ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 33
ILIPOISHIA
“Kumbe babu yako alikuwa na mke jini, ndiyo maana alipata utajiri ghafla! Lakini hakuwahi
kunieleza hata siku moja. Alikuwa msiri
sana”
“Huyo jini sasa amejitokeza
kwangu na anataka nimrithi ili anipe utajiri aliokuwa nao babu yangu”
“Sasa ulitaka nikupe ushauri
gani?”
“Nimkubalie au nimkatalie?”
Mganga baada ya kutafakari
aliniambia.
Umefanya vizuri kuja kwangu.
Mimi nitakupa ushauri mzuri”
“Nitakushukuru sana”
“Usikubali. Huyo jini atakusumbua sana na pengine atakuja
kukuua. Sasa nimeanza kugundua kuwa hata babu yako aliuawa na huyo jini”
SASA ENDELEA
Maneno ya mganga huyo yakanishitua.
“Kumbe hivi viumbe vina
madhara makubwa?” nikamuuliza
“Wewe hujui tu. Hawa viumbe si
wazuri. Uliona wapi jini akaolewa na binaadamu?”
“Sijawahi kuona”
“Sasa ujue kuwa hicho kitu
hakiwezekani. Huyo jini anakilazimisha kwa nia mbaya. Amemuua babu yako, sasa
anataka kukuua wewe”
Nikabaki nimepigwa na butwaa
la mshangao.
“Wewe angalia vituko na
miujiza aliyokufanyia ndipo utajua ana madhara ya kiasi gani”
“Sasa nifanye nini ili niweze
kuepukana naye?”
“Njoo kesho asubuhi, nitajua
jinsi ya kukusaidia. Huyo hawezi kuondoka mwenyewe mpaka nimuondoe mimi”
“Sasa hapo kesho utakuja
kumuondoa?”
“Nitamuondoa na utaishi kwa
usalama. Wewe ni binaadamu, wajibu wako ni kuoa binaadamu mwenzako mzae watoto
na sio jini. Kama utaoana na jini mtazaa
watoto gani? Mtazaa binaadamu au majini?”
Mganga aliniuliza swali
hilo lakini sikuwa na jibu. Nikaona kweli
ushauri wa kumrithi yule jini haukuwa na maana.
“Kama ulivyoniambia nitakuja
kesho unishighulikie” nilimwambia mganga huyo kabla ya kuagana naye.
Nilipoondoka nyumbani kwa
mganga huyo niliona mawazo yake yalikuwa
sahihi. Si tu ningejitafutia
matatizo mimi mwenyewe kwa
kukubali kuishi na jinni bali pia sikuwa
na uhakika tungezaa watoto wa aina gani.
Kama tungezaa watoto wa kijini
wasingekuwa na manufaa kwangu na hata kama watoto hao wangekuwa ni binaadamu
bado wasingekuwa binaadamu kamili, wasingeweza kuishi na watu wengine.
Lakini kulikuwa na kitu
kilichojificha ambacho nilikuwa sikijui. Nilikuwa sijui kwamba yale maneno ya yule mganga yalikuwa ni ya roho mbaya. Alikuwa akitia fitina ili mimi nisimrithi yule mwanamke wa
kijini kwa kuona kwamba nitaidi utajiri wa bure.
Lengo lake la kuniambia
niende kesho lilikuwa ni kutafuta
mbinu ili amchukue yeye jini huyo.
Asubihi ya siku ya pili yake
nikaenda tena kwa mganga huyo.
“Sasa mwanangu unajua hii
kazi haitafanyika hapa. Itafanyika shanbani kwangu. Itabidi twende shamba”
akaniambia.
“Sawa. Tunaweza kwenda. Gari
lipo”
Mganga akaandaa vifaa vyake.
Akawachukua wasaidizi wake wawili ambao bila shaka alishawaeleza tunakwenda
shamba kufanya nini.Tukaondoka na gari.
Shamba hilo lilikuwa kule kule Chanika lakini lilikuwa mbali kidogo. Akaniambia tuingize gari ndani ya shamba hilo.
Nikaliingiza gari na kulisimamisha mbele ya nyumba yake ya miti na udongo
iliyokuwa katikati ya shamba.
Tukashuka na kuingia kwenye
ile nyumba.
Kwa jinsi
nilivyofahamu baadaye ni kuwa ili aweze kumchukua Maimun alitaka kwanza
aniue mimi na ndiyo madhumuni ya kunipeleka huko shamba.
Baada ya kuniua alitaka achukue
damu yangu na kuioga mwilini mwake kisha ajipake mafuta ya waridi.
Tulipoingia kwenye ile nyumba
nikaambiwa nikae chini. Kwanza kilianza
kisomo. Nilisomewa na watu watatu bila
kuambiwa ninasomewa nini.
Baada ya kisomo hicho mganga
alikoroga dawa kwenye kikombe akanipa ninywe.
“Kunywa hii dawa” alinaimbia
kisha akaongeza.
“Nitakupa na dawa nyingine ya
kuoga”
Kumbe ile haikuwa dawa.
Ilikuwa sumu! Alitaka niinywe ili nife
pale pale na kisha wanitoe damu kabla haijakauka.
Kile kikombe nilikipokea nikakisogeza midomoni
mwangu ili ninywe ile dawa niliyoambiwa. Hapo hapo niliona kikombe kinabetwa.
Kikanitoka mkononi na kuanguka chini. Sumu
iliyokuwamo ikamwagika. Yule mganga na wasaidizi wake walikuwa wameshangaa.
Aliyenibeta kikombe hakuonekana!
Ghafla nikasikia mganga
anapigwa kibao cha nguvu na kuanguka
chini. Alivyoanguka alinza kutokwa na
povu mdomoni. Wale wasaidizi wake walipoona hivyo walitimua mbio.
Nikabaki nimekaa nikiwa sijui
kinachoendelea. Ikabidi niinuke na kumtazama yule mganga. Nikaona amekauka. Tukio
hilo likanishitua.
Nikatoka nje ya ile nyumba kuwatazama
wale waliokimbia lakini sikuwaona.
Nikasikia ninaitwa ndani ya gari langu. Niliposogea kwenye mlango nikamuona
Maimun amekaa kwenye siti ya upande wa pili wa dereva.
“Ingia twende zetu”
akaniambia.
Nikafungua mlango wa gari na
kujipakia.
“Washa gari tuondoke”
Nikawasha gari.
“Umeuona upuuzi wako?” Maimun akaniuliza.
Kwa vile nilikwenda pale kwa ajili ya kumfukuza yeye, sikujibu kitu.
Nilihisi pengine upuuzi aliokusudia ulikuwa ni huo.
“Sisi tunakubaliana kitu
vizuri halafu wewe unakwenda kwa mganga! Ulikwenda kwa mganga kufanya nini?”
Maimun akaniuliza.
Kwa kweli nilitahayari
aliponiuliza hivyo. Nikaendelea kubaki kimya.
USIKOSE Uhondo huu kesho hapahapa