Sunday, August 28, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 65

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
 
MWANAMKE
 
ILIPOISHIA
 
“Wanakushangaa kwani hawawajui binaadamu? Wewe si binaadamu wa kwanza kufika huku”
 
“Na hao binaadamu wengine wanafikaje huku?”
 
“Wanaletwa na majini wao kufundishwa uganga au kutembea tu. Tena wanakaa muda mrefu hadi wanajua lugha yetu”
 
“Na mimi naweza kuwaona hao binaadamu wenzangu?”
 
“Huku kila mmoja ana lake. Siwezi kujua wako wapi na hao waliowaleta sihusiani nao”
 
Tukafika katika jabali moja lililokuwa na mnara mrefu. Zainush akaniambia kuwa pale ndio kwao.
 
Wakati tunataka kuingia kwenye mlango wa jabali hilo wakaja majini watatu kutupokea. Walikuwa wanawake watupu tena wasichana wadogo. Lugha ya Zena ikabadilika, akawa anaongea kikwao.
 
Walitupokea yale mabegi wakatangulia nayo ndani na sisi tukafuata nyuma. Zena akaniambia kuwa wale walikuwa wadogo zake.
 
“Sisi tuko thelathini, wanawake tuko kumi na saba, waliobaki ni wanaume”
 
“Mko wengi sana. Nyote ni baba mmoja na mama mmoja?”
 
“Baba mmoja na mama mmoja”
 
“Wewe ni wa ngapi kuzaliwa?”
 
“Ni wa saba lakini kwa wanawake mimi ni wa pili”
 
“Hao ndugu zako wengine wako humu?”
 
“Wale wakubwa wana masikani zao zingine. Walioko hapa ni wale wadogo tu”
 
Tukafika mahali ambapo tulikuta pazia zito la rangi nyeupe.
 
SASA ENDELEA
 
Zena alilipenua pazia hilo tukapita na kutokea kwenye chumba kipana kilichokuwa kama sebule. Kilikuwa kimetandikwa mazulia yenye mistari rangi tatu tofauti, rangi nyeupe, rangi nyekundu na rangi ya bahari.
 
Kulikuwa na mito ya pamba ya kukalia ambayo ilikuwa imewekwa chini kuzunguka sebule nzima.
 
Wale wadogo zake Zena walielekea kwingine. Zena akaniambia.
 
“Tukae hapa”
 
Akatangulia yeye kukaa kwenye mto mmojawapo na mimi nikakaa kwenye mto mwingine.
 
“Hapa ndio nyumbani kwetu” akaniambia.
 
Nilikuwa nikikizungushia macho kile chumba kuangalia nakshi zilizokuwa zimetiwa mle ndani. Kwa mbali nikasikia harufu kama ya marashi na udi wa Unguja.
 
“Kwa hiyo wazazi wako wako hapa?” nikamuuliza Zena.
 
“Wako hapa. Mama yangu atakuja sasa hivi, yuko ndani”
 
Haikutimu hata dakika moja mwanamke mmoja wa kiarabu akachomoza na kusogea karibu yetu. Alikuwa mtu mzima sana. Mwili wake wote ulikuwa umezibwa na shuka nyeupe. Sikuweza kuona hata miguu yake.
 
Kilichokuwa kikionekana ni uso wake. Ingawa alikuwa mwanamke lakini alikuwa na ishara za kutoka sharafa. Alikuwa na macho ya kijivu yaliokuwa na mboni zilizounda mstari mwembamba.
 
Akatuambia. “Assalaam alaykum”
 
Tukamuitikia. “Waalayka ssalaam”
 
Baada ya hapo mwanamke huyo alibadili lugha akawa anaongea kijini na Zena. Sikuelewa walikuwa wakizungumza nini.
 
Yule mama hakukaa. Alibaki amesimama vile vile. Wakati anazungumza na Zena mara kwa mara alikuwa akinitazama mimi.
 
Mwishowe Zena akaniambia kwa Kiswahili.
 
“Umemuona mama yangu”
 
“Ndiye huyu?” nikamuuliza huku nikiogopa kumtazama kutokana na macho yake.
 
“Ndiye yeye lakini hajui Kiswahili vizuri. Hutaweza kuzungumza naye”
 
Yule mama akacheka.
 
“Ninajua. Kwanini yeye ajue mimi nisijue” akaniambia kwa Kiswahili chenye lafidhi ya kiarabu kisha akaniuliza.
 
“Unaitwaje mwanangu?”
 
“Naitwa Amour”
 
“Mmekubaliana nini na Zena?”
 
Kidogo nilisita kujibu. Zena akanitazama na kuniambia.
 
“Mwambie”
 
“Aliniambia  tuje huku” nikamjibu.
 
“Kufanya nini?”
 
Nikamtazama tena Zena.
 
“Amour unaulizwa, mbona unanitazama mimi”
 
“Nisaidie kujibu, wewe ndiye uliyenileta huku”
 
Mama akabadili lugha na kuanza kuongea na Zena kwa ukali.
 
Walijibizana kwa muda kidogo kisha Zena akaniambia.
 
“Si tumekubaliana tuje huku tuoane?”
 
Kabla sijajibu yule mama akamuuliza Zena kwa Kiswahili.
 
“Muoane kwa idhini ya nani?”
 
Zena akanyamaza kimya.
 
“Mwenye idhini ni baba yako, umeshamwambia?” mwanamke huyo akamuuliza Zena.
 
“Si ndiyo tumekuja hivi?”
 
“Sasa mwambie baba yako, akikukubali uoane na huyo kijana ndio mtaweza kuoana”
 
“Wewe pia si unaweza kutoa idhini”
 
“Nitoe idhini mimi ni mwanume?”
 
Yule mama alipouliza swali hilo na kukosa jibu aligeuka na kuondoka. Nikamuona Zena akishusha pumzi ndefu.
 
“Kwanini mama yangu anapokuuliza maswali unasita kujibu?’ akaniuliza.
 
“Sijui nijibu nini”
 
“Kwani mimi na wewe si tumekwishaoana kule Somalia?”
 
“Mimi nilioana na Shamsa. Baadaye ndio ukatokea wewe”
 
“Ulioana na mimi si Shamsa, si nilikwambia?”
 
ITAENDELEA kesho ni kitatokea ungana nami hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment