Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma ikiwemo Komputer na Lugha za kigeni. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 7727246
Homa ya Uchaguzi Mkuu imeifanya Chadema
kuitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu ili kujadili mambo ya kitaifa,
ikiwamo adhabu waliyopewa wabunge wa Ukawa kabla ya kutoa tamko.
Kikao hicho kilichofanyika jana, pia
kilihusisha wabunge walioadhibiwa kwa kufanya fujo bungeni wakipinga
kuwasilishwa kwa miswada mitatu ya mafuta na gesi kwa hati ya dharura na
hivyo kupewa adhabu tofauti ya kutohudhuria vikao kuanzia viwili hadi
vyote vilivyosalia.
Manaibu katibu mkuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika
(Bara) walisema kutokana na kuongezeka kwa homa ya uchaguzi, chama
hicho kimelazimika kuitisha kikao hicho na kwenda tofauti na ratiba yake
ya mwaka ili kuweka sawa baadhi ya mambo.
“Pamoja
na ratiba iliyopo, kila litakapokuwa linajitokeza jambo muhimu tutakuwa
tunaitana ili kulijadili kwa kina. Hali ya uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura Zanzibar ina ishara zote kuwa hatutakuwa na mwisho
mzuri,” alisema Mwalimu na kufafanua kuwa kikao hicho kitakuja na jibu… “Kama hali hiyo haitarekebishwa, upo uwezekano wa athari zake kufika Bara pia.”
Mwishoni mwa wiki, polisi walifyatua
risasi kwenye kituo cha kuandikisha wapigakura baada ya wananchi kwenda
eneo hilo kujaribu kuzuia kile walichokiita “wapigakura mamluki” na
kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa na baadhi yao kulazwa hospitalini.
Mwalimu alisema majibu rahisi
yanayotolewa na Serikali kuhusu vurugu hizo kuwa zinafanywa na vikundi
vya wahuni, yanatia shaka hasa kwa kuzingatia kuwa vyombo vya ulinzi na
usalama vipo na vinashuhudia mambo hayo yakitokea.
Alieleza kuwa matukio yasiyo ya kawaida
hayatokei Zanzibar pekee, bali hata maeneo mengine, akitoa mfano kwenye
uandikishaji wapigakura kwa kutumia teknolojia ya BVR ambako alisema
kuna hali inayokanganya hivyo kufanya kuwapo umuhimu kwa chama kutoa
tamko juu ya kinachoendelea.
“Wale
walioandikishwa mwanzo kwenye wilaya za Mlele mkoani Katavi na
Kilombero, Morogoro wameambiwa warudishe kadi walizopewa na waandikishwe
upya. Hii siyo hali ya kawaida na hasa inafanywa katika majimbo ambayo
ni ngome ya Chadema,” alisema na kuongeza:
“Pamoja na hayo yote, tutatangaza ushindi mapema sana wilayani Kilombero katika uchaguzi mkuu ujao.”
Kuhusu kikao hicho, Mnyika alisema
kilijadili maandalizi ya jumla ya Uchaguzi Mkuu, kupokea taarifa za
wagombea udiwani, ubunge na urais, taarifa ya majadiliano ya Ukawa
pamoja na ile ya wabunge waliopewa adhabu.
Akitoa msimamo wa awali wa chama chake,
Mnyika alisema wabunge hao walikuwa na sababu zote za msingi za kupinga
miswada hiyo na kwamba taarifa zilizoripotiwa kuwa wanatumiwa hazina
mashiko yoyote.
NIPASHE
Wapiga kura 11,248,198 kati ya milioni
22 waliotarajiwa kuandikishwa mwaka huu katika Daftari la Kudumu la
Wapiga kura nchini, wameshaandikishwa na sasa wanamiliki vitambulisho
wakisubiri kuvitumia katika uchaguzi mkuu Oktoba, 25 mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ina uhakika wa kukamilisha uandikishaji kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) mapema mwezi ujao.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Danian Lubuva,
alitoa kauli hiyo jana huko Msoga, Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani
ambako Rais Kikwete alikuwa mmoja wa wananchi wa eneo hilo waliojitokeza
kujiandikisha ikiwa ni siku ya kwanza kwa uandikishaji mkoani Pwani.
Jaji Lubuva alimueleza Rais Kikwete kuwa
licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika mchakato huo, hali ya
uandikishaji ilipofikia nchini hadi Julai 06 inaendelea vema na
matumaini ni makubwa kuwa uandikishaji ujao utakamilika mapema na
kuwafikia walengwa wote waliokusudiwa.
“Mheshimiwa
Rais, pamoja na changamoto nyingi na kelele nyingi zilizokuwa
zikisikika huku na kule, tayari tumeandikisha watu 11,248,198 mpaka jana
(juzi) kati ya lengo tulilojiwekea la kuwafikia watu kati ya milioni 21
mpaka 23, na mikoa iliyokuwa tayari imekamilisha ni 13, bado 11 ambayo
nayo nakuhakikishia itakamilisha na mapema Agosti, kazi hii
itakamilika,” Jaji Lubuva.
Baada ya kujiandikisha, Rais Kikwete
aliipongeza Nec kwa hatua iliyofikiwa hadi sasa na kuwataka wasife moyo
bali wachape kazi kikamifu ili uandikishaji ukamilike ndani ya muda na
wananchi wawe na uhakika wa kupiga kura kwa kutumia vitambulisho hivyo.
Rais Kikwete alisema changamoto ambazo
zimekuwa zikijitokeza wakati wa zuandikishaji zichukuliwe kama fursa ya
kukamilisha kwa wakati.
Rais Pia ametumia fursa hiyo kuwataka
Watanzania kujitokeza kujiandikisha ili watumie haki yao kumchagua
kiongozi wanayemtaka kuanzia diwani, mbunge na rais na kwamba
wasipofanya hivyo baadaye wasije kulalamikia viongozi watakokuwa
madarakani ambao wamechaguliwa na wenzao waliojiandikisha.
NIPASHE
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa, amesema moja ya sababu inayochangia vurugu bungeni kwa sasa ni staili inayotumiwa na kiti cha Spika wa sasa, Anne Makinda, katika kuongoza mhimili huo.
Msekwa amesema kanuni zote za Bunge zipo
vile vile tangu yeye alipokuwa madarakani na kwamba kilichobadilika kwa
sasa ni aina ya wabunge waliopo.
Hata hivyo, hakufafanua kuhusiana na
aina ya wabunge, lakini kwa sasa Bunge hilo lina idadi kubwa ya wabunge
vijana pamoja na wabunge wengi kutoka upinzani.
Aliyasema hayo juzi usiku katika kipindi
cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV na kituo
cha redio cha Redio One.
Msekwa ambaye pia aliwahi kuwa Makamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, alisema
kinacholeta mzozo ni namna kiti kinavyoongoza Bunge kwa maana ya staili
inayotumika.
Aliongeza kuwa Bunge hilo lina
mchanganyiko wa wabunge wa upinzani na CCM ambao pia wamo vijana wa
kutosha na kwamba kiti hakiwezi kuendelea kutumia staili ile ile ya siku
zote.
Msekwa ambaye pia ni Katibu wa Baraza la
Ushauri la Wazee la CCM, alikiri kwamba siku za nyuma kiti cha Spika
kilikuwa kinaheshimika tofauti na ilivyo sasa.
Mwanasiasa huyo alisema ni aibu na
fedheha kwa wabunge kusimama na kuzomea huku Spika naye akiwa amesimama
na kwamba jambo hilo halikuwapo wakati wa uongozi wake.
Alifafanua kuwa haya yanayotokea kwa
sasa yanatokana na wakati huu kuwa ni wa kizazi kipya na kwamba ili
kuongoza mhimili huo, ni lazima staili ibadilike.
