HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA IBADA YA MAADHIMISHO YA JUBILEE YA MIAKA 125 YA INJILI YA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI MASHARIKI MBUYUKENDA, TANGA JANA.
Mheshimiwa
Baba Askofu, Dkt. Stephen Munga, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki;
Waheshimiwa Maaskofu;
Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula;
Waheshimiwa Wageni Wote Toka Ndani
na Nje ya Tanzania;
Waheshimiwa
Wana-Dayosisi na Wananchi Wote Mliopo Hapa;
Mabibi na Mabwana;
Bwana Yesu Asifiwe:
Nakushukuru sana Baba Askofu Stephen
Munga kwa kunialika na kunishirikisha kwenye ibada hii ya kihistoria ya Maadhimisho
ya Miaka 125 ya Injili katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Kwa
kweli ni jambo la furaha na heshima kubwa
kwangu kujumuika na Maaskofu na waumini
wa Kanisa hili kwa tukio hili kubwa na la kihistoria. Mwaliko
wenu huu kwangu ni uthibitisho wa uhusiano mzuri uliopo baina ya KKKT na
Serikali nchini. Uhusiano ambao umekuwa na
manufaa makubwa kwa nchi yetu na watu wake. Uhusiano ambao umejitafsiri katika
umoja, upendo, amani, na mshikamano uliopo baina ya Watanzania wa rangi zote,
dini zote, makabila yote na wa popote watokako na walipo.
Maadhimisho ya Miaka
125
Mheshimiwa
Baba Askofu,
Waumini
Wote na Wageni Waalikwa;
Siku kama ya leo, miaka 125 iliyopita
ndio siku ambayo Wamisionari wa Kijerumani wa Bethel wapoliwasili mahala
hapa.
Kwa maelezo yako, walipachagua hapa kuwa ni mahala pa kuwahifadhi vijana
waliokombolewa kutoka utumwani. Hivyo
mahala hapa paliwapa uhuru, na matumaini
mapya watu ambao walikwishakata tamaa. Aidha, kutokea hapa, ndipo kazi
ya
injili ilipoenea na kusambaa mkoani Tanga. Kusimama na wanyonge,
kuwafuta
machozi na kuwatua mzigo wao, ni jambo la heri, ni jambo jema na ni
jambo linalompendeza Mungu. Na huo ndiyo msingi imara wa Kanisa hili.
Huo
pia ndiyo msingi ambao juu yake imejengeka kazi na wajibu wa Serikali. Sisi
katika Serikali tunao wajibu wa kuwaondolea wananchi unyonge, kuwapunguzi
umaskini, kuwalinda na kuwakinga dhidi ya dhuluma na uonevu na kuwajengea
msingi bora wa maendeleo yao. Jitihada zetu
za kuondoa umasikini, kutoa fursa za elimu, kuboresha huduma za afya na mambo
mengi mengineyo tufanyayo yana malengo hayo. Jitihada za Serikali zinapounganika na zile za
madhehebu ya dini tunatengeza nguvu kubwa ya kuwaondolea wananchi wetu siyo tu unyonge
wa kiroho, bali pia kuwapunguzia changamoto za maendeleo zinazowakabili na
kusaidia kuinua hali zao za maisha.
Mchango wa Dayosisi
ya Kaskazini Mashariki
Waheshimiwa
Maaskofu, Ndugu Wananchi;
Ninaposema hivyo, natambua mchango wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika kuwaletea maendeleo
jamii na watu wa Mkoa wa Tanga. Mimi ni shahidi, maana nilifika kule Magamba,
Lushoto mwaka jana kufungua ukumbi wa
kisasa katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (SEKOMU) kilichojengwa na
Dayosisi hii. Pamoja na Chuo Kikuu,
natambua mnazo shule za sekondari za Lwandai, Bangala na Dinari. Dayosisi hii
inatoa pia huduma za kipekee ambazo hazipatikani kwa urahisi hapa nchini. Ninyi
mna shule ya wasioona ya Irente, shule ya msingi ya watoto wenye ulemavu wa ubongo
(Autism) na kituo cha kutunza wagonjwa wa akili cha Lutindi.
Kwa
upande wa Afya nako mmefanya mambo makubwa. Tunawashukuru kwa hospitali teule
ya Wilaya ya Kilindi (Kilindi CDH) ambayo nilishiriki kuweka jiwe la msingi na kuizindua.
Aidha nawapongeza kwa Hospitali yenu ya Bumbuli kuwa Hospitali Teule ya
Halmashauri ya Bumbuli. Hatua hiyo
itaimarisha pia Chuo cha Waganga Wasaidizi (Clinical Officers Taining College) cha Bumbuli.
