Tuesday, August 30, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 66

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
 
MWANAMKE 66
 
ILIPOISHIA
 
Mama akabadili lugha na kuanza kuongea na Zena kwa ukali.
 
Walijibizana kwa muda kidogo kisha Zena akaniambia.
 
“Si tumekubaliana tuje huku tuoane?”
 
Kabla sijajibu yule mama akamuuliza Zena kwa Kiswahili.
 
“Muoane kwa idhini ya nani?”
 
Zena akanyamaza kimya.
 
“Mwenye idhini ni baba yako, umeshamwambia?” mwanamke huyo akamuuliza Zena.
 
“Si ndiyo tumekuja hivi?”
 
“Sasa mwambie baba yako, akikukubali uoane na huyo kijana ndio mtaweza kuoana”
 
“Wewe pia si unaweza kutoa idhini”
 
“Nitoe idhini mimi ni mwanume?”
 
Yule mama alipouliza swali hilo na kukosa jibu aligeuka na kuondoka. Nikamuona Zena akishusha pumzi ndefu.
 
“Kwanini mama yangu anapokuuliza maswali unasita kujibu?’ akaniuliza.
 
“Sijui nijibu nini”
 
“Kwani mimi na wewe si tumekwishaoana kule Somalia?”
 
“Mimi nilioana na Shamsa. Baadaye ndio ukatokea wewe”
 
“Ulioana na mimi si Shamsa, si nilikwambia?”
 
SASA ENDELEA
 
Nikanyamaza kimya.
 
“Huyu mama nilitarajia atakuwa upande wangu, naye ameshaanza kuleta taabu” Zena akajisemea peke yake kisha akainuka na kuniambia.
 
“Twende”
 
“Twende wapi?’ nikamuuliza huku nikiinuka.
 
“Nifuate”
 
Tukatoka katika lile jabali ambalo ukiingia ndani yake ni kama uliyeingia kwenye nyumba, tukaelekea katika jabali jingine dogo lililokuwa kando ya lile.
 
Tulipoingia katika jabali hilo Zena aliniambia kuwa pale ilikuwa ni sahemu yake ya kupumzika.
 
“Tukae hapa” akaniambia. Palikuwa na sebule ndogo iliyokuwa na mito iliyowekwa chini.
 
Tukakaa.
 
“Amour usiwe muoga. Kama utaulizwa umenipenda, sema ndio usisitesite. Ukisitasita watajua nimekulazimisha”
 
Wakati Zena akiniambia hivyo akaingia jini mmoja aliyekuwa kifua wazi. Alikuwa amejifunga shuka nyeupe kiunoni. Ndevu zake nyeupe zilikuwa zikikaribia kufika kweye tumbo lake kubwa. Kifua chake kilikuwa kimejaa manyoya meupe na marefu.
 
Alimsalimia Zena kisha akamwambia ana ujumbe kutoka kwa baba yake Mzee Jabalkeys.
 
“Anasemaje?” Zena akamuuliza.
 
“Amenituma nikwambie kwamba huyo kijana uliyekuja naye umrudishe huko huko ulikomtoa”
 
Moyo wangu ulishituka na kuanza kwenda mbio.
 
“Nitamrudishaje wakati tumekuja kuoana na ametaka kuwajua wazazi wangu!” Zena akasema.
 
“Unajua baba yako amekasirishwa na kitendo chako cha kutaka kuoana na binaadamu. Amesema yeye hawezi kutoa idhini uoane na binaadamu na hataki kabisa kusikia kitu kama hicho”
 
“Lakini wenyewe si tumeshakubaliana”
 
“Lakini Zena wewe ni jinni, utaolewaje na binaadamu halafu mtaishi vipi?”
 
“Majini wanaoa binaadamu na wengine wanaolewa na binaadamu labda useme baba hajui tu”
 
“Hata kama ni hivyo lakini huko ni kukiuka kawaida yetu. Hilo jambo halifai”
 
“Kama yeye baba amesema hivyo basi mimi nitajiozesha mwenyewe, si lazima nipate idhini yake”
 
“Sasa huo ni ukosefu wa adabu kwa baba yako”
 
“Potelea mbali!”
 
“Sasa nikamwambie hivyo?”
 
“Nenda”
 
Yule jinni aliyeonekana kukasirika akatoka na kumuacha Zena akigomba peke yake.
 
“Najuta  kuja huku! Wazee gani hawa wasiolewa mambo. Wamekuwa washamba kiasi hiki!”
 
Ghafla nikamuona mzee mwingine aliyekuwa amefuatana na yule mzee aliyeondoka pamoja na mzee mwingine.
 
“Wewe mtoto mwenye laana ulimjibu nini huyu Subyani?” Yule mzee akamuuliza Zena kwa sauti ya ukali.
 
“Lakini baba ungenisikiliza mimi mwenyewe badala ya kusikiliza watumishi wako. Hao wanaongeza maneno”
 
“Mimi sihitaji kukusikiliza kwa sababu najua wewe umekuwa jeuri na asi. Ninachokwambia ni kwamba mrudishe huyu kijana ulikomtoa na kwamba sitaki kusikia tena kwamba unataka kuoana na binaadamu!”
 
Zena akafura kama chatu.
 
“Mimi lazima nitaoana naye, iwe itakavyokuwa. Kama hamtaki nitajiozesha mwenyewe!”
 
Zena akainuka pale alipokuwa ameketi akatoka kwa hasira huku yule mzee niliyemdhania kuwa ndiye Jabalkeys akimtazama.
 
“Huyu mtoto amekuwa shetani kabisa, si jini tena” akasema kisha akanisogelea mimi.
 
“Mwanangu amekutoa wapi yule shetani?” akaniuliza.
 
“Amenitoa kwetu”
 
“Wapi”
 
“Tanga”
 
“Mlikubaliana mje muoane huku?”
 
“Yeye ndiye aliyekuwa analazimisha. Amenitia kwenye matatizo mengi. Naomba msaada wako”
 
“Hata kama nitawambia hawa watumishi wangu wakurudishe, bado ataendelea kukufuata na atakusumbua lakini suala lake nitalipeleka kwa Sultani wetu. Wewe subiri hapa hapa”
 
Majini hao wakaondoka. Nikabaki peke yangu. Sikujua Zena alikuwa amekwenda wapi na angerudi saa ngapi. Na pia sikujua ningeendelea kukaa pale hadi muda gani. Kusema kweli ile hali ya Zena kuanza kutibuana na wazazi wake ilianza kunitia hofu.
 
Baada ya kama nusu saa hivi yule jini aliyekuja kwanza akarudi peke yake akiwa ameshika bahasha.
 
“Begi lako ni lipi na lipi?” akaniuliza.
 
Nikamuonesha yale mabegi mawili niliyokwenda nayo. Yule jini akayabeba yote mawili kisha akaniambia.
 
“Twende”
 
Nikatoka naye katika lile jabali tukashika njia ambayo mimi na Zena tulikwenda nayo. Tukashuka chini baharini. Ikumbukwe kwamba muda ule ulikuwa ni usiku lakini ulikuwa usiku wa mbalamwezi.
 
ITAENDELEA kessho hapahapa tangakumekuchablog usikose uhondo ;;;;;;

No comments:

Post a Comment