Tuesday, December 30, 2014

HIFADHI YA TAIFA MKOMAZI YAKABIDHI JENGO LA MAMA NA MTOTO LENYE THAMANI YA MILIONI 81 SAME

Kumekucha blog

Same,MKUU wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, amewataka wakazi wanaokaa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuacha kushirikiana na majangili na badala yake wawafichue vyenginevyo atakaebainika kufanya hivyo atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mheza kata ya Maore wakati wa kukabidhi mradi wa jengo la wodi ya mama na mtoto lililojengwa na Hifadhi ya Taifa Mkomazi(Tanapa), Kapufi amesema Serikali imejipanga kukabiliana na ujangili ndani ya hifadhi hiyo.

Amedai kuwa ziko taarifa za baadhi ya watu kuwahifadhi na kuficha taarifa za majangili ndani ya hifadhi hiyo na hivyo kuwataka kuacha kufanya  mara moja vyenginevyo wanaweza kujikuta wakikabilia na mkono wa sheria.

“Ndugu zangu  munaokaa ndani na nje ya hifadhi ya taifa ya Mkomazi tuache kuwalinda majangili wanaotumalizia rasilimali zetu----tukiwalinda watatumalizia vivutio vyetu na watalii hawatakuja na tutakaoathirika ni sisi” alisema Kapufi

“Hifadhi ni ya kwenu ninyi wenyewe na matunda yake ni kama haya ya leo---kama sio hifadhi ya taifa mkomazi jambo hilo lisingekuwepo na taarifa nilizonazo ni kuwa kuna mengi wamewafanyia” alisema

Akizungumzia baadhi ya watu kuchimba madini na kukata miti ndani ya hifadhi hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amekemea vikali na kusema Serikali imejipanga kukabiliana na jambo hilo na kuwataka kuacha mara moja.

Alisema  vitendo hivyo vinachangia kuwakimbiza wanyama na mvua kunyesha na kusema kuwa hakikubaliki na operesheni ya kulikomesha jambo hilo litaanza mara moja ikiwa ni kuzilinda rasilimali za nchi.

Awali akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Donat Mnyagatwa, alisema mradi huo hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya shilingi milioni 81 ikiwa wananchi wamechangia milioni 24.

Alisema mradi wa jengo la wodi ya mama na mtoto limekuja baada ya hifadhi hiyo kuona kero wanayoipata wakazi wa vijiji vya Mheza na Maore pamoja na vijiji jirani.

“Sisi Mkomazi baada ya kuona kero ya wananchi wanayoipata wenzetu mama wajawazito tukaona ni vyema tutawapunguzia usumbufu wa kufuata huduma masafa marefu kwa kujenga kituo hapa Maore” alisema Kapufi

Alisema mradi wa jengo hilo litakuwa msaada mkubwa kwa wakazi hao na vijiji vya jirani kwani kwa muda mrefu walikuwa katika adha na mateso na hivyo kuwataka kulitunza ili kuwa mkombozi kwa mama wajawazito na watoto.

                                  Mwisho

No comments:

Post a Comment