Hadithi
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572, 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA 8
ILIPOISHIA
"Huwezi
kunilazimisha. Mimi siwezi kushirikiana na wewe kwenye jambo hilo. Tusubiri
asubuhi nikuache"
"Uniache wende
wapi?"
"Nitakwenda
kupandisha chumba mahali pengine"
"Kwa vile
umeshaijua siri yangu huendi kokote utabaki na mimi!"
"Usinieleze
upumbavu wako. Sitaweza kuendelea kuishi na mtu kama wewe"
"Kama wewe
unajifanya umeshika kisu jua kuwa ulichoshika ni makali. Mpini nimeshika
mimi. Kama tutavutana atakaye katika vidole ni wewe"
"Kwanini unaniambia
hivyo?"
Chausiku akatabasamu.
"Nimekuambia hivyo
kwa sababu kama wewe umeujua uhalifu wangu na mimi ninaujua wako.Ingawa
ulinificha lakini najua kuwa wewe ulimuuua mke wako kwa kumchoma kisu kisha
ukakimbilia huku kijijini.Mpaka leo polisi wanakutafuta.Kesho nikienda kituo
cha polisi kukutolea ripoti ujue umekwisha!"
Hapohapo
nikanywea.Maneno yake yalinikata kauli yakanifanya nibaki nimeduwaa.
SASA ENDELEA
Niliduwaa si kwa sababu
tu ya mshituko nilioupata kutokana na maneno aliyoniambia Chausiku bali pia
kutokana na kumuona msichana huyo ni mjanja.
Siku zote nilikuwa
nikijua kuwa tukio lile la kuuawa mke wangu lilikuwa ni siri yangu.Na Chausiku
nilimdanganya kuwa mke wangu niliachana naye.Kumbe alikuwa akijua kuwa mke
wangu aliuawa na anayetuhumiwa kumuua ni mimi.
Lakini jambo la ajabu ni
kwamba hata siku moja Chausiku hakupata kunieleza chochote kuhusu tukio
hilo.Alikuwa ameamua kunyamaza.
Nikawa najiuliza
amejuaje kuwa ninadaiwa kumuua mke wangu wakati tukio hilo lilitotokea Handeni?
Na kwanini hakuwahi kuniambia?
"Sasa
unasemaje?" Chausiku akaniuliza aliponiona nimeduwaa.
"Lakini sikumuua
mimi,wananizulia tu" nikamwaambia lakini sasa sauti yangu ilikuwa
imenyweea kabisa
"Kama
wanakusingizia kwanini ulikimbia Handeni na kuja kujificha huku?"
"Nikanyamaza kimya,
sikuwa na la kumjibu.
"Sasa niambie
utakuwa tayari kujiunga na kundi letu nikufichie siri yako?" Chausiku
akaniuliza.
Ilikuwa ni kweli
Chausiku aliposema yeye ameshika mpini, mimi nimeshika kwenye makali.Tukivutana
mimi ndiye nitakayekatika vidole.
Kumuacha yeye kama mke
wangu au kumtolea siri yake kuwa ni mchawi kusingemletea athari kubwa. Ni madai
ambayo sitoweza kuyatolea ushahidi na anaweza kuyakana.
Lakini yeye atakapo
kwenda kituo cha polisi kutoa habari zangu, polisi watakuja kunikamata.Na moja
kwa moja nitakwenda kushitakiwa kosa la mauaji. Kulikuwa na wanawake wengi tu
ambao walikuwa tayari kwenda kunitolea ushahidi kuwa ni kweli nimemuua mke
wangu. Kwa vyovyote vile adhabu ya kifo haitaweza kuniepuka.
Niliinamisha kichwa
changu nikawaza sana kabla ya kumjibu chochote.
"Mbona hujajibu
swali langu?" Chausiku akaniuliza.
"Sasa sikiliza
nikuambie, mimi sitakutolea siri na nitaendelea kuwa mume wako. Naomba hiyo
habari kwamba nimemuua mke wangu iishie hapahapa" nikamwaambia.
Ingawa sikuweza kuyaona
lakini nilikuwa na hakika kuwa macho yangu yalikuwa madogo na mekundu kwa
fadhaa
"Hapana. Sitaki
hivyo.Nitakuaminije wakati umeshaniona.Nataka na wewe uwe mchawi kama
mimi" Mke wangu akaniambia.
Chausiku alikuwa
amenishika pabaya. Jinsi alivyokuwa amenitolea macho alionyesha wazi kuwa
nikimkatalia atakwenda kunifichua kituo cha polisi kesho asubuhi.
"Basi acha
nifikiri, nitakujibu kesho asubuhi" nikamwaambia kwa sauti ya taratibu.
"Hapana, kama
unakubaliana na mimi nataka unijibu sasa hivi na kama hutaki unijibu sasa
hivi"
"Nimekubali"
nikamjibu.
Niliona bora kuwa mchawi
kuliko kwenda kuhukumiwa kifo tena kwa kosa ambalo sikulitenda.
Nilipomjibu hivyo mke
wangu alicheka kwa furaha mpaka jino lake la mwisho nikaliona.
"Umeniambia kweli
kuwa umekubali?"
"Nimekubali, ilimradi
tu usende kunifichua polisi"
"Kama umekubali
sitakufichua"
Ingawa nimezushiwa
mauaji ambayo siyatambui lakini bora nikubali yaishe.
Mke wangu akatoka mle
chumbani,nikasikia akifungua mlango wa chumba cha pili.Baada ya muda kidogo
alirudi akiwa ameweka mavumba kwenye kiganja chake cha mkono wa
kushoto.Akaniwekea mbele ya midomo yangu.
"Ramba!"akaniambia. Nikayaangalia
yale mavumba kisha nikamuangalia usoni mwake. Alikuwa ametaharuki.
"Nirambe
nini?" nikamuuliza.
"Kama kweli
umekubali kuwa mchawi ramba hii dawa yangu"
"Ni ya nini?"
"Wee! ramba
tu!"
"Ramba wewe
kwanza!"
Chausiku akairamba ile
dawa yake na kuimumunya kisha akaimeza.
"Ramba na
wewe" akaniambia huku akikileta kiganja chake kwenye midomo yangu.
Ukiyavulia nguo maji
yaoge, nikajiambia. Nilitoa ulimi nikairamba ile dawa kidogo na kuisikiliza. Ladha
yake ilikuwa ya chumvi chumvi.
"Ramba yote!"
Nikairamba yote.
"Ugomvi wetu
umekwisha.Sasa nakuamini.Wewe ni mume wangu na mimi ni mke wako.Kesho usiku
nikitoka tutatoka wote. Sasa twende tukalale”
Tukaenda kulala lakini
mimi sikupata usingizi.Mwenzangu alipitiwa na usingizi mara moja,akaniacha mimi
nikihangaika kwa mawazo.
Sikujua ile dawa
aliyonirambisha Chausiku ilikuwa ni ya nini.Ilikuwa ni dawa ya kuniingiza
kwenye uchawi?.Au ni ya kunifanya nimfichie siri zake?
Isitoshe, nilijiambia, sasa
ninalazimika kuingia katika uchawi ili kuokoa maisha yangu. Sikuwa na ujanja
mwingine. Punde tu na mimi nitaanza kutoka usiku....nitakula nyama za maiti...,niliwaza
kwa fadhaa.
Kulipokucha asubuhi
hatukuyaendeleza tena yale mazungumzo ya usiku.Nikatoka kwenda zangu shamba.
Mke wangu aliniletea
chakula saa saba mchana.Nilipomaliza kula aliniuliza.
"Unakumbuka tulivyokubaliana jana usiku?'
"Ninakumbuka"nikamjibu
"Nataka nijue kama
mawazo yako bado ni yaleyale au yamebadilika"
"Tutazungumza jioni
nitakapo rudi" nikamwambia
Mke wangu
akachukua vyombo na kuondoka.Jioni niliporudi nyumbani hatukuzungumza kitu, hakuniuliza
kitu na mimi sikumueleza kitu.
Baada ya kuoga
nilikwenda mtaa wa pili ambako kulikuwa na baraza la vijana.Vijana tulikuwa
tunakutana hapo na kucheza bao.
Nilicheza bao hadi saa
mbili usiku nikarudi nyumbani kula chakula. Baada ya kula sikutoka tena. Nilikaa
barazani na redio yangu hadi saa nne usiku nilipoingia ndani kulala.
Nilimkuta mke wangu
akikoroma.Sikumshangaa. Kutokana na kazi yake ya kuamka usiku ilimbidi alale
mapema.
Nilipanda kitandani na
mimi nilale lakini sikupata usingizi.Usiku ule kwa upande wangu ulikuwa ni
fainali. Ni usiku wa kuamua kwenda kujiunga na wachawi au kukataa na niwe
tayari kuripotiwa polisi na Chausiku.
Kwa ajili ya kuokoa
maisha yangu niliona nikubaliane na Chausiku.Na si kukubaliana kiukweli bali
nilipanga nijiingize katika kundi lao kama kutalii tu na kumridhisha Chausiku
Kwa kweli niliendelea
kukaa macho mpaka saa nane usiku, ndipo nilipolala. Baada ya kulala kidogo tu
Chausiku akaniamsha.
"Amka..amka...muda
umeshafika!"akaniambia
Je nini kitatokea?
Mwenzetu ameshatekwa na mke wake. Haya ndio masahibu ya kidunia. Hebu endelea
kufuatilia hapo kesho ili ujue nini kitamtokea kijana huyo masikini. Blog yetu
ni ile ile TANGA KUMEKUCHA!
No comments:
Post a Comment