Monday, July 20, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, JULY 20 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma zikiwemo za Umeme na Ufundi. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

to know
MWANANCHI
Wanasiasa wa upinzani nchini wamepinga kitendo cha mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kutumia ndege ya Serikali kwenye shughuli za kichama za kujitambulisha wakisema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa.
Dk Magufuli, juzi alikwenda Mwanza kwa ziara maalumu ya kujitambulisha akitumia ndege ya Serikali aina ya Fokker F28, jambo ambalo limeibua hisia tofauti.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kapteni Keenan Mhaiki alisema kitendo cha CCM kutumia ndege ya Serikali hakivunji sheria na taratibu zozote kwa kuwa mbali na kusafirisha viongozi wa Serikali, pia wanaruhusiwa kufanya biashara kwa kuhudumia umma.
Pia, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema walifuata taratibu zote kuikodi ndege hiyo na kwamba chama chake ni kikubwa na hakiwezi kushindwa kukodi usafiri huo.
“Ile ni ndege ya Serikali, yeyote anayetaka kuitumia aende kulipia tu, atapewa. Sisi tumekwenda kama wateja wa kawaida tukalipia, ukitaka kujua ni kiasi gani kawaulize wahusika watakueleza,” Nape.
Kuhusu suala hilo la gharama, Kapteni Mhaiki alisema gharama ya kukodi ndege hizo zipo tofauti kutokana na aina inayohitajika akisema aliyoitumia Dk Magufuli inagharimu Dola za Marekani 4,000 sawa na Sh8.4milioni kwa saa moja.
Kiongozi wa chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema viongozi wa Serikali wamekuwa na utamaduni wa kutumia mali za umma kwa shughuli za kisiasa na kusahau kwamba rasilimali hizo ni za Watanzania wote bila kujali itikadi zao.
Zitto alisema jambo hilo halijaanzia kwenye ziara ya Dk Magufuli, bali hata mawaziri wote waliochukua fomu walitumia magari ya Serikali kuzunguka nchi nzima kutafuta wadhamini wao kwa nafasi ya urais.
“Jambo hili si kwa CCM pekee, tunaona pia gari la Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), likitumika kwenye mikutano yake ya kichama. Lile ni gari la Serikali; kwa hiyo lazima tuupige vita utamaduni huu,” alisema Zitto.
Alisema CCM ina wajibu wa kuwaeleza Watanzania sababu za kutumia ndege ya Serikali na kama wamelipia fedha ni kiasi gani kilicholipwa huku akisisitiza kuwa utamaduni huu uliokithiri unaligharimu Taifa.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema limekuwa ni jambo la kawaida kwa CCM kutumia vyombo vya Dola katika kufanikisha mambo yao na kwamba sababu za kwamba ndege za Serikali zipo wazi kwa umma ni ‘danganya toto’ ili kufurahisha wananchi.
“Eti ndege hizo zinaweza kukodiwa na mtu binafsi au chama, nani kakwambia? Nenda kakodi kama utapata. Ukweli ni kwamba Magufuli hakuikodi hiyo ndege, kama ni kweli wamekodi watuonyeshe walilipaje?” alihoji Mbowe na kuongeza. “Chadema haijawahi kwenda kukodi kwa sababu ina uhakika haitaipata, hasa ikizingatiwa “viwanja tu vya michezo vinavyomilikiwa na CCM havijawahi kutolewa vitumike kwa mikutano ya upinzani tangu mfumo wa vyama vingi uanze zaidi ya miaka 20 iliyopita.
MWANANCHI
Mbunge wa Kahama aliyemaliza muda wake, James Lembeli amekataa kubadili msimamo wake wa kutogombea ubunge kupitia CCM akisema atagombea nafasi hiyo kupitia chama kingine.
Lembeli alisema hawezi kubadili msimamo wake wa kuondoka CCM, kutokana na masharti mazito ya kimila aliyopewa kabla ya kutangaza kuondoka katika chama hicho.
Baada ya uamuzi wake, watu mbalimbali, wakiwamo maofisa wa Serikali na wafanyabiashara waliahidi kumsaidia hata nguvu ya kifedha, wakimtaka atengue uamuzi wake achukue fomu katika Jimbo la Kahama Mjini.
Alisema hawezi kukiuka masharti ya kimila kwa kuwa yeye ni mtoto wa chifu. Mtoto huyo wa Chifu Daud Lembeli alisema kabla ya kutoa uamuzi huo alikaa na mama yake mzazi, Maria Kalembo kuanzia saa 10 jioni hadi saa nane usiku akizungumzia suala hilo hadi walipokubaliana.
Alisema baada ya mama yake kukubali na kutoa baraka za kuhama CCM, alipigiwa ngoma za kimila za Waswezi, ambazo hutumika kutoa baraka katika imani za kichifu akisema ndizo zilizohitimisha fursa za kugombea kwake ubunge kupitia chama hicho.
“Najisikia amani kubwa kuondoka CCM, kabla sijachukua uamuzi huu nilikuwa nikiishi kwa presha, hivi sasa nipo huru, niacheni tu kama ni ubunge sikuzaliwa nao na unaweza kuishi bila ubunge na maisha yakawa mazuri,” alisema Lembeli.
Juzi, Lembeli alifika katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Kahama na kutangaza kuwa hawezi kugombea kupitia chama hicho kwa kuwa kimejaa rushwa na matukio ya wagombea kugawa kadi kwa wanachama ili wachaguliwe.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Mabala Mlolwa alielezea kusikitishwa na uamuzi huo wa Lembeli kuamua kuhama bila kushauriana na uongozi wa wilaya.
Alisema CCM inatambua mchango mkubwa aliotoa katika miaka 10 ya uongozi wake na imeshangazwa na tukio hilo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja alisema pamoja na kulisikia suala hilo, hivi sasa yupo mapumzikoni kisiasa kutokana na dhoruba kubwa ya kitaifa waliyoipata katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais.
Niacheni kwanza nipumzike suala hilo nalisikia lakini muda mwingi sikuwapo. Najua suala la Lembeli kuhama litaibomoa CCM Kahama, ataondoka na wengi lakini mimi sizungumzi lolote juu ya hilo,Mgeja.
MWANANCHI
Baada ya mchakato wa kuwania urais, sasa vita ya Uchaguzi Mkuu imehamia kwenye ubunge na udiwani hasa kutoka katika vyama vikubwa vya CCM kinachotawala na Chadema kinachoongoza upinzani.
Hadi jana, ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa vyama hivyo kuchukua na kurejesha fomu, jambo moja lilijidhihirisha katika baadhi ya majimbo kwa upande wa CCM; baadhi ya majina makubwa katika siasa za ubunge yanachuana hivyo kufanya mchakato wa kumpata mteule mmoja kuwa mgumu.
Mchuano huo na kuimarika kwa Chadema mikoani hasa kutokana na majeraha ya mchakato wa urais ndani ya CCM, vinaufanya upinzani wa kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuwa sawa na vita.
Makada wawili wa chama hicho, Lucas Selelii na Dk Hamisi Kigwangalla wamechukua fomu kuwania ubunge wa Nzega Vijijini.
Katika uchaguzi uliopita wa 2010, makada hao walivaana katika Jimbo la Nzega lakini wote wakaangushwa na Hussein Bashe aliyeibuka wa kwanza akifuatiwa na Selelii.
Hata hivyo, matokeo hayo yalibatilishwa na Halmashauri Kuu ya CCM na kumchukua Dk Kigwangalla aliyekuwa mshindi wa tatu.
Mgawanyo wa majimbo uliofanywa wiki iliyopita na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), umerahisisha mpambano wa makada hao, hivyo wawili hao wakamwachia Bashe Nzega Mjini.
Akichukua fomu hiyo jana, katika ofisi za CCM za Wilaya ya Nzega, Dk Kigwangalla akiwa ameambatana na wazee wa jimbo hilo, alisema shinikizo la kugombea Nzega Vijijini limetoka kwa wananchi wanaotambua umuhimu wake.
Selelii aliyekuwa Mbunge wa Nzega kwa miaka 15 hadi 2010, alichukua fomu kimyakimya bila kuzungumza na vyombo vya habari.
Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega, Empimark Makuya alithibitisha kuwa kada huyo alishachukua fomu. Wawili hao watakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wengine wawili waliochukua fomu, John Dotto na Paul Kabelele.
Baada ya kukwama katika harakati za kuwania urais kupitia CCM, Balozi Dk Augustine Mahiga amejitokeza kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.
Dk Mahiga aliyechukua fomu jana na kurudisha, atapambana na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela na mwandishi wa habari, Frank Kibiki ambao tayari wamechukua na kurejesha fomu zao.
Mchuano katika jimbo hilo unatarajiwa kuwa mkali wakati na baada ya kura za maoni ndani ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba Mwakalebela alikuwa amechukua namba moja katika kura za maoni za chama hicho mwaka 2010 kabla ya jina lake kukatwa na NEC.
NIPASHE
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,  amekataa ombi la wakazi wa jimbo lake la uchaguzi la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango ya maendeleo aliyoianzisha.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilimnukuu Pinda akijibu maombi ya wakazi hao baada ya Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kigango cha Kanisa Katoliki cha Kibaoni Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Pinda alisema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa Jimbo la Katavi.
Alisema ataendelea kuwa karibu na wakazi wa jimbo hilo wakati wote na kwa vile atakuwa na muda wa kutosha kushiriki kikamilifu katika mikakati ya kuwaletea maendeleo ili wajikwamue kutoka kwenye umaskini.
Kwa upande mwingine, Pinda aliwaasa wakazi wa jimbo hilo wawe makini kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akimshukuru Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani humo, Padri Aloyce Nchimbi, aliwaasa wakazi wa  Mlele kumuenzi Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea maendeleo.
Pinda yuko kijijini kwake Kibaoni ajili ya mapumziko mafupi na alitoa msimamo wake huo jana ikiwa ni siku ya mwisho kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa na kupokea fomu kwa makada wake wanaoomba wateuliwe kugombea ubunge na udiwani katika uchaguzi huo utakaovishirikisha pia vyama vya upinzani.
Msimamo huo wa Pinda umekuja siku chache baada ya jina lake kukatwa katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM hivi karibuni mjini Dodoma.
Pinda alikuwa kati ya wanachama 38 wa CCM waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, jina lake lilikuwa miongoni mwa majina yaliyokatwa kwa mara ya kwanza na kubakia matano ambayo yalipelekwa kwenye Kamati Kuu (CC) ya CCM.
Majina yaliyopelekwa kwenye kamati hiyo yalikuwa ni ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Said Salum na January Makamba.
Majina hayo yalipelekwa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM ambapo wajumbe wake walipitisha majina matatu kati ya matano.
Waliopenya katika kinyang’anyito hicho ni Dk. Magufuli, Dk. Migiro na Amina na kupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu na wajumbe kupiga kura na kumpata Dk. Magufuli atakayepeperusha bendera ya chama hicho kumtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pinda aliteuliwa kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu na Rais Jakaya Kikwete, baada ya aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Edward Lowassa, kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond mwaka 2007.
NIPASHE
Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya aliyekuwa Mbunge  wa Viti Maalum CCM mkoa wa Mara, Ester Bulaya, kutangaza kukitosa kwa kutangaza uamuzi wake wa kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
Bulaya ambaye alikuwa mbunge machachari kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvunjwa na Rais Jakaya Kikwete, hivi karibuni , ametangaza kutogombea ubunge kupitia CCM wakati akizungumza baada ya kazi ya kuchukua fomu ndani ya chama hicho na kurejesha kuhitimishwa rasmi nchini jana.
Tangu mwanzo mwa mwaka huu, Bulaya alitangaza kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda kupambana na Mbunge aliyemaliza muda wake ambaye ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Bulaya amekuwa kada wa pili ambaye alikuwa mbunge kutangaza kutogombea ubunge kwa tiketi ya CCM, mbunge wa kwanza kutangaza kutogombea ubunge  kupitia CCM baada ya James Lembeli, ambaye alikuwa Mbunge wa Kahama.
Hata hivyo, Bulaya hakuweka wazi kama ana mpango wa kuhamia chama kingine cha siasa na kutimiza azma yake ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ingawa Bulaya hajaweka wazi, vyama ambavyo vimekuwa vikitajwa kusubiri makada kutoka CCM kujiunga navyo ili wawanie ubunge ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (Cuf).
Wakati ikiwa hivyo kwa Bulaya, hali bado si shwari ndani ya CCM Wilaya ya Monduli baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Edward Sapunyo, Kupigilia msumari wa mwisho na kubariki hatua ya madiwani wake 20 kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Sapunyo ambaye alikuwa Diwani wa kata ya Moita, alisema madiwani wake hawawezi kusubiri hadi Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, atoe kauli kuhusu hatma yake ya kisiasa ndani ya CCM.
Kauli ya Sapunyo ambaye hatagombea udiwani uchaguzi wa mwaka huu, imekuja siku moja baada ya madiwani 20 wa jimbo hilo kutangaza rasmi kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Hatuwezi kuona baba yetu anapigwa na kuanguka chini halafu tusubiri kauli yake, ni lazima tuchukue hatua mara moja…hii haivumiliki, kitendo alichofanyiwa (Lowassa) na vikao vya CCM mjini Dodoma hivi karibuni kwa kukata jina lake pasipo kumpa haki ya kumsikiliza siyo cha kidemokrasia,” alisema.
Lowassa na makada wenzake wa CCM 38 walichukua fomu ya kuomba  ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Katika kinyanyang’anyiro hicho, jina la Lowassa na wenzake yalikatwa katika hatua ya mwanzo, hali ambayo imezua malalamiko kwamba ikidaiwa kuwa hawakupewa nafasi ya kuhojiwa.
“Tumepigwa, tumesambaratika (CCM) Monduli, hatuwezi kuchukua fomu za kuomba kugombea au kutetea nafasi zetu ndani ya chama hiki, tumehamia Chadema,” alisema.
Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, alidai kuwa siyo kweli kwamba madiwani wote wamekihama chama chao.
Kimaro alidai kuwa baadhi ya madiwani waliotangaza kukihama chama hicho wameanza kusalitiana.
Alisema madiwani hao ambao anawaita ni makada baada ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Monduli kuvunjwa, walifanya mkutano kwa kushawishiwa na mmoja wao.
Alisema ushawishi huo unatokana na uchu wa madaraka alionao kwa kuwa tayari wananchi wa Jimbo la Monduli, wanapenda aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM, Namelok Sokoine, kuchukua fomu za ubunge wa jimbo hilo.
Alisema kutokana na ugumu huo, diwani huyo wa zamani ametumia mbinu ya kuwarubuni wenzake wakihame chama hicho ili agombea ubunge kwa tiketi ya Chadema.
“Huo ni uchu wa madaraka aliyo nayo,” alisema na kuongeza: “Diwani huyo hakubaliki na wananchi wa kata yake.”
Alidai kabla ya kutangaza kukihakama chama hicho, madiwani hao walikuwa wameshafanya kikao na kuweka azimio la pamoja la kuondoka CCM, lakini juzi walipotangaza uamuzi wao, walijikuta wapo madiwani watatu.
Alisema baadhi ya madiwani walimfuata ofisini kwa lengo la kumuomba radhi lakini yeye aliwaambia waende kuwaomba radhi wananchi katika kata zao.
Madiwani wachache walikuja hapa ofisini kuomba radhi kwa Katibu wa CCM Wilaya, nikawaambia waende kuwaomba radhi wananchi,” alisema.
NIPASHE
Wakati bado haijafahamika lini mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) atatangazwa rasmi, imefahamika kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amekuwa ndiyo kikwazo cha kutopatikana kwa mgombea huyo.
Uchunguzi uliofanywa kwa siku nne sasa umebaini kuwa hatua ya Prof. Lipumba kukwepa vikao vya Ukawa, ni mkakati mahsusi unaolenga kukwamisha mchakato wa kupatikana mgombea urais wa umoja huo.
Ukawa unaundwa na Cuf, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD.
Taarifa kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vimeeleza kuwa kikao cha kwanza cha umoja huo, Profesa Lipumba aliulizwa kwanini anataka kugombea urais na kujibu kuwa anaamini kuwa yeye ndiye bora kuliko wengine.
Hata hivyo, alipoulizwa kama amejiandaa vipi kirasilimali iwapo atateuliwa kuwania nafasi hiyo kupitia Ukawa, hakuwa na majibu ya kujitosheleza na badala yake ilibainika kuwa Cuf imejiandaa zaidi Zanzibar kuliko Tanzania Bara.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Profesa Lipumba amekuwa aking’ang’ania agombee urais na hata mkutano wa mwisho wa Ukawa ambao hakuhudhuria, inadaiwa kwamba ni mkakati wa kushinikiza ateuliwe yeye kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Tangu Alhamis wiki iliyopita, gazeti hili limekuwa likimtafuta Profesa Lipumba atoe ufafanuzi wa madai yanayotolewa kwamba anakwamisha mchakato wa kumpata mgombea urais, lakini simu yake imekuwa ikiita bila kupokelewa na hata akitumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hajibu.
Ofisa Habari wa Cuf, Silasi Mpinga, alipoulizwa namna gani Profesa Lipumba atapatikana kujibu madai hayo, alisema aendelee kutafutwa tu atapatikana.
Katika vikao vya Ukawa, hoja kubwa imekuwa ni suala la mgombea urais, nafasi ambayo inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye tayari ameshachukua fomu kupitia chama chake cha Cuf pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, anayeungwa mkono na vyama vyote vinne.
Profesa Lipumba ameshagombea urais mara nne bila  mafanikio, wakati Dk. Slaa aligombea mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, akiwa ameitikisa CCM iliyopoteza asilimia takriban 20 ya kura za mwaka 2005.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, akizungumza na waandishi wa habari Julai 14, mwaka huu, alisema umoja huo utamtangaza mgombea wao wa urais baada ya siku saba ambazo zinaisha wiki hii.
Alisema wamekubaliana kutangaza mgombea baada ya siku saba ili kutoa nafasi kwa viongozi walioshiriki majadaliano hayo kutoa taarifa kwa wanachama wa vyama vyao juu ya mambo waliokubaliana.
Aidha, Mbatia alikanusha uvumi kuwa kada wa CCM na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ana mpango wa kujiunga na umoja huo ili apewe nafasi ya kugombea urais baada ya kukosa nafasi hiyo kupitia chama chake.
Mbatia pia alikanusha uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna mvutano mkubwa ndani ya Ukawa katika suala la mgombea urais ambao umesababisha Cuf kutaka kujitoa.
“Hakuna ukweli katika hilo na hata leo (jana), nimeongea na Profesa Lipumba kumtaarifu hatua tulioyofikia, hivyo hakuna mpasuko wowote,”Mbatia.
Kabla ya taarifa hiyo ya Mbatia,Ijumaa iliyopita Ukawa walitoa taarifa ya kwamba wangemtangaza mgombea wake ndani ya saa 24, ahadi ambayo haikutimizwa.
NIPASHE
Chama  cha Wananchi (CUF), kimeibuka na kumtetea aliyekuwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilimuonea kwa kukata jina katika ngazi ya Kamati ya Maadili na kushindwa kulifikisha  Kamati Kuu ya CCM (CC).
Lowassa alikatwa jina lake akiwa ni miongoni mwa wagombea 38 wa urais kupitia CCM, lakini inadaiwa kwamba aliondolewa katika hatua za awali kwenye Kamati ya Maadili.
Kadhalika, CUF kimesema kipo tayari kumpokea Lowassa ndani ya chama hicho kwa kuwa ni msafi na hajawahi kufikishwa hata mahakamani kwa ajili ya kushitakiwa kutokana na madai ya rushwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Pilikapilika za uchaguzi nchini kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Star Tv.
Kambaya alirejea ripoti ya Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe mwaka 2008 kuchunguza kashfa ya Richmond ambayo ilimng’oa Lowassa katika nafasi ya Waziri Mkuu.
Alisema katika kamati hiyo, Dk. Mwakyembe aliweka bayana kwamba kila mtu aliyehusishwa ama kutajwa katika kashfa ya Richmond angefikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Kambaya alisema mpaka sasa Lowassa hajawahi kufikishwa mahali popote kushitakiwa na kwamba hatua hiyo inaoonyesha kwamba kiongozi huyo hakuwa na kashfa yoyote.
Alisema lengo la CUF ni kuing’oa CCM na kwamba ukiona kuna mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuitikisa chama hicho na kukipasua wapo tayari kumkaribisha ili washirikiane naye.
Alifafanua kuwa mtu ambaye siyo msafi hawezi kukaribishwa CUF na kwamba Lowassa kama angekuwa mchafu angekuwa ameshitakiwa mahakamani tangu alipojiuzuru mwaka 2008. Katika mjadala huo washirki walijadili matumizi makubwa ya fedha yaliyojionyesha ndani ya CCM tangu mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ulipoanza.
Watu wengine waliojitokeza kumtetea Lowassa ni pamoja mwanachama mwenye kadi namba nane ya CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye alitamka wazi kwamba kanuni na sheria ndani ya chama zilikiukwa.
Kingunge alisema haki haikutendeka kwa sababu Kamati ya Maadili kwa mujibu wa kanuni na taratibu za CCM haina mamlaka ya kukata jina la mgombea kwa sababu siyo kikao cha maamuzi. Wakati hayo yakisemwa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amewaonya watu wanaokisema vibaya chama hicho na kwamba kitawachukulia hatua.
HABARILEO
Mgombea urais mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema kama si kuombwa kuwania urais, alipanga kuachana na siasa mwaka huu, kwani alijiwekea lengo la kuachana na ubunge baada ya kuwa mbunge wa Chato kwa miaka 20 sasa.
Alisema hayo mbele ya umati wa wakazi wa mkoani Geita na baadaye Jimbo la Chato waliojitokeza kumlaki, huku yeye mwenyewe akisema anaamini kwa aina ya mapokezi anayoyapata kila anakopita, ana imani CCM itavigaragaza vibaya vyama vya upinzani.
Magufuli aliyekuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1995,alisema alitarajia baada ya miaka 20 ya ubunge wake astaafu, kwani hakutaka tena kuendelea na shughuli za siasa, lakini baada kila kona ya nchi kuombwa kugombea, alichukua fomu kimya kimya na kuirudisha kimya, hivyo kuteuliwa kugombea urais ni matokeo ya maombi ya Watanzania.
Katika mkutano huo uliofanyika Stendi ya zamani ya Chato, mamia ya wananchi wa vyama mbalimbali vya upinzani, hususan Chadema walirudisha kadi zao na kujiunga na CCM.
Magufuli alisema maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mikoa aliyokwenda kujitambulisha ni salamu kwa wapinzani.
“Nilitamani kikombe hiki kiniepuke, maana nilitaka baada ya miaka 20 ya ubunge nipumzike mwaka huu, lakini hili la urais limekuja baada ya kila kona ninayopita naambiwa kagombee urais, sasa nikaona ngoja nijaribu lakini sikulitilia maanani, ndio maana niliamua kufanya kimya kimya kila kitu, kwa bahati nzuri kikombe hiki kimekuja chenyewe, msiniangushe,”
Dk. Magufuli alisema atakuwa mwadilifu na katika utumishi wake na alitumia fursa hiyo kuwaaga rasmi wananchi wa jimbo lake, kwani hatagombea ubunge.
HABARILEO
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), imefungia kwa miezi sita leseni za udereva za madereva sita wa mabasi wa mkoani Arusha na kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma ya ulevi.
Aidha, imewaonya wamiliki wa vyombo mbalimbali vya moto nchini, wasiwaajiri wakati huu wanapotumikia adhabu yao, kuepuka magari yao yasinyang’anywe leseni ya biashara ya usafirishaji abiria kwa kosa la kuajiri walevi.
Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Leo Ngowi, alisema, “Madereva hao walikamatwa wakati wa ukaguzi maalumu, ulioendeshwa na mamlaka yetu Arusha, kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani”.
Aliwataja madereva hao, magari waliyokuwa wakiyaendesha na namba za leseni zao kwenye mabano kuwa ni; Sarikiaeli Mosses Niko  namba za usajili T137BCX lililokuwa likisafiri kati ya Arusha na Ngarenanyuki na dereva mwingine wa gari lenye namba za usajili T586 BWP, Shaaban Daudi Mdoe, lililokuwa linafanya safari kati ya Stendi Kuu na Usa River.
Wengine ni dereva wa gari lenye namba za usajili T107 DCT, ambalo njia zake hazikuelezwa, Prosper Joseph  na wa gari lenye namba T613BSD, Jeremiah Joseph Francis, ambaye gari alilokuwa akiliendesha lina leseni ya kufanya safari kati ya Arusha na Namanga.
Madereva wengine waliofungiwa ni pamoja na Elibariki Wariaeli Kimaro, aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T137 BCX, linalofanya safari kati ya Arusha na Ngarenanyuki na Yohanes Posolo Sanga aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T530AZE, ambalo njia zake hazikuelezwa.
Alisema, kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani, mamlaka hiyo, pamoja na kikosi cha usalama barabarani vilikubaliana kuendesha ukaguzi maalumu wa kushitukiza katika maeneo mbalimbali, wakianzia na Arusha ambapo Mei 2, mwaka huu, madereva watano walikutwa wakiendesha magari ya abiria wakiwa wamelewa pombe.
Kutokana na maelezo yake, wameamua kuchukua hatua ya kinidhamu na kisheria, kuwafungia leseni zao, kuzuia wasiajiriwe mahali kokote na mmiliki yoyote ndani ya Tanzania, iwe fundisho kwa madereva wengine wenye tabia hiyo.
“Madereva hao hawatapaswa kuajiriwa na mmiliki wa chombo chochote cha moto kwa sababu leseni zao tumezifungia kwa miezi sita, kuanzia Mei 2 hadi Novemba 2, mwaka huu. Atakayekamatwa kwa kuwaajiri atakuwa amepoteza sifa ya kufanya biashara ya kusafirisha abiria”, Ngowi alisema. 
SEMA USIKIKE
Baadhi ya wnaanchi wa jimbo la Mtama, lindi wamejikuta wakikesha na kufanya sherehe usiku kucha wakifurahia kushindwa kwa Mbunge wao Benard Membe katika kinyang’anyiro cha kuwania Urais.
Furaha za wananchi hao ziliizbuka baada ya kupata taarifa ya kushindwa kwa membe katika mchakato wa mbio za Urais.
Baadhi ya wananchi hao walioonyesha furaha yao waziwazi walichinja wanyama wakiwemo ng’ombe na mbuzi idadi isiyopungua kumi,kupika chakuna na kuserebuka kwa muziki.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananachi hao walisema wameyapokea matokeo hayo kwa furaha kubwa kutokana na kushindwa kushirikiana na wananchi wake kuwaletea maendeleo na kupunguza kero zinazowakabili ikiwemo kero ya maji, miundombinu ya barabara na afya.
Wamesema hawatamsahau Membe kwa  kushindwa kutekeleza ahadi zake azlizokuwa akizitoa kwao wakati akiomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wao.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment