammbia hivyo mtu huyo alinyamaza tena kama aliyekuwa akiwaza.
 
Baada kimya cha sekunde kadhaa aliniambia.
 
“Sasa sikiliza, nipe  muda niweze kukutayarishia pesa zako”
 
“Muda gani?” nikamuuliza.
 
“Muda wa siku moja tu, yaani kesho asubuhi ninakupatia pesa zako uende zako”
 
“Naweza kusubiri mpaka kesho. Hata hivyo nisingeweza kuondoka leo”
 
“Sawa. Nimekuchukulia chumba hapa hoteli, utakula, utakunywa. Gharama ni juu yangu. Wewe hutalipa chochote hadi hapo kesho tutakapomalizana mimi na wewe”
 
“Sawa”
 
“Nitakufuata kesho saa tatu”
 
Aliniambia na kuinuka kwenye kiti. Tukaagana kisha akaondoka pamoja na dereva wake. Walikwenda kwenye ile meza aliyoketi yule msichana. Yule mtu alikaa kwenye kiti lakini dereva wake aliondoka.
 
Niliona wakiagiza vinywaji. Wakaendelea kunywa na kuzungumza kwa karibu masaa matatu kabla ya kuondoka.
 
Kitu ambacho kilitia shaka katika moyo wangu ni kuhusu yule msichana muuaji ambaye alidaiwa kumuua mtu kule Zimbabwe na hatimaye kuibukia hapo Botswana.
 
Nilijiuliza yule msichana ni nani na ni kwanini alipotoka kumuua Chusama, mtu ambaye nilikuwa na mipango naye, amekwenda huko Boswana kwa mtu mwingine ambaye pia nilikuwa na mipango naye.
 
Nikaendelea kujiuliza iwapo Muhoza alikuwa na uhusiano na yule msichana na kama alikuwa anajua kama msichana huyo alikuwa anatafutwa na polisi wa Zimbabwe kwa mauaji.
 
Kusema kweli sikupata jibu licha ya kujiuliza maswali kadhaa kichwani mwangu.
 
Mwenyeji wangu alipoondoka na yule msichana na mimi niliondoka na kwenda chumbani kwangu. Nikajilaza kwenye kitanda huku mawazo yangu yakiwa kwenye utajiri.
 
Nilijiambia ingawa nilizikosa pesa a Chusama baada ya kuuawa, nitaziata pesa za Muhoza ambazo nikichanganya na pesa nitakazopata kutoka kwa Dube wa Afrika Kusini nitakuwa tajiri.
 
Nikajiwazia mipango ya maendeleo. Nilijiambia nitakaporudi Tanzania nitanunua gari la kifahari pamoja na kuanzisha miradi mikubwa ya biashara. Baada ya hapo nitatafuta mke nioe.
 
Wakati nikiwaza hayo nilisikia mlango ukibishwa, nikainuka na kwenda kuufungua. Niliona wasichana wawili waliokuwa wamejipodoa huku nyuso zao ziking’ara kwa mkorogo.
 
Walikuwa  wamesimama kando ya mlango wakiwa wamevaa nguo fupi huku matiti yao yaliyokuwa yametuna kama mipira yakiwa nusu nje.
 
“Naweza kuwasaidia? Nikawambia.
 
Walinisalimia kwa heshima na kuanza kujitambulisha majina yao  lakini sikujua mara moja kitu walichokuwa wanahitaji.
 
Nikawambia kuwa nimefurahi kuwafahamu. Mmoja wapo akaniuliza jina langu. Nikamtajia.
 
 
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu nini kitatokea hapo baada ya wasichana wawili warembo kuingia ndani ya chumba, Usikose

No comments:

Post a Comment