Saturday, August 13, 2016

HANDENI WALIA KILIO CHA MAJI



Tangakumekuchablog
Handeni, WAKAZI wa Misima, Sindeni na Kwamatuku  Wilayani Handeni Mkoani Tanga, wamelalamika kero ya maji na kumuomba Waziri wa Maji kuimaliza kero hiyo ambayo imedumu kwa miaka mingi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwandishi wa habari hizi jana, wakazi hao wamesema wamekuwa wakitumia maji mito na madimbwi kwa matumizi ya nyumbani jambo ambalo linahatarisha usalama wa afya zao.
Walisema maji hayo ambayo hutumiwa na mifugo kwa  kunyweshea wamedai kuwa mara nyingi hupatwa na magonjwa ya kichocho na kuugua matumbo jambo ambalo  ni hatari.
Hapa kilio chetu kikubwa ni  kero ya maji na kwa sasa tunatumia ya madimbwi ambayo hutumiwa pia na mifugo, hii ni hatari na ndio mara nyingi tunaugua magonjwa ya matumbo na kichocho” alisema Saiomon Mkokoi
“Kero hii imedumu miaka mingi hatujui tatizo liko wapi wakati mji wetu uko na ardhi yenye rutuba nzuri, basituchimbiwe kisima kimoja tu na kuwa na uhakika wa maji safi ili kuepukana na kununua maji kila siku “ alisema Mkokoi
Alisema kwa sasa kilio chao wanakipeleka  kwa Waziri wa maji kwa imani kuwa
ndio kimbilio pekee na mkombozi   baada ya jitihada za viongozi waliopita kushindwa
Kwa upande wake  mfugaji jamii ya kimasai mkazi wa Sindeni Olengusa Papai, alisema mara nyingi huingia ugomvi wa wananchi juu ya matumizi ya maji ya mabwawa ambayo huwa ni yakunyeshea  mifugo.
Alisema ugomvi huo unakuja kutokana na maji hayo kutumika kwa matumizi ya binadamu na mifugo hivyo huwa na wakati mgumu kutokana na mabwawa hayo kuwa  machache.
“Kila siku sisi wafugaji na wananchi tumekuwa tukiingia katika ugomvi juu ya matumizi ya mabwawa, ni kweli kero ya maji ni kubwa lakini hakuna mbadala maji haya haya ni matumizi ya binadamu na mifugo” alisema
Alisema awali kulikuwa na utaratibu wa matumizi ya mabwawa  ambapo ya  mifugo lilitengwa peke yake lakini shida inakuja wakati wa kiangazi ambapo madimbwi mengi hukauka na kila mmoja kukimbilia lililo na maji.
                                          Mwisho

No comments:

Post a Comment