Tangakumekuchablog
Korogwe, POLISI
Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, unawashikilia watu wanne kwa tuhuma za
kusafirisha mihadarati aina ya mirungi wakiwa wameificha kwenye lori lililokuwa
likisafirisha chuma chakavu.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana ofisini kwake, kamanda wa pilisi Mkoani Tanga, Zubery Mombeji, alisema
tukio hilo lilitokea juzi saa 1 usiku katika kizuizi cha polisi Mombo na kusema
kuwa mirungi hiyo ilikuwa na uzito wa kilo 328.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni
Phillipo Martin (29), Emannuel Mafika (20), Juma Ali (28) na Lucas Mirart (25)
wote wakiwa ni wakazi wa Kilimanjaro na
wanahojiwa ili kukamilisha
upelelezi na kuweza kufikishwa mahakamani.
“Wakati wa ukaguzi wa gari polisi
ilisikia harufu kali ya mirungi jambo lililowasukuma kuamini kuwa imebeba
mihadarati baada ya watu wanne kuweko katika tela la gari” alisema Mombeji na
kuongeza
“Wale watu walipobaini polisi
imeshagundua walitaka kutoroka na ndipo ilipowaweka chini ya ulinzi wakati wako
katika upekuzi----lile lori lilibeba chuma chakavu na chini ndiko walikoficha magunia manne
yenye uzito wa kilo zaidi ya mia tatu” alisema
Alisema kukamatwa kwa watu hao,
polisi Tanga inataka kukomesha biashara haramu na upitishaji wa mali za
kimagendo kwa kuweka vizuizi vingi jambo ambalo litasaidia kukomesha biashara
hizo haramu.
Katika tukio jengine kamanda Mombeji
alilitaja tukio la bibi wa miaka 70 mkazi wa kijiji cha Kimbe Wilayani Kilindi
, Mariam Omary kujihusisha na uuzaji wa bangi .
Alisema kwa muda mrefu polisi
ilikuwa ikifuatilia nyendo za bibi huyo na ndipo ilipoweka mitego ya kumnasa
nyumbani kwake akiwauzia wateja bangi pamoja na unga.
“Polisi kwa muda ilikuwa na taarifa
za kuwepo kwa bibi muuza bangi na unga---lakini tulikuwa makini na taarifa hizo
kwani ilichukua miezi mitatu tunamchunguza na ndipo juzi walipovamia nyumba
yake na kumkuta akiwa na fuko la bangi na unga akiwauzia wateja wake” alisema
Mombeji
Alisema kwa sasa ajuza huyo anahojiwa na polisi kutaka kujua mtandao
mzima wa biashara hiyo na kwa sasa imepata taarifa za watu ambao wamekuwa
akishirikiana nae.
Alisema taarifa za awali zimepelekea
kukamatwa kwa watu watano ambao hata hivyo kamanda hawakuwataja na kusema kuwa
hadi ushahidi utakapokamilika watatajwa hadharani.
Mkuu wa Operesheni Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Jeremia Ouko (kulia) akiwaonyesha waandishi wa habari mihadarati aina ya mirungi viroba vinne vilivyokuwa na uzito wa kilo 328 vilivyokamatwa katika lori lililokuwa likisafirisha chuma chakavu kutoka Kilimanjaro kuelekea Dar es Salaam juzi katika geti la Mombo.
Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zubery Mombeji (kushoto) akiwaonyesha waandishi wa habari mihadarati aina ya mirungi viroba vinne yenye kilo 328 iliyokamatwa Wilayani Korogwe kwenye lori lilikuwa limepakiza chuma chakavu. Kulia ni Mkuu wa Operesheni Wilaya ya Korogwe, Jeremia Ouko.
No comments:
Post a Comment