HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (6)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Si tu tuliona tungeweza
kujisitiri katika lile jumba pia tungeweza kufanya uchunguzi wetu na kujua kama huyo Harishi tuliyeambiwa ameshakuja au bado.
Tukaanza tena safari ya
kurudi katika lile jumba. Mvua ilikuwa imeshaanza kunyesha kidogo dogo huku
upepo mkali ukiendelea kuvuma pamoja na radi.
Tulitembea kwa mashaka
mashaka tukikwepa kuwa karibu na miti kwa kuhofia kupigwa na radi.
Kulikuwa giza na hatukuweza kupata mwanga ila pale
radi ilipopiga ndipo tulipoona tulikokuwa tunaelekea. Kutokana na giza hilo tulihangaika
katika pori kwa
muda kabla ya kufanikiwa kutokea katikati ya ule mji uliohamwa.
Tulikuwa tunaendelea kutota
na mvua na huku tukiendelea kwenda. Tukawa tunalitafuta lile jumba. Tulidhani
tusingeliona kwa urahisi lakini lilikuwa linawaka taa. Tukaliona kwa mbali. Tukalifuata.
Kwanza tulinyata kwenye madirisha. Tukawa tunachungulia na
kutega masikio kusikiliza. Hatukusikia sauti yoyote. Kulikuwa kimya. Ndipo
tukaamua tuingie.
SASA ENDELEA
Tukaingia ndani ya jumba hilo lililokuwa linawaka
taa ndani. Lakini tuliingia kwa kunyata ili hatua zetu zisisikike. Jumba hilo lilikuwa kimya kama
vile tulivyoliacha mchana.
Kila tulipofikia kona tulichungulia
kwanza kabla ya kuendelea kwenda. Tukaenda hadi katika kile chumba tulichomkuta
Yasmin binti wa rais wa Comoro.
Mlango wa chumba hicho
ulikuwa umefungwa. Tukaenda jikoni tukapekua pekua na kukuta vyakula
vilivyokuwa vimebaki. Tukakaa chini na kuanza kula kwani njaa ilikuwa inatuuma na
hatukutarajia kupata chakula usiku huo.
Baada ya kula tulitoka humo
jikoni tukaamua kutafuta mahali pa kulala ndani ya jumba hilo
hilo. Karibu
vyumba vyote tulivyofungua ukiacha kile cha Yasmin vilikuwa na vitanda. Kila
kitanda kilikuwa na chumba kimoja kilichowezesha kulala watu wawili.
Tukaamua tulale kila chumba
watu wawili. Tulikuwa tupo saba. Mmoja wetu akaamua kuchukua godoro kutoka
chumba kingine na kuliingiza katika chumba tulichokuwemo mimi na mwenzangu.
Akalilaza chini. Kwa vile yeye hakuwa na mwenzake wa kulala naye na asingeweza
kulala peke yake, ndipo aliamua kuja kulala na sisi.
Mvua likuwa inaendelea
kunyesha na radi ilikuwa inapiga. Kama
tungekuwa tuko kwenye boti yetu tungejuta.
Mimi nilisoma aya zangu kisha
nikajifunika shuka. Naamini na wenzangu kila mmoja alisoma dua yake kabla ya
kulala.
Tulikuwa tumepanga tuamke
alfajiri tutoke kwenye hilo
jumba bila hata kumshitua Yasmin.
Hata hivyo usingizi
hatukuupata kirahisi kwa sababu ya hofu. Tuliendelea kukaa macho hadi usiku
mwingi. Wenzangu walipata usingizi lakini mimi sikulala.
Kulikuwa na wakati usingizi
ulikuwa umeanza kunijia nikaamshwa na mwenzetu aliyekuwa amelala chini.
“Unasemaje?” nikamuuliza.
“Mkojo umenibana nisindikize
chooni” akaniambia.
Vyoo vilikuwa nje.
Nikatenga shuka na
kunyanyuka. Mwenzangu niliyelala naye alikuwa anakoroma.
“Twende!” nikamwambia yule
aliyeniamsha.
Tukatoka pamoja. Vyoo
vilikuwa ukumbini karibu na mlango wa kutokea.
Tulikwenda hadi karibu na
milango ya vyoo. Kulikuwa na vyoo vinne. Mwenzangu alishaingia choo kimojawapo.
Mimi nikasikia hatua za mtu nyuma yangu nikageuka. Alikuwa ni yule mwenzetu
tuliyemuacha amelala, naye aliamka na kutufuata.
Alikuwa anakuja harakaharaka
kutukimbizia. Nilijua ni sababu ya uoga. Wakati huo huo nikaona mlango wa
chumba cha Yasmin unafunguliwa. Nikaingia chooni haraka ili niweze kumchungulia
aliyekuwa anatoka bila yeye kuniona.
Ghafla nikaliona jitu
likitoka katika kile chumba. Lilikuwa jitu la kutisha lililojifunga kilemba
kikubwa. Lilikuwa na msitu wa nywele zilizotokeza nje ya kilemba chake. Lilivaa
kanzu nyeupe iliyochafuka kwa madoa ya damu na iliyokatwa mikono.
Mikono yake minene iliyoota
manyoya marefu ilikuwa imeshupaa. Mkono mmoja alishika upanga mrefu.
Uso wake ulikuwa na ndevu
nyingi na sharafa kiasi kwamba sura yake haikuweza kutambulika. Kilichoonekana
kwenye uso wake ni pua yake iliyofura kamailiyopachikwa na macho yake makubwa
yenye makengeza.
Miguu yake ilikuwa pekupeku.
Alikuwa na vidole virefu na vinene vya miguu, tena vilikuwa na kucha ndefu kama kucha za mnyama.
Hapo hapo nikahisi kwamba
yule alikuwa ndiye Harushi. Alikuwa ametufuma vizuri ndani ya hilo jumba.
Uso wake ukiwa na hasira
kali, macho yake ya makengeza yalielekea kwa yule mwenzetu aliyekuwa
anatufuata. Alikuwa ameshafika karibu yake kiasi kwamba jitu hilo lilinyoosha mkono wake wa kushoto na
kumshika shati.
ITAENDELEA KESHO USIKOTE NA UHINDO HUU WA KUSISIMUA
No comments:
Post a Comment