BAADA YA KUSIMAMA KWA MUDA
KUWALETEA MFULULIZO WA HADITHI YETU YA “NILIJUA NIMEUA” SASA TUTAANZA TENA
KUWALETEA HADITHI HIYO. TUNALAZIMIKA
KUIANZA MWANZO ILI MUWEZE KUIFUATILIA VIZURI.
Hadithi hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa na Mkombozi Sanitarium Clinic. Mabingwa wa tiba Asilia. Mkombozi wanasifika kwa kuwa na vipimo vya magonjwa sugu, Wapo Chuda Tanga mkabala na Kampuni ya Mabasi ya Raha Leo simu, 0654 361333
NILIJUA NIMEUA (1)
Kujuana kwangu na Halima
kulikuwa kwa bahati sana.
Awali sikuwa na mawazo kabisa ya kwamba nitakuja kukutana na kusuhubiana na
msichana mrembo kama yeye.
Siku moja ambayo ninaikumbuka
hadi leo nikiwa kwenye teksi yangu maarufu kama
Majombi Teksi, nilikuwa ninatoka hospitali ya Bombo ambayo ni hospitali ya mkoa
iliyoko Tanga.
Nilikuwa nimempeleka mama
mmoja mjamzito kutoka hospitali ya Ngamiani. Mama huyo alipelekwa hospitalini
hapo kujifungua lakini kutokana na umri wake kuwa mkubwa madaktari wakaamua
wamhamishie Bombo.
Ndugu zake waliiona teksi
yangu ambayo huiegesha karibu na hospitali hiyo kusubiri abiria, wakanikodi
niwapeleke Bombo.
Wakati narudi kutoka Bombo
mvua ilikuwa imeanza kunyesha. Nikaona msichana aliyekuwa amesimama pembeni mwa
barabara akinipungia mkono kwa bidii huku akitota na mvua. Ilikuwa wazi kuwa
mvua ilimkuta ghafla njiani na mahali alipokuwa hapakuwa na sehemu ya
kujisitiri. Mimi kama dereva wa teksi nilishukuru kwa hilo.
Nilipunguza mwendo na
kuisimamisha gari pembeni mwa barabara. Nilikuwa nimempita kidogo. Alipoona
teksi imesimama aliifuata haraka akafungua mlango wa nyuma na kujipakia.
“Unakwenda wapi?”
nikamuuliza.
“Nipeleke barabara 20 nyuma
ya CCM” akaniambia. Sauti yake ilikuwa nyembamba na nyororo.
Alijisogeza katikati ya siti
ili kukwepa upepea wa mvua uliokuwa ukipenya kwenye dirisha. Nikawa namuona
vizuri kwenye kioo cha gari cha kutazamia nyuma.
Wakati naiondoa teksi nilikuwa
namkodolea macho kupitia kwenye kioo hicho bila mwenyewe kujua.
Uso wake ulikuwa umenywea
kutokana na fadhaa ya kutoswa na mvua lakini alikuwa na sura jamali ya macho
makubwa aliyoyapaka wanja mzito. Juu ya macho yake pembeni mwa kopi alikuwa amepaka
rangi iliyoendana na nguo aliyokuwa amevaa.
Pua yake ilikuwa ndefu na
midomo ya wastani aliyokuwa ameipaka rangi hafifu ya waridi.
Nilimuona tangu alipokuwa
amesimama alikuwa mrefu , mweupe na mwenye mwili wa wastani. Vazi alilokuwa
amevaa, dera la maua ya rangi ya bluu ya
kung’aza na ushungi wake aliokuwa ameutanda kichwani vilimfanya aonekane
alikuwa msichana aliyejistahi sana.
“Mvua za ghafla namna hii
zinatuharibia bajeti” akasema kwa sauti ya kuchukia.
“Kwanini?” nikamuuliza huku
nikitia gea ya pili.
“”Mahesabu yangu yalikuwa
kupanda bodaboda, sasa nalazimika nipande teksi ili nisitote, huoni kuwa
nimeshaharibu bajeti yangu?’
Nikatoa tabasamu jepesi.
“Na sisi ndio tunapata riziki
zetu, usiilani”
“Kwa hiyo unaiombea ili upate
abiria kwa wingi eti?”
“Ndiyo maisha yalivyo. Huwezi
kumwambia daktari unaombea watu waumwe ili waje kwako upate pesa, au huwezi
kumwambia muosha maiti kuwa anafurahia watu wafe apate kazi. Yeye pia
anasikitika mtu akifa lakini ndiyo maisha. Kwa mmoja kukienda kilio kwa
mwingine kunakwenda furaha”
“Sawa bwana, umeshinda wewe”
Nikacheka. “Sasa unataka
nikalie wapi dadangu kama sio kwenu?”
“Basi nipunguzie kidogo”
“Ni shilingi elfu tano tu”
“Ndiyo nakwambia nipunguzie,
nitakupa elfu tatu”
Nikatikisa kichwa. Tabasamu
lililokuwa usoni kwangu likatoweka. Sikutaka masihara yaingie kwenye kazi
yangu. Teksi ile haikuwa mali
yangu. Nilikuwa nimeajiriwa na mwenyewe alitaka nimpelekee shilingi elfu
ishirini kila baada ya masaa ishirini na nne, bila kujali nimeingiza kiasi gani.
“Elfu tano ndio kima chetu,
haipungui. Petroli imepanda sana”
nikamwambia.
Wakati nampa
jibu hilo simu
yake iliyokuwa kwenye mkoba wake ilianza kuita. Akaitoa na kuipokea.
“Ninakuja, nisubiri” akasema
kwenye simu.
Alisikiliza kidogo kisha
akaendelea.
“Nimekodi teksi…poa…”
Akairudisha simu kwenye
mkoba.
Nilikuwa nimetokea kwenye
eneo la Tangamano. Mvua ilikuwa imezidi. Eneo hilo lilikuwa halipitiki kwa maji.
Niliipitisha teksi yangu kwa taabu kwa kutumia gea kubwa. Mpaka nakaribia
kufika stendi ndio nilipata afadhali kidogo.
Nikaendelea na safari hadi
barabara 20. Nilikata kulia, nikalipita jingo la ofisi ya CCM na kuingia mtaa
wa nyuma yake. Mtaa huo ulikuwa umejaa matope.
“Twende kwenye nyumba ile
pale” abiria wangu akaniambia.
Alinionesha nyumba iliyokuwa
katikati ya mtaa huo upande wa kulia. Ilikuwa nyumba ya kawaida iliyoonekana
kuwa tulivu.
Niliposimamisha teksi,
msichana aliniuliza.
“Nikupe kiasi gani?”
“Elfu tano”
ITAENDELEA KESHO
No comments:
Post a Comment