Sunday, July 5, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO JJULY 05 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kiko na Hostel pamoja na kutoa kozi ya Kiingereza na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

RGMWANANCHI
 Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano ambalo uhai wake unaisha Julai 9, linaonekana dhahiri kwenda mrama baada ya wabunge 23 kumlazimisha Spika kuwatimua kikaoni wakipinga kuwasilishwa kwa miswada mitatu kwa hati ya dharura.
Kwa siku tatu mfululizo, Spika Anne Makinda amekuwa akipata shida kuendesha chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na mbinu waliyogundua wapinzani ya kupiga kelele kukwamisha shughuli za Bunge.
Juzi, kiongozi huyo wa Bunge aliamua kuwapeleka wabunge 11 mbele ya Kamati ya Maadili kwa makosa ya kudharau kiti chake na chombo hicho kikaibuka na adhabu ya kuwafungia wabunge wanne kutohudhuria vikao vyote vilivyosalia, wengine wawili kufungiwa vikao viwili.
Jana, hali iliendelea kuwa ya mapambano baada ya wabunge hao kuhoji uhalali wa adhabu hiyo, huku wakihoji sababu ya miswada hiyo kuwasilishwa kwa dharura.
Ezekia Wenje, mbunge wa Nyamagana, aliendelea kubishana na Spika na kusababisha atangaze kumzuia kushiriki vikao vitano, uamuzi uliosababisha wabunge wengine wa upinzani kusimama na kupiga kelele wakitaka nao waadhibiwe.
Spika Makinda alisema kuwa ametumia kanuni ya 74(i) kuwatimua wabunge hao kwa kushindwa kuheshimu kiti kwa kupiga kelele.
Wakati wabunge waliopewa adhabu wakiongezeka, wenzao ambao hawakuwapo sasa wamehamasishwa kwenda mjini Dodoma kuendelea na walichokiita mapambano, hali inayoweza kusababisha Bunge hilo likavunjwa likiwa limepukutika wabunge wa upinzani.
Sakata lilivyoanza
Kabla ya kikao kuanza jana asubuhi, Wenje aliomba mwongozo wa Spika na baada ya kupewa nafasi, alipinga adhabu waliyopewa wabunge saba juzi akisema wameonewa na kuhoji sababu za mbunge wa Mbozi, David Silinde kuzuiwa kuingia wakati hakutajwa kwenye taarifa ya Kamati ya Maadili iliyopendekeza adhabu hizo juzi.
Hata hivyo, Spika Makinda alimjibu kuwa hilo lilitokana na makosa ya uchapaji, lakini Silinde alimtaja na ni miongoni mwa waliokuwa wakifanya vurugu juzi na aliitwa kuhojiwa kwenye maadili.
Wenje aliendelea kupinga huku akibishana na Spika, ndipo zogo likaibuka upya na Spika akaagiza atolewe nje ya Ukumbi wa Bunge na asihudhurie vikao vitano kuanzia jana.
Baada kufukuzwa Wenje, wabunge wa upinzani na walisimama wote huku wakipiga kelele.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba amesema CCM inakabiliwa na kazi ngumu ya kupata mgombea wa urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka huu, akionya kuwa makundi ya urais yasipomalizwa yanaweza kufika hadi ngazi ya kata.
Makada 38 wamejitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho tawala ya kugombea urais katika kipindi ambacho kuna ongezeko kubwa la nguvu ya vyama vya upinzani, huku vyama vinne vikiwa vimeamua kusimamisha mgombea mmoja.
Tayari vikao vya kujadili jinsi ya kumpata mteule wa kupeperusha bendera ya chama hicho vimeshaanza kwa wenyekiti na makamu wao kukutana na jana Kamati Kuu ilikuwa inakutana mjini Dodoma.
Akiangalia hali hiyo, Jaji Warioba aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho tawala kinatakiwa kuwa makini katika mchakato huo, kwa maelezo kuwa unaweza kuacha majeraha makubwa kutokana na makundi yaliyoibuka.
