Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu.Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma zikiwemo za umeme na Computer. Kituo kipo Tanga mkabala na bank ya CRDB wasiliana nao kwa simu 0715 772746
Mambo yamekuwa mazito. Ndivyo
inavyoonekana baada ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) kushindwa kutangaza mgombea urais jana badala yake
ukatoa ahadi mpya kwamba sasa atatangazwa muda wowote ndani ya siku
saba.
Kauli hiyo inayoibua maswali mengi
imekuja baada ya viongozi wa umoja huo waliofanya vikao hadi usiku jana
bila ya viongozi wakuu wa CUF ambao wameahidi kutoa msimamo wao leo saa
5.00 asubuhi.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia
alisema wamekamilisha mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye
watamtangaza kwenye mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi
na viongozi wengine wa vyama hivyo alisema hakuna mpasuko kama
inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.
Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na naibu wake wa Bara, Magdalena Sakaya hawakuhudhuria kikao hicho kilichofanyika kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.
Badala yake, Sakaya aliiambia Mwananchi
jana jioni kuwa CUF haikuweza kushiriki kikao hicho kwa kuwa kulikuwa na
mambo ambayo hawajakubaliana ndani ya chama na kwamba kama wangemaliza
mapema, wangekwenda kwenye kikao hicho.
Baadaye usiku, CUF ilituma taarifa kwa
vyombo vya habari ikisema kuwa itazungumza na waandishi wa habari leo
saa 5.00 asubuhi kwenye ofisi za chama hicho Dar es Salaam kutoa taarifa
kuhusu Ukawa.
Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF jana na
habari kwamba chama hicho kitatoa taarifa peke yake leo, kunaweka giza
nene mbele ya vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD, ambavyo vilikubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF
kulisababisha Ukawa kushindwa kumtaja mgombea wake na habari ambazo
zilipatikana awali, zilisema huenda vyama hivyo vikatangaza jina la
chama kitakachotoa mgombea urais badala ya jina la mgombea.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho
zilisema hoja kubwa ilikuwa katika suala la mgombea urais, nafasi ambayo
inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye ameshachukua fomu za CUF na Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye anaungwa mkono na vyama vyote vinne.
Tayari Profesa Lipumba ameshagombea
urais mara nne bila ya mafanikio, wakati Dk Slaa aligombea mwaka 2010 na
kushika nafasi ya pili, akiwa ameitikisa CCM iliyopoteza asilimia
takriban 20 ya kura za mwaka 2005.
Sakaya alisema jana kuwa CUF
haikushiriki kikao cha jana kutokana na kutoafikiana baadhi ya mambo
ndani ya chama chake, ikiwa ni pamoja na suala hilo la kusimamisha
mgombea mmoja wa urais kupitia Ukawa.
MWANANCHI
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema akichaguliwa kuwa rais, hatamwogopa mtu wala hataacha mtu aonewe, hasa wanyonge.
Dk Magufuli alikuwa akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Zakhem, Mbagala.
Katika mkutano huo ulioandaliwa CCM
mkoani Dar es Salaam, Dk Magufuli alikuwa akitoa angalizo kila mara kuwa
hawezi kuzungumza sana kwa kuwa wakati wa kampeni haujafika, ingawa
katika hotuba yake fupi alitoa ahadi mbalimbali zenye sura ya kampeni.
Aliahidi kuwa atawashughulikia watendaji
wa Serikali ambao ni wazembe na kuhimiza utekelezaji wa ilani ya CCM.
Aliongeza kuwa hatamwonea haya mtu yeyote atakayekuwa kikwazo kwa
maendeleo ya Taifa.
“Mimi
siyo mkali, mimi ni mtu mpole sana lakini nawachukia watendaji wa
Serikali ambao ni wazembe, na hao ndiyo nitakao lala nao mbele,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliohudhuria mkutano huo.
Dk Magufuli alisisitiza kuwa atasimamia
ilani ya chama ambayo imezingatia masuala ya kilimo na biashara. Alisema
ilani inawalinda wafanyabiashara wadogo na wakubwa, pia kuongeza fursa
za ajira kwa vijana.
“Maendeleo
hayana chama lakini maendeleo ya kweli yataletwa na CCM. Wakati wa
uchaguzi ukifika mchague wabunge na madiwani wa CCM ili kukamilisha
mafiga matatu,”Magufuli.
“Ukiwa
na tochi inayotumia betri tatu, wewe ukaweka betri mbili halafu
katikati ukaweka gunzi, hiyo tochi itawaka?” Dk Magufuli aliuliza
makutano ambao nao walimjibu kwa pamoja “haiwaki”.
Dk Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi,
aliwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata kuanzia Uwanja
wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) hadi viwanja vya Zakhem, Mbagala.
Alisema yeye na mgombea mwenza
watahakikisha wanalipa fadhila kwa vitendo, endapo watashinda Uchaguzi
Mkuu ujao na kuongoza Serikali.
“Ninawashukuru
wakazi wa Dar es Salaam kwa kuweka pembeni kambi zenu na kujitokeza
kutupokea wagombea wenu. Tulikuwa wagombea 42 wenye sifa sawa, na kila
mmoja alikuwa na kambi yake. Kuwa na kambi siyo kosa. Lakini wote
wamevunja kambi zao na kuniunga mkono ili kukipa ushindi Chama cha
Mapinduzi,” alisema.
MWANANCHI
Siku moja baada ya watu wanaosadikiwa
kuwa ni majambazi kuvamia kituo cha Polisi Stakishari kuua na kupora
silaha, mmoja wa walionusurika katika tukio hilo askari Gaston Shadrack amesimulia hali ilivyokuwa.
Askari huyo aliyejeruhiwa bega la kulia
na kifua kwenye uvamizi huo juzi usiku alisema alikuwa kwenye lindo
kituoni hapo kabla ya wanaume wanane kufika na kudai wamedhulumiana.
“Ilikuwa
saa 4 kuelekea saa 5 usiku. Lilikuja kundi la wanaume wanane wakiwa
wamevaa makoti makubwa lakini hawajafunika nyuso. Walikuwa wakilalamika,
“haiwezekani unidhulumu’ huku wakielekea ndani ya kituo.”
Aliongeza kuwa: “Utaratibu
wetu ni lazima mtu akifika apite getini kwa mlinzi kwa ajili ya kupewa
maelekezo ili aende ndani. Ila wao walitaka kwenda moja kwa moja,” alisimulia Shadrack ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Kutokana na utaratibu huo wa kuanzia
getini, aliwaita watu hao kwa ajili ya kupata maelekezo ya kwenda ndani.
Wakati huo akiwa na askari wenzake wanne hapo nje.
“…Kitendo
cha kuwaita na kuwauliza mnakwenda wapi, wale jamaa waligeuka na kuvua
makoti kumbe ndani walikuwa na bunduki. Wakaanza kutushambulia mimi na
askari wenzangu ambao walianguka chini huku wengine wakifyatua risasi
juu, nikageuka haraka na kulalia tumbo lakini wakati nageuka jambazi
mmoja alinipiga risasi ikanipata kwenye bega la kulia na kifuani,” alisema Shadrack huku akionyesha majeraha hayo.
Alisema baada ya hapo majambazi hao waliingia kituoni na kuendelea kufyatua risasi lakini mmoja wao alibaki nje ya kituo.
“Nilitumia mwanya huo kunyanyua bunduki niliyokuwa nayo na kumfyatulia risasi akandondoka na mimi nikakimbia.”
Katika hatua nyingine, mmoja kati ya
askari polisi wanne waliouawa katika tukio hilo, atazikwa siku moja na
mama yake ambaye alifariki dunia baada ya kusikia kifo cha mwanaye,
Koplo Gaudin.
Mkuu wa Polisi Ukonga, Mrakibu Mwandamizi, Jiliyo Simba alisema, mama wa askari huyo, alipoteza maisha baada ya kupokea habari za msiba wa mwanaye.
“Mama wa Koplo Gaudin alikuwa mgonjwa na alipopokea taarifa za kifo cha mwanaye naye alifariki dunia,”.
UHURU
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Kagame kati ya Yanga na Gor Mahia.
Dk Magufuli aliyepitishwa na mkutano
mkuu wa chama hicho, Jumatatu mjini Dodoma amepewa heshima hiyo ikiwa ni
kutambua mchango wake katika maendeleo wakati akiwa waziri.
Hilo litakuwa kusanyiko la kwanza kwa
mwanasiasa huyo ambaye hakuwahi kujiainisha kwenye ushabiki wa soka,
hasa kwa klabu kubwa, Simba na Yanga.
Wakati hayo yakiendelea, Shirikisho la Soka Tanzamia (TFF) limeahidi kuweka ulinzi maalumu wakati wa mashindano hayo.
Shirikisho hilo limeahidi usalama na ulinzi wakati wakati wote mashindano hayo kwa mashabiki na timu zote zitakazoshiriki.
Hakikisho hilo la TFF limekuja siku
chache kufuatia kuibuka kwa matukio ya uhalifu jijini Dar es Salaam
yanayohusisha uvamizi wa vituo vya polisi kwenye maeneo kadhaa.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na
TFF ni kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimeombwa
kutoa ulinzi maalumu kwa timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo.
Ulinzi huo kwa timu utahusisha misafara,
hoteli zote ambako timu hizo zitafikia huku mikakati kiulinzi, ikiwa
pia kwa mashabiki kwenye viwanja vitakavyotumika, Karume na Taifa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
wa TFF, Baraka Kizuguto alisema kuwa pamoja na vyombo vyote vya ulinzi
na usalama, pia wameweka mikakati kabambe ya kuhakikisha hakuna matukio
ya aina yoyote yanayoweza kuvuruga au kuhatarisha amani kipindi chote
cha michezo hiyo.
“Tunawahakikishia
wapenzi wa soka na Watanzania kwa jumla kuwa kutakuwa na usalama wa
kutosha kwani vyombo husika tayari vimeshachukua hatua madhubuti ili
kuhakikisha kuwa hakuna aina yoyote ya uvunjifu wa amani na ulinzi
utakuwa ni wa uhakika, hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi,” Kizuguto.
Katika hatua nyingine, Alhamisi kutakuwa
na mtihani maalumu kwa waamuzi, Cooper Test ambako wale wakatakaofuzu
ndiyo watachezesha mashindano hayo.
NIPASHE
Wakati bado hakuna mtuhumiwa
aliyekamatwa kufuatia tukio la kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi cha
Stakishari, jijini Dar es Salaam, imefahamika kuwa bunduki zilizoibwa ni
20, huku Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP ), Ernest Mangu, akitangaza bingo ya Sh. milioni 50 kwa mtu atayekatoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa majambazi waliofanya tukio hilo.
Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi
walikivamia kituo hicho usiku wa kuamkia Julai 12, mwaka huu na kuwaua
askari polisi wanne, raia watatu na kisha kupora silaha kadhaa na
kutokomea nazo kusikojulikana.
Kwa nyakati tofauti, IGP Mangu wa idadi ya silaha zilizna Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, kila wanapoulizoporwa na majambazi hayo, wamekuwa wakishikwa kigugumizi kusema.
Hata hivyo, taarifa zilizothibitishwa na
baadhi ya askari wa kituo cha Stakishari zimeeleza kuwa jumla ya silaha
zilizoporwa katika kituo hicho ni 20 ambazo ni aina ya Sub Machine Gun (SMG).
“Kisingi majambazi waliovamia kituo chetu siyo majambazi wa kawaida hawa ni magaidi, wamepora SMG 20…Hali inatisha, “alisema askari polisi mmoja wa kituo hicho .
Wakati hayo yakiendelea, Mkuu wa jeshi
hilo, Mangu ametangaza zawadi ya Sh. milioni 50 kwa mtu yeyote
atakayefanikisha kukamatwa kwa majambazi waliovamia kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Kamishna Kova, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio
hilo wamelichukulia kwa uzito wa kipekee na wanafanya jitihada za kufa
na kupona kuhakikisha wahalifu waliohusika wanakamatwa.
Kamishna Kova alisema katika kukabiliana
na majambazi wanaovamia vituo vya polisi, zitafungwa kamera za CCTV
katika vituo vyote vya polisi nchini.
Aliongeza: “IGP ameamua kutoa fedha hizo
ili kumzawadia atakayefanikisha kupata taarifa za wahalifu, fedha hizo
zipo tayari na tunawahakikishia kwamba tutamlinda mtoa taarifa na zawadi
yake tutamkabidhi kimya kimya kama ambavyo tumekuwa tukifanya vipindi
vilivyopita.”
Alisema hadi sasa bado hakuna mtu
aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi
linaendelea na uchunguzi wa kuhakikisha wahalifu wanatiwa mbaroni.
Kova alitaja baadhi ya namba za
Makamanda wa Polisi watakaokuwa wanapokea taarifa za watoa taarifa za
watuhumiwa kuwa ni 0754 034224 ya kwake mwenyewe, Msemaji wa Jeshi hilo,
Advera Bulimba (0713 631667) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Diwani Athumani 0715 323444.
NIPASHE
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, Isaya Mungurumi,
amewataka wafanyabiashara waliovamia viwanja vya Jangwani kuondoka mara
moja kutokana na kujimilikisha maeneo hayo kinyume cha sheria.
Alitoa agizo hilo jana jijini Dar es
Salaam alipozungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa Manispaa
ilikubaliana na Serikali kutenga sehemu ndogo katika viwanja hivyo kwa
ajili ya wafanyabiashara wadogo ili kupunguza msongamano katika soko la
Kariakoo.
Aidha, alisema kitu cha kushangaza ni
kuwa kabla ya manispasa kuanza ugawaji wa maeneo hayo kwa
wafanyabiashara wadogo, kuna watu walijitokeza na kuwauzia
wafanyabiashara wengine kinyume cha sheria na kusababisha kero kubwa.
“Nimeandaa
timu ya kuwashughulikia watu hao, hivyo naomba waondoke eneo hilo mara
moja kabla sheria haijachukuliwa dhidi yao, hatuwezi kuruhusu watu
kuanza shughuli zao za kibiashara katika maeneo ambayo hayajaandaliwa na
kuwekwa huduma muhimu za kibinadamu,” Mngurumi.
Aliongeza kuwa baada ya maeneo hayo
kutengwa na kuwa katika hali ya usafi, vitawekwa vyoo vya kuhamisha ili
vitumike kwa wafanyabiashara na watu wote watakaotembelea maeneo hayo.
Mungurumi alisisitiza zaidi kuwa eneo
litakalotumika ni moja na kubainisha kuwa maeneo yaliyopo karibu na
ofisi za Dart hayaruhusiwi kuguswa na kuongeza kuwa utaratibu maalum
utatumika kuyagawa maeneo yaliyopangwa kwa wafanyabiashara na siyo
kuwamilikisha ili kutumika katika kipindi hiki cha kiangazi.
Kadhalika, alisema Manispaa imeamua
kutumia eneo hilo kutokana na wafanyabiashara wengi wadogo kupanga
bidhaa zao barabarani hasa katika soko la Kariakoo hivyo kusababisha
kero kwa watembea kwa miguu na wakati mwingine kufunga barabara kabisa
na kusababisha msongamano wa magari.
Alisema wakati wakiwatafutia hifadhi ya
muda wafanyabiashara hao, manispaa inajiandaa kujenga masoko matatu ili
wawe na maeneo sahihi ya kufanyia shughuli zao.
Masoko yatayojengwa ni Kisutu,
Mchikichini na Buguruni na kwamba mazungumzo yameanza na benki kwaajili
ya kutoa mkopo kufanikisha mkakati huo unaotarajia kuanza mapema
iwezekanavyo.
NIPASHE
Wadau wa mawasiliano mkoani hapa, wameiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
kudhibiti matumizi mabaya ya simu za mkononi na mitandao hususani
katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini
Oktoba 25, mwaka huu.
Wadau hao walitoa rai hiyo juzi mjini
hapa, kwenye warsha iliyotolewa na TCRA kwa lengo la kuwakumbusha
wananchi manufaa ya mawasiliano.
Wadau hao walisema kadri siku za
uchaguzi zinavyokaribia, ndivyo ujumbe wa kupigana vijembe kwa lengo la
kuchafuana kisiasa zinazidi kukithiri na kuendelea kuwachanganya
wananchi.
Akizungumza kwenye warsha hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe, Edward Mgaya,
aliwataka wananchi wasitumie simu zao vibaya kwa kuchafuana au kufanya
malumbano kwenye mitandao ya kijamii hasa wakati huu wa uchaguzi.
“Ndugu
zangu wananchi wa Njombe ninawaombeni kipindi hiki cha uchaguzi tumieni
simu zenu vizuri msichafuane ili muweze kufanya uchaguzi kwa amani na
mpate kiongozi atakayewatatulia changamoto zenu, ”alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi
waliohuduria warsha hiyo, walitoa tahadhari ya matumizi ya simu
kifamilia kwa kutopokea picha zinazoweza kuhatarisha au kuvunja ndoa
zao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana, aliwataka wakazi wa Njombe kutumia mawasiliano ya simu kutafuta masoko ya mazao yao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, aliitaka Mamlaka hiyo kupunguza gharama za simu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi, amewaondoa hofu wananchi wanaoishi karibu na minara ya mawasiliano kuwa haina madhara kwao.
Mungi alisema hakuna mionzi yoyote
inayoweza kuwadhuru wananchi kwa sababu minara hiyo imefungwa vifaa
muhimu na vyenye kiwango vya kimataifa.
HABARILEO
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limesema Raia wa India, Amit Kevalramani mfanyabiashara, mkazi wa Dar es Salaam aliyekamatwa na Sh milioni 772 katika Hoteli ya St Gasper Mjini Dodoma wiki iliyopita hana hatia yoyote, kwani hakuna tuhuma zozote za rushwa zilizothibitika.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma, David Misime alisema hakuna tuhuma zozote za rushwa
zinazomhusisha moja kwa moja na masuala ya uchaguzi.
“Katika
tukio hili na uchunguzi tulioufanya, tumebaini kuwa hakuna kosa la
jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma
za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo
hazikuthibitika, kwani hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna
aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo,” alisema.
Akielezea mazingira ya tukio hilo,
Misime alisema Julai 11, mwaka huu katika Hoteli ya St. Gasper ya mjini
Dodoma, wananchi walitoa taarifa majira ya saa 10:00 jioni kuwa kuna mtu
mmoja mwenye asili ya Kiasia, amekamatwa na wananchi akiwa na fedha
nyingi na kuna vurugu kubwa.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, polisi walifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli.
“Askari
walithibitisha kuwa ni kweli walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia
akiwa na fedha kiasi cha milioni 722.5 na alipohojiwa alisema alifika
Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka,” alisema.
Misime alisema kwa mujibu wa mtu huyo,
alifika Dodoma Julai 10, mwaka huu majira ya asubuhi na kufikia Hoteli
ya St. Gasper na siku iliyofuata Julai 11, aliamua kurudisha fedha benki
kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye
viashiria vya vurugu.
Misime alisema mtu huyo akiwa katika
harakati ya kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa
katika eneo la Hoteli ya St. Gasper, walimtilia shaka na kumzuia
asiondoke na ndipo taarifa zilitolewa Polisi.
“Mashaka
ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa na mchakato wa uchaguzi
kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe,” alisema.
Alisema taarifa za aina hiyo, hata Jeshi
la Polisi lilikuwa limepokea bila uthibitisho. Alisema Jeshi la Polisi
limethibitisha kuwa fedha hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna
ushahidi mwingine uliothibitisha vinginevyo, amerejeshewa fedha zake.
HABARILEO
Mkongo wa Taifa wa mawasiliano unaounganisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi na Zambia, umehujumiwa miundombinu yake na baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo yanayopitiwa.
Meneja wa Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), Ekaeli Manase alisema hayo jana wakati akizungumza ukaguzi wa maeneo yaliyo karibu na yanayopitiwa na mkongo huo mkoani Dodoma.
Alisema jamii ina nafasi kubwa kufichua wanaohujumu miundombinu hiyo kwa faida ya taifa.
Manase alisema kwa mkoa wa Dodoma pekee,
zaidi ya Sh milioni 30 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa maeneo
yaliyoharibiwa kwa ajili ya kuunganisha nyaya zilizokatwa na kuibiwa na
wananchi.
Manase alisema jamii ina nafasi kubwa
kufichua wanaohujumu miundombinu hiyo kwa faida ya serikali, kutokana na
umuhimu wake unaochangia kupunguza gharama za upatikanaji wa huduma
bora za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) zenye ufanisi kupitia kuboreshwa kwa huduma za miundombinu hiyo.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Polisi Tarafa ya Dodoma, Ramadhan Mambea,
aliwataka wananchi kushirikiana na vikosi vya ulinzi shirikishi kwa
ajili ya kuulinda mkongo huo wa mawasiliano, ambao ni muhimu katika
mawasiliano ndani ya nchi na nje.
Alisema Jeshi la Ulinzi shirikishi
limejipanga kutumia vikundi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi
kuhakikisha wanalinda mkongo huo kwa kuwafichua na kuwakamata wahalifu.
Faustina Bendera, mkazi wa Chinyoya,
akizungumza kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo, aliishauri serikali kutoa
elimu juu ya umuhimu wa kuwepo kwa mkongo huo, ambao umekuwa ukihujumiwa
na watu kutokana na kukosa elimu.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment