ZULIA LA FAKI, 0655 340572
NILIKIONA CHA MTO URITHI
WA BABU 11
ILIPOISHIA
“Mbona umekimbia?” Sauti ya
msichana ikaniuliza.
“Hebu niambie ukweli wewe ni
nani?” nikamuuliza.
“Kama ulikuwa hunijui kwanini
umenikimbia?”
“Nimekukimbia kwa sababu”
“Sababu gani?”
“Wewe si nilikukuta Botswana
siku chache ziliopita halafu nikakuona tena Zimbabwe na jana ulikuwa Afrika
Kusini?”
“Kumbe umenikariri vizuri”
“Nimekukariri kwa sababu
nimeona kila nchi niliyokwenda nilikuwa nakuona”
“Ndiyo sababu nilitaka
kukutana na wewe”
“Kwani wewe ni nani?
Unamjuaje marehemu babu yangu na umenijuaje mimi?”
SASA ENDELEA
“Sasa hayo ndiyo mambo ambayo
tutazungumza tutakapokutana”
Nikatikisa kichwa changu
ingawa niliyekuwa nikizungumza naye hakuwa karibu yangu.
“Hilo la kukutana na wewe
litakuwa gumu kidogo”
“Hutaki kujua zilipo
mali za marehemu babu yako”
“Ninataka sana lakini kuna
mambo ambayo yamenishitua”
“Niambie ni mambo gani?”
“Kuna watu ambao ulikuwa
karibu nao. Hao watu waliuawa katika mazingira ya kutatanisha”
nikamwambia.
“Wapi huko?”
“Botswana, Zimbambwe na
Afrika Kusini”
“Umetaja lakini bado mmoja”
“Abdul Baraka wa Mbezi hapa Dar aliuawa pia”
“Waliuawa na nani?”
“Nilikuona wewe na Abdul
Baraka mkishuka kwenye ndege kutoka
Afrika Kusini”
“Swali nililokuuliza, wameuawa na nani?”
Hapo niligwaya kujibu.
Niliona kama nitamwambia aliwaua yeye anaweza kukasirika
na akajua kuwa nina ushahidi kuwa yeye
nndiye muuaji. Akipata uhakika huo nilihofia kuwa anaweza kunisaka kwa udi na
uvumba ili aniue.
Nikamuuliza. “Uliponiambia bado mmoja ulikuwa na maana
gani?”
“Nilikuwa nina maana
unayoijua wewe”
“Mimi sijui kitu”
“Haiwezekani kuwa hujui kitu.
Usingeniambia kuwa kuna watu walikuwa karibu na mimi na wameuawa. Ulikuwa na
maana gani?”
“Usinielewe vibaya. Nilimaanisha
hao watu walikuwa na wewe kabla ya
kuuawa”
“Hao watu wanakuhusu?”
“Walikuwa wakidaiwa na marehemu babu yangu”
“Tunarudi pale pale katika
mali ya marehemu babu yako. Bado hutaki kujua kile kilicho nyuma ya pazia”
“Ninataka”
“Sasa naomba kukutana na wewe
kwa mara nyingine”
Nikafikiri kidogo kisha
nikamwambia.
“Kwanini tusizungumze kwenye
simu?”
“Hatuwezi kuzungumza kwenye
simu kila kitu. Kuna
maongezi mengine ni lazima tukutane mimi na wewe”
“Ungejitambulisha kwanza ili
niweze kukujua vizuri, wewe ni nani
na unamjuaje babu yangu?”
“Sasa ili unijue vizuri mimi,
nitakuelekeza mahali ambapo utapata habari
zangu kikamilifu na tutaweza kuonana mimi na wewe”
“Nielekeze ni mahli gani??”
Msichana akanielekeza mtaa
mmoja ulioko eneo la Mwananyamala. Pia akanitajia namba ya nyumba.
“Ukifika uliza Sharif Nasri”
akaniambia.
“Huyo Sharif Nasri
ni nani?”
“Ni baba yangu”
“Umeniambia wewe unaitwa nani?”
“Naitwa Ummy Sharif Nasri”
“Wewe ni sharifu?”
“Hilo ni jina tu”
“Kwa hiyo kama nitampata huyo
mzee nimuulize kuhusu wewe?”
“Ndiyo muulize na mimi
utanipata hapo hapo”
“Sawa. Nitafanya hivyo”
“Basi nakutakia mchana mwema”
Msichana akakata simu.
Aliniacha na mawazo
yaliyochanganyika na fadhaa. Nilijiuliza maswali mengi sana yaliyokosa majibu.
Imani niliyokuwa nayo ni kuwa
huyu msichana ndiye aliyewaua wale watu niliowafuata kule
Botswana, Zimbbabwe na Afrika Kusini. Na ndiye pia aliyemuua Baraka Abdul
aliyeuawa nyumbani kwake Mbezi.
Kama kweli ndiye aliyewaua,
ilikuwa ni lazima niwe na hofu naye na ni lazima nishuku kuwa pengine
alitaka kuniua na mimi ingawa sababu za kufanya mauaji hayo nilikuwa
sizijui.
Sasa kwa kunielekeza kwa mtu
mwingine ambaye aliniambia ni baba yake, alizidi kunichanganya. Nilijiuliza
huyo mtu atanieleza nini kuhusu msichana huyu aliyeonesha kila dalili ya kupata
mafunzo ya uuaji.
Nikaendelea kujiuliza, huyo
mzee anajua nini kuhusu watu hao waliouawa
na mwanawe na anajua sababu za mauaji hayo?
Au mzee huyo anamjua babu yangu au ananijua
mimi?
ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu nini kitatokea,
No comments:
Post a Comment