Hata hivyo, Msekwa hakusema ni staili ya
namna gani itakayoweza kulibadilisha Bunge na kuondoa mizozo ambayo
imekuwa ikijitokeza mara kwa mara ikiwamo wabunge kutoka nje na kususia
vikao.
NIPASHE
Wazee wanaolipwa pensheni na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuanzia sasa watakuwa wakitumia kadi maalum kulipwa pensheni yao ya kila mwezi ili kuwalinda wasiibie fedha zao za mafao.
Hayo yalisemwa na Ofisa Operesheni wa NSSF, Joyce Mruma, kwenye Maonyesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam jana.
Alisema mfumo huo mpya utamwezesha
mzee mstaafu kupata mafao yake ya kila mwezi kupitia mashine za kutolea
fedha (ATM), na vituo vya mauzo na mitandao mingine kwa kutumia kadi
hiyo.
“Wazee
wenye pensheni ambao ni wanachama wa NSSF hawatatembea tena na pesa
mkononi. Katika mfumo wa zamani, wanachama wa NSSF wazee waliostaafu
walikuwa wanalipwa mafao yao kupitia ofisi za posta hali iliyosababisha
matatizo mengi kwa wazee hao, ikiwamo kuibiwa njiani na vibaka, lakini
sasa tumeamua kubadilisha mfumo wa zamani na kutumia mfumo wa kisasa,”.
Mruma alisema kuanzia sasa wazee
watalipwa kupitia ‘Smart Cards’ ambazo zitawawezesha kupata fedha zao
wakati wowote na mahali popote na hawatatembea tena na fedha mkononi.
Aliongeza kuwa kadi hizo pia
zitaunganishwa na mifumo ya maduka makubwa ili kuwawezesha wazee kununua
vitu na huduma mbalimbali kupitia kadi zao.
HABARILEO
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
imeiomba serikali kuu kulisuka upya jiji hilo kimuundo ili liwe na nguvu
kisheria ya kutekeleza majukumu yake, kwa kuwa hivi sasa linashindwa
kutokana na kuingilia mamlaka nyingine, hivyo linaonekana halifanyi
kazi.
Hayo yalibainishwa jana jijini hapo na Meya wa Jiji hilo, Dk Didas Masaburi
kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam,
lililokutana kwa ajili ya kuvunjwa rasmi kwa baraza hilo, kama ambavyo
sheria ya kuundwa kwake inavyoelekeza.
Katika kikao hicho kilichowakutanisha
wajumbe wa baraza hilo, Meya wa jiji hilo alisema moja ya changamoto
zinazolikabili jiji la Dar es Salaam ni muundo wake ambao kisheria
unaingiliana na mamlaka nyingine kiutendaji, hivyo kukosa nguvu ya
kutekeleza majukumu yake.
“Ni
kweli jiji letu lina tatizo la kimuundo, ambalo linasababisha jiji
kukosa nguvu za kisheria kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake na hivyo
linaonekana halifanyi kazi, ni vyema serikali ikaona sasa haja ya
kuliduka upya kimuundo”,Dk Masaburi.
Awali wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi
wa Jiji hilo, Wilson Kabwe alielezea mafanikio ya jiji hilo kwa kipindi
cha miaka mitano ya uwepo wa baraza hilo ni pamoja na ujenzi wa vituo
vya kisasa vya mabasi ya mikoani cha Mbezi Louis na Boko Basihaya pamoja
na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Aidha alisema miradi kadhaa iko kwenye
hatua za utekelezaji kama mradi wa uendelezaji makazi kwenye viwanja
vitatu tofauti katika maeneo ya Kinondoni na Oysterbay jijini hapo.
Pamoja na mafanikio hayo, Kabwe alisema
zipo changamoto kama ambavyo Meya ya jiji hilo alivyoeleza na kuongeza
kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hujikuta wakishindwa kwa kuwa
maeneo ya utekelezaji yako kwenye mamlaka nyingine kama vile Manispaa,
na wakati mwingine huitaji kibali kutoka kwenye Manispaa husika.
Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam liliundwa Januari 7, mwaka 2011.
CHAPAKAZI
Mgombea Ubunge Jimbo la Njombe Kusini, Rose Mayemba ambaye anagombea Jimbo ambalo lilikuwa la Spika Anne Makinda juzi alimkuta nyoka amejiviringisha kwenye siti ya abiria kwenye gari yake wakati akiwa Hotelini Njombe.
Nyoka huyo alikutwa kwenye siti kama
abiria anayesubiri dereva aingie awashe gari waondoke, Mbunge huyo
alikuwa kwenye Hoteli ambayo walikutana na Viongozi wa CHADEMA.
Mayemba ambaye ni
Mtunza Takwimu Mkuu wa CHADEMA Wilaya ya Njombe alisema baada ya kuingia
kwenye gari yake aina ya RAV 4 alishangaa kuona kitu kimejiviringisha
kwenye siti ya mbele.
“Nilipokiona hicho kitu wazo la haraka
nikajua ni mkanda wa abiria ambaye nilikuwa nimembeba ameusahau…
nilipoona ni nyoka anataka kujiviringisha mkononi nilitoka mbio kwenda
kuwaita wenzangu” >>> Rose Mayemba.
Mgombea Ubunge huyo amesema hajui nyoka
aliingiaje kwenye gari lake na hawezi kumlaumu mtu ila safari yake
Bungeni anamtegemea zaidi MUNGU na hatishiki na chochote.
CHAPAKAZI
Maafisa toka Mamlaka ya Chakula na Dawa
TFDA waliokuwa katika Operesheni ya kukagua maduka ya dawa katika
Manispaa ya Temeke wanadaiwa kuomba wapewe Tshs. 500,000 kutoka kwa
mmiliki wa duka ili wasilifungie duka hilo.
Mwenye duka huyo Suleiman Vuai
amesema maafisa hao walifika dukani kwake na kujitambulisha kuwa
wanatoka TFDA lakini walisema hawakutembea na Vitambulisho vyao.
Vuai anasema baada ya
kukagua duka lake walimwambia lina mapungufu ikiwemo kuiibia Serikali
Milioni nane hivyo anatakiwa atoe pesa hizo vinginevyo wanachukua dawa
zote zilizopo dukani.
Alipojibu kuwa hana kiasi hicho cha pesa
kulitokea vuta nikuvute na baadae walimtaka awape pesa ya daku kwa kuwa
wao ni Waislamu wamefunga, akawajibu kuwa hana labda awape 50,000 kama
nauli.
Vuai amesema baada ya
majadiliano maafisa hao waliondoka na kuahidi kurudi baadae kwa ajili ya
kupatiwa 500,000 na baadae wakaendelea kumpigia simu wakiulizia waje
muda gani kuchukua pesa hiyo.
Msemaji wa TFDA amesema hakuna watu walioagizwa kufanya Oparesheni yoyote na hao sio maofisa wa Mamlaka hiyo.
MTANZANIA
Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Joshua Nassar,
amenusurika kifo baada ya kupata ajali ya helkopta wakati akiwa katika
ziara kuhamasisha wananchi wa jimbo lake kujindikisha kwenye daftari la
kudumu la wapigakura.
Afisa habari wa CHADEMA Tumaini Makene
alisema ajali hiyo ilitokea jana jioni katika eneo la Leguruki na
taariza za awali ni kwambwa watu waliokuwa kwenye helkopta hiyo wamepata
majeraha madogo madogo.
Kwenye ndege hiyo walikuwepo viongozi
wengine wa ngazi ya jimbo ambapo wao pamoja na Nassari walipelekwa
hospitali ya Seliani kwa matibabu zaidi.
Taarifa zinasema helkopta hiyo ambayo inamilikiwa Mbunge Philemon Ndesamburo inasemekana chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali.
Kwa habari ,matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment