Monday, August 22, 2016

HADITHI, MWANAMKE

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
 
MWANAMKE
 
ILIPOISHIA
 
Abdi alitaka kuniua kwa sababu ya fedha. Alijua nikishakufa atampata jini ambaye atampa fedha ili atajirike, ainunue Mogadishu yote iwe mali yake.
 
Wenzake nao walinipiga chuma bila kujali ningedhurika kiasi gani kwa sababu ya fedha. Abdi alivunja udugu na wenzake walivunja urafiki kwa sababu ya kitu fedha.
 
Nikaendelea kujiambia, sasa mimi ni nani niiachie, nitawatafuta na kuwasulubu. Watajua mimi nani.
 
Nilirudi nyumbani nikamueleza Shamsa masahibu yaliyonipata. Nilimuonesha lile jaraha ambalo nilikuwa na hakika kwamba  nilipigwa chuma.
 
Shamsa aliposikia ile habari alisikitika sana.
 
“Pole sana. Walitaka kukuua” akaniambia.
 
“Lakini sikufa na nimeshawajua, sitawaachia”
 
“Utawatafuta?” Shamsa akaniuliza.
 
“Sitawaachia wachukue ile dhahabu pamoja na dola zangu. Abdi alikwishanipa mimi”
 
“Watakuumiza!”
 
“Hawathubutu. Kama ni kwa ngumi hakuna yeyote anayeweza kusimama na mimi. Nina hakika nitawagaragaza vibaya sana”
 
“Una uhakika na unachokisema?”
 
“Mirungi imeshawamaliza, hawanitishi!”.
 
“Sasa sikiliza nikuambie”
 
“Unataka uniambie nini?”
 
“Mimi napajua anapokaa Esmail. Sasa nataka ukimfuata twende sote”
 
“Hakuna tatizo, tutakwenda lakini ujue kama litazuka suala la ngumi tutazichapa”
 
“Kama tumekubaliana hivyo, sawa”
 
Shamsa akaingia chumbani. Alipotoka alikuwa amebadili nguo. Alivaa baibui na ndani yake alivaa jinzi.
 
“Twende” akaniambia.
 
Tukatoka. Wakati tunataka kujipakia kwenye gari Shamsa aliniambia.
 
“Nitaendesha mimi”
 
Nikampisha kwenye sukani. Shamsa aliliwasha gari tukaondoka. Tulikwenda katika eneo moja lililokuwa kando kidogo ya jiji hilo. Tuliingia katika  mtaa mmoja uliokuwa mtulivu.
 
“Mtaa huu ndio anaoishi Esmail” Shamsa akaniambia na kuongeza.
 
“Nyumba yake ni ile pale yaliposimama magari”
 
Niliyaona magari hayo. Yalikuwa yameegeshwa nje ya nyumba ya saba mbele yetu.
 
Shamsa alikuwa amepunguza mwendo. Kitu ambacho kilinipa moyo ni kuwa moja ya gari hilo ndilo lile nililoliona limeegeshwa kule shamba.
 
SEkunde chache tu baadaye tukawa tumeifikia nyumba hiyo. Shamsa akaliegesha gari nyuma ya gari la Esmail. Wakati analizima moto gari hilo tuliona mtu akitoka katika nyumba hiyo. Alikuwa amebeba begi lililokuwa limejaa na alionekana dhahiri kuwa alikuwa na wasiwasi na alikuwa akikimbizia kitu.
 
Alishuka haraka haraka kwenye baraza ya nyumba akajipakia kwenye lile gari lililokuwa mbele ya gari la Esmail na kuondoka kwa kasi.
 
Tulishuka haraka kwenye gari tukaenda kwenye mlango wa nyumba ya Esmail. Mimi nilitaka kubisha mlango lakini Shamsa aliusukuma. Mlango ukafunguka. Shamsa akaingia na mimi nikamfuata.
 
Kisaikolojia tu nilikgundua kuwa Shamsa alikuwa amebadillika. Macho yake yalionesha dhahiri kuwa alikuwa amepanga shari.
 
Kusema kweli sikujua nini kingetokea humo ndani.
 
Tulipofika sebuleni tulikuta maiti ya mtu iliyokuwa ikivyja damu kichwani.
 
Shamsa akanitazama na kuniambia.
 
“Unaona! Wanamalizana wenyewe kwa wenyewe. Yule aliyetoka na begi amemuua mwenzake ili apate yeye pesa na dhanhabu”
 
“Na ameshakimbia. Sijui tutampataje?’
 
“Tutampata. Napajua anapoishi Esmail”
 
“Basi twende tumfuate kabla hajatokomea  na zile pesa”
 
Tukatoka.
 
Tulijipakia kwenye gari. Aliyekuwa akiendesha alikuwa Shamsa.
 
Tulikwenda hadi nyumbani kwa Esmail. Shamsa akaniambia nijifiche nyuma ya mlango. Yeye ndiye aliyebisha mlango.
 
Dakika chache baadaye mlango ukafunguliwa.  Shamsa akaingia.
 
“Amour njoo” akanimbia.
 
Na mimi nikaingia. Niliona Shamsa alikuwa amemtolea bastola Esmail.
 
“Tunataka zile pesa pamoja na dhanhabu a Abdi” Shamsa alimwambia Esmail akiwa amemuelekezea bastola.
 
Esmail alikuwa ameinua mikono juu akirudi kinyume nyume.
 
“Sina pesa wala dhahabu za Abdi” akasema huku macho yake yakionesha wasiwasi.
 
“Eti nini? Si tumekuona ukikimbia na begi la pesa na dhahabu baada ya kumuua mwenzako. Toa lile begi mpumbavu wewe kabla sijakisambaratisha kichwa chako kwa risasi!”
 
“Subirini, nitawapa”
 
“Hakuna cha kusubiri. Toa lile begi haraka”
 
Esmail alifungua mlango wa chumba kimojawapo.
 
“Unataka kwenda wapi?” Shamsa akamuuliza.
 
“Lile begi liko humu”
 
“Huwezi kuingia peke yako. Ngoja tuingie sote”
 
Shamsa akaingia pamoja na Esmail ndani ya kile chumba na mimi nikawafuata.
 
Kilikuwa chumba kilichotumika kama astoo. Esmail alilitoa begi alilokuwa amelificha nyuma ya kabati bovu.
 
Wakati anampa begi hilo Shamsa alipambana na risasi ya kichwa. Esmail akaanguka chini. Shamsa akalichukua lile begi.
 
Alilifungua na kulitazama ndani kasha akaniambia.
 
“Twende zetu”
 
Tukatoka na kujipakia kwenye gari.
 
Tulirudi nyumbani. Shamsa akanimabia tusilale nyumbani tutakamatwa. Tulikusanya nguo zetu pamoja  na vitu vyetu muhimu rukavitia kwenye begi kasha tukatoka tena.
 
Tulijipakia kwenye gari. Shamsa akaniambia tunakwenda katika mji ulioko mpakani mwa Kenya ili tuondoke nchini humo.
 
ITAENDELEA KESHO.

No comments:

Post a Comment