Friday, December 26, 2014

KISIWA HARISHI (19)

HADITHI
 
KISIWA CHA HARISHI (19)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Nilipofika katika ile nyumba niliwakuta wenzangu tayari wameshaanza kupata wasiwasi.
 
“Ilibaki kidogo tu tukufuate kwa maana tuliona unachelewa” Haji akaniambia.
 
“Mlijua na mimi nimeshakwenda na maji?” nikawatania.
 
“Si ajabu. Haa tunahesabiana siku na saa tu”
 
“Tusikate tama kiasi hicho. sisi ni wanaume. Mmeshakula?”
 
“Tulikuwa tunakusubiri wewe” Shazume akaniambia.
 
“Mimi nimeshakuja. Toeni chakula tule”
 
Chakula kikatolewa. Tukakaa chini na kuanza kula.
 
Tulipomaliza kula tulikaa uani tukawasha moto na kuuzunguka. Kiza kilikuwa kimeshaingia na kulikuwa na baridi.
 
Tuliota moto hadi majira ya saa mbili usiku. Tukaingia vyumbani kulala. Usiku ule haukuwa wa mawazo sana. Nilipitiwa na usingizi mara moja.
 
Nilipoamka asubuhi nilishituka nilipoona mlango wa nje ulikuwa umeng’olewa mzima mzima. Palibaki uwazi mtupu. Mlango wa chumba alicholala Haji pia ulikuwa umeng’olewa. Mlango wa chumba cha Shazume ulikuwa mefungwa.
 
Nikaenda katika ule mlango wa chumba cha Haji na kuchungulia. Nilimkuta Haji akiwa amelala chini amekufa. Kichwa chake kilikuwa kimetobolewa kwenye utosi. Damu iliyoganda ilionekana kwenye nywele zake.
 
Hapo nilijua kuwa tulikuwa tumeingiliwa. Bila shaka Harishi alikuwa amekuja usiku akang’oa milango na kumuua Haji.
 
SASA ENDELEA
 
Lilikuwa tukio ambalo sikulitegemea. Katika kundi letu Haji ndiye aliyekuwa mdogo kuliko sote. Kifo chake kilinisikitisha na kunikatisha tamaa kabisa.
 
Nilijiambia kama Harishi ameweza kutufuata huku na kumuua Haji na sisi hatutabaki. Tilichokuwa tunasubiri ni siku na saa zetu ziwadie.
 
Baada ya kushangaa kwenye mlango kwa sekunde kadhaa nilikwenda kumgongea Shazume. Shazume akaamka na kufungua mlango.
 
“Una habari gani?” nikamuuliza nikiwa nimetaharuki.
 
“Sina habari yoyote” Shazume akanijibu huku akionesha kupata hofu.
 
“Haji ameuawa!” nikamwambia.
 
Shazume akagutuka.
 
“Haa! Haji naye ameuawa? Si tulilala naye humu ndani jana usiku?”
 
“Tazama ule mlango wa nje”
 
Nilimuonesha Haji ule mlango uliong’olewa kisha nikamwambia. “Harishi ameung’oa usiku”
 
Shazume aliutazama huku akitikisa kichwa.
 
“Ameng’oa na mlango wa chumba cha Haji” nikaendelea kumwambia.
 
Shazume akasogea kwenye mlango wa kilichokuwa chumba cha Haji. Alipoiona maiti ya Haji alishituka sana.
 
“Mimi naona hatutapona”
 
“Kupona tusitegemee ndugu yangu. Harishi ameshajua tupo hapa, usishangae kesho tukiamka mmoja wetu akawa hayupo!”
 
“Hapa nyumbani hapafai tena kukaa. Tutafute sehemu nyingine ya kujificha”
 
“Tutajificha wapi Shazume?”
 
“Popote tu, nyumba ziko nyingi”
 
“Sawa. Tumngoje Yasmin aje tumueleze kuwa mwenzetu ameuawa”
 
“Pia tumueleze kuwa tunaondoka hapa. Harishi akija tena asitukute”
 
“Sawa, tutamueleza”
 
Tukaenda kunawa uso na kusukutua maji bila kupiga mswaki. Tulikuwa tumeshachanganyikiwa. Tulipomaliza tulikaa kumsubiri Yasmin.
 
Yasmin alikuja majira ya saa tatu hivi. Hakuwa amechukua kitu.
 
Akatusalimia na kutuuliza kwanini tumeng’oa milango.
 
“Hebu chungulia kwenye hicho chumba” nikamwambia.
 
Yasmin akachungulia na kugutuka.
 
“Haji amepatwa na nini?”
 
“Haji ameuawa usiku na Harishi” nikamwambia.
 
“Mama yangu!” Yasmin alimaka huku akijishika kichwa. “Kumbe Harishi alipotoka usiku alikuja huku?”
 
“Sisi tumeona asubuhi Harishi ameuawa na milango imeng’olewa”
 
“Sasa tumepanga tuondoke hapa” Shazume akamwambia Yasmin.
 
“Muondoke muende wapi?”
 
“Twende mahali pengine. Tukiendelea kukaa hapa Harishi atakuja tena usiku”
 
“Sasa mmepanga muende wapi?’
 
“Mimi naona kama tunajisumbua, kama ni kufa tutakufa tu” nikasema.
 
“Hata kama tutakufa lakini hapa tuondoke” Shazume akasisitiza.
 
“Ni sawa. Sasa tufikirie hapo pa kwenda. Tutakwenda wapi?”
 
“Nyumba ziko nyingi”
 
“Yasmin unatushauri nini?”
 
Machozi yalikuwa yanamtoka Yasmin. Bila shaka yalimtoka kutokana na ukweli kwamba sote tutakufa. Hakunijibu.
 
“Yasmin usilie. Tunaomba ushauri wako” nikamwambia.
 
Yasmin alijifuta machozi kisha akatuambia. “Niwapeleke katika nyumba nyingine”
 
“Huko utakakotupeleka Harish hatafika?” nikamuuliza.
 
Yasmin akaguna kisha akajibu. Hatafika”
 
Nilijua alitujibu hivyo kututia moyo tu lakini mawazo ya Shazume yalikuwa tofauti.
 
“Ni mahali gani?” Shazume akamuuliza haraka.
 
“Kwanza twendeni mkanywe uji”
 
“Turudi kule tena?” Shazume akamaka.
 
“Mnakunywa uji tu halafu tunaondoka”
 
Shazume akanitazama.
 
“Mimi sitakwenda”
 
“Si tunakwenda kunywa uji tu” nikamwambia.
 
“Kwanza Harishi hatakuja muda huu” Yasmin akasema.
 
“Mimi sitaki uji”
 
“Utashinda hivyo hivyo na njaa?” Yasmin akamuuliza.
 
“Sioni njaa na ile hamu ya kula pia sina”
 
“Kama tumeandikiwa kuuawa tutauawa tu Shazume hata kama hutakula, ni bora ule tu” nikamwambia Shazume.
 
ITAENDELEA KESHO. TUMA MAONI YAKO KUHUSU HADITHI HII KWA NAMBA 0655 340572

No comments:

Post a Comment