Thursday, December 25, 2014

KISIWA HARISHI



HADITHI
 KISIWA CHA HARISHI (18)
 ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA

Yalipofika majira ya saa kumi na mbili jioni Yasmin akaja.Alikuwa ametuletea chakula cha jioni. Ulikuwa ni wali ule ule tuliokula mchana. Tukakiweka chakula hicho kusubiri usiku.

Yasmin akataka nimsindikize arudi. Nikawambia wenzangu “Namsindikiza Yasmin”

“Usije ukachelewa kurudi. Kumbuka usiku umekaribia” Shazume akaniambia.

“Sitachelewa” nikamjibu.

Tukaondoka na Yasmin. Tukiwa njiani Yasmin alinitazama machoni mwangu kisha akaniambia.”Nimefurahi sana leo kuwa peke yetu mimi na wewe”

“Kwanini?” nikamuuliza.

“Tangu juzi hatujapata nafasi ya kuwa pamoja peke yetu. Mara nyingi unakuwa na wenzako. Jana jioni nilitaka kukwambia nisindikize lakini marehemu Masudi akawahi yeye. Sikuweza kumkatalia. Najua roho ilikuuma na mimi pia iliniuma” Yasmin akaniambia.

“Unajua jana niliwafuatilia nikawakuta mnafukuzana ndani. Kuna wakati marehemu alikushika kiuno mkaanguka chini pamoja”

Nilipomwambia hivyo Yasmin alinywea.

“Kumbe ulikuja kutuchungulia?” akaniuliza.

“Nilikuja, nilipouona mchezo wenu nikaamua kurudi”

SASA ENDELEA

“Si mchezo wetu. Masudi ndio alikuwa analazimisha. Alikuwa akinitaka kimapenzi nikamkatalia” Yasmin aliniambia.

“Basi tusimseme sana kwa sababu ameshakufa lakini nilishituka”

“Naomba unisamehe kwa hilo kama limekuudhi”

Nikanyamaza kimya.

“Umeshanisamehe?” Yasmin akaniuliza huku akinitazama machoni mwangu. Alinitazama kwa macho ya huruma sana.

“Kwani wasiwasi wako ni wa nini?”

“Nataka unisamehe!” Yasmin akasisitiza.

“Nimekusamehe”

“Sasa tusizungumze tena habari hiyo. Tuzungumze yanayotuhusu mimi na wewe. Kama tutafanikiwa kuondoka katika kisiwa hiki utanioa?”

“Wewe ndio uniambie mimi kama utakubali kuolewa na mimi”

“Mimi niko tayari hata sasa hivi”

“Unadhani wazazi wako watakubali?”

“Watakubali”

“Ujue kuwa wewe ni binti wa rais na mimi ni mtoto wa kimasikini”

“Kusema hivyo si sahihi. Sasa hapa tulipo mimi na wewe tuna tofauti gani?”

“Kwa hapa tuko sawa ila ukirudi kwenu wewe utakuwa mwana wa rais”

“Huo ni ufinyu wa mawazo ya binadamu. Binaadamu wote ni sawa. Mfano halisi ni wa hapa tulipo. Umesema tupo sawa, basi tutakuwa sawa popote. Hata kama wewe ni mtoto wa kimasikini lakini nimekupenda, utakataa?”

“Labda wewe unikatae mimi”

“Una majibu yasiyoniridhisha. Kwanini huniambii kuwa unanipenda na utanioa. Mimi nataka utamke hivyo”

“Nimekupenda na nitakuoa”

Yasmin nilipomwambia vile alitabasamu. Nilihisi alikuwa akijaribu kuufariji moyo wake uliokosa mapenzi kwa muda mrefu.

“Yasmin unaweza kusema maneno hayo hapa kwa vile hatuna matumaini ya kupona. Lakini kama tutafanikiwa kuondoka hapa unaweza kubadilika na kuniona mimi kama takataka”

“Nakuhakikishia kaka yangu mpenzi sitabadilika. Mimi si kinyonga”

“Tuombe tuokoke katika balaa hili lililotukabili”

“Ishaalah tutaokoka. Tena wewe ndio utaniokoa mimi”

“Sio wewe uniokoe mimi?”

“Mimi nataka wewe uniokoe mimi”

“Basi ishaala itakuwa hivyo unavyotaka”

“Nikuimbie nyimbo?”

“Niimbie”

Yasmin aliacha kutembea akasimama mbele yangu akiwa amenigeukia mimi. Kitendo hicho kilisababisha na mimi nisimame. Akapeleke mikono yake kwenye mabega yangu.

“Mimi ni nani wako?” akaniulza. huku akinitazama machoni mwangu.

“Wewe ni mpenzi wangu” nilijua kuwa alikuwa anataka jibu hilo.

Nilipomjibu hivyo alitabasamu na kuishusha mikono yake mabegani mwangu na kugeuka.

“Sasa ngoja nikuimbie” akaniambia huku tunaenda.

Akaimba wimbo mzuri kwa lugha ya Kikomoro. Wakati akiimba alikuwa akitingisha tingisha kichwa chake kufuatia mawimbi ya sauti yake. Wakati akiimba alikuwa akitia mziki kwa mdomo. Alionekana kuwa hodari sana wa kuimba na kutia mziki. Wimbo huo ulikuwa unavutia ingawa sikujua tafsiri yake.

Alipomaliza kuimba alinitafsiria kwa Kiswahili. Akaniambia “Ndege wawili dume na jike wamepotea juu ya bahari. Hawajui watokako wala waendako. Wanalia swi! swi! swi!”

“Wamesafiri mchana kutwa bila kupata mahali pa kutua. Sasa jua limekucwa na giza linaingia. Hawataweza kusafiri usiku. Wanalia swi! swi! swi!”

Japo niliufurahia wimbo huo tafsiri yake ilinisikitisha.Nikahisi kama ndege wawili hao walikuwa ni mimi na yeye.

“Kumbe Yasmin unajua sana kuimba!” nikamwambia.

“Hapana, najaribu tu”

“Si kujaribu, unajua”

“Kweli eh?”

“Umeniburudisha sana”

“Ukinioa nitakuwa nakuimbia kila siku”

Tulikuwa tumeshafika kwenye lile jumba analokaa.

Nikasimama kwenye mlango.

“Mimi sitaingia ndani” nikamwambia.

“Kwanini?” Yasmin akaniuliza.

“Si nimekusindikiza tu”

“Ukinisindikiza ndio huingii ndani, mbona siku nyingine unaingia?”

“Yasije yakanikuta yaliyomkuta Masudi”

“Mimi naamini wewe huko kama Masudi lakini kama umeamua uwahi kurudi, unaweza kurudi na nakutakia usiku mwema. Tutaonana kesho.

“Asante. Usiku mwema na kwako”

Nikamuacha Yasmin amesimama akinitazama. Mimi nikarudi kule nyumbani tulikotoka. Nilirudi kwa mwendo wa haraka haraka ili kiza kisinikute njiani kwani jua lilikuwa limekuchwa sana.

Nilijikuta nikiwa na furaha na mwenye matumaini kutokana na maneno ya Yasmin. Upendo aliouonesha kwangu ulitosha kunipa hamasa ingawa tulikuwa katika hali ngumu.

ITAENDELEA KESHO, USIKOSE KESHO KISA HIKI CHA KUSISIMUA

No comments:

Post a Comment