Monday, July 13, 2015

HADITHI NILIJUA NIMEUA SEHEMU (6)

HADITHI
 
NILIJUA NIMEUA 6
 
ILIPOISHIA JANA
 
Alipokubali kima changu nilifungua  gari nikashuka.
 
“Una kamba?” nikamuuliza.
 
“Kamba sina’
 
Nilikuwa na kamba ya akiba kwenye boneti la teksi yangu. Nilikwenda nyuma ya gari, nikafungua boneti na kutoa kamba. Nikaiweka chini.
 
Kisha niliisogeza teksi mbele ya gari la mtu huyo lililokuwa pembeni. Nikashuka tena na kufunga ncha moja ya kamba nyuma ya gari langu na ncha nyingine nikaifunga mbele ya lile gari. Nilipomaliza nilimwambia mtu huyo ajipakie kwenye gari lake.
 
Wakati anajipakia na mimi nilikwenda kwenye mlango wa teksi nikaufungua na kujipakia. Nilitia gea na kuiondoa teksi taratibu. Kamba ilinyooka na kukaza kabla ya kuanza kulivuta gari la nyuma.
 
Niliingia barabarani nikawa naendesha taratibu. Kwa vile niliendesha kwa mwendo mdogo tulifika Bombo saa kumi na mbili asubuhi.
 
Nilishuka kwenye teksi nikaifungua ile kamba na kuiweka kwenye boneti.
SASA ENDELEA
 
“Nakushukuru sana” Mtu huyo akaniambia baada ya kushuka kwenye gari lake.
 
Alitoa pochi mfukoni akaifungua na kutoa noti mbili za elfu kumi kumi akanipa.
 
“Sasa nipe namba yako, naweza kukuhitaji tena” Mtu huyo akaniambia.
 
Nikampa namba yangu ya simu akaiandika kwenye simu yake kisha akaniuliza.
 
“Unaitwa nani?”
 
“Andika Majomba Teksi”
 
Baada ya kuandika jina hilo aliniambia.
 
“Vizuri, nitakutafuta”
 
“Sawa” nikamjibu. Nilijipakia kwenye teksi yangu nikaiwasha na kuondoka.
 
Wakati naendesha nilijikuta nikumuwaza huyo mwanamke mjamzito aliyetakiwa kufanyiwa operesheni. Sikuwa na hakika kwamba alikuwa katika hali gani muda ule kwani kwa vyovyote vile yule daktari alikuwa amechelewa sana kufika pale hospitali kutokana na gari lake kuharibika.
 
Sikuendelea kumuwazia sana mwanamke huyo ambaye hata hivyo sikuwa nikimfahamu, nikajiambia sasa kumeshakucha. Nisingeweza tena kurudi kulala kwani muda ule ulikuwa ndio wa kuanza kazi.
 
Sikujali kupoteza usingizi wangu kwani nilikuwa nimeingiza zaidi ya shilingi elfu thelathini haraka haraka.
 
Nilichokuwa ninakiwazia ni kwenda kutia mafuta teksi yangu, nirudi nyumbani kuoga kisha nitoke tena.
 
Mpaka inafika saa mbili na nusu nilikuwa kwenye mgahawa mmoja nikipata kifungua kinywa. Nilikuwa nimeshaoga, kuvaa nguo nyingine na kuondoka nyumbani.
 
Baada ya kumaliza kufungua kinywa nilikwenda kwenye kituo changu jirani na hospitali ya Ngamiani. Nilipata safari mbili za haraka haraka, nikaingiza elfu kumi na mbili.
 
Wakati naegesha tena gari simu yangu ikaita. Nilipoipokea niligundua aliyekuwa akinipigia alikuwa ni yule daktari wa hospitali ya Bombo.
 
“Nimemaliza operesheni, sasa ninataka uje ulivute gari langu twende kwa Habib Garage pale Gofu”
 
“Sawa. Ninakuja”
 
Nilitazama saa yangu. Ilikuwa saa sita na robo. Nikaiondoa teksi yangu kuelekea hospitali ya Bombo.
 
Nilimkuta yule daktari ameliegemea gari lake ambalo tuliliegesha nyuma ya mti.
 
Nilisimamisha teksi mbele ya gari hilo nikashuka. Nilikwenda kufungua boneti la nyuma ya teksi nikatoa ile kamba. Ncha moja nikaifunga nyuma ya teksi na ncha nyingine nikaifunga mbele ya gari la yule daktari.
 
“Tayari” nikamwambia.
 
Daktari huyo akaingia kwenye gari lake. Na mimi nikaingia kwenye teksi yangu. Nilipowasha teksi tukaanza safari ya kuelekea Gofu.
 
Tulipofika huko nililiingiza gari hilo ndani ya gereji ya Habib. Daktari huyo akanilipa pesa yangu niliyotaka, nikaondoka.
 
ITAENDELEA KESHO, usikose uhondo huu ni kitaendelea,

No comments:

Post a Comment