Napenda
pia kupitia sherehe hii kuwashukuru ninyi wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa kazi yenu nzuri muifanyayo. Vile
vile, nawashukuru sana kwa kuiunga mkono Serikali katika jitihada za kuwaletea
maendeleo Watanzania. Nawaomba muendelee na moyo huo mwema. Namuomba
Mwenyezi Mungu awaongezee pale mlipopunguza na kuendelea kuwashushia baraka
tele.
Mheshimiwa
Baba Askofu,
Serikali
inatambua na kuthamini sana ushirikiano baina yake na madhehebu na mashirika ya
dini. Ndiyo maana tumekuwa tunatengeneza mazingira mazuri kwa mashirika ya dini
kuendesha shughuli zake. Tumekuwa tunatoa msamaha wa kodi, tunatoa mikopo kwa
wanafunzi wa Vyuo Vikuu vyenu na kutoa ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa zahanati,
vituo cha afya na hospitali ambazo Serikali inaingia ubia na Kanisa katika kutoa huduma kwa wananchi. Aghalabu hata pale
ambapo Serikali hujenga zake utaratibu
huo huachwa kuendelea. Nimetaja baadhi tu ya mambo ambayo tumekuwa
tukishirikiana na kusaidiana.
Napenda
kutumia nafasi hii kuwahakikishia kuwa tumekuwa tunafanya hivyo na tutaendelea
kufanya hivyo kwa kutambua kuwa huduma za kijamii zitolewazo na mashirika ya
dini zinawanufaisha Watanzania wote bila ubaguzi.
Maadili ya Jamii
Mheshimiwa
Baba Askofu;
Ndugu
Waumini na Wageni Waalikwa;
Napenda
kutumia nafasi hii kuwaomba viongozi wa dini kuongeza maradufu kazi ya malezi ya jamii kimaadili.
Sote ni mashahidi kuwa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili. Nadhani tumefika njia
panda tusipofanikiwa kugeuza mwelekeo huu na kuchukua njia hiyo nyoofu
tutaharibikiwa zaidi. Maadili mema ya
jamii pamoja na mila na desturi zetu vinapita katika mtihani mkubwa sana hivi
sasa. Vitendo vya utovu wa maadili vinaendelea kufanyika na kuchukua nafasi kubwa katika maisha ya watu siku hizi.
Inaanza kutaka kujengeka dhana potofu ati kuwa ni mambo ya kawaida au ndiyo usasa. Hali
hii haistahili kuachwa kuendelea kumong’onyoa misingi ya uadilifu ya jamii zetu
na ya ubinadamu wetu.
Viongozi
wa
dini mnalo jukumu zito na nafasi maalum
kwenye hili: kubwa ya kukemea na kurekebisha jamii mkianzia na waumini
wenu
wanaokwenda kinyume na maadili mema ya dini, jamii na nchi yetu. Hamna
budi kujitahidi kuwarudisha kwenye
mstari mwema na maadili mema wanakondoo mliopewa kuwachunga. Nasema
hivyo kwa kutambua kuwa wengi wa watu wote isipokuwa wachache sana
katika wale wanaofanya maasi na maovu ni waumini wenu na wafuasi wa dini
ambazo
Mungu amewapa jukumu la kuongoza. Sisi katika
Serikali tuko tayari kutimiza ipasavyo wajibu wetu wa kisheria katika
mapambano
haya adhimu. Naomba tuendelee
kushirikiana kujenga maadili mema katika jamii na nchini kote kwa
manufaa ya
watu wetu na nchi yetu.
Dhima ya Viongozi wa
Dini na Uchaguzi Mkuu
Mheshimiwa
Baba Askofu;
Waumini Wote na Wageni Waalikwa Wenzangu;
Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambao pia una
umuhimu wa aina yake katika historia ya nchi yetu. Tunaiaga Awamu ya Nne na kuikaribisha Awamu
ya Tano ya uongozi wa nchi yetu. Niruhusuni nitumie fursa hii kuwaomba viongozi
wa dini muiombee nchi yetu ipite kipindi hiki kwa salama na amani. Uzoefu wa nchi
nyingi za Afrika, chaguzi hutoa mwanya kwa uvunjifu wa amani. Haijawa hivyo
kwetu, lakini haina maana kuwa tunayo kinga ya milele. Hata na sisi tunaweza kuwa
kama wale iwapo yale yaliwafikisha wenzetu hapo hatutayaepuka.
Mafanikio
yetu ya kuendesha uchaguzi kwa amani na
usalama yametokana na tahadhari ambazo Serikali na viongozi wa dini tumekuwa
tukizichukua. Tuendelee kufanya hivyo.
Tusiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu kuwafarakanisha Watanzania. Tuendelee kukemea matumizi mabaya ya
fedha, rushwa, hila, ghilba na hujuma
katika chaguzi. Tunapaswa kufanya hivyo
tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani ya vyama vya siasa na baadae
wakati wa uchaguzi. Tuwakemee wanasiasa wapenda madaraka kwa gharama yoyote, ambao
watataka kutumia fedha kununua ushindi au ubaguzi wa rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua
wapinzani wao na kujijenga kisiasa.
Nawaomba msiwasikilize wala kuwaendekeza kwani mchezo wao ni mauti yetu.
Wakatalieni kwa macho makavu na kwa
kweli muwanyanyapae.
Hatupaswi
kukaa
kimya dhidi ya watu wanaokiuka maadili na kuchochea mifarakano katika
taifa letu. Hawa si watu wema watatufikisha pabaya. Hawaitakii mema nchi
yetu. Kamwe tusiruhusu wachezee dini zetu ambazo ni
mhimili muhimu sana wa amani yetu. Tofauti na ukabila ambao pamoja na
ubaya
wake, lakini unaweza kuhusisha eneo dogo, dini unahusisha nchi nzima.
Hakuna mtu, dini wala eneo litakalonusurika. Tutapoteza
ile sifa yetu ya kihistoria ya kuwa lulu na mfano wa amani katika
Afrika. Tusikubali kumchukiza Mungu akatukasirikia na kutuadhibu kwa
jambo ambalo
liko ndani ya uwezo wetu kulizuia lisitokee.
Kwa kweli mambo yakiharibika, hatuwezi kumlaumu mtu mwingine yeyote
bali sisi wenyewe.
Katu hatuwezi kusema ni mapenzi ya Mungu bali itakuwa ni makosa yetu
wenyewe.
Nawaomba
viongozi
wa dini mlisaidie taifa letu. Limeni
mraba wenu vizuri nasi tulime wetu. Msiwape nafasi viongozi wa siasa na
hata wa
dini kutumia majukwaa ya dini kuendeleza maslahi yao ya kisiasa na hasa
kupandikiza chuki katika jamii. Tunawategemea viongozi wa dini msiwe
sehemu ya makundi ya
wagombea au vyama vya siasa. Mnatakiwa msiwe na upande bali muwe juu ya
pande zote. Hapo ndipo
mtakapofanya vizuri kazi yenu ya ulezi na kuponya taifa iwapo kutatokea
matatizo.
Hatuwategemei
viongozi wa dini muwapangie waumini wenu vyama au viongozi wa kuwachagua.
Tunawategemea kuwahimiza na kuwakumbusha kuutumia haki na wajibu wao vizuri, muwahimize na kuwakumbusha kuwa watatakiwa
kufanya mambo matatu muhimu. Kwanza,
kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura na tatu kuchagua viongozi wazuri, wasiokuwa
waovu, wasiofanana na uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la
maendeleo na kujali maslahi mapana ya jamii husika na nchi yetu.
Mheshimiwa
Baba Askofu;
Ndugu
Waumini, Wageni Waalikwa;
Nawaomba
muendelee kuiombea nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu, watu wake
wadumishe upendo na mshikamano miongoni mwao.
Aidha, muuombee Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2015 uwe wa salama, amani
na haki ili taifa letu lipate viongozi wazuri na liendelee kuwa tulivu kabla,
wakati na baada ya uchaguzi.
Hitimisho
Mheshimiwa
Baba Askofu;
Kama
mnavyofahamu,
nakaribia kumaliza kipindi changu cha uongozi wa nchi yetu. Baada
ya uchaguzi wa Oktoba, 2015 tutakuwa na Rais mwingine. Napenda kutumia
fursa hii kuwaaga maana
naweza nisipate fursa kama hii tena katika kipindi kilichobaki.
Nawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa
mlionipa mimi binafsi na Serikali yangu katika kipindi cha miaka kumi ya
uongozi wangu. Tumeishi vizuri,
tumeshirikiana na kufanikisha mambo mengi mazuri pamoja. Kwa kweli
nafarijika kuwa ninapoondoka
madarakani, uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa la Kanisa
la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania ni mzuri na umeendelea kuimarika. Ndivyo
nilivyoupokea kutoka kwa Rais wa Awamu
ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, na ndivyo nitakavyoukabidhi
kwa
Rais wa Awamu ya Tano. Ningependa sana kuuona uhusiano na ushirikiano
huu ukikua
zaidi na zaidi, siku hadi siku kwani uhusiano wenye maslahi kwa nchi
yetu na
watu wake. Ni uhusiano wenye kujenga umoja, amani, upendo na
mshikamano miongoni wa watu wa Taifa letu hili moja, na la watoto wa
Mungu mmoja. Daima nitawakumbuka na kuthamini mchango wenu
na upendo wenu kwangu.
Nawashukuru
tena kwa kunialika na nawatakia maadhimisho mema ya miaka 125 ya Injili. Mungu
awabariki.
Asanteni Sana, na Mungu Ibariki KKKT,
Mungu Ibariki Tanzania na Watu Wake,
Bwana Asifiwe.
No comments:
Post a Comment