Tangakumekuchablog
Tanga, MBUNGE
wa jimbo la Tanga mjini,(CUF) Mussa Mbarouk, amewataka wananchi kumpa
ushirikiano kuleta maendeleo jimboni humo na kusema kuwa ahadi zake zote
alizozitoa wakati wa kampeni uchaguzi
mkuu uliopita atazitekeleza.
Akizungumza nje ya mahakama baada ya
kushinda kesi yake iliyofunguliwa na aliekuwa mpinzani wake , Omari Nundu (CCM)
alisema kwa sasa anajisikia furaha na kujiona Mbunge kamili ambapo kasi yake ya
kuwaletea maendeleo wananchi anaianza.
Alisema kesi hiyo ilikuwa ikimyima
usingizi na kushindwa kufanya lolote la maendeleo kwa wananchi na badala yake
akili na nguvu ilikuwa iko katika kesi jambo ambalo wananchi walikuwa katika
sintofahamu ya kujua hatima ya kesi hiyo.
“Leo niko na furaha na kujiona ni mbunge kamili baada ya mahakama kunipa ushindi
wa kesi iliyofunguliwa na mpinzani wangu
katika kinyang’anyiro cha ubunge Omari Nundu” alisema Mbarouk na kuongeza
“Niwaambie wananchi wa jimbo la
Tanga bila kuangalia itikadi za vyama mimi ndie mbunge wao hivyo nitahakikisha
ahadi zangu nilizozitoa wakati wa kampeni nitaanza kuzitekeleza” alisema
Akizungumzia usafi wa mazingira
Mbunge huyo alisema jiji la Tanga ni chafu na haliendani na hadhi ya jiji hivyo
kuwataka wananchi kuhakikisha wanaweka mazingira ya usafi maeneo yao kujikinga
na magonjwa ya miripuko.
Alisema jiji hilo ni chafu na
limejaa madampo ambayo takataka zake zimekuwa zikikaa kwa muda mrefu bila
kuondolewa hivyo kuahidi kulipatia ufumbuzi kwa kuiomba halmashauri kuongeza
gari la kuzolea takataka.
“Jiji letu kwa kweli haliendani na
hadhi ya jiji limejaa madampo na kuwa kero kwa wananchi hasa kipindi hiki cha
vitisho vya magonjwa ya miripuko ukiwemo wa kipindupindu” alisema Mussa
Alisema ili kuliweka katika
mazingira ya usafi kwanza ni mtu ahakikishe eneo linalomzunguka linakuwa katika
usafi pamoja na kuwa na utaratibu maalumu kwa chombo cha kuhifadhia takataka.
Mwisho
No comments:
Post a Comment