SITASAHAU NILIVYOGEUZWA
PAKA SEHEMU YA 9
Na Faki A Faki 0655 340572
ILIPOISHIA
Mke wangu
akachukua vyombo na kuondoka.Jioni niliporudi nyumbani hatukuzungumza kitu, hakuniuliza
kitu na mimi sikumueleza kitu.
Baada ya kuoga
nilikwenda mtaa wa pili ambako kulikuwa na baraza la vijana.Vijana tulikuwa
tunakutana hapo na kucheza bao.
Nilicheza bao hadi saa
mbili usiku nikarudi nyumbani kula chakula. Baada ya kula sikutoka tena. Nilikaa
barazani na redio yangu hadi saa nne usiku nilipoingia ndani kulala.
Nilimkuta mke wangu
akikoroma.Sikumshangaa. Kutokana na kazi yake ya kuamka usiku ilimbidi alale
mapema.
Nilipanda kitandani na
mimi nilale lakini sikupata usingizi.Usiku ule kwa upande wangu ulikuwa ni
fainali. Ni usiku wa kuamua kwenda kujiunga na wachawi au kukataa na niwe
tayari kuripotiwa polisi na Chausiku.
Kwa ajili ya kuokoa
maisha yangu niliona nikubaliane na Chausiku.Na si kukubaliana kiukweli bali
nilipanga nijiingize katika kundi lao kama kutalii tu na kumridhisha Chausiku
Kwa kweli niliendelea
kukaa macho mpaka saa nane usiku, ndipo nilipolala. Baada ya kulala kidogo tu
Chausiku akaniamsha.
"Amka..amka...muda
umeshafika!"akaniambia
SASA ENDELEA
"Kitu gani?.Mwenzio
ndiyo naanza kulala!"
"Eti
nini!.Tulizungumza nini jana? tulizungumza nini jana? usiniletee upuuzi
wako!.Hebu amka tutoke"
Nikaguna kisha nikaamka
"Acha uvivu bwana,
changamka"Chausiku akajidai kunibembeleza
Nilishuka
kitandani.Mwenzangu alikuwa ameshavaa kaniki yake kisha juu yake kajitanda
khanga.Mkononi alikuwa ameshika kitu ambacho sasa nilikiona vizuri. Kilikuwa ni
pembe ya ng'ombe ambayo ilifungwa kwa kitambaa cheusi na chekundu.
"Vaa nguo"
akanihimiza
Nikavaa suruali yangu na
shati
"Nyoosha kiganja
chako"akaniambia
Nikanyoosha.Akanikung'utia
mavumba kutoka kwenye lile pembe aliloshika
"Jipake usoni"
Nikajipaka.Na yeye
akajikung'utia kwenye kiganja chake kisha akajipaka usoni mwake.Uso wake
ukaonekana kama kinyago cha mpapure kilichopakwa masinzi.Bila shaka na mimi
nilikuwa ni hivyohivyo
"Sasa tutoke twende
zetu.Wenzetu wanatungoja.Nilishawaambia kuwa nitakwenda na wewe"
Tukatoka.Huko nje
kulikuwa kumetulia.Sauti zilizokuwa zikisikika zilikuwa za vidudu na mbwa waliokuwa
wakibweka kwa mbali.
Mke wangu akanishika
mkono "Twende! twende!" akanihimiza
Tukaingia kwenye
vichochoro vilivyokuwa giza.Tukatokea kwenye mapori, tukayapita na kutokea
kwenye lile eneo la makaburi
Niliona wanawake kadhaa
wakiwa kwenye uwanja wa makaburi.Mimi na Chausiku tuliingia kwenye kichaka
kimoja. Chausiku akaniambia nivue nguo zangu.
"Nibaki uchi
kabisa?" nikamuuliza
"Hapa hapatakiwi
nguo"
Wakati akiniambia,
Chausiku naye alikuwa akivua nguo zake.Akabaki uchi wa mnyama.Shanga tatu za
kiunoni alizokuwa amevaa zilikuwa zikionekana.
"Nitabaki na chupi,
kukaa uchi sitaweza"nikamwaambia
"Wee mwanaume
usitake kuniponzea!.Hutaweza nini?.Kwani sisi tuliovua ni wanyama,wewe ndiyo
mtu peke yako?"
Chausiku akanivua ile
chupi
"Wale wanawake
watakwenda kuniona!"
"Na wewe
utawaona,unaona aibu gani?"
Loh! Kumbe uchawi ni
ushenzi hasa!
“Twende” mke wangu
akaniambia huku akinishika mkono
Tulitoka katika kile
kichaka tukiwa watupu kama tulivyozaliwa.Kwa sababu ilikuwa ni mwanzo,niliona
baridi na mwili wangu ulinywea kutokana na kuwa wazi hadharani.Sikuzoea kukaa
uchi mbele za watu.
