SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0715 340572 au 0655 340572
ILIPOISHIA
Bibi huyo alichukua ile
pembe ambayo ilikuwa imechomekwa kifiniko, akakichomoa na kumimina mafumba
kwenye kiganja chake kisha akayatia mate yake na kuyatabania maneno ya kichawi
na kisha akaniambia kwa sauti kali “Ramba!”
Alielekeza kile kiganja
chake kwenye midomo yangu.Niliguna lakini si kwa kutoa sauti.Nikayaangalia yale
mavumba yaliokuwa yameroa mate.Niliona kinyaa kwelikweli
“Ramba mara moja halafu
umeze” kikongwe akaendelea kuniambia
Nikamtupia jicho kali mke
wangu.
“Si umeambiwa
urambe,unaniangalia nini?”mke wangu akaniuliza kwa kunisuta
Sikuwa na la
kufanya.Nilikaza roho na kuyaramba yale mafumba
“Meza!” bibi akaniambia
huku akiniangalia kwa macho yake makali.
Nikameza
Yale yaliobaki mkononi
mwake akaongezea mate mengine kisha akanipaka mwilini
Kitu cha ajabu
nilichokiona hapo ni kwamba baada ya kumeza yale mavumba mawazo yangu yalianza
kubadilika.Ile hofu niliokuwa nayo ilianza kunitoka, nikapata ujasiri wa ajabu.
Hapo mwanzo niliona kitendo hicho kilikuwa cha kipuuzi lakini sasa niliona si
cha kipuuzi bali kilikuwa kitendo cha maana.
SASA ENDELEA
Mwili wangu uliokuwa
umejaa baridi ulianza kupata joto na kujaa ujasiri baada ya yule bibi kunipaka
yale mavumba aliyoyachanganya na mate yake
Sasa hata ile aibu ya
kukaa uchi sikuwa nayo tena
“Sasa inuka” bibi
akaniambia
Nikainuka kiujasiri.
Kundi kubwa la wachawi lilikuwa limekusanyika kuniangalia
“Jamani nataka
kuwatambulisha huyu mgeni aliyejiunga na sisi.Nataka mumpokee, tangu sasa huyu
ni mwenzetu” bibi akawaambia wachawi hao na kuendelea
“Ni mume wa Chausiku.
Sasa aje mtu mmoja mmoja asalimiane naye na kujuana naye”
Hapo hapo akaibuka
mwanamke mmoja akainama na kunielekezea makalio yake.Mtindo huo nilikwisha ujua
nami nikainama,tukagonganisha makalio. Kisha akanigeukia na kuniambia jina
lake,shughuli zake na mahali anapoishi
Baada ya hapo akaondoka.
Akaja mwingine na mwingine mpaka wachawi wote wakamalizika
“Sasa shughuli yetu ya
leo tutakwenda kumsimika mgeni wetu na kumtambulisha kwenye mzimu wetu” bibi
akaendelea kueleza. Ingawa sikupata kuelezwa lakini tangu nimefika hapo
niligundua kuwa yule bibi alikuwa gunge,yaani mkuu wa wachawi hao
Mara moja niliona
nikiletewa chano kilichowekwa makorokoro ya kichawi.Hata sikujua vilitolewa
wapi.Kile chano kiliwekwa juu ya kichwa changu.Yule bibi akanitangulia na
kuniambia nimfuate
Nikakishika kile chano
juu ya kichwa changu na kumfuata yule bibi huku nyuma kundi hilo la wachawi
likawa linatufuata.Bibi kikongwe alikuwa akiimba nyimbo za kichawi na wale watu
waliokuwa nyuma yetu walikuwa wakimuitikia
Tuliondoka katika eneo
hilo la makaburi tukaenda katika eneo jingine lilikuwa kando ya mto.Hapo
palikuwa na mti wa mbuyu wa miaka mingi ambao ulizungukwa na kichaka.Yule bibi
aliyekuwa mbele yangu aliingia kwenye kile kichaka na mimi nikamfuata. Akawa
anauzunguuka ule mbuyu huku akiendelea kuimba. Lile kundi la watu likawa
limesimama kuuzunguka ule mbuyu.
Wakati yule bibi
akizunguuka ule mti, mimi nilikuwa nikimfuata nyuma nyuma nikiwa na chano
changu kichwani. Baada ya kuuzunguuka mti huo mara saba akasimama kuuelekea mti
huo na kuanza kuzungumza maneno ya kichawi huku akilitaja jina langu bila shaka
mke wangu ndiye aliyemtajia jina hilo
Baadaye akaniambia
nikiweke kile chano chini ya ule mti kisha na mimi nikae kuuelekea mti huo.
Hapo nilifanyiwa mambo
ya ajabu ajabu ambayo sikupata kuyaona popote.Wale wachawi walikuwa wakicheza
kwa sherehe kuuzunguuka ule mti wakati yule bibi alichukua kiwembe akawa
ananichanja sehemu mabalimbali za mwili wangu kisha damu yangu alikuwa akiipaka
kwenye ule mti na kisha alichukua uchafu wa ule mti akawa ananipaka mimi kwenye
zile chale
Nilikatwa sehemu ya
vywele zangu pamoja na kucha za mikiono na miguu,vikachanganywa pamoja na
kutiwa kwenye kitambaa cheusi.
“Tia mate” yule bibi
akaniambia akiwa amenielekezea kile kitambaa alichokitia nywele zangu na kucha
Nikakitia mate.Bibi huyo
naye akatia mate yake kisha akakikunjakunja na kukichomeka kwenye jitundu
lililokuwa kwenye shina la ule mbuyu.Wakati anakichomeka alikuwa akisema maneno
ambayo sikuweza kuyaelewa
Baada ya hapo bibi huyo
akaniambia “Tayari umeshakuwa mwenzetu.Masharti yetu ni kuwa hutakiwi
kutoa siri zetu na unatakiwa ufuate kila ninachokuamrisha mimi, hata
nikikuambia uende ukamuue mama yako unakwenda. Umenielewa?”
“Nimekuelewa”
“Uko tayari kufuata
masharti yetu?”
“Niko tayari”
“Sawa.sasa kuna mambo
mengine atakufundisha mke wako nyumbani.Hii leo tutakufundisha hii ngoma yetu”
yule bibi aliponiambia hivyo nikatakiwa niinuke. Hapo ndipo nilipoanza
kufundishwa ngoma za kichwi.Kwa ule usiku mmoja tu nikaweza kuijua na kuwa
fundi wa kucheza.
Ilikuwa ngoma
inayopandisha mori na kutia furaha.Nilisahau kwamba uchawi ni laana.Nikaona ni
jambo la kawaida kama vile mtu anapojiunga na kundi la muziki.
Ilipokuwa inakaribia
alfajiri gunge letu lilivunja ngoma.Akatuambia turudi kule tulikoacha nguo
zetu,tukarudi. Mimi na Chausiku tukaenda kwenye kile kichaka tulikoweka nguo
zetu.Tulipovaa mke wangu akaniambia “Sasa tunarudi nyumbani”
Tukiwa njiani tunarudi
Chausiku akaniuliza “Umeionaje ngoma?”
“Ngoma ni nzuri”
“Yule bibi si unamjua?”
“Hata simjui”
“Kesho nitakuonyesha
anapoishi. Anauza mbaazi zake katika ile shule yetu ya msingi. Lakini mbaazi
zenyewe si mbaazi, ni mavi ya mbuzi wake ameyageuza kwa uchawi!”
"Eh! kumbe analisha
watu mavi ya mbuzi?" nilimuuliza kwa kung'aka
"Sasa unashangaa
nini?"
"Mavi ya mbuzi ni
chakula kweli!"
"Hata nyama za watu
zinaliwa, achilia mavi ya mbuzi"
"Nyama za watu si
mnakula nyinyi"
"Wewe pia
utakula"
"Ingawa nimekubali
kujiunga na nyinyi, sitaweza kula nyama za maiti"
"Usianze kuniletea
maneno yako.Nitakwenda kumueleza yule bibi kuwa unaleta upinzani"
"Lakini kula nyama
za watu ni hiari si lazima"
"Sasa nakuambia
tena ni lazima utakula!"
"Mke wangu sasa
unanitisha"
"Mwanaume mzima
unasema maneno hayo! mbona mimi ninakula siku zote?"
Nikaona
ninyamaze.Tulipofika nyumbani tulilala hadi asubuhi ambapo nilienda zangu
shamba.Kutokana na mawazo ya vile vitendo vya kichawi tulivyovifanya usiku
uliopita sikuweza kulima wala kufanya kazi yoyote.Niliketi na jembe langu
kwenye shina la mnazi nikiwaza.Suala lililonikera sana ni lile la kula nyama za
maiti.
Ilipofika saa saba mke
wangu aliniletea chakula.
"Mbona
umekaa?" akaniuliza.
"Nimepunzika"
nikamjibu
Chausiku akaketi kando
yangu
"Umeniletea chakula
gani?" nikamuuliza huku nikikifunua
"Wali"
"Na hii ni nyama ya
nini?" niliona kipande cha nyama juu yake
"Mbona siku zote
nikikuletea chakula huniulizi, leo kwanini unaniuliza"
Aliponijibu hivyo
nikamwaambia "Leo sijisikii kula"
"Kwanini?"
"Tumbo
linaniumauma"
"Wewe muongo.Hebu
kula hicho chakula!"
"Basi utakiacha
hapahapa, nitakula baadaye"
"Kula sasa hivi na
mimi nione.Najua iliyokutisha ni hiyo nyama”
Je nini kitatokea?
Usikose kutembelea blog hii hapo kesho.
|
Wednesday, May 4, 2016
HADITHI SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA SEHEMU 9
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment