Wednesday, July 15, 2015

NILIJUA NIMEUWA SEHEMU (6)


HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Tiba, Mkombozi Sanitarium Clinic mabingwa wa magonjwa sugu. Mkombozi wako na vipimo vya mwili mzima vinavyoweza kugundua magonjwa yaliyofichikana. Wapo Chuda Tanga na wanapatikana simu 0654 361333
 
Sehemu ya hadithi yetu iliyopita ilikuwa na mapungufu mengi. Katika sehemu hii ya leo tumeamua kuyarekebisha mapungufu hayo na tunairudia tena sehemu hiyo kikamilifu pamoja na sehemu iliyofuata.
 
NILIJUA NIMEUA 6
 
ILIPOISHIA
 
Tangu siku ile nikaanza kujuana na daktari Augostino Kweka. Alikuwa daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali ya Bombo. Mara kwa mara gari lake lilipokuwa na matatizo alikuwa akiniita mimi nimpeleke safari zake.
 
Tulijuana na hatimaye tukawa marafiki wakubwa.
 
SASA ENDELEA
 
Kuna siku Mariam alinibainishia jina lake halisi. Aliniambia anaitwa Halima.  Si unajua wanawake wa kitanga wanavyopenda kuficha majina yao. Mpaka mzoeane sana ndio atakutajia jina lake.
 
Wakati  huo tulikuwa tumezoeana vya kutosha kiasi kwamba aliweza kunikodi nimpeleke safari zake kIsha akaweka deni na huja kunilipa siku nyingine.
 
Nilimuamini kwa sababu alikuwa muaminifu na hakuwa akisahau deni. Siku anayoahidi kunilipa hunilipa bila matatizo.
 
Ule ukaribu wetu ukafanya tuwe marafiki. Kulikuwa na siku ambayo nilikuwa nimempakia kumpeleka sehemu. Nikamueleza undani wangu kuwa nilimpenda.
 
“Umenipendaje?” akaniuliza. Lilikuwa  swali la kitoto lakini baadaye niligundua lilikuwa na maana.
 
“Nataka uwe mke wangu”
 
“Kwani wewe huna mke, au unataka niwe mke mwenza?”
 
“Sio mke mwenza, mimi sina mke. Sijaoa bado’
 
“Sawa. Nipe muda nikufikirie”
 
“Usichukulie mzaha Halima, nakwambia ukweli”
 
“Na mimi nakwambia ukweli”
 
“Sasa unataka nikupe muda unifikirie nini, kwani ninaomba kazi?”
 
Halima akacheka.
 
“Si unaomba uchumba. Nataka nikufikirie unanifaa au hunifai”
 
“Lini utanipa jibu?”
 
“Siku yoyote tu”
 
“Basi usinicheleweshe sana, nisije nikabadili uamuzi wangu”
 
“Usijali”
 
Kutoka siku ile mara kwa mara nikawa nampigia simu kumsalimia. Na yeye pia alikuwa akinipigia kuniuliza hali hasa kama nimepitisha siku mbili au tatu bila kumpigia.
 
Kuna siku nilikuwa naumwa kichwa. Akanipigia simu na kuniambia alitaka kunitembelea nyumbani. Nikamuelekeza ninapoishi. Baada ya muda kidogo akanipigia tena akaniambia yuko nje ya nyumba yangu.
 
Nikatoka na kumkuta amesimama pembeni mwa nyumba yangu. Nikamkaribisha ndani.
 
“Nilikuwa nimepotea, kama nisingeiona ile teksi yako pale barazani, nisingeitambua hii nyumba” akaniambia wakati tumo chumbani.
 
“Lakini hapapotezi, labda wewe hufiki sana huku Msambweni”
 
“Labda. Unajisikiaje kuumwa?”
 
“Sijambo kidogo, nikuletee soda?”
 
“Acha tu. Unaumwa na nini?”
 
“Kichwa. Kichwa kinauma sana. Siwezi hata kuendesha gari. Sijui waswahili wameniroga?”
 
“Acha kuamini sana uchawi. Umepima malaria?”
 
“Nimepima, sina malaria”
 
“Umetumia dawa gain?”
 
“Nimeandikiwa dawa na daktari, ndizo ninazotumia tangu jana”
 
“Tangu utumie hizo dawa, unajisikiaje?’
 
“Kwa sasa nina nafuu, nashukuru sana”
 
“Pole sana”
 
“Asante”
 
“Hii ni nyumba yako au umepangisha?”
 
“Ni nyumba yangu?”
 
“Unaishi na wazazi wako humu?”
 
“Hapana. Wazazi wangu wameshafariki”
 
“Hawa watu waliomo humu ndani ni akina nani?”
 
“Ni wapangaji wangu”
 
“Wewe mwenyewe umechukua chumba kimoja tu”
 
“Kinanitosha. Sina mke wala motto”
 
Tulipofika hapo msichana akanyamaza kimya. Alikuwa kama anayewaza.
 
“Mbona kama unawaza, unawaza nini?” nikamuuliza.
 
“Nikwambie kitu?”
 
“Niambie”
 
“Si unanitaka mimi, sasa mimi nakupa sharti la kukukubali”
 
“Sharti gani?”
 
“Wafukuze wapangaji wote halafu uikarabati hii nyumba” nikamwambia.
 
“Unataka tuishi peke yetu?”
 
“Ndiyo. Sitaki kero. Chumba kimoja uweke sebule”
 
“Kwa vile nakupenda nitafanya hivyo”
 
Baada ya wiki moja nikaufanyia kazi ushauri wa Halima. Niliwapa notisi wapangaji wote, nikaikarabati nyumba na kuweka chumba kimoja kama sebule.
 
Nilikuwa na shamba langu la minazi. Fedha nilizopata kutokana na mauzo ya nazi zilinisaidia sana kukamilisha nyumba yangu.
 
Halima aliendelea kunitembelea mara kwa mara. Alipohakikisha nimetimiza matakwa yake akanielekeza kwa wazazi wake nipeleke barua ya uchumba.
 
Wazazi wa Halima walikuwa wakishi Pongwe, mwendo wa karibu kilometa kumi na tano kutoka Tanga mjini. Baba yake Halima mzee Moto Bwagizo alikuwa mtu mzima sana. Niliambiwa kuwa Halima alikuwa mtoto wake wa mwisho na alizaliwa bila kutegemewa kwani tayari baba yake alikuwa mzee. Mama yake mzazi alishafariki.
 
Mzee Moto Bwagizo alikuwa na wake wawili, mama yake Halima na mke mwingine. Baada ya kufariki mama yake Halima, mzee Moto aliendelea kuishi na mke wake wa pili.
 
Niliwasilisha ujumbe wangu kwa wazazi wa Halima. Baba mkwe aliponiona aliniambia hazitambui mila za kutuma barua ya uchumba kwani mimi sikuwa nikiomba kazi. Ukiomba kazi ndio unatuma barua.
 
“Mila ninazizijua mimi za kutpka enzi na enzi ni za kutuma mshenga, anakuja na maneno tu”
 
“Samahani baba yangu, sikujua ndio kama unanielimisha”
 
Mzee akacheka.
 
“Umenijibu vizuri. Sasa fungua barua yako unisomee”
 
Nikafungua ile barua yangu na kumsomea yale niliyoandika.
 
Mzee akafurahi akaniambia.
 
“Nimekuelewa. Unataka kuunga udugu na sisi. Mimi kama baba wa Halima nakujibu hapa hapa kuwa nimekukubali. Halima ni mchumba wako tangu sasa”
 
Mzee Moto alinitajia kiasi cha pesa alichotaka ili aniozeshe binti yake.
 
Siku ya pili yake nilimchukua rafiki yangu nikaenda naye kupeleka pesa hizo.
 
Mipango ya harusi ikafanywa.
 
Baada ya wiki mbili nikaenda Ponwe kumuoa Halima.
 
Baada ya kuoana na Amina ndipo nilipoanza kufaidi maisha ya ndoa. Kuse,ma kweli yalikuwa matamu kinyume na kuishi kihuni.
 
Kwanza gharama ya maisha ilipungua sana. Pesa ambayo hapo mwanzo nilitumia peke yangu kwa siku  kwa kula kwenye mikahawa, ilitumika kwa siku mbili nilipokuwa na mke wangu.
 
Kadhalika nilikuwa na mwenzangu wa karibu wa kuniliwaza, kunishauri na kunisaidia pale nilipohitaji mwenza wa kunisaidia.
 
Kwa kweli nilihisi raha na nilijilaumu kwa kuchelewa sana kumuoa Halima.
 
Niliendelea na kazi yangu ya teksi. Fedha nilizopata ntulitumia, kiasi kingine tuliwek kama akiba yetu. Miezi michache tu baad ya kuoana, ndoa ilijibu. Halima akapata ujauzito.
 
Halima alinijulisha usiku kuwa alikuwa mjamzito. Wakati tunataka kulala aliniambia.
 
“Subiri”
 
“Nisubiri nini?” nikamuuliza.
 
“Subiri nikuoneshe kitu”
 
“Kitu gani?”
 
“Una haraka gani?”
 
Halima akasimama mbele yangu na kuushika mkono wangu kisha akaushikisha kwenye tumbo lake chini ya kitovu. Akawa anautomasisha kwenye tumbo lake.
 
“Unaona nini?” akaniuliza.
 
“Sioni kitu” nikamjibu.
 
“Huoni kitu kigumu gumu?”
 
“Nakiona, ni nini?”
 
Halima akauachia mkono wangu kisha akapanda kitandani. Wakati anavuta shuka nilimuuliza.
 
“Mbona hukiambii ni nini?”
 
“Mimba!” akanijibu huku akiendelea kijifinika.
 
“Hiyo ni mamba?”
 
Ndiyo”
 
“Mbona ndogo sana?”
 
“Si ndio inaanza, ina mwezi mmoja. Ujue mwezi uliopita sikupata siku zangu”
 
Ni kweli ilikuwa mamba ya mwezi mkmoja. Ilitupa furaha sote wawili. Tukaona karibuni tutaitwa baba na mama.
 
Lakini kadiri siku zilivyoendelea Halima alikuwa akiniambia anapolala usiku anaota ndoto amejifungua watoro wawili mapacha. Watoto hao ni wazuri na weupe kama wazungu!
 
TULIISHIA HAPA, SASA TUNAENDELEA MBELE
 
Nikadhani labda ni kweli atajifungua mapacha. Mimba ilipoiza miezi mitatu Halima aliota akifanya tendo la ndoa na mwendawazimu. Alipoamka akaanza kuumwa tumbo!
 
“Una nini?” nikamuuliza nilipomuona akifurukuta.
 
Akanihadithia ile ndoto aliyoota kasha akaniambia alipoamka aliona tumbo linamuuma.
 
Wakati ananieleza hali ilizidi kuwa mbaya. Nikafikiria nimpeleke hospitali lakini ile mamba ikatoka muda ule ule.
 
Sikujua alikuwa amepatwa na tatizo gani. Ilikuwa saa kumi na mbili asubuhi. Nikatoka naye na kumpakia kwenye teksi, tukaenda hospitali ya Bombo.
 
Tulipofika hospitali nilimpigia simu rafiki yangu Dk Augostino Kweka. Kwa bahati njema alikuwa pale pale hospitali, akaja kumtazama mke wangu kisha  akaniambia.
 
“Anahitaji kusafishwa. Mimba haikutoka yote”
 
Dk Kweka alinisaidia sana. Alilichukua jukumu lile kirafiki. Mpaka inafika saa tatu mke wangu alikuwa ameshasafishwa.na kupelekwa wodini. Mimi mwenyewe nilikuwa hapo hapo hospitali muda wote.
Usikose uhondo huu kesho

No comments:

Post a Comment