HADITHI
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572, 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA 7
ILIPOISHIA
lakini sikumjibu kitu.
Akatoka mle chumbani.Alipotoka na mimi nikashuka kitandani, nikanyata hadi
mlangoni kumchungulia. Nikamuona ameingia katika kile chumba cha pili. Baadaye kidogo
akatoka, mimi nikarudi kitandani. Akaingia tena mle chumbani na
kunichungulia.Mkononi alikuwa ameshika kitu ambacho sikuweza kukiona vizuri kwa
sababu nilikuwa namwaangalia kwa kumuibaiba.
Nilitulia kimya pale
kitandani, nikasikia akifungua mlango wa nje.Nikainuka na kwenda
kumchungulia.Nikamuona anatoka na kuufunga mlango.Nilisubiri kwa dakika chache
kisha nikaenda kwenye mlango huo. Nikaufungua taratibu na
kumchungulia.Nikamuona anapotea kwenye kiza upande wa kushoto mwa nyumba yetu
ambako palikuwa na pori.
Yule msichana anakwenda
wapi usiku huu? nikajiuliza kwa mshangao bila kupata jibu. Nikatoka nje na
kuufunga mlango.Niliamua kumfuatilia ili nijue anakwenda wapi.
Kulikuwa na baridi
l;akini sikuisikia kwa sababu ya kutaharuki. Nilipoingia kwenye lile pori
nilimuona Chausiku ametokea upande wa pili wa pori hilo na kuendelea
kwenda.Nami niliendelea kumfuatilia taratibu huku nikijifichaficha kwenye miti
ili asinione.
Nikaendelea kumfuatilia
hadi kwenye eneo la makaburi mahali ambako kwa usiku ule palikuwa panatisha
kweli kweli na isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote mwenye akili zake timamu kufika
mahali hapo wakati ule usiku akiwa peke yake tena bila taa na akionekana hana
wasiwasi.
SASA ENDELEA
Palikuwa na vichaka
vifupifupi. Nikajiingiza kwenye kichaka kimoja na kuchungulia. nikashituka
nilipoona palikuwa na wanawake zaidi ya kumi, wengine wakiwa vikongwe
kabisa.Niliweza hata kuwatambua baadhi ya wanawake ambao walikuwa wakazi wa
kijiji chetu.
Lakini jambo
lililonishitua zaidi si tu kuwaona wanawake hao bali kuwaona wakiwa uchi wa
mnyama huku wakiwa wamejifunga mikia makalioni.
Kulikuwa na kikongwe
mmoja aliyekuwa akitembea kwa kuinamainama ambaye alikuwa ameshika mwengo
akiwaputia wenzake huku akicheza na kuimba.
Wakati nikiwachungulia sikumuona
mke wangu lakini ghafla naye aliibuka kwenye lile kundi akiwa uchi wa mnyama naye
akiwa amejifunga mkia kama wenzake.
Mwili ulikuwa
ukinitetemeka. Sikujua ilikuwa kwa hasira ama kwa hofu. Mazingira niyoaona
mbele ya macho yangu yalionesha kuwa lile lilikuwa ni kundi la wachawi na mke
wangu akiwemo.
Kile kitendo cha
kugundua kuwa mke wangu ni mchawi ndicho kilichonifanya nitetemeke.
Nilijiuliza maswali
mengi bila kupata jibu.
Kama mke wangu ni mchawi
alianza lini? na ni nani aliyemuingiza katika kundi hili la wachawi?
Kumbe siku zote
anapoondoka usiku anakuja huku kwa wenzake? masikini mke wangu amekwisha!
Wakati ninawaza
nililiona kundi hilo likisogea kwenye kaburi moja.Nikakumbuka lilikuwa la yule
mtoto aliyekufa na kuzikwa jana yake.Nikasogea kwa karibu kwenye kichaka
kingine ili niweze kuwaona vizuri.
Nikawaona wamelizunguuka
lile kaburi na kulicheza ngoma.Kisha wote wakaliinamia na kuanza kuchimba kwa
mikono.Pale nilipokuwa nimejificha pia sikuweza kuona vizuri nikasogea kwenye
kichaka kingine kilichokuwa karibu zaidi.
Mpaka nafika kwenye kile
kichaka walikuwa wamekwisha fukua sehemu kubwa ya lile kaburi kwa mikono tu.
Ilikuwa ni ajabu!
Yule kikongwe aliyekuwa
na mwengo aliingia kwenye kaburi hilo. Baada ya muda kidogo niliona ameishika
ile maiti ya yule mtoto tuliyemzika ikiwa kwenye sanda. Mke wangu akaipokea kwa
juu na kuiweka chini. Kisha wakamvuta yule bibi na kumtoa ndani ya lile kaburi.
Wakaanza kulifukia kwa kutumia makalio yao. Walifukia hadi michanga ikamalizika
kabisa.
Yule bibi kikongwe
alimfungua sanda yule mtoto, akawa anamrambaramba kwa ulimi. Vitendo vyote
hivyo vya kuifukua maiti ya yule mtoto,kumfunua sanda na hatimaye yule bibi
kumrambaramba kwa ulimi vilinishitua na kunishangaza sana.Nikawa nimeduwaa pale
penye kichaka.
Yule bibi
alipourambaramaba mwili wa yule mtoto, alimpa mke wangu akaubeba. Wakaondoka na
kwenda sehemu nyingine iliyokuwa na mti wa mwembe.Wakakaa chini ya mti huo.Kule
sikuweza kuona walitaka kuifanya nini ile maiti ikabidi nisogee karibu kwenye
kichaka kilichokuwa karibu na wao.
Nilipofika nikaona
wanamla yule mtoto.Nilimshuhudia waziwazi mke wangu akiwa ameshika pande
la nyama mbichi alilolikata kutoka mwili wa mtoto huyo na kulila.
"Ha! mke wangu
unakula nyama ya maiti?" nilishitukia nikisema kwa sauti bila
kujitambua.Wanawake hao wakashituka na kugeukia pale penye kichaka nilipokuwa
nimejificha
Nikamuona mke wangu
pamoja na wanawake wengine wawili wakija pale penye kichaka ilipotokea sauti
yangu
Nilipoona wamefika
karibu nikatimua mbio. Mke wangu akanifukuza lakini hakunipata.Akaamua kurudi
kwa wenzake.
Nikarudi nyumbani huku
nikitweta kwa fadhaa na hofu.Niliingia chumbani mwangu nikaketi kwenye kiti na
kuanza kujiwazia
Kila kitu nilichoona
kilikuwa kimenidhihirishia kwamba mke wangu alikuwa mchawi tena mchawi wa
kiwango cha kutisha cha kufikia kula nyama za maiti
Ni ajabu kwa mtu
aliyeonesha ushirikiano kwenye msiba wa yule mtoto na pia kuonyesha huruma na
majonzi halafu anaweza kufukua kaburi lake usiku na kula nyama yake! hii ni
roho ya kibinaadamu kweli!
Huyu si binaadamu wa
kuendelea kuishi naye. Mwisho wa siku anaweza kuja kuniua mimi! nikajiambia kwa
hofu.
Usinginzi ulikuwa
umeniruka.Nilikuwa nikimsubiri Chausiku nimueleze kuwa sitaweza kuishi naye.
Baada ya kupita saa moja hivi niliona mlango wa chumbani ukisukumwa. Chausiku
akaingia chumbani akiwa na nguo zake alizoondoka nazo. Mkononi alikuwa ameshika
kandambili zangu. Nikakumbuka kwamba kandambili hizo niliziacha kulekule
makaburini wakati ninakimbia na nikarudi nikiwa miguu mitupu bila kujielewa.
"Wee mgosi!
ulifuata nini kule makaburini?" Chausiku akaniuliza kwa ukali.
"Kumbe na wewe
ulikwenda kufanya nini?" na mimi nikamuuliza
"Hivyo
nilivyokwenda kuvifanya mimi umeshaviona. Huna haja ya kuniuliza.Nataka nijue
kilichokuleta wewe kule ni kitu gani?"
"Nilikufuata wewe
ili nijue ulikuwa unakwenda wapi usiku huu?"
"Ulikuwa
unanichunguza?"
"Ndiyo nilikuwa
nakuchunguza"
"Sasa
umeshaniona,unasemaje?"
"Kumbe wewe mke
wangu ni mchawi?"
"Ndiyo ni
mchawi.Nakama umeshajua kuwa mimi mke wako ni mchawi na wewe mume wangu utakuwa
mchawi vilevile"
"Hata siku
moja,tena nasubiri kuche nikuachie chumba chako niende zangu. Siwezi kuishi na
wewe"
"Eti nini? ndivyo
ulivyojidanganya hivyo? huondoki na mimi nitabaki kuwa mke wako.Na wewe ni
lazima utaingia kwenye uchawi ili siri yetu isitoke nje"
"Huwezi
kunilazimisha. Mimi siwezi kushirikiana na wewe kwenye jambo hilo. Tusubiri
asubuhi nikuache"
"Uniache wende
wapi?"
"Nitakwenda
kupandisha chumba mahali pengine"
"Kwa vile
umeshaijua siri yangu huendi kokote utabaki na mimi!"
"Usinieleze
upumbavu wako. Sitaweza kuendelea kuishi na mtu kama wewe"
"Kama wewe
unajifanya umeshika kisu jua kuwa ulichoshika ni makali. Mpini nimeshika
mimi. Kama tutavutana atakaye katika vidole ni wewe"
"Kwanini unaniambia
hivyo?"
Chausiku akatabasamu.
"Nimekuambia hivyo
kwa sababu kama wewe umeujua uhalifu wangu na mimi ninaujua wako.Ingawa
ulinificha lakini najua kuwa wewe ulimuuua mke wako kwa kumchoma kisu kisha
ukakimbilia huku kijijini.Mpaka leo polisi wanakutafuta.Kesho nikienda kituo
cha polisi kukutolea ripoti ujue umekwisha!"
Hapohapo
nikanywea.Maneno yake yalinikata kauli yakanifanya nibaki nimeduwaa.
Je mambo yatakuwaje
hapo? Usikose kuendelea na hadithi hii hapo kesho. Ina mengi ya kujifunza
kuhusu maisha yetu. Hapa hapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment