Monday, July 20, 2015

WANANCHI JIMBO LA MKINGA KUPATA MKOMBOZI WAO


Tangakumekuchablog

Mkinga, KIVUMBI cha uchukuaji fomu za kugombea nafasi za Ubunge zinazidi kushika kasi kila kona na  makada   kupigana vikumbo katika ofisi za CCM huku baadhi wakitegea kuona wapinzani wao.

Jimbo la Mkinga limeanza kuchomoza baada ya kada wa CCM, Bakary Mohammed, kuchukua fomu makao makuu ya CCM barabara ya 20 Tanga na kusema kuwa endapo atachaguliwa kuwa Mbunge ataifanya Sekta Uvuvi kuwa kitega uchumi kikuu Wilayani humo.

Alisema Wilaya hiyo kuwa na bahari ni utajiri tosha lakini neema hiyo imesahaulika na hivyo kuwaahidi wananchi wa jimbo la Mkinga  endapo atapata ridhaa ya kuwa Mbunge wao ataifanya sekta hiyo kuwa kimbilio la wengi.

“Mkinga ni Wilaya changa ila ni kubwa lakini iko na rasilimali ya kujaliwa kuwa na bahari---hii ni utajiri tosha kwa watu wa jimbo la Mkinga kwani nitawashawishi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza” alisema Mohammed na kuongeza

“Endapo nitapata ridhaa ya kuwa mgombea na kufanikiwa kuwa mbunge nadhani niseme kuwa ugumu wa maisha umepatiwa muarobaini----nasema hivi kwa uzoefu wa wenzetu kama tunavyowaona pale tunapotembea” alisema

Akizungumzia kero ya maji safi na upatikanaji wa huduma ya afya, Mohammed alisema akiwa Bungeni atahakikisha vitu hivyo Serikali inavipatia ufumbuzi kwani ndio misingi ya maendeleo na maisha bora kwa kila mtu.

Alisema changamoto hiyo anaitambua na imekuwa kero kwa muda mrefu na hivyo kusema kuwa ni wajibu wa kiongozi kusimama kidete kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma muhimu za kijamii kwa kushirikiana na Serikali.

“Changamoto ya huduma za afya na maji limekuwa likishughulikiwa na Serikali ila endapo kama nitakuwa Mbunge wa jimbo hili nitahakikisha nashirikiana na Serikali angalau kupunguza kero” alisema Mtia nia huyo

Alisema maji ni kero ya muda mrefu mbali ya Serikali kwa kiwango kikubwa kupunguza hivyo akiwa Mbunge atamalizia palipofikiwa kwa kusaidiana na viongozi wengine wa Serikali.

Alisema maendeleo ya watu wa Mkinga yataletwa na watu wa Mkinga na Serikali hivyo kuwataka wananchi kumuunga mkono ili kuweza kuwatumikia kwa kufuata ilani ya CCM.

                                                Mwisho



 Mtia nia jimbo la Mkinga Tanga, Bakary Mohammed (kushoto) akipokea fomu jana  kutoka Katibu Msaidizi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mkinga katika ofisi za Wilaya hiyo Makao Makuu ya CCM, Tanga

Mtia nia jimbo la Mkinga, Bakary Mohammed, akitoa shukrani zake mara baada ya kukabidhiwa fomu ya Ubunge kugombea jimbo ambalo ametaja vipaombele vyake  kulifanya jimbo hilo kuwa kituo kikuu cha Maendeleo kwa kutumia rasilimali ya bahari na ardhi.

No comments:

Post a Comment