Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma ikiwemo ya ufundi umeme pamoja na kutoa kozi ya Kiingereza na Computer. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
UHURU
Watu wanne wamezirai na kukimbizwa katika hospitali ya Nyahururu, Kenya baada ya kuzidiwa kwa kukosa pombe.
Kulingana na madaktari katika hospitali
hiyo, wanaume hao walilazwa baada ya juhudi za kuwarejeshea fahamu kwa
kuwanywesha maziwa kugonga mwamba.
Ofisa matibabu katika hospitali hiyo
ambaye alikataa jina lake kutajwa alisema wanaume hao walianguka na
kukosa fahamu baada ya kukosa pombe walioachishwa gafla.
“Kawaida mtu akiwa na mazoea ya kunywa pombe kisha kumwachisha ghafla mwili huhisi kukosekana kwa kiungo muhimu”.
Alisema kwa sasa watu hao wanaendelea
vizuri na matibabu na kufuatia tukio hilo walevi waliokuwa kwenye
kampeni ya kuacha ulevi wameishutuma Serikali kwa hatua ya kuwalazimisha
kuacha pombe gafla.
Wakazi wengi wa eneo hilo walisema hawawezi kufanya kazi bila kunywa pombe kwa kuwa inawasaidia kuwaongezea ari ya kujituma
MWANANCHI
Mbunge wa Singida Mjini (CCM) na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji
amewaliza baadhi ya wapigakura wake wakati akitangaza kutogombea tena
nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa ya madai ya kubanwa na
majukumu ya kifamilia na biashara.
Dewji ambaye amekuwa mwakilishi wa jimbo
hilo kwa awamu tatu mfululizo, alitangaza uamuzi wake huo kwenye
mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
Alisema kuwa aliomba ridhaa ya
kuwatumikia wananchi wa Singida Mjini mwaka 2000, hakuwa na familia na
pia biashara zake hazikuwa kubwa kama ilivyo sasa.
Alisema katika kipindi chote cha
uwakilishi wake, wakazi wa Singida Mjini wamempa heshima kubwa, ukarimu
wa hali ya juu, wema uliotukuka na uvumilivu usio na kifani na kwa hali
hiyo, hatawasahau kamwe na ataendelea kuwatumikia kupitia mfuko maalumu
aliouanzisha.
Aliwataka wakazi hao kuendeleza moto wa
maendeleo waliouwasha miaka 10 iliyopita kwa miaka mingine kama hiyo
ijayo ili jimbo hilo lipige hatua zaidi.
“Kwa
kutambua heshima mliyonipa na imani kubwa mliyonionyesha kwa vipindi
vyote vya uongozi wangu, ingawa nina huzuni lakini sina budi niwaombe
kuwa mwaka huu wa uchaguzi sigombei tena na ninatoa fursa kwa kada
mwingine wa CCM anipokee kijiti hiki kuliongoza jimbo letu,” alisema kwa
huzuni. Baada ya kutamka maneno hayo, wananchi wengi katika walipiga
kelele kwa nguvu wakionyesha kutokubaliana na uamuzi wake. Huku moja ya
sauti ikisikika… “Hatutaki mbunge mwingine ni wewe tu hadi tukuchoke.”
Awali, Dewji alitaja baadhi ya maendeleo
yaliyofanyika katika vipindi vyake, kuwa ni pamoja na kujenga shule 15
za sekondari kutoka mbili zilizokuwapo.
Alisema kwa kutumia fedha zake alijenga na kuchimba visima 45 vya majisafi na salama.
MWANANCHI
Mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru
amemshukia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kwa
kauli zake alizodai zinaminya demokrasia na kwamba CCM haiwezi kusimama
wanapopambana wenyewe kwa wenyewe.
Kingunge ambaye hivi karibuni aliweka bayana kumuunga mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
katika harakati zake za kuwania urais, alisema hakubaliani na kauli ya
Nape kuwa wagombea wasioridhika na uamuzi wa Kamati Kuu (CC), hawawezi
kukata rufaa kwa sababu ya muda kuwa mfupi.
Alisema CCM imeweka utaratibu wa wanachama kudai haki zao ndani ya chama, pindi wasiporidhishwa na uamuzi wa vikao vya chini.
Alisema mwaka 2005, mgombea wa nafasi ya
urais, John Malecela alikata rufaa katika Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) baada ya jina lake kutopelekwa.
“Aliyekuwa
mwenyekiti wa chama wakati ule Mkapa (Benjamin), alikubali baada ya
kushauriana na wenzake kwa sababu haikuwa zawadi, bali ni haki yake,” .
Hata hivyo, alisema baada ya kujielezea
mbele ya NEC na wajumbe kuulizwa, walikubali kuwa majina matano
yaliyoletwa na CC yanatosha.
“Kufikiria kwamba mtu akose haki kwa sababu ya kukosa muda huko ni kuwakosesha watu haki,” .
Kingunge alisema amani na utulivu ni mambo yanayojengwa kwa haki na lazima imani ijengwe na viongozi.
Alisema lugha za kibabe ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi huku chama kikaa kimya ndizo zinazowatia watu shaka.
“Sasa
hivi kumekuwa na nguvu kubwa ya kupambana ndani ya chama kuliko
wapinzani… nyumba ikigawanyika haiwezi kusimama na CCM haiwezi kusimama
inapopambana yenyewe kwa yenyewe,” alisema.
Alisema kukiwa kuna jitihada za kunyima haki watu, kunaweza kusababisha machafuko.
MWANANCHI
Wakati Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akisema anashindwa kuamini kilichotokea na kunusurika katika ajali ya helikopta juzi, mmiliki wa chopa hiyo, Philemon Ndesamburo amesema atanunua nyingine haraka kabla ya kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Kauli hizo zilitolewa jana ikiwa ni siku moja baada ya helikopta hiyo inayomilikiwa na Ndesamburo kupitia kampuni yake ya Keys Aviation kupata ajali wakati ikitumiwa na Nassari na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Wakati ikipata ajali, ilikuwa imekodishwa na Kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd inayomilikiwa na Kapteni William Slaa.
Katibu wa Ndesamburo, Basil Lema alisema
ilipata ajali baada ya kupigwa na kimbunga wakati anga likiwa
limefunikiwa na wingu zito.
“Mheshimiwa
Ndesamburo amemshukuru Mungu kwa kuwanusuru watu waliokuwa kwenye ndege
hiyo ambao ni pamoja na Mbunge Joshua Nassari.
“Ameweka wazi kwamba atalazimika kununua nyingine mapema kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu,” alisema Lema akimnukuu Ndesamburo.
Lema alisema rubani aliyekuwa akiendesha
helikopta hiyo alifanikiwa kuielekeza juu ya miti alioutumia kupunguza
kasi ya kushuka chini na kusaidia abiria kutoka salama.
“Imeharibika lakini abiria wote ni
wazima. Walikuwamo wanne,” alisema na kuongeza kuwa helikopta hiyo ndiyo
iliyotumiwa na Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 na Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa mwaka jana na chama hicho kilitegemea kuitumia katika
Uchaguzi Mkuu ujao.
Pia, imewahi kutumiwa na makada
mbalimbali wa CCM akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba na
kada maarufu wa Moshi mjini, Buni Ramole.
Akizungumza na waandishi wa habari
katika wodi alikolazwa kwenye Hospitali ya Seliani – Arusha, Nassari
alisema waliporuka kutoka Leguruki, hakukuwa na dalili zozote za
kuchafuka kwa hali ya hewa, lakini dakika chache baada ya kuruka angani
wingu zito lililoambatana na upepo mkali liliwafunika ghafla.
“Wingu
lile na upepo ule sijawahi kuona katika maisha yangu yote zaidi ya
kusoma kwenye vitabu vya simulizi vya mambo ya ushirikina. Namshukuru
Mungu wote tuko salama kwani hatukuwa na matumaini ya kupona ajali ile,”Nassari.
NIPASHE
Watoto watano wa familia moja wamefariki
dunia na mama yao mzazi kujeruhiwa vibaya, baada ya nyumba waliyokuwa
wakiishi kuteketea kwa moto wakati wamelala usiku.
Tukio hilo lilitokea Julai 6, mwaka
huu, saa 3:00 usiku katika kitongoji cha Muleba kijiji cha Muleba kata
ya Rwabwere Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni
kibatari kilichokuwa kimewashwa kudondoka chini na moto kushika nyumba
hiyo ambayo ilikuwa imejengwa kwa makuti ya migomba na kuteketea kwa
moto.
Watoto waliokufa papo hapo kutokana na kuungua vibaya kwa moto ni Zaituni Mohamed (mwaka mmoja na miezi 3); Atwaibu Mohamed (4); Sajira Mohamed (3) na Shine Mohamed (7). Khadija Mohamed (5) alifariki dunia baada ya kufikishwa Hospitali Teule ya wilaya hiyo ya Nyakahanga kwa matibabu.
Mama mzazi wa watoto hao, Sania Mohame, amejeruhiwa na kulazwa hospitalini hapo akiendelea kupata matibabu.
Katika wodi ya hospitali hiyo alikolazwa kwa matibabu, Sania alisema ameungua mwilini wakati akiwaokoa watoto wake.
Hata hivyo, alisema hakufanikiwa kuwaokoa watoto hao kutokana na moto kumzidi.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Edson Salvatory,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwashauri wananchi kutumia taa
zinazotumia mwanga wa jua (solar) au tochi za gharama nafuu ili
kuepuka madhara yatokanayo na vibatari.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Andrew Cesari,
pia alithibitisha kupokelewa kwa majeruhi wawili, mama na mwanawe na
mmoja kufa kabla ya kuanza kupatiwa matibabu kutokana na kuungua vibaya
sehemu kubwa ya mwili wake.
Dk. Cesari alisema mama wa watoto hao wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
NIPASHE
Kikao cha 46 cha Mkutano wa 20 wa Bunge
la kumi, jana kilihairishwa na wabunge wa CCM kujifungia kutaka kujua
kama kiinua mgongo chao ni Sh. milioni 160 au 238 kwa kila mbunge.
Taarifa zinadai kuwa wabunge hao hawajalipwa kiinua mgongo hadi jana na hawajui kitakuwa ni kiasi gani.
Gazeti moja liliripoti kuwa wabunge hao
waliwasilisha ombi la kuongezea mafao yao kutoka Sh. milioni 160 hadi
238, ambalo lilikubaliwa na rais, lakini Hazina ilipopiga hesabu wakaona
wanachostahili kulipwa Sh. milioni 160 kila mmoja.
Hata hivyo, Bunge jioni lilishindwa
kuendelea kutokana na wabunge wa CCM kujifungia kwenye kikao cha
kujadili suala hilo huku Spika akiwa na kikao cha uongozi wa Bunge.
Kuhairishwa kwa kikao hicho, kulitokana
na kauli ya Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Mkumba, kutoa hoja ya
kuhairishwa ili wabunge wa CCM wajadili kwa kina maslahi ya walimu kwa
maana ya mishahara, posho na kiinua mgongo chao.
Naibu Spika aliwahoji wabunge ambao
waliunga mkono na kwenda kwenye kikao cha chama na alitangaza kuahirisha
kikao hadi leo kwa ajili ya kukaa kama kamati kupitisha vifungu vya
muswada huo.
Asubuhi, wakati wa mjadala wa muswada wa
Tume ya Utumishi wa Walimu 2015, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis
Kigangwala, aliomba muongozo wa Mwenyekiti, Mussa Zungu, juu ya
minongono iliyopo ambayo itapelekea ratiba ya leo kubadilika.
Mbunge huyo ambaye ni mjumbe wa Kamati
ya Uongozi, bila kuweka bayana suala husika, alisema ni vyema
likaandaliwa na wabunge ili kuifanya kamati hiyo kulijadili na kutoa
uamuzi.
Baada ya mjadala kuhitimishwa na
Mawaziri kujibu hoja mbalimbali, Dk. Kigangwala aliomba muongozo na
kutaja vifungu vya kanuni vinavyoweza kuondolewa kwa hoja iliyopo kwa
wakati huo ili kupatia ufumbuzi suala lolote.
“Kanuni inaruhusu hoja inayoendelea,
nipewe fursa ya kuondoa hoja ya shughuli zilizopangwa kesho, tutatue
ufumbuzi ili kesho kamati ya uongozi ikikutana liwe limeisha,” alisema.
Aidha, Mwenyekiti alisema anatambua hoja
inayozungumziwa lakini hawezi kuruhusu ikajadiliwa kwa kuwa itapata
ufumbuzi na kiti cha Spika kitatoa majibu.
Wakati wa kikao hicho jioni, baada ya
Naibu Spika, Job Ndugai, kuruhusu shughuli kuendelea, Mbunge wa Sumve,
Richard Ndassa, aliomba muongozo juu wa kutaka shughuli za Bunge
kusitishwa, ili washughulikie jambo lenye maslahi kwao na wafanye kazi
kwa amani na akili zikiwa zimetulia.
Naibu Spika, aliwataka wabunge kuwa na
subira kwa kuwa Tume ya huduma za Bunge imekutana na Spika huku
akiwataka watulie kwa kuwa walianza vizuri hivyo wamalize vizuri. Hata
hivyo, Ndassa hakuridhishwa na kauli hiyo na kutaka kikao kiahirishwe
kusubiri kauli ya Tume au Spika kuzungumzia hatma yao.
“Sisi wabunge wako tunajitolea,
tumejitolea vya kutosha, tulivyokutana ukumbi wa Msekwa mliahidi mambo
yatakuwa sawa leo, kesho (leo) Bunge linavunjwa, siku haziko na sisi,
unaweza kuona ni dogo kumbe ni kubwa, tumejitolea ndani na nje kwa ajili
ya serikali na chama chetu,” alisema.
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia,
aliwataka wabunge kutulia na kumaliza kazi iliyo mbele yao kwa
kutanguliza busara mbele, kwa kuwa suala hilo linafanyiwa kazi.
Naibu Spika aliwahoji wabunge ambao waligawanyika wanaosema kikao kiahirishwe na wengine wakitaka kusiahirishwe.
Ndugai baada ya kupokea ushauri wa
Mbunge wa Longido, Michael Laizer, aliitaka serikali kulibeba kwa uzito
unaotakiwa suala hilo vinginevyo hali itakuwa mbaya siku ya kuvunja
Bunge.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah,
alipoulizwa alisema anakwenda kwenye kikao na kumtaka Mkurugenzi
msaidizi wa Bunge, Said Yakubu, kusikiliza waandishi. Akizungumza na
waandishi, Yakubu, alisema masuala ya kiutawala ya wabunge
yaneshughulikiwa ipasavyo na kuwataka waandishi kusubiri leo kama hali
hiyo itaendelea.
Alipotakiwa kuweka wazi masuala ya
utawala, alisema hawezi kuyataja kwa kuwa yametajwa kwenye sheria na
kanuni za Bunge, hivyo yote yanashughulikiwa na kila mbunge atapata
stahili yake.
NIPASHE
Vituo vitatu vya televisheni vimetozwa faini na kupewa onyo kwa kurusha taarifa zilizokiuka kanuni za huduma ya utangajaji.
Vituo hivyo ni Chanel Ten kupitia
kipindi chake cha Kanjanja Time kimepewa onyo na kutozwa faini ya Sh.
milioni 2.5, Star Tv kupitia kipindi chake cha Min Buzz kimepewa onyo
na faini ya Sh. 500, 000 na Tanzania Broadcasting Corporation (TBC1)
onyo na faini ya Sh. 500, 000 kwenye mojawapo wa taarifa za habari
zilizorushwa na kituo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Margeret Munyangi, alisema wameamua kuchukua hatua hizo baada ya kamati hiyo kukaa na kujadili ukiukwaji wa kanuni za utangazaji za mwaka 2005.
Alisema Mei 30, mwaka huu, kituo cha
Chanel Ten kupitia kipindi cha Kanjanja Time kilichorushwa hewani
kuanzia saa 2:45 hadi saa 3:10 usiku taarifa iliyoonyesha picha ya
mgonjwa akiwa katika wodi ya Hospitali ya Serikali mjini Songea huku
sehemu ya makalio yake yakiwa wazi na kuonyesha vidonda.
Pia kipindi hicho kilionyesha taarifa ya
walemavu wawili wakipigana hadharani huku watangazaji wakishangilia na
kukirudia mara kadha na uchochezi dhidi ya serikali kwa madaktari ili
wafukuzwe na hospitali hiyo ifungwe.
Aliongeza kuwa kipindi hicho kilionyesha
taarifa ya watu wenye ulemavu ambao walikuwa wanapigana hadharani na
mtangazaji wa kipindi alisikika akishabikia kitendo hicho huku
akifananisha na pambano la ngumu za kulipwa.
Kwa upande wa Star Tv, alisema Juni 3,
mwaka huu kituo hicho kilikiuka maudhui, 2005 kupitia kipindi cha Mini
Buzz kilichorushwa hewani kati ya saa 12:30 jioni hadi saa 1:00 usiku.
Alisema kipindi hicho kilikiuka kanuni
za utangazaji kwa kujadili mada iliyohusu ubakaji katika ndoa kwa muda
ambao watoto hupata fursa ya kuangalia na kusikiliza.
Aliongeza kuwa washiriki wa kipindi
hicho ambao walikuwa ndani ya gari walijadili maana ya ubakaji katika
ndoa na uhalali wa mwanaume kumuingilia mkewe bila ridhaa yake huku
mtangazaji akirejea masuala hayo kama nchi ya Uganda.
Kwa upande wa TBC1, alisema Machi 21,
mwaka huu kituo hicho kilivunja kanuni za huduma ya utangazaji 2005,
kupitia kipindi cha taarifa ya habari kilichiorushwa hewani kati ya saa
2:00 hadi 3:00 usiku taarifa hiyo ilionyesha mtoto wa kiume wa miaka 11
ambaye alilawitiwa na vijana wawili wenye umri wa kati ya 22 na 25.
Alisema kituo hicho kilionyesha
utambulisho wa picha, majina ya ya wazazi wa mtoto, mahali anapoishi na
kuonekana sehemu kubwa ya mwili wa mtoto huyo na sauti yake ikisikika,
hivyo kurahisisha utambuzi wake katika jamii.
Akisema kituo hicho kimekiuka kanuni za huduma ya utangazaji 2005, Na. 9(2), (3) zinzosomeka kuwa:
NIPASHE
Ongezeko na ushuru wa mabasi mapya yanayoingizwa kutoka China limewashtua wamiliki wa mabasi kiasi cha kumtaka Rais Jakaya Kikwete aingilie kati.
Hatua hiyo imefikiwa na wafanyabiashara hao kupitia Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), wakidai kuwa hawakushirikishwa katika mchakato uliosababisha hali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Taboa, Ennea Mrutu,
alisema ongezeko hilo la kutoka Sh. milioni 40 hadi kufikia Sh. milioni
100 litazuiwa ikiwa Rais Kikwete pekee ataingilia kati kupata suluhu
yake.
Ingawa msemaji wa Mamlaka ya Mapato (TRA) hakupatikana
kuelezea hali hiyo, lakini Mrutu alisema ongezeko hilo limefikiwa
mapema wiki hii hivyo kuibua hofu kwao wamiliki kumudu gharama hizo.
Alisema litakuwa jambo lenye heshima kwa
jumuiya ya wamiliki wa mabasi ikiwa Rais Kikwete atalizungumzia suala
hilo kabla ya kulivunja Bunge leo.
“Kama
hali hii ikiendelea hivi hakuna mmiliki atakayeingiza basi jipya kutoka
China. Kama unakumbuka miaka iliyopita mabasi mengi yalikuwa na chesesi
za malori na yalisababisha ajali ambazo zimepoteza maisha ya
Watanzania wengi, hatutaki kuona hali hii inajirudia,” Mrutu.
Taarifa za ndani kutoka Taboa na baadhi
ya wamiliki zinaeleza kuwapo wafanyabiashara wanaokadiriwa kuingiza
mabasi 15 wakati mengine 60 yakitarajiwa kuingizwa wiki ijayo.
“Kwa
hali ya kawaida hatuwezi kuyatoa mabasi hayo kwa maana hatuna fedha za
kulipa ushuru mkubwa kiasi hicho, kama utaratibu huu ukiendelea
hatutaweza kusafirisha abiria,” Mrutu.
Kwa habari matukio na michezo ni hapa hapa tangakumechablog
No comments:
Post a Comment