Saturday, August 13, 2016

WAZIRI MUHONGO ALITAKA SHIRIKA LA UMEME KUPUNGUZA BEI NA KUSEMA FIDIA HAKUNA



Tangakumekuchablog
Handeni, WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Mohongo, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupunguza bei ya umeme na kupunguza gharama ya kunganisha wateja wapya,  ili kila mwananchi kumudu gharama ya nishati hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya siku ya kwanza ya  kutembelea miradi ya Rea Mkoani Tanga, Muhongo alisema shirika hilo hupandisha bei ya umeme lakini huwa haishushi bei hivyo na  kulitaka kupunguza ili mwananchi wa kipato cha chini aweze kumudu.
Alisema Serikali ya awamu ya tano ndani ya miaka mitano inataka mwananchi wa mjini na vijijini awe anatumia nishati hiyo ya umeme majumbani na kumudu gharama zake.
“Ili kwenda na sera ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ndani ya miaka mitano tunataka umeme umeshasambaa nchini kote mjini na vijijini, mwekezaji wa ndani na nje umeme usiwe kuwa ni kikwazo” alisema Muhongo na kuongeza
“Lakini yote hayo hayatafanikiwa kama shirika halitapunguza bei ya umeme majumbani na gharama ya ufungaji kwa kweli hiki ndio kilio cha watanzania wote hivyo niwatake kupunguza kwani kila siku huwa munapandisha na kusahau kupunguza” alisema
Akizungumzia miradi ya Rea vijijini, Muhongo alisema hakutokuwa na fidia mradi utakapopita na yoyote ambaye atang’ang’ania kulipwa mradi huo utabadilisha uelekeo.
Alisema Serikali ikiendelea kulipa fidia pesa zote za mradi zitaenda kwa kulipa wananchi fidia na mradi kukwama hivyo kuwataka wananchi kutambua kuwa mradi huo ni kwa maslahi yao wenyewe.
Alisema pesa zilizotengwa kwa ajili ya usambazaji umeme vijijini ni za usambazaji na sio za kuwalipa wananchi fidia hivyo kijiji au mwananchi ambaye atataka kulipwa fidia atambue kuwa pesa hizo hazipo na hakuna.
“Serikali haijatenga kuwalipa fidia wananchi ili kupisha mradi wa usambazaji umeme vijijini, na yoyote ambaye anadhani kuwa kuna pesa hizo asijidanganye na kupoteza muda” alisema Waziri huyo wa Nishati na Madini
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha umeme huo unasambazwa nchini kote na wananchi kufaidika pamoja na kutoa fursa za maendeleo kwa wananchi na wawekezaji.
                                               Mwisho

No comments:

Post a Comment