Wednesday, July 8, 2015

KITUMBO JOTO UTEUZI MGOMBEA URAIS CCM

Nani atakaye mrithi Kikwete katika CCM?

Wiki hii masikio yote ya Watanzania yanaelekezwa mjini Dodoma, mji mkuu wa Tanzania ambapo  Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinamchagua mtu mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa wabunge na rais unaotarajiwa kufanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Vikao vya mchakato huo vimeanza rasmi leo Jumatano huku vikitanguliwa na kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo kimsingi pamoja na mambo mengine kitapitia wasifu wa watia nia wote lakini pasipo kupunguza jina lolote.
Siku ya Alhamisi (09 Julai), Kamati Kuu ya chama yenye wanachama takribani 32 itakutana na hapo ndipo upungazaji wa majina utafanyika hadi kufikia majina matano tu.
Baada ya hapo, Halmashauri kuu ya chama itakutana siku ya Ijumaa tarehe 10 Julai ambapo itachuja majina hayo matano hadi kufikia matatu kupitia mtindo wa kupiga kura. Majina haya matatu ndiyo yatakayokwenda katika Mkutano Mkuu wa Chama ambao ndio utakaochagua jina moja la huyo mgombea urais kwa tiketi ya chama
Mkutano Mkuu huo unajumisha takribani wanachama 2100 ikiwa ni pamoja na Wabunge wa CCM Tanzania bara na wawakilishi wengine kutoka Zanzibar lakini pia wawakilishi wa chama kutoka ngazi mbalimbali hadi zile za chini.
Mkutano huu umepangwa kufanyika tarehe 11 hadi 12 Julai
Uteuzi waibua hisia
Wakati watu wakingojea kwa hamu ni nani atapenya katika mchujo huo na kuibuka kidedea, tangu mwanzo wa zoezi zima la kutafuta nafasi hiyo kwa wanachama wa CCM kumeibua hisia kubwa na za tofauti miongoni mwa Watanzania.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya CCM na nchi kwa ujumla, idadi ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu na kusaka ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho ilifikia 42.
Idadi hii ilijumuisha makada kutoka kila aina ya haiba. Walikuwemo waliokuwa mawaziri wakuu wa zamani, maofisa wa ukachero wastaafu na hata mwanachama mmoja ambaye elimu yake inasemekana kuwa ni ya shule ya msingi tu. Hata hivyo orodha hii ilisheheni jinsia ya kiume zaidi huku idadi ya wanawake waliojitokeza kuchukua fomu ikiwa ni wanne tu.
Mchakato huu wa CCM kuelekea uteuzi wa mgombea wao wa urais ni wa muhimu sana kwa chama hicho na unafuatiliwa kwa karibu sana na wapenzi lakini hata wapinzani wa chama hicho kwa sababu mwisho wake unatarajiwa kutoa picha ya mwelekeo wa chama hicho kikongwe nchini.
Umuhimu wa mchakato
Kwa mfano, huu ndio msimu wa kwanza ambapo chama hicho kitamteua mgombea urais pasipo baraka za moja kwa moja za mwasisi wa chama hicho na taifa kwa ujumla Mwalimu Julius Nyerere.
Hata kama vyombo husika vya uchaguzi na utaratibu mzima wa kumpata mgombea umekuwepo tangu kitambo, Mwalimu Nyerere alifanyika mshawishi mkubwa katika kuwapata wagombea hasa wa nafasi nyeti kama ya urais wa nchi ambao hatimaye kweli walipata kuwa marais.
Kwa upande mwingine baadhi ya wanaosaka kuteuliwa kuwa wagombea wa chama chama hicho wamehusishwa na kashfa kadhaa za matumizi mabaya ya madaraka na rushwa vilivyoisababishia serikali hasara kubwa na kuzua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania
CCM inaonekana kuwa na kazi ngumu ya kuwahakikishia wanachama wake lakini pia wapinzani wake kwamba ina uwezo wa kumuweka kando mtuhumiwa yeyote kwa usalama wa chama. Kwamaneno mengine, kuthibitisha kwamba chama ndicho kinachotangulia halafu mgombea anafuata.
Lakini wakati CCM inapiga hesabu ya kuruka kihunzi hicho, bila shaka inapiga hesabu nyingine pia ya namna gani itahakikisha chama kinabaki imara hata baada ya kuwanyima fursa hiyo wanachama hawa wanaonekana kuwa na madoa
Ikumbukwe kwamba hao wanaoshutumiwa ni makada wenye ushawishi wa hali ya juu na wafuasi wengi ndani ya chama ambao bila shaka wanauwezo wa kuhatarisha umoja na uhai wa chama ikiwa wagombea wao watanyimwa fursa hiyo.
Mwaka jana CCM ilionesha makeke yake baada ya kuwasimamisha makada wake sita kwa muda wa takribani miezi 17 ambao walibainika kukiuka kanuni za uchaguzi cha chama.
Ni nani ataaminiwa kupewa dhamana ya kupeperusha bendera ya CCM? Na ni nini mustakabali wa chama hicho baada ya mchakato wa kumpata mgombea huyu wa tiketi ya chama? Maswala haya na mengine mengi bila shaka yapata majibu yake baada ya kikao cha chama hicho. Chanzo BBC

No comments:

Post a Comment