Wakati tunakwenda kwa
wale wenzetu huku nikiwa nimejaa aibu na moyo wangu ukiwa umesongwa na fadhaa,
niliona wenzetu wengine wakichomoka kwenye vichaka wakiwa uchi.Usiku wa jana
yake nilipokwenda pale kuwachungulia sikuona wanaume. Kumbe wanaume pia
walikuwepo.Niliona wanaume wawili.
Lakini tofauti yangu na
wenzangu ni kwamba wao walikuwa wamejichomeka vitu vilivyoonekana kama mikia ya
wanyama makalioni. Hata mke wangu alikuwa amejipachika mkia wake.
Nikawa najiuliza maswali
mengi yaliyokosa majibu. Nilijiuliza kwanini wachawi wanapendelea kukaa uchi?.
Mbali ya kukaa uchi, kwanini walazimike kujipachika mikia kama wanyama?
Angalau wengekuwa ni
wanawake peke yao, kukaa uchi kusingekuwa tatizo kubwa. Lakini tupo na wanaume.
Wanawake wengine walikuwa ni wasichana na ni wake za watu.Si balaa hili!
Katika hali kama hii,
niliendelea kujiuliza,mwanaume kweli ataweza kujizuia?
Falsafa ya kwanza ambayo
ilikuja katika akili yangu kuhusu imani hii ya uchawi ni kwamba kama vile
ambavyo vitendo vya kichawi ni kinyume na ubinaadamu, ndivyo ambavyo hata
wachawi wenyewe wanatakiwa wajibadili ili wawe kinyume na ubinaadamu wao kwa
kukaa uchi na kujifunga mikia.
Huu sasa ni unyama
mtupu!, nilijiambia.
Laiti kama si ile hofu
yangu kwamba nikikataa kujiunga na kundi lao mke wangu atakwenda kuniripoti
polisi,nisingekubali upuuzi ule kwa sababu haukuwa na tija.
Mke wangu alinipeleka
kwa kikongwe aliyekuwa ameshika mwengo ambaye naye pia alikuwa uchi.Lakini
mbali ya kuwa uchi alikuwa amevaa hirizi mbili kubwa.Moja ya rangi nyekundu
ilikuwa mbavuni na mwingine nyeusi aliifunga kiunoni.
“Bibi nimemleta mume
wangu,ndiye huyu hapa” mke wangu akamwaambia yule kikongwe.Moyo ukanipasuka.
Bibi huyo aliinama
akageuka na kunielekezea makalio yake.Nikawa namtazama.
“Na wewe geuka uiname
mgusane makalio, ndiyo mnasalimiana” mke wangu akaniambia
Nikampa mgongo yule bibi
na kumuinamia. Akayagonganisha makalio yake na yangu.Makalio yake yalikuwa
baridi na yalibaki ngozi na mifupa mitupu.
Baada ya kugonganishana
makalio, yule bibi aligeuka akanishika mkono.
“Haya kaa hapa!”
akaniambia. Pamoja na uzee aliokuwa nao alionekana shupavu kwelikweli
Nikakaa pale chini.
“Nyoosha miguu yako.Hapa
hakuna cha aibu. Utazoea tu”
Nikanyoosha miguu. Pale
chini nilipoketi palikuwa na pembe kubwa ya ng’ombe iliyofungwa kitambaa
cheusi.
Bibi huyo alichukua ile
pembe ambayo ilikuwa imechomekwa kifiniko, akakichomoa na kumimina mafumba
kwenye kiganja chake kisha akayatia mate yake na kuyatabania maneno ya kichawi
na kisha akaniambia kwa sauti kali “Ramba!”
Alielekeza kile kiganja
chake kwenye midomo yangu.Niliguna lakini si kwa kutoa sauti.Nikayaangalia yale
mavumba yaliokuwa yameroa mate.Niliona kinyaa kwelikweli
“Ramba mara moja halafu
umeze” kikongwe akaendelea kuniambia
Nikamtupia jicho kali
mke wangu.
“Si umeambiwa
urambe,unaniangalia nini?”mke wangu akaniuliza kwa kunisuta
Sikuwa na la
kufanya.Nilikaza roho na kuyaramba yale mafumba
“Meza!” bibi akaniambia
huku akiniangalia kwa macho yake makali.
Nikameza
Yale yaliobaki mkononi
mwake akaongezea mate mengine kisha akanipaka mwilini
Kitu cha ajabu
nilichokiona hapo ni kwamba baada ya kumeza yale mavumba mawazo yangu yalianza
kubadilika.Ile hofu niliokuwa nayo ilianza kunitoka, nikapata ujasiri wa ajabu.
Hapo mwanzo niliona kitendo hicho kilikuwa cha kipuuzi lakini sasa niliona si
cha kipuuzi bali kilikuwa kitendo cha maana.
Je nini hatima ya kijana
huyo katika kundi hilo la wachawi? Blog yetu ni TANGA KUMEKUCHA. Tukutane tena
hapo kesho.
No comments:
Post a Comment