HADITHI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 27
ILIPOISHIA
Mara nikamuona Inspekta Amour
akiingia katika chumba hicho.
Alipoona namtazama alimuuliza
daktari kama angeweza kuongea na mimi.
“Mnaweza kuzungumza” alipata
jibu kutoka kwa daktari.
“Pole sana” Inspekta akaniambia.
“Asante”
“Nini kimetokea pale”
“Kwa kweli palitokea kitu
kama miujiza….”
SASA ENDELEA
Nilimueleza inspekta huyo hali iliyotokea pale. Inspekata
Amour akashangaa.
“Una uhakika kwamba aliyekupigia simu ni Ummy na
alikwambia kwamba utaona?”
“Nina hakika”
“Na una uhakika kwamba
ulimuona amesimama mbele yako wakati unafika pale hoteli?”
“Nina uhakika”
“Tangu tulipooanza uchunguzi
wa Ummy, namba ya Ummy imetegwa na kila
anapopiga au kupigiwa simu inarekodiwa. Tutakwenda kampuni ya simu ili
tuhakikishe kwamba ni namba ya Ummy
iliyokupigia na pia tuhakikishe wakati alipokuwa anakupigia alikuwa karibu na
wewe”
“Nilimuona mbele ya gari
akiwa ameshika simu. Nikafunga breki ili nisimgonge. Kumbe nilikanyaga pedeli
ya mafuta, nikamgonga. Nilipomgonga alitoweka pale pale, nikaona nimegonga
nguzo ya umeme” nikamwambia Inspekta Amour kwa mkazo.
“Ni kitu kisochoeleweka
lakini nitakwenda kwenye kampuni ya simu
kufanya utafiti. Laiti tungeuona mwili wake uliogongwa tusingepata utata lakini
mwili wa Ummy haukuwepo!”
“Alitoweka kimiujiza. Yule
kweli si binaadamu, ule ni mzuka. Ulitaka
kuniua!” nikasema kwa jazba.
“Tulia upate matibabu. Tukio lililotokea
ni kubwa”
“Nimekuelewa Inspekta”
Inspekta huyo akaniaga na kutoka.
Yule daktari pamoja na
wauguzi wake nao waliondoka. Akabaki yule polisi aliyekuwa na bunduki ambaye
sikujua alikuwa akisubiri nini.
Baadaye kidogo muuguzi mmoja alikuja na chano cha dawa.
Akanipa tembe za kumeza kisha akanipiga sindano na kuondoka.
Tukio lile lililotokea
lilikuwa limeushitua moyo wangu na kuniacha katika hali mbaya. Kila wakati ile
picha ya kumuona Ummy akiwa amesimama mbele ya gari huku akiniambia.
“Utaona leo...utaona leo!”
ilinijia akilini ikifuatiwa na ile picha ya kumgonga kisha ghfla akanipotea na
kuona nimegonga nguzo ya umeme.
Zilikuwa picha
zilizonisisimua na kunitia hofu ya kufa. Kama
nilinusurika kufa pale, nilijua si muda mrefu Ummy ataniua kama
alivyowaua wadaiwa wa babu yangu.
Nilijua kikubwa kilichompa
hasira ni kugundua kuwa nilishirikiana na polisi kumuwekea mtego wa kumkamata. Bila
shaka Ummy aligundua kuwa polisi walitaka
kumkamata ndipo akaona anikomoe.
Sikuweza kujua gari langu liliharibika kiasi gani na
lilikuwa wapi. Na pia sikuweza kujua ule
moto uliendelea kuwaka hadi muda gani na
ulisababisha hasara ya kiasi gani.
Laiti ningejua kuwa tukio
lile lingetokea, katu nisingekwenda kule
Lux Hotel wala nisingekubali kumuwekea mtego Ummy wakati nikijua fika kuwa
alikuwa mzuka.
Lakini nikajiuliza, Mzuka
huo ulikuwa una lengo gani na
mimi?
Sikuweza kupata jibu mara
moja.
Baada ya muda kidogo niliona
polisi watatu wa usalama barabarani
ambao walikuja kuchukua maelezo yangu.
Walitaka kujua jinsi ile ajali ilivyotokea, nikawaelezo
lakini niliona wazi kuwa polisi hao hawakuamini maelezo yangu yote. Nusu waliyamini
lakini nusu hawakuyaamini.
Kwamba yule msichana ambaye
nilipanga na Inspekta Amour tumuwekee
mtego alitokea mbele ya gari langu na kisha
nikafunga breki na yakatokea yaliyotokea, polisi hao hawakuamini.
Lakini walitimiza jukumu lao
la kuandikisha maelezo yangu kama nilivyoyatoa
wakaniambia niweke saini,
nikaweka saini.
Walipokuwa wanataka kuondoka
niliwauliza hali ilivyokuwa baada ya ajali hiyo. Polisi hao walinieleza kwamba
ajali hiyo ilikuwa kubwa na kwamba transfoma iliyokuwa katiika nguzo za umeme
ililipuka moto na kusababisha nyaya za umeme kutoa cheche za moto na moto kusambaa
katika eneo kubwa.
Walinieleza kuwa baadhi ya
nyaya zilikatika kwa mlipuko na kuanguka chini.
Patashika iliyotokea
ilisababisha shughuli kusimama kwa muda
katika hotelli ya Lux ambapo wateja walikimbia ovyo kwa hofu.
Ile habari nayo ikazidi kunifadhaisha. Nikajiambia huo mpango ulipangwa na polisi, mimi nilifuatisha
tu maelekezo ya polisi.
Baada ya kupita kama saa nne
hivi, Inspekta Amour akarudi tena pale hospitali.
“Ni kweli ulivyosema”
akaniambia na kuongeza.
“Sauti ya Ummy imenaswa na
amesikika akisema “Utaona leo!” Alikuwa akipiga simu kwenye namba yako.
Vile vile mionzi ya simu yake ilionesha
kuwa ilirushwa katika mnara mmoja na mionzi ya simu yako. Watu wa kampuni ya
simu wameniambia hii inaonesha kuwa ni
kweli mlikuwa karibu au mllikuwa katika
eneo lile lile”
Inspekta huyo aliponiambia
hivyo nikamuuliza kwa pupa.
“Umeamini sasa…umeamini
sasa….? Yule msichana ni mzuka! Kama
alikuwa pale, sasa yuko wapi?
Mbona hakuonekana tena?”
Inspekta Amour akanyamza kimya.
Nilikaa pale hospitali kwa
siku tatu. Polisi aliyekuwa na bunduki alikuwa akibadilishana zamu na mwenzake
kila baada ya saa nane. Baadaye niligundua
kuwa polisi hao walikuwa wakinilinda
mimi kwani nilikuwa chini ya
ulinzi.
Asubuhi ya siku ya tano
nilitolewa hapo hospitali. Nikapelekwa mahakamani moja kwa moja. Huko nilifunguliwa mashitaka ya kuendesha
gari kwa uzembe, kugonga nguzo ya umeme na kusababisha hasara ya karibu
shilingi milioni hamsini.
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose
No comments:
Post a Comment