Tuesday, August 16, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 58

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 58

ILIPOISHIA

Baada ya kuikunja kamba yote, aliwarushia wale watu waliokuwa juu ya shimo. Watu hao waliidaka na kuanza kuivuta.

Ile kamba ilipita juu ya lile tawi la mti kisha ikaenda kwa wale watu, hivyo walipoivuta ilipitia juu ya lile tawi. Waliivuta hadi mwisho. Sasa miguu yangu ambayo ilifungwa kwa  kamba hiyo ikaanza kuinuliwa. Iliinuliwa hadi ikawa juu.


Kamba iliendelea kuvutwa. Mwisho nikawa nimenin’ginizwa kichwa chini kama mkungu wa ndizi. Kamba iliendelea kuvutwa hadi mwili wangu wote ukawa unanin’ginia kichwa chini miguu juu.

Ghafla nikamuona Abdi akiingia kwenye lile shimo akiwa ameshika kikombe cheupe na nyundo.

“Abdi ndio nini hivi” nikamuuliza.

Abdi hakunijibu chochote. Aliimpa mtu mmoja ile nyundo akatoa msumari kutoka mfukoni mwake na kumpa.

“Sasa mtoboe utosi wake. Mimi nitakinga damu yake kwenye kikombe” alimwambia yule mtu aliyempa ile nyundo na msumari.

Jamaa akaupachika msumari kwenye utosi wangu. Nikajua ni yale aliyoniambia Shamsa. Nikaanza kupiga kelele.

“Abdi mbona  unataka kuniua…nimekukosea nini…?”

Wakati napiga kelele Abdi alikuwa akimuihimiza yule mtu aupige nyundo ule msumari ili  atoboe utosi wangu.

“Mpige nyundo haraka Garbela…toboa utosi huo…?”

SASA ENDELEA

“Abdi acha ukatili huo…usiniue Abdi…!” niliendelea kumpigia kelele Abdi ambaye hakuonesha kunijali hata chembe.

Nilikuwa nikiwatazama kiupande upande kwani nilikuwa nimening’inizwa kichwa chini kama mnofu wa nyama buchani.

Nikamuona yule mtu aliyetajwa kwa jina la Garbela akiinua nyundo ili aupige ule msumari ambao tayari alikuwa ameukita kwenye utosi wangu na  kunisababishia maumivu makali. Ghafla nikaona  kitu kama kiza kikivamia katika lile eneo. Lakini hakikuwa kiza, kilikuwa kivuli kilichotokea kwa juu na kushuka chini kwa kasi ya ajabu.

Naam kilikuwa kivuli cha nondo! Joka kubwa ambalo lilianguka  kutoka juu ya ule mti. Lilikuwa ni lile lile lililoibuka katika ile boti siku ile niliyotaka kutoswa baharini.

Joka hilo liliugonga utosi wa Abdi kwa meno yake yaliyokuwa nje Nikamuona Abdi anaanguka chini kwa taratibu kama mlevi huku utosi wake ukitokwa na damu.

Yule mtu aliyekuwa anataka kunitoboa utosi aliduwaa ghafla. Alipozinduka alitupa nyundo na msumari pembeni, akawa anawania kupanda juu ya lile shimo ili akimbie. Lakini hakuwahi. Wakati ule anaparamia lile shimo, joka hilo liligeuza kichwa na kumgonga utosini.

Nikamuona anarudi chini taratibu kama mtu aliyepoteza nguvu zote. Akaanguka.

Wale watu waliokuwa wameshikilia kamba niliyokuwa nimening’inizwa nayo waliiachia na kukimbia. Walipoiachia kamba ilijivuta nikaanguka chini kama gunia.

Lile joka lilitoka kwenye lile shimo na sikujua lilitokomea wapi.

Nikajifungua ile kamba kisha nikamsogelea Abdi na kumuinua. Hakuweza kuinuka. Alikuwa amepoteza nguvu zote na alionekana alikuwa taabani.

Pengine lile joka lilipomgonga lilimtia sumu. Nikajua Abdi asingeweza kupona tena.

Huku nikiwa nimekishikilia kichwa chake nilimtazama kwa huzuni hasa vile nilivyoona kuwa anakufa.

“Abdi  ulikuwa unataka kuniua ndugu yanngu…nilikukosea nini?” nikamuuliza.

“Nisamehe sana. Wewe ni ndugu yanngu wa damu. Baba yako mkubwa alikuja  huku Somalia kutoka Tanzania na kunizaa mimi na Yusufu. Lakini nilifanya makosa. Nakiri kuwa nilifanya makosa…”

Alinyamaza baada ya kuishiwa na pumzi. Alipumua kwa sekunde kadhaa kisha akaendelea.

“Nilitaka kukuua kwa sababu niliambiwa na mganga kuwa una jini wa utajiri ambaye mimi nilikuwa namtaka na hicho ndicho kilichonifanya nikulete huku Somalia….”

Abdi alinyamaza tena akapumua kwa sekunde kadhaa kisha akaendelea.

“Kwa kudhani nikimpata huyo jini ningetajirika, nilimuua mke wangu na juzi juzi tu nilimuua mdogo wangu na leo nilitaka kukuua wewe kwa sababu mganga aliniambia nikutoboe utosi kisha nijipake da,mu yako…”

Abdi hakuweza kuendelea kusema baada ya pumzi kumuishia. Alipumua tena kwa sekunde kadhaa kabla ya kuweza tena kufungua mdomo wake.

“Anayeniua mimi ni jini wako. Alikuja kukuokoa baada ya kuona utakufa…”

Wakati Abdi anazungumza, mimi nilikuwa nikitikisa kichwa wakati wote  kumsikitikia.

“Kweli ninaamini sasa kuwa usiilalie mlango wazi bahati ya mwenzako. Nisamehe ndugu yangu kwa upumbavu wangu”

Abdi alitia mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa funguo mbili zilizofungwa pamoja akanipa.

“Ufunguo mmoja ni wa nyumba yangu iliyoko shamba. Ukiingia ndani katika chumba cha mkono wa kulia kuna mlango wa kuteremka chini ambako pia kuna chumba. Ukiingia katika chumba hicho utakuta sefu ya chuma. Utaifungua kwa huo ufunguo wa pili ambao ni mrefu…”

Kuna nini humo ndani?” nikamuuliza baada ya kuona amenyamaza.

“Nimeweka sanduku lililojaa dhahabu pamoja na dola za kimarekani. Kuna dola milioni moja. Utachukua wewe hilo sanduku. Pia utachukua magari yangu, nyumba zangu na hoteli zangu. Utakuwa mrithi wangu….”

Abdi hakumaliza maneno yake, sauti yake ilififia akakata roho mikononi mwangu. Bila shaka ile sumu ya lile joka ilikuwa imeshamuathiri moyo wake.

Nikakiweka kichwa chake chini huku nikijiambia.

“Ameyataka mwenyewe”

Nilimpekua mifukoni nikachukua pochi yake pamoja na funguo ya gari na funguo ya nyumbani kwake. Nikasimama na kutoka kwenye lile shimo. Niliona jamaa wawili miongoni mwa wale watu waliokuwa pamoja na Abdi wakikimbia. Kumbe walikuw a wakituchungulia ndani ya lile shimo.

Nilitembea kwa hatua za ukakamavu kuelekea pale lilipokuwa gari la Abdi. Nikafungua mlango wa dereva na kuliwasha. Nikarudi mjini.

Nilikuwa nimepata majonzi kweli kweli kutokana na kifo kile cha Abdi. Nilihuzunika kama vile si yeye aliyekuwa anataka kuniua.

Nilijiambia kama maisha ya Abdi yamekwisha na maisha yangu pale Somalia pia yamekwisha. Kama nitaendelea kuishi pale Somalia, mwenyeji wangu atakuwa nani? Nikajiuliza bila kupata jibu.

Nilifika nyumbani kwangu nikamueleza Shamsa mkasa mzima uliotokea. Shamsa akashangaa sana.

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment