ZULIA LA FAKI 0655 340572
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 19
ILIPOISHIA
“Hakunidanganya. Baba yako
alinionesha picha yake, ndiye yeye niliyemuona na hata namba ya simu anayotumia
ulisema ni yake”
“Namba ya simu ni yake kweli,
niliikariri kichwani mwangu”
“Basi ndiyo ujue niliyemuona
alikuwa ni Ummy kweli”
“Sasa mbona hapokei simu?”
“Tena mwanzo alikuwa
akinipigia yeye, ndiyo nikaipata hii
namba yake”
“Basi atakapokupigia tena
utakuja kutuambia”
Nikaagana na yule msichana.
Sikwenda kwao tena. Nikaenda kupanda daladala na kurudi nyumbani.
Vile nafika nyumbani tu, simu
yangu ikapigwa. Nilipoangalia namba inayonipigia, nikaona namba
ya Ummy.
Nilishituka halafu mwili
ulinisisimka.
SASA ENDELEA
Nikajiuliza niipokee au
nisiipokee? Kama nitaipokea msichana huyo atanieleza nini? Nikajiambia chochote
ambacho ataniambia kitazidi kuniweka njia panda kwa vile nimeshathibitisha kuwa
msichana huyo alikuwa ameshakufa.
Vile vile tayari nilikuwa na
hofu ya kuzungumza na mtu ambaye kuna ushahidi kuwa alikuwa amekufa.
Lakini kwa upande mwingine
nilikuwa na shauku ya kumsikia yeye mwenyewe atakachojibu kuhusu madai kuwa alikuwa
ameshakufa miaka mitano iliyopita.
Nikajiambia nisipopokea simu
yake, bado nitabaki kuwa njia panda kwani sitapata mtu mwingine wa kunipa
ufafanuzi kuhusu madai ya kufa kwake.
Mbali na hayo, bado nilitaka
kujua ni siri gani ambayo alitaka
kunieleza kuhusu mali za babu yangu. Nikaamua kupokea ile simu.
“Hello!” Nikasema kwa sauti
ya kujikaza ili nisioneshe hofu niliyokuwa nayo.
“Hello! Kassim unajua
nimekupenda sana, ninataka uwe mume wangu!”
Maneno hayo yalinishitua.
Niwe mume wa mtu aliyekwisha kufa!
“Natumaini kuwa naongea na
Ummy?” nikamuuliza.
“Mimi ni Ummy Nasri”
“Uliniambia nifike
nyumbani kwenu Mwananyamala, nimefika
jana na leo lakini sikukuona”
“Ulimkuta nani?”
“Nilimkuta baba yako mzee
Nasri”
“Vizuri sana. Alikuambia
nini?”
“Aliniambia maneno ya
kunishitusha sana”
“Kama yapi”
“Aliniambia kwamba mwanawe
anayeitwa Ummy alikwishakufa miaka mitano iliyopita”
“Na mimi ni nani?”
“Umeniambia kuwa wewe ni Ummy
Nasri”
“Na uliyembiwa amekufa ni
nani?”
“Ni Ummy Nasri”
“Sasa una shaka gani?”
“Kwanza nataka unieleze ni
kwanini nimeambiwa kuwa umekufa?”
“Kuna umuhimu wa mimi na wewe
kukutana”
“Kwanza nataka ujibu, kwanini
nimeambiwa kuwa umekufa?”
“Ndiyo maana nikakwambia kuna
umhimu tukutane ili tuzugumzie hilo pamoja na kukueleza kuhusu mali za babu
yako”
Nikanyamaza kwa sekunde
kadhaa nikifukiria la kumjibu.
“Lakini ni kweli kuwa
ulikufa?” nikamuuliza baada ya kimya kifupi.
“Ni kweli?”
“Sasa wewe ni nani?”
“Ni Ummy”
“Umekubali kuwa ulishakufa,
sasa mbona uko hai?”
“Mimi ni kivuli cha Ummy”
“Sijakuelewa. Kivuli maana
yake nini?”
“Maana yake ni mzuka wa
Ummy!”
Moyo wangu ulipiga kwa nguvu
kisha ukaanza kunienda mbio. Nikahisi mkono ulioshika simu ulikuwa ukitetemeka.
“Kassim tutakapokutana kila
kitu utakielewa vizuri”
“Unadhani nitakutanaje na
mzuka?”
“Tutakutana tu na tutazungumza, usijali”
“Mmmh…!”
Pakapita kimya kingine.
“Niambie nikiuone wapi na
muda gani?” Sauti ya Ummy ikautanzua ukimya uliokuwepo.
“Acha nifikirie kwanza”
“Ufikirie nini Kassim?”
“Umenitisha. Umeniambia
kwamba wewe ni mzuka”
“Sasa unataka ufikirie nini?”
Sikujibu.
“Kassim!” Sauti ya Ummy ikaita
kwenye simu.
Sikujibu. Nilibaki nimeduwaa
kama gogo.
“Nitakupa muda wa kufikiria
lakini usizidi saa arobaini na nane”
“Sawa” nikamuitikia.
Ummy akakata simu.
Yale maneno ya kwanza ya Ummy
kuwa ananipenda na anataka niwe mume wake, yalipita katika akili yangu.
Nikajiambia hata wale watu
aliowaua kule Buswana. Zimbabwe , Afrika Kusini na hapa Dar, inaelekea
walianzana kwenye mapenzi,
Kitendo cha kuniambia anataka
niwe mume wake si tu kimebadili mada yake ya kwanza ya kutaka tukutane ili
anieleze ziliko mali za babu yangu bali pia nilifikiri kwamba ilikuwa ni
hatua ya kutaka kuniua.
ITAENDELEA kesho hapa hapa usikose ni kitaendelea wa Kassim akiwa katika mtihani mzito wa kusuka au kunyoa
No comments:
Post a Comment