Monday, December 29, 2014

KISIWA HARISHI

KISIWA CHA HARISHI (21)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Yasmin naye akaomba dua.
 
Kwa muda wa nusu saa hivi mahali hapo pakawa kama madarasa kutokana na kurindima visomo vyetu vya dua.
 
“Pia tungekuwa tunaswali” Shazume akatukumbusha.
 
Sikuzote binaadamu humkumbuka sana mola wake pale anapofikwa na matatizo. Siku zote hizo tulikuwa hatukumbuki kuswali ila ni kwa siku ile ambayo tuliona tutamalizika.
 
“Pia ilitakiwa leo tufunge” na mimi nikawakumbusha.
 
“Ni kweli” Shazume akanikubalia na kuongeza “Lakini tumeshakunywa uji”
 
“Kama tutanusurika leo tutafunga kesho. Umesikia Yasmin?”
 
“Nimesikia” Yasmin akanijibu.
 
“Sasa sisi hatuko tohara, tutaswali vipi?’ nikawauliza wenzangu.
 
“Twendeni tukaoge baharini tujitoharishe” Shazume akasema.
 
“Hizi nguo zetu pia hazina tohara”
 
“Tuoge na nguo zetu ziweze kutoharika, zikikauka tutaswali”
 
Tukakubaliana.
 
 SASA ENDELEA
 
Tukaamua sasa twende baharini tukaoge. Tukaenda sote watatu, mimi, Shazume na Yasmin. Yasmin alipotuona sisi tunajitosa kwenye maji na yeye akajitosa. Tukawa tunaoga na kuogelea pamoja.
 
Tuliendelea kukaa kwenye maji kwa muda kidogo ili kujisahaulisha matatizo yaliyokuwa yanatukabili.
 
Asubuhi ile maji yalikuwa matamu kwa mtu ambaye alikusudia aogelee kwa starehe ila kwa sisi ilikuwa starehe ya kujilazimisha. Mawazo mabaya yalituepuka kwa muda yakitusubiri tumalize kuogelea.
 
Tulitamani tusitoke ndani ya maji lakini nilipomuona Yasmin aliyekuwa akiogelea karibu yangu anarudi ufukweni na mimi nikaamua kurudi.
 
Tukakaa ufukweni na kumsubiri Shazume. Naye alipotuona tumerudi ufukweni akatufuata.
 
Tukakaa kuota jua. Nguo zetu zilikuwa zimetota. Kitendo cha kuogelea na nguo zetu hakikuwa cha maana sana kwani mzizimo ungeweza kutuletea madhara ya kiafya lakini hatukuwa na la kufanya.
 
Yasmin ambaye alikuwa na nguo za kubadili alizokuwa akiletewa na Harishi alikuwa akifuata mkumbo tu, haikumpasaaloweshe nguo zake ila alipotuona sisi tunaoga na yeye akajitosa.
 
Tulikaa kwa muda kwenye ufukwe tukiangalia bahri na ndege waliokuwa wakiruka ruka. Ili miiliyetu isisinyae tuliamua kufanya mazoezi ya kukimbizana.
 
Tulikimbizana mpaka tulipochoka tukarudi kwenye ile nyumba. Tukapanga kwamba itakapofika sa saba tuanze kuswali swala ya adhuhuri. Yasmin alituaga akatuambia kuwa anakwenda kupika chakula cha mchana.
 
Kwa mustakabali wetu tatizo la chakula halikuwepo. Chakula kilikuwepo kwa Yasmin. Tatizo lilikuwa ni la kuuliwa na Harishi. Kama si tatizo hilo mahali pale pangekuwa ni pazuri pa kuishi. Sikuvutika na kisiwa hicho pekee bali pia nilivutika na Yasmin. Nilifarijika sana kuona jinsi alivyokuwa akitupa moyo na matumaini japokuwa hali ilikuwa tete.
 
Baada ya Yasmin kuondoka tuliendelea kukaa, hatimaye tukapitiwa na usingizi.
 
Tulipokuja kuamka yalikuwa majira ya saa nane. Tukaenda kutawadha kwenye maji ya bahari na kuswali swala ya adhuhuri.
 
Yasmin alikuja saa tisa akiwa amechukua kapu la chakula. Alikuwa amebadili nguo zake na kuvaa mavazi mengine.
 
“Mmepauka kwa chumvi. Mnasikitisha sana kaka zangu” akatuambia.
 
“Ndiyo hivyo, tutafanyaje sasa” nikamwambia huku nikimpokea lile kapu.
 
“Mmeshaswali?” akatuuliza.
 
“Tumeswali na wewe umeswali?” Na mimi nikamuuliza.
 
“Mimi naswali kila siku kuomba nusura na kuwaombea na nyinyi. Sijui kama nyinyi mmekumbuka kuniombea”
 
“Tumekuombea” nikamdanganya. Tulikuwa tumemsahau.
 
“Mngesema mmesahau kuniombea ningejua hamnipendi”
 
“Tunakupenda sana. Umetuletea chakula gani?”
 
“Wali”
 
“Roho zetu zimekinai, hatutamani hata kula” Shazume akasema.
 
“Shazume unaanza maneno yako!” Yasmin akamwambia Shazume.
 
“Unafikiri nakudanganya, mimi sina hamu ya kula kabisa”
 
“Mbona juzi na jana ulikuwa unakula?”
 
“Nilikuwa na matumaini”
 
“Si vizuri hivyo. kuleni japokuwa kidogo mpate nguvu. Mkiacha kula mtakuwa mnajitesa wenyewe. Mimi pia sikula. Nimekuja huku nile na nyinyi”
 
Yasmin alitoa kile chakula akakiweka chini. Akatoa tasa la maji tukaosha mikono kisha tukaanza kula.
 
Mimi pia sikuwa na hamu ya kula lakini nilikula kumridhisha Yasmin.
 
Tuliendelea kula kidogo kidogo hadi Shazume alipomuuliza Yasmin.
 
“Yasmin ukibaki peke yako itakuwaje?”
 
“Hatuombei hivyo, tuombee tubaki sote. Ukiomba dua uweke matumaini, isiwe unakata tama”
 
“Ni kweli Yasmin huwezi kuomba kitu bila kukiwekea matumaini. Kama huna matumaini na kitu hicho kwanini unakiomba?” nikasema.
 
Shazume akaguna.
 
“Pamoja na kuomba kwetu bado naona wakati wetu umekaribia sana” Shazume akasema kwa hali ile ile ya kukata tama.
 
“Shazume usiseme hivyo, mnaweza kunusurika. Harishi ni kiumbe kama nyinyi”
 
“Lakini mwenzetu amepewa uwezo”
 
yasmin naye akaguna. Pakawa kimya. Yasmin ndiye aliyeutanzua ukimya huo alipotuambia. “ Jamani tukinusurika nitawachukua Comoro. Nitamwambia baba yangu nyinyi ni ndugu zangu wa damu. Mtaenziwa kama watoto wa rais”
 
ITAENDELEA KESHO USIKOSE NI KITATOKEA

No comments:

Post a Comment