Friday, August 19, 2016

HADITHI,MWANAMKE SEHEMU YA 59

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 59

ILIPOISHIA

Abdi alitia mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa funguo mbili zilizofungwa pamoja akanipa.

“Ufunguo mmoja ni wa nyumba yangu iliyoko shamba. Ukiingia ndani katika chumba cha mkono wa kulia kuna mlango wa kuteremka chini ambako pia kuna chumba. Ukiingia katika chumba hicho utakuta sefu ya chuma. Utaifungua kwa huo ufunguo wa pili ambao ni mrefu…”

“Kuna nini humo ndani?” nikamuuliza baada ya kuona amenyamaza.

“Nimeweka sanduku lililojaa dhahabu pamoja na dola za kimarekani. Kuna dola milioni moja. Utachukua wewe hilo sanduku. Pia utachukua magari yangu, nyumba zangu na hoteli zangu. Utakuwa mrithi wangu….”

Abdi hakumaliza maneno yake, sauti yake ilififia akakata roho mikononi mwangu. Bila shaka ile sumu ya lile joka ilikuwa imeshamuathiri moyo wake.

Nikakiweka kichwa chake chini huku nikijiambia.

“Ameyataka mwenyewe”

Nilimpekua mifukoni nikachukua pochi yake pamoja na funguo ya gari na funguo ya nyumbani kwake. Nikasimama na kutoka kwenye lile shimo. Niliona jamaa wawili miongoni mwa wale watu waliokuwa pamoja na Abdi wakikimbia. Kumbe walikuw a wakituchungulia ndani ya lile shimo.

Nilitembea kwa hatua za ukakamavu kuelekea pale lilipokuwa gari la Abdi. Nikafungua mlango wa dereva na kuliwasha. Nikarudi mjini.

Nilikuwa nimepata majonzi kweli kweli kutokana na kifo kile cha Abdi. Nilihuzunika kama vile si yeye aliyekuwa anataka kuniua.

Nilijiambia kama maisha ya Abdi yamekwisha na maisha yangu pale Somalia pia yamekwisha. Kama nitaendelea kuishi pale Somalia, mwenyeji wangu atakuwa nani? Nikajiuliza bila kupata jibu.

Nilifika nyumbani kwangu nikamueleza Shamsa mkasa mzima uliotokea. Shamsa akashangaa sana.

SASA ENDELEA

“Amenirithisha kila kitu. Nataka kwenda nyumbani kwake nikapekua. Kama kutakuwa na kitu muhimu nikichukue”

Shamsa alikuwa akiendelea kuhuzunika.

“Masikini Abdi. Amejidhulumu mwenyewe nafsi yake…”

“Muda wake umeshafika” nikamwambia Shamsa.

“Lakini naona huyo jini bado anakuandama”

“Bila shaka, lakini ajabu ni kwamba hajanitokea wala kunisumbua kama zamani”

“Kama si yeye ungekufa wewe leo”

“Ni kweli ningekufa. Sasa mimi naenda kwa Abdi”

“Twende sote” shamsa akanimbia.

“Twende”

Shamsa akavaa baibui lake tukatoka. Tulijipakia kwenye gari ya Abdi tukaondoka.

Tulifika nyumba kwa Abdi nikafungua mlango. Nyumba ilikuwa kimya. Abdi hakuwa na mke wala mtoto na alikuwa ameshafukuza wafanyakazi wake wote.

Tuliipekua nyumba nzima. Katika kabati la Abdi lililokuwa chumbani mwake tulikuta shilingi za kisomali milioni kumi. Shamsa akaniambia tuzichukue. Tukazichukua. Tukafunga milango na kurudi nyumbani kwetu.

Nilimshusha Shamsa pamoja na zile shilingi milioni kumi. Nilimwambia kuwa nilitaka kwenda shambani kwa Abdi kuchukua hilo sanduku la dhahabu ambalo pia lilikuwa na dola za Kimarekani.

Nikaanza safari ya kuelekea shambani kwa marehemu Abdi. Nilipofika. Nilikuta gari la Ismail, rafiki yake Abdi likiwa limeegeshwa mbele ya nyumba ya Abdi.

Niliposhuka kwenye gari nilikwenda kuujaribu mlango wa nyumba hiyo,. nikakuta ulikuwa umefungwa. Nikaizunguka ile nyumba kumtafuta aliyekuja na gari lile.

Sikuona  mtu. Nikapatwa na wasiwasi. Ghafla nikasikia hatua za mtu anayenyata nyuma yangu. Nikageuka haraka nitazame nyuma lakini sikuwahi, nilihisi kitu kizito kama nyundo kikipiga kichwani kwangu. Hapo hapo nilidondoka na kuzirai.

Nilipozinduka nilijikuta nilikuwa nimelala mahali pale pale nilipoanguka. Kabla ya fahamu kunijia sawasawa nilijiuliza nilikuwa wapi na kwanini nilikuwa nimelala chini.

Kichwa kilikuwa kizito kama kilichokuwa kimebebeshwa mzigo na mwili ulikuwa umechoka utadhani nililala kwenye sakafu kwa masaa kadhaa.

Nilipojaribu kukumbuka nini kimenitokea, kichwa kiliniuma na nilihisi kizunguzungu.

Lakini taratibu kumbukumbu zilianza kunijia. Kumbukumbu ya kwanza kunijia ilikuwa ni ile ya kutaka kuuliwa na Abdi.

Nikakumbuka nilivyokuwa kwenye shimo huku Abdi akimuihimiza mtu aliyekuwa amempa nyundo apigilie msumari kwenye utosi wangu.

Kumbukumbu hiyo ilinijia kama sinema ya kutisha akilini mwangu. Ingawa ni tukio ambalo lilishapita lilinitia hofu kama vile ndio kwanza linatokea.

Kumbukumbu ya pili kunijia ilikuwa ni ya kufika katika shamba la Abdi, kusimamisha gari na kukuta gari la Esmail. Nikakumbuka jinsi nilivyozunguka nyuma ya nyumba ya Abdi kumtafuta mwenye gari lile lakini ghafla nikasikia hatua za mtu nyuma yangu.

Niliposikia hatua hizo nikataka kugeuka ili nitazame nyuma lakini sikuwahi kuona kitu, nilishitukia nikipigwa na kitu kizito kama nyundo kichogoni kwangu, macho yangu yakafunga kiza na sikuelewa tena kilichotokea.

Nikapeleka mkono wangu kichogoni na kupapasa pale mahali nilipopigwa, nikaona palikuwa na jeraha na dami ilitoka na kuganda.

Sasa nikainuka huku nikijiuliza ni nani aliyekuwa amenipiga. Nilitazama kila upande, sikuona mtu. Kila  wakati nilikuwa najipapasa pale kwenye kijaraha na kutazama ile damu mkononi mwangu.

Swali la nani aliyenipiga lilikuwa halina jibu kwani sikuona mtu yoyote. Eneo lote lilikuwa kimya. Nilirudi kwenye mlango wa ile nyumba, nikauona uko wazi. Wakati nilipokuja na gari langu mlango huo ulikuwa umefungwa.

Sasa nikaanza kupatwa na wasiwasi.

Ni nani aliyeufungua huo mlango wakati funguo nilikuwa nayo mimi?

Wakati najiuliza hivyo nilijipekua mifukoni. Zile funguo sikuziona. Nikaingia haraka mle ndani. Niliingia katika kile chumba alichonielekeza Abdi. Milango yote niliikuta wazi. Nikashuka katika kile chumba cha chini kwa chini ambacho Abdi aliniambia kulikuwa na sefu ya chuma na ndani ya sefu hiyo kulikuwa na sanduku lenye dhahabu pamoja na dola za Kimarekani alizokuwa amezificha.

Sefu niliikuta lakini ilikuwa wazi. Nilipochungulia ndani ya sefu hiyo sikukuta chochote. Sefu ilikuwa tupu kama mkono uliorambwa!

Nikatoka nje ya ile nyumba. Sasa fahamu zikanijia vizuri. Nilikumbuka wakati ule natoka katika lile shimo nililoingizwa na kina Abdi, niliona watu wawili wakikimbia. Bila shaka walisikia wakati Abdi alipokuwa ananiagiza nije nichukue lile sanduku lililokuwa na dola pamoja na dhahabu.

Kwa kutaka wanufaike wao, walikimbilia wao kuja hapa lakini wakashindwa ama kuingia katika ile nyumba au walishindwa kulifungua ile sefu kwa sababu hawakuwa na funguo. Ndipo wakaamua kunisubiri na mmoja wao ndiye aliyenipiga chuma hadi nikazirai.

Ndio sababu nilikuta lile gari la Esmail lakini baada ya kuzirai na kurejewa na fahamu, gari hilo sikuliona. Walikuwa wameshalichukua lile sanduku na kuondoka.

Esmail rafiki yake Abdi nilikuwa nikimfahamu vizuri. Bila shaka na yeye alikuwemo katika ule mpango wa kutaka kuniua.

Nikajimbia sitawaachia wachukue dhahabu ile pamoja na dola za Kimarekani ambazo Abdi alikwishanipa

“Hawa watu kweli ni majambazi!” nikajiambia kimoyomoyo na kuongeza.

“Huu walionifanyia ni ujambazi kamili. Lakini nitapambana nao!”

Nilirudi kwenye gari langu nikaliwasha na  kuondoka.

Kwanza nilikwenda kwenye zahanati moja nikaoshwa lile jeraha kisha nikafungwa dawa. Nilipotoka katika zahanati hiyo nilikwenda katika duka la nguo nikanunua pama na kulivaa kuficha lile jaraha.

Nikaendesha gari kuelekea nyumbani kwangu huku nikiwaza jinsi majambazi hao wa Abdi walivyonizunguka. Nilishukuru kwamba nilikuwa na afya njema, vinginevyo kile chuma walichonipiga kichogoni kingenimaliza kabisa.

“Fedha haina udugu wala urafiki” niliwaza kimoyo moyo.

Abdi alitaka kuniua kwa sababu ya fedha. Alijua nikishakufa atampata jini ambaye atampa fedha ili atajirike, ainunue Mogadishu yote iwe mali yake.

Wenzake nao walinipiga chuma bila kujali ningedhurika kiasi gani kwa sababu ya fedha. Abdi alivunja udugu na wenzake walivunja urafiki kwa sababu ya kitu fedha.

Nikaendelea kujiambia, sasa mimi ni nani niiachie, nitawatafuta na kuwasulubu. Watajua mimi nani.

Nilirudi nyumbani.ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment