Wednesday, December 31, 2014

KISIWA CHA HARISHI (23)

HADITHI
 
KISIWA CHA HARISHI (23)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Kile kitendo cha kutoniona mimi inawezekana kilimpa hisia kuwa na mimi nilikuwa nimeuawa kama Shazume. Tatizo ni kuwa mwili wangu hakuuona. Bila shaka alitoka nje kuutafuta mwili wangu.
 
Alisimama mbele ya ile nyumba akaangalia kila upande kisha akarudi tena mle ndani. Mimi nikashuka kwenye ule mti.
 
Yasmin alipotoka tena akanikuta nimesimama mbele ya mlango. Akashituka na kuniuliza. “Ulikuwa wapi?”
 
“Nilikuwa nimepanda juu ya huu mti” nikamjibu.
 
Akaja kunikumbatia kifuani kwangu. Kumbe alikuwa analia. Nilipoona analia na mimi nikaanza kulia. Kama Yasmin alikuwa anaona uchungu jinsi tulivyokuwa tunauliwa na Harishi, mimi niliona uchungu nilipowaza nitakavyouliwa na Harishi hapo kesho.
 
“Buriani Yasmin, ndio tunaagana. Kesho hatutakuwa pamoja tena. Shazume ametutangulia leo” nikamwambia Yasmin.
 
Yasmin akajifuta machozi yake na kunitazama.
 
“Wewe hutaniacha, kama ni kufa tutakufa sote. Mwili wangu utalala juu ya mwili wako” Yasmin akaniambia kwa sauti nzito lakini ya kijasiri.
 
Akaongeza. “Ili uamini kuwa wewe utakufa na mimi turudi kule kule kwenye lile jumba,hatuna sababu yoyote ya kujificha. Akija Harishi nitamwambia atuue sote, Anitangulize mimi kisha wewe”
 
SASA ENDELEA
 
“Twende!” nikamwambia Yasmin bila kusita.
 
Yasmin akanishika mkono tukatembea kuelekea katikalile jumba. Hatukuzungumza kitu tena mpaka tulipofika katika jumba hilo Yasmin aliniuliza.
 
“Utakunywa uji?”
 
“Sitakunywa” nikamjibu kwa mkato
 
“Kwanini?”
 
“Roho yangu imefadhaika sana”
 
“Hata roho yangu imefadhaika lakini kama wanipenda tunywe kidogo”
 
Ilikumridhisha Yasmin nilimkubalia. Yasmin aliniacha ukumbini akaenda jikoni. Baaada ya muda kidogo alikuja na vikombe viwili vilivyojaa uji wa ngano uliotiwa asali.
 
Alinipa kikombe kimoja kisha aliketi nami.
 
“Yasmin kweli tumeshindwa kuondoka kwenye kisiwa hiki cha mauti” nikamuuliza Yasmin
 
“Tutaondokaje wakati tumezungukwa na bahari na hatuna chombo!”
 
“Nashangaa kwamba hakuna wavuvi wanaokuja katika kisiwa hiki!”
 
“Hiki kisiwa kiko mbali na pia kinajulikana. Hakuna wavuvi wanaoweza kufika hapa”
 
“Chombo chetu kilipotuharibikia tulipokiona kisiwa hiki tulidhani tumeokoka kumbe tumekuja kuangamia”
 
“Hata kama msingekiona hiki kisiwa pia mngeangamia. Mngekula nini? Mngekufa kwa njaa”
 
“Mimi naona bora kufa kwa njaa kwa sababu njaa itakuwa imekulevya, hutajijua. Kuliko kusubiri….” sikumalizia sentensi yangu.
 
Niliona nilikuwa najikumbusha kifo kibaya cha kutobolewa utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na ubongo1.
 
Siku zote tulizokaa hapa kisiwani niliweza kujikaza na kuondoa hofu licha ya wenzangu kuendelea kuuawa lakini kwa siku ile ambayo nilibakimimi na Yasmin peke yetu, sikuweza kuzuia hofu yangu.
 
Mawazo ya kifo cha kutobolewa utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na ubongo yalikuwa yametawala akili yangu.
 
“Harishi ni kiumbe na sisi ni viumbe. Huwezi kujua Mungu amepanga nini” Yasmin akaniambia.
 
“Namuamini Mungu na simkatii tamaa”
 
“Hapo umezungumza kitu cha maana sana. Haifai kukata tama. Nimeshakwambia kama ni kufa leo tutakufa sote. Na mimi ndio nitakufa kwanza”
 
“Unataka tuendelee kukaa humu hadi usiku”
 
“Ndiyo. Unafikiri utakwenda wapi?”
 
“Sioni pa kwenda”
 
“Basi tukae tu humu”
 
“Harishi akija atukute pamoja?”
 
“Ndiyo”
 
“Aniue mbele yako!”
 
“Hapana. Ataniua mimi kwanza”
 
“Mimi sipendi nikusababishie kifo, niache nife mwenyewe”
 
“Na mimi sitapenda nikusababishie kifo”
 
“Wewe hutanisababishia kifo, ni Harishi”
 
“Sikiliza kaka yangu. Sisi tukae hapa hadi usiku.Litakalotokea lolote na litokee lakini kama ni kufa nitatangulia mimi”   
 
Nilimuangalia tu Yasmin, sikumjibu kitu tena. Nikaendelea kunywa uji huku nikiwaza kama ni kweli alikuwa amejitolea nafsi yake kwa ajili yangu.
 
Maneno yake yalionesha alichokuwa akisema kilikuwa na udhati.
 
Hata hivyo niliwaza kuwa msimamo wa Yasmin haukuwa na msaada wowote kwangu zaidi ya kuonesha upendo. Ulikuwa msimamo wa kukata tamaa na haukuwana maana.
 
Atangulie yeye kufa halafu nifuatie mimi? Maana yake ni kuwa sote tutafikwa na mauti. Jambo hilo kwangu lilikuwa tishio ingawa yeye aliona lilikuwa la kijasiri.
 
Jambo la maana lilikuwa kupata wazo la kutunusuru sote na sio tufe sote.
 
Tulibaki kimya tukinywa uji. Uji huo niliunywa kwa kujilazimisha ili kumridhisha Yasmin. Kama ningekuwa peke yangu ningebaki na njaa hadi mauti yatakaponikuta.
 
Nilipomaliza kikombe changu cha uji Yasmin aliniuliza.
 
“Nikutilie tena?”
 
“Umetosha’ nikamjibu.
 
Yeye pia alikuwa amemaliza uji wake akaniambia.
 
“Basi nenda ukaoge, umeshatia nguvu kidogo”
 
Pamoja na kukabiliwa na tishio hilo la kifo kusema kweli nilihitajika sana kuusafisha mwili wangu. Nilikuwa nimechafuka sana na nilikuwa sijaoga kwa siku tatu.
 
Niliona aibu kumwambia Yasmin kuwa sitaoga. Nikainuka.
 
Yasmin akanipeleka bafuni kisha akaondoka. Nilioga haraka haraka. Nilipomaliza niliondoka bafuni na kumbishia Yasmin mlango.
 
Yasmin alinifungulia mlango na kuniambia.
 
“Karibu”
 
Niliingia mle chumbani alimokuwa. Hamkuwa na kiti. Akaniambia.
 
Kaa kitandani”
 
Nikakaa.
 
“Unajisikia vizuri kidogo?” akaniuliza.
 
Nilijaribu kutabasamu bila kufanikiwa. Niliishia kubenua midomo tu, uso haukukunjuka.
 
ITAENDELEA KESHO, USIKOSE
 
 
 

No comments:

Post a Comment