“CCM inakabiliwa na wakati mgumu wa kupitisha jina la mgombea urais kutokana na waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 38, na mpaka sasa imekuwa ni vigumu kutabiri atakayepitishwa, jambo ambalo halikujitokeza wakati wa upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995 na 2005,” alisema Jaji Warioba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kila unapofika Uchaguzi Mkuu kunakuwa na changamoto zake, lakini mwaka huu CCM inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kwa sababu uchaguzi huo utamleta rais mpya na mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Alisema jambo la kwanza lililotokea katika mchakato wa kumpata mgombea urais litakalokifanya chama hicho kuwa na wakati mgumu ni kitendo cha baadhi ya wagombea kueleza sera zao, wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya uchaguzi.
“Waliotangaza nia wamekuwa wakieleza sera zao na ukiwasikiliza unaona kama walikuwa wagombea binafsi hivi kwa sababu CCM ina sera, wanayo ilani ambayo ipo tayari na yeyote atakayepeperusha bendera ya CCM lazima ajikite kwenye ilani ya chama,” alisema jaji Warioba.
“Kama mtu ametangaza sera na vipaumbele vyake na havifanani na vipaumbele vya ilani ya chama unafanyaje? Ni mtihani mwingine huo.”
Alisema jambo la pili ni kukiukwa kwa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote anayehusika kwenye ngazi ya maamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais, huku akiwatolea mfano wajumbe wote wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao ndio humchagua mgombea urais wa chama hicho.
“Nimeambiwa kwamba wajumbe wa mkutano mkuu walikatazwa kudhamini wagombea, lakini tulivyoona ni kwamba viongozi wengi wameonyesha waziwazi wapo kundi gani, wapo waliojitokeza na kusema na wengine hawakusema lakini wanajulikana wanamuunga mkono mgombea gani,” alisema.
“Hawa ndio watakwenda kuchuja, sasa hapa itakuwa kazi ngumu na inawezekana kukawa na mgongano wa maslahi na hilo lisipoangaliwa linaweza kufanya mchujo ukaonekana kuwa haukuwa wa haki. Jambo hili linatakiwa kuangaliwa na hasa kwa kuwa kuna makundi.”
MWANANCHI
 Wakati watu watano wakijeruhiwa, wawili kwa kupigwa risasi, kwenye uandikishaji wa wapigakura eneo la Makunduchi, mkutano baina ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wadau umevunjika kutokana na mzozo wa mgwanyo wa majimbo.
Vurugu hizo zimetokea baada ya watu waliokuwa wamekusanyika katika Msikiti wa Kubini kwa madhumuni ya kupinga kazi hiyo ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura wakituhumu kuwapo kwa mamluki waliokuwa wakiandikishwa, lakini wakajikuta wakivamiwa na kundi la askari wasiokuwa na sare ambao walikuwa na silaha za moto.
Waliojeruhiwa kwa risasi ni Kheri Makame Hassan (42) na Ramadhani Hija Hassan (29) wote wakazi wa Makunduchi wakati Ali Seif Issa (38), Ali Hassa Hassan (70) kutoka Paje akiwa amepigwa kwa magongo na nondo na kuumia vibaya miguuni, na Hassan Ali Ameir (43).
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, majeruhi wao walisema walikuwa katika kituo cha Nganani, Shehia ya Nganani Kusini Unguja ndipo walipokuja watu waliovaa vinyago na kuwaamuru waondoke eneo hilo wakati uandikishaji ukiendelea.
“Ilikuja gari na watu waliojifunika nyuso zao wakatuambia tuondoke na sisi tukakataa kwa sababu tulikuwa tunazuia kuandikishwa mamluki katika eneo letu. Baada ya kubishana pale wakaenda kuchukua gari nyingine wakaanza kutupiga,” alisema Kheri ambaye amepigwa risasi ya pajani.
“Watu waliojifunika nyuso walikuja mara mbili na kuondoka kabla ya kufanya shambulio na kufanikiwa kuondoka katika eneo la tukio la Nganani kwa kutumia magari mawili,’ alisema Faki huku akilalamika kusikia maumivu.
Shuhuda wa tukio hilo, Ameir Mussa, mkazi wa Makunduchi, alisema kwamba waliamua kukusanyika eneo la msikiti wakitafakari jinsi ya kuzuia uandikishaji wa wapigakura mamluki, ambao ni pamoja na walio na umri mdogo.
“Lilikuja kundi la watu mara mbili na kuondoka. Walikiwa wamefunika nyuso zao na waliporudi kwa mara ya mwisho walitushambulia kwa kutumia silaha za kienyeji na baadaye kufyatua risasi za moto na kujeruhi watu wawili,” alisema Mzee Ameir.
Daktari wa zamu wa Hospitali ya Al Rahma, Seif Suleiman alithibitisha kupokea majeruhi na kusema kwamba katika hatua za awali wanazuia damu kuvuja kutoka kwenye majeraha.
Alisema wanaendelea na vipimo ili kujua majeraha hayo yamesababishwa na nini. “Tumewafanyia x-ray ili kujua majeraha yao yanatokana na nini lakini yanaonesha wazi kuwa ni majeraha kama ya risasi kwa kuwa risasi jeraha lake linakuwa ni kitobo kidogo inapoingia lakini kitobo kikubwa inapotokea risasi.” Dk Suleiman alisema majeruhi hao wanaendelea vizuri baada ya kutibiwa na wengine wataruhusiwa watakapopata nafuu.
“Wapo walioumia sana hao wataendelea kuwepo hospitali kwa sababu wametokwa damu nyingi sana na kutoka Makunduchi hadi Mjini ni mbali kwa hivyo wanahitaji kupumzishwa kwanza hadi hapo watakapopata nafuu,” aliongeza Dk Suleiman.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saadi alisema kuwa katika mkoa wake kuna uandikishaji wananchi kuwaingiza kwenye Daftari la Wapigakura, lakini hana taarifa za watu kupigwa risasi na kwamba anachojua ni risasi hizo kupigwa hewani na hivyo hazijajeruhi mtu.
MWANANCHI
Kiongozi mkuu wa chama chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe jana alianika orodha ya majina ya watu wanaotuhumiwa kuhodhi akaunti zenye mabilioni ya fedha nje ya nchi, lakini akasita kuyataja kutokana na sababu za kisheria.
Zitto aliwapa waandishi wa habari orodha hiyo akisema waende kufanyia kazi kwa kuwahoji wahusika kulingana na taaluma yao.
Orodha hiyo ina majina yenye asili ya kiasia isipokuwa wachache ambao wanaonekana wana majina ya kibantu.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Zitto alisema: “Majina ninayo haya hapa niwataje nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki kampuni kubwa.”|
Alisema Zitto alisema wamejaribu kuishinikiza Serikali ichukue hatua, lakini inaonekana kutotaka kufanya hivyo na kwamba anaamini waandishi wa habari kwa kutumia taaluma yao wataweza kuwaanika wahusika.
Wakati maofisa wa ACT wakigawa orodha ya majina hayo, wananchi walionekana kuwa na shauku ya kupata nakala ya karatasi hiyo yenye majina 99 ya wafanyabiashara hao maarufu ndani na nje ya nchi, lakini kiongozi huyo hakuwa tayari kuwapatia na badala yake akiwaambia wasome magazeti ya kesho (leo).
Zitto alisema kwamba kati ya majina ya raia hao wenye mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kuna wengine wanamiliki kihalali lakini wengine wamejirundikia isivyo halali.
‘’Nimeamua leo kuiweka orodha hii wazi kama shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi kabla ya Bunge kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa habari aliyepo kwenye mkutano huu nimempatia nakala yenye majina 99 ya Watanzania au watu wenye uhusiano na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya Uswisi. Jumla ya akiba katika akaunti benki hii pekee ni Dola 114 milioni za Marekani,’’ alisema.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ametawazwa kuwa chifu wa mkoa na wazee wa Dar es Salaam na kuitaka serikali kuhakikisha inawarudishia wananchi chenji zinazotokana na ufisadi wa Escrow , EPA na Richmond. Akizungumza katika kongamano hilo la wazee la kutafakari uchaguzi wa mwaka 2015, Dk Slaa alisema ingawa wazee waliungana na Hayati Mwalimu Nyerere kupambana na maadui wa tatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini kwa sasa ameongezeka adui wa nne ambaye ni ufisadi.
“Ujinga alioupinga Mwalimu na wazee umeondoka? Lakini ujinga, umaskini na maradhi na kuna adui wa nne ambaye ni ufisadi,” alisema.
Alisema hakuna Mtanzania ambaye atakwenda dukani na Sh10,000 kununua chumvi na kibiriti halafu akaacha chenji yake dukani kwa makusudi na hivyo Watanzania bado wanadai fedha zao zilizopotea kutokana na ufisadi.
Kadhalika Dk Slaa alisema kitendo cha wazee hao kukutana katika kongamano hilo kinaashiria kuwa wana kiu, njaa na matumaini ya kutaka mabadiliko.
HABARILEO
JITIHADA za Serikali kuhakikisha rasilimali adimu ya gesi yenye fursa ya kutokomeza umasikini kwa Watanzania wote inanufaisha umma zaidi, zimeendelea kupingwa ili rasilimali hiyo inufaishe sehemu ndogo ya jamii.
Katika kuhakikisha gesi inakuwa fursa ya kuondoa umasikini kwa umma wa Watanzania na kutimiza ndoto za Rais Jakaya Kikwete kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania masikini, mwishoni mwa wiki hii Serikali iliwasilisha bungeni miswada mitatu ya sheria ukiwemo Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015.
Mingine ni Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015.
Hata hivyo, kazi ya kuzuia manufaa hayo kwa umma iliyoanza tangu kuvumbuliwa kwa gesi nyingi baharini inayozidi futi za ujazo trilioni 55, iliendelea na kuvuruga vikao vya Bunge, ambavyo vimelazimika kuendelea leo na kesho kutwa, siku ya Sikukuu ya Sabasaba.
Sehemu ya kazi hiyo ilihusisha baadhi ya wabunge walioamua kuzuia jitihada hizo za Serikali, huku baadhi yao wakitamka wazi bungeni kwamba, wenzao wameshawishiwa na kampuni na wafanyabiashara wanaonyemelea kunufaika zaidi na rasilimali hiyo.
Fursa mtaji
Gesi hiyo inayozidi futi za ujazo trilioni 55, pekee ni mtaji katika kuanzisha na kuendeleza miradi yoyote ya umma, katika sekta zote zinazogusa maisha ya Watanzania.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa miamba, Profesa Sospeter Muhongo, kiasi hicho ni sawa na mapipa bilioni 10 ya gesi na kwa bei ya chini ya dola za Marekani 50 kwa pipa, ni sawa na mtaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 500.
Mtaji huo ni sawa na karibu nusu ya bajeti ya nchi kubwa ya Uingereza ya mwaka 2014, ambayo ilikuwa Dola za Marekani trilioni 1.1. Uwazi, elimu.
Akizungumza juzi na jana bungeni kuhusu namna miswada hiyo ilivyo na manufaa kwa umma wa Watanzania, Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM) alisema miswada hiyo ikipitishwa na kuwa sheria, itaweka uwazi katika leseni na mikataba ya madini, gesi na mafuta.
Naye Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema miswada hiyo isipopitishwa kuwa sheria, itakuwa hasara kubwa kwa Watanzania, ikisubiri Bunge lijalo Serikali italazimika kuanza kuwajengea upya uwezo wabunge hao katika jambo hilo, wakati wabunge wa sasa walishapata elimu hiyo.
“Wabunge hawa w a m e j e n g e w a uwezo, wameenda nchi mbalimbali kujifunza masuala ya gesi na mafuta na tangu mwaka 2010 tumeanza mchakato wa jambo hili, ndiyo sababu tunataka itungwe sasa vinginevyo itakuwa matatizo mbele,” alisema Simbachawene.
Hasara uchelewaji Simbachawene alisema masuala ya kujadili mikataba na kampuni za gesi, inachukua kati ya mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu, hivyo kama sheria haitakuwa tayari, uzalishaji uliopangwa uwe kati ya mwaka 2018 na 2019, utalazimika kucheleweshwa, maana yake muda utazidi kusonga mbele na itakuwa hasara kwa Watanzania.
“Suala la majadiliano ya mkataba si la wiki moja au mwezi, ni kati ya mwaka mmoja na zaidi, sasa unasema Bunge lijalo ndiyo lifanye kazi hiyo unajua litakuwaje?” Alihoji.
Alisisitiza kuwa Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji ukipitishwa, utafanya mikataba yote ya madini na gesi iwe wazi na halitakuwa jambo la siri kama ilivyo sasa.
HABARILEO
HATIMAYE baada ya hujuma ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani kushindwa, Serikali imewasilisha bungeni miswada ya sheria kuhusu masuala ya mafuta na gesi, huku matumizi ya mapato ya gesi yakiwekewa vizingiti.
Akisoma hotuba ya Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 bungeni jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema muswada unaweka masharti kuhusu uanzishwaji wa Mfuko wa Mafuta na Gesi, ambao utakuwa na akaunti mbili zitakazotunzwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alizitaja akaunti hizo ni Akaunti ya Kupokea Mapato na Akaunti ya Kutunza Mapato na kwamba mfuko wa mapato yatokanayo na mafuta na gesi, unapendekezwa kuanzishwa kwa madhumuni ya kupokea na kugawa mapato yatokanayo na mafuta na gesi kwa kuzingatia malengo makubwa matatu.
Malengo, mapato
Malengo hayo ni kuhakikisha uimara wa kifedha na kiuchumi, kugharamia uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kulinda rasilimali kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Katika muswada huo, Nchemba pia alitaja vyanzo vya mapato vya mfuko huo kuwa ni mirabaha, gawio na faida ya Serikali katika shughuli za mafuta na gesi.
Vingine ni kodi za mapato ya makampuni, ambayo hukatwa baada ya kupata faida ghafi na gawio litokanalo na tasnia ya mafuta na gesi pamoja na faida itakayopatikana kutokana na uwekezaji wa fedha za mfuko.
Mwenendo wa akaunti
Nchemba alisema inapendekezwa katika muswada kwamba mapato yote ya mfuko yawekwe kwenye Akaunti ya Kupokea Mapato.
Baadaye, Akaunti ya Kutunza Mapato itapokea kiasi cha asilimia ya mapato kutoka kwenye Akaunti ya Kupokea Mapato kwa kuzingatia miongozo ya kibajeti.
NIPASHE
Kamati Kuu Maalum (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imekutana kwa dharura mjini Dodoma kupokea, kuchambua na kutoa baraka kwa vipaumbele na ahadi za Rais ajaye vilivyoainishwa katika ilani mpya ya uchaguzi ya mwaka 2015.
Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete; iliwaita Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam ya Kuandaa Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi, pamoja na wajumbe wake kwa ajili ya kuikabidhi na  kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo.
Kamati hiyo ilikuwa na kibarua kizito cha kutoa ufafanuzi kuhusu Rasimu za awali ambazo zilikuwa zimefanyiwa maboresho na kisha kupatikana kwa ilani mpya itakayotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kabla ya Rais Kikwete kuwasili mjini hapa saa, 8:37 mchana na kuendesha kikao hicho kwa zaidi ya saa nne; wapambe wa makundi ya baadhi ya wagombea wa kiti cha urais, walionekana wakirandaranda Makao Makuu ya CCM kwa lengo la kutaka kujua kinachoendelea baada ya kuitishwa ghafla kwa kikao hicho.
Wajumbe wa Kamati ya Wassira ni Anamringi Macha (Katibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali-Zanzibar, Ali Juma Shamhuna.
Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Anthony Mavunde, Mbunge wa Manyoni Mashariki, Kapt. John Chiligati, na Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Aboud; ndio walioitwa ili kukabidhi ilani hiyo.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya CC hiyo, vilieleza kuwa ajenda nyingine ilikuwa ni kuwajadili wenyeviti 18 wa mikoa wa CCM ambao wanadaiwa kujilipua kwa kumuunga mkono mmoja wa wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, kupitia chama hicho.
Ajenda ya tatu ilikuwa ni kupata mrejesho wa hali halisi ya mwenendo wa bunge; kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo inaundwa na vyama vinne vya Ukawa kuchafua hali ya hewa kwa siku mbili na kulazimika kuahirishwa ili kupata utulivu.
Awali, akifungua kikao hicho, Rais Jakaya Kikwete alisema, kikao hicho ni maalum kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
CC YA ZANZIBAR LEO (JULAI 5)
Aidha, Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar, nayo inakutana leo Makao Makuu ya CCM-Kisiwandui, Zanzibar kwa ajili ya kupendekeza jina la mgombea wa urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ); kwa tikiti ya chama hicho.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai ally Vuai, alisema kikao hicho kitafanyika saa 4 asubuhi, chini ya Makamu Mwenyekiti, atakayeteuliwa na kikao hicho, kwa kuwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein ni mgombea urais, kwa hiyo hawezi kujijadili.
NIPASHE
Wazee  wa Mkoa wa Dar es Salaam wamempa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, majukumu ya kuikomboa nchi kwa  mara ya pili kama alivyofanya mwalimu Julius Nyerere wakati akiitoa mikononi mwa wakoloni.
Jukumu hilo alipewa jana na wazee hao baada ya kumvisha vazi la uchifu na kumkabidhi vitu mbalimbali vikiwamo kisu, panga, shoka, jembe, nundu na usinga ikiwa ni ishara ya kumtawadha kushika madaraka hayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo sasa atatambuliwa kama Chifu Mwinyikambi.
Mzee Ally Mwinyikambi, ambaye alimkabidhi Dk. Slaa uchifu huo kwa niaba ya  wazee wa mkoa huo, alisema wanamtaka ahakikishe anakiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
Katika hotuba yake, Dk. Slaa alisema kuwa, kilichotokea kimekumbusha enzi za Nyerere wakati akiwa anatoka masomoni.
Alisema kitendo hicho kimekihakikishia chama hicho ushindi wa kuelekea Ikulu katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Aliwahakikishia wazee hao na Watanzania kwa ujumla kuwa, uchaguzi huu lazima washinde kwa kishindo.
Alisema licha ya Mwalimu Nyerere kuwataja maadui wa nchi kuwa ni umaskini, ujinga, maradhi lakini CCM katika utawala wake wote imeshindwa kuyaondoa hayo.
“CCM imekuwa ikikusanya wazee wa chama chao pekee kwenye ukumbi na kuwapa Sh. 5,000 bila kuangalia matatizo yao, sisi hatuna ubaguzi  na tunawatambua wazee wote wa nchi hii,” alisema.
Alisema licha ya CCM kutawala muda mrefu lakini huduma za jamii kama barabara, afya, elimu utekelezaji wake bado ni hafifu wakati wananchi wamekuwa wakitozwa kodi.
“Tunadai chenji zetu kwenye Richmond, Epa, Escrow kwa sababu hizi ni fedha za watanzania ambao ndio walipakodi,” alisema.
Dk. Slaa alisema watakapoingia madarakani miaka kumi watahakikisha nyumba zilizojengwa kwa nyasi zinatoweka huku huduma za afya zilipungua gharama zake kulingana na kipato cha Mtanzania.
Kuhusu mashine za kuandikisha wapiga kura za Kieletroniki Biometrick Voters Registration,  katibu huyo aliwataka wazee kutumia muda wao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji na kuhakikisha hawatoki vituoni hadi vinafungwa.
Akiongelea migogoro ndani ya nchi ukiwemo ule wa madereva ambao waligoma hivi karibuni, alisema kuwa serikali haipaswi kutafuta mchawi bali itafute muafaka.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, wakili mashuhuri, Mabere Marandu, alisema kuwa Chadema haina tamaa ya madaraka na kwamba wakiingia madarakani muda wake ukiisha na wananchi wakiona hawajafanya kitu, wapo radhi kuondoka.
Naye, mwenyekiti wa Wazee Tanzania, Hashimu Issa Juma, alisema kuwa Chadema ikiingia madarakani itatoa pensheni ambao haitapungua 100,000.
Pia alisema watatoa matibabu bure na huwahakikishia usafiri wa daladala utakuwa bure.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment