HADITHI
NILIJUA NIMEUA 2
ILIPOISHIA HADITHI YA JANA.
Alisikiliza kidogo kisha
akaendelea.
“Nimekodi teksi…poa…”
Akairudisha simu kwenye
mkoba.
Nilikuwa nimetokea kwenye
eneo la Tangamano. Mvua ilikuwa imezidi. Eneo hilo lilikuwa halipitiki kwa maji.
Niliipitisha teksi yangu kwa taabu kwa kutumia gea kubwa. Mpaka nakaribia
kufika stendi ndio nilipata afadhali kidogo.
Nikaendelea na safari hadi
barabara 20. Nilikata kulia, nikalipita jengo la ofisi ya CCM na kuingia mtaa
wa nyuma yake. Mtaa huo ulikuwa umejaa matope.
“Twende kwenye nyumba ile
pale” abiria wangu akaniambia.
Alinionesha nyumba iliyokuwa
katikati ya mtaa huo upande wa kulia. Ilikuwa nyumba ya kawaida iliyoonekana
kuwa tulivu.
Niliposimamisha teksi,
msichana aliniuliza.
“Nikupe kiasi gani?”
“Elfu tano”
SASA ENDELEA
Nikadhani ataanza tena
kulalamika kutaka kupunguziwe kiasi cha pesa. Lakini haikuwa hivyo, alifungua
mkoba wake akatoa noti ya shilingi elfu tano na kuniambia.
“Shika”
Niligeuka nikaipokea kisha
nikamfungulia mlango.
Akashuka haraka na kukimbilia
kwenye baraza ya ile nyumba. Wakati anabisha mlango nikaiondoa teksi.
Nilirudi katika egesho langu
lililokuwa karibu na hospitali ya Ngamiani.
Nililipendelea egesho hilo kwa maana. Kwanza lilikuwa karibu na hospitali ambapo mara kwa mara
kunakuwa na wagonjwa wanaohitaji huduma ya teksi. Pili nilikuwa peke yangu na
tatu kulikuwa na mahoteli mengi yaliyokuwa karibu na hapo na kufanya nipate
wateja wengi.
Wakati naliegesha gari
nilisikia mlio wa simu ndani ya gari.
Nikashituka na kudhani ilikuwa simu yangu. Lakini niligundua haikuwa simu
yangu. Simu yangu haikuwa na mlio kama huo niliousikia.
Nikatega masikio yangu ili
nijue mlio huo ulikuwa unatokea wapi. Nikapata jibu. Mlio huo ulitoka nyuma
yangu. Nikageuza kichwa na kutazama nyuma. Ndipo nilipoiona simu ikiita kwenye
siti.
Mara moja niligundua kuwa
yule msichana niliyempakia alisahau simu yake. Ilikuwa simu ileile aliyokuwa
akiitumia wakati nimempakia.
Sikuweza kujua ni nani
aliyekuwa anapiga. Iliwezekana alikuwa
yeye mwenyewe, aliamua kupiga baada ya kugundua kuwa aliisahahu simu
ndani ya teksi yangu. Au alikuwa ni mume wake ingawa sikuwa na hakika kama alikuwa na mume.
Nikajiuliza niipokee ile simu
au nisiipokee? Nikapata jibu kuwa nisiipokee kwa vile sikujua nani anapiga na
isitoshe haikuwa ikinihusu.
Baada ya kuita kwa muda simu
ikakatika lakini baadaye kidogo simu ikaita tena. Nikaiacha iite.
Kwa vile nyumba aliyoingia
yule msichana ninaifahamu nitampelekea wakati wowote, nikajiambia.
Hata hivyo sikupata amani
kwani simu ilikuwa ikiita kwa mfululizo. Ufumbuzi ulikuwa niizime au niipeleke
kwa mwenyewe haraka. Kwa vile nilishindwa kuizima niliamua niwashe teksi
nimrudishie mwenyewe.
Mvua sasa ilkuwa imeacha
kabisa. Nilifika katika mtaa aliokuwa akiishi yule msichana. Tangu natokea
katika mtaa huo niliona msichana amesimama kwenye baraza ya ile nyumba akiwa
amejaa wasiwasi. Nilipokaribia zaidi niligundua kuwa alikuwa ni yule
msichana niliyempakia.
Niliposimamisha teksi mbele
ya ile nyumba aligutuka, akanikodolea macho ya tashiwishi.
Mara moja akashuka kwenye
baraza na kuja kwenye mlango wa teksi wa dereva.
“Kaka umeniletea simu
yangu?” akaniuliza kwa matumaini.
Kwa kutaka kumshitua a mimi
nikamuuliza.
“Simu gani?”
“Jamani nilisahau simu yangu
kwenye siti. Simu yenyewe niliinunua juzi tu shilingi laki tatu”
Nilipoona amehamanika
nilimwambia.
“Hebu angalia kwenye siti
uliyokuwa umekaa”
Akasogea mlango wa nyuma na kuchungulia kwenye
dirisha.
“Si ile pale!” akasema huku
akifungua mlango.
Aliingia ndani ya teksi
akaichukua ile simu na kutoka.
“Asante kaka. Kumbe ulikuwa
unanitania!”
Sote tukacheka. Huzuni
ilikuwa imeshamtoka.
“Wewe ni muaminifu sana. Nitakuwa nachukua
teksi yako kila siku” akaniambia.
“Kwaheri, nakwenda zangu”
nikamuaga.
“Ulikuwa umeniletea simu
yangu. Asante sana kaka, endelea kuwa na
moyo huo huo”
“Asante bibie”
Wakati natia gea niondoe gari
sauti yake ikanisitisha.
“Nipe namba yako.
Nitakuhitaji tena siku nyingine”
Nikamtajia namba yangu.
ITAENDELEA KESHO, usikkose uhundo huu
No comments:
Post